Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa utashi wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Hayati, Dkt. John Magufuli wa kuamua kuwekeza katika
Sekta ya Uvuvi umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta hiyo.
Dkt. Tamatamah alisema hayo alipokuwa
akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa
Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi
30-31, 2021.
Akiongea na wadau wa Sekta ya uvuvi
waliohudhuria warsha hiyo ya siku mbili, Dkt. Tamatamah alisema kuwa utayari wa
Hayati Dkt. Magufuli kuwekeza katika sekta ya uvuvi umesababisha kuanzishwa kwa
miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta hiyo.
“Sisi ambao tupo katika ngazi za juu za
Wizara tunatambua kwamba utayari wake wa kuona kwamba mchango wa sekta ya uvuvi
unakuwa mkubwa katika pato la Taifa umepelekea mipango mikubwa ya uwekezaji
ambayo itatekelezwa wizarani katika mwaka ujao wa fedha,” alisema Dkt.
Tamatamah
Aliendelea kusema kuwa utayari wake wa
kununua Meli nane (8) za kufanya uvuvi katika bahari kuu ulipelekea timu ya
wataalamu wa Serikali iliyokuwa kwenye majadiliano na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kuhusu mkopo wa kuendeleza sekta ya uvuvi waweke
kipaumbele ununuzi wa meli hizo miongoni mwa vitu vitakavyofadhiliwa na mradi
huo.
“Katika mwaka ujao wa fedha 2021/22,
Serikali itatumia kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
Bandari ya kwanza ya uvuvi ambao utafanyika katika eneo la Mbegani Bagamoyo,
hizi zote ni juhudi na msukumo wake,”alifafanua Dkt. Tamatamah
Aidha, Dkt. Tamatamah alisema pamoja na
nchi kupata msiba huo, uongozi uliopo sasa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hakuna shaka kuwa mipango yote ya uwekezaji iliyoachwa na
Hayati, Dkt. Magufuli katika Sekta ya Uvuvi itatekelezwa kama ilivyopangwa ili
kutimiza malengo yaliyowekwa katika utawala wake.
Kuhusu Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza
Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini, Dkt. Tamatamah
alisema kuzinduliwa kwa mpango huo kutakuwa ni ukombozi kwa wavuvi wadogo kwa
sababu mwongozo huo umeweza kuonesha njia bora zitakazowezesha hali ya wavuvi
wadogo kuimarika na kuinua uchumi wao.
“Mpango huu utasaidia wavuvi wadogo
kufanya uvuvi endelevu ikiwemo kusimamia rasilimali za uvuvi katika muktadha wa
chakula na kuondoa umasikini,” alisema Dkt. Tamatamah
Kwa upande wa wadau, Katibu wa Kikundi
cha Ulinzi Shirikishi cha Rasilimali za Bahari (BMU), Kilindoni, Wilayani Mafia
alisema kuwa wanaishukuru serikali kutambua mchango wa wavuvi wadogo na kuamua
kuandaa mpango huo ambao utawasaidia kupata masoko ya uhakika na zana bora za
uvuvi kwa ajili ya uvuvi endelevu.
Naye, Suzana Ezekiel, Mvuvi Mdogo
anayefanya shughuli zake katika Mwalo wa Kibirizi, Kigoma alisema kuwa wavuvi
wengi wadogo bado wanafanya shughuli zao kwa kubahatisha lakini Mpango kazi huo
utawawezesha kuondokana na hali hiyo na kufanya uvuvi endelevu na wa uhakika.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) wakati akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini ambapo alieleza kuwa Uvuvi mdogo una mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na kuondoa umasikini hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.Warsha hiyo ya siku mbili inafanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ( katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa uvuvi muda mfupi baada ya kufungua Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Sehemu ya wadau wa uvuvi wakifuatilia matukio yanayoendelea katika Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi, Merisia Sebastian akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) alipokuwa akitoa maelezo mafupi kuhusu Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuandaa Mpango Kazi wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini, Yahya Mgawe akiwasilisha mada kwa wadau wa uvuvi kuhusu mchakato wa uandaaji wa mpango kazi wa Kitaifa wa Utekelezaji wa mwongozo wa hiari wa uendelezaji wa uvuvi mdogo nchini katika Warsha ya uzinduzi wa mpango kazi huo inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa nne kutoka kulia) akionesha wadau Kitabu cha Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini muda mfupi baada ya kukizindua katika Warsha inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30- 31, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuandaa Mpango Kazi wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini, Yahya Mgawe.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini katika Warsha ya Uzinduzi wa Mpango huo inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni