Na Mbaraka Kambona, Ruvuma
Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa
Serikali imepanga kutumia Shilingi Milioni 110 kwa ajili ya kuimarisha miundo
mbinu ya Kituo cha Kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila ili kiweze
kuzalisha vifaranga vitakavyokidhi mahitaji yaliyopo sasa.
Dkt.
Tamatamah aliyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na kituo
hicho kilichopo Mkoani Ruvuma Februari 6, 2021.
Alisema
kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na
Uvuvi imepanga kuzalisha vifaranga Milioni 22, na kati ya hivyo, vifaranga
Milioni 16 vitazalishwa na vituo vya kutotolesha vya watu binafsi na vifaranga
Milioni 6 vitazalishwa na vituo vya Serikali.
Dkt.
Tamatamah aliongeza kuwa hivi karibuni Wizara itatangaza zabuni kwa ajili ya
kuimarisha na kuboresha kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa
kuzalisha vifaranga utakaowezesha kukidhi mahitaji yaliyopo sasa.
“Baada
ya kukiimarisha kituo hiki mwaka huu, mwaka ujao wa fedha tutafanya ukarabati
mkubwa na ukarabati huo ukikamilika tunatarajia uwezo wa uzalishaji wa kituo
hiki kuongezeka mara tatu zaidi ya sasa na hivyo kutaongeza uhakika wa
upatikanaji wa vifaranga vya samaki,’’alisema Dkt. Tamatamah
Naye,
Mkurugenzi wa Idara ya Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.
Nazael Madalla alitoa rai kwa Watanzania hasa wale wanaoishi mbali na vyanzo
vikubwa vya maji kama maziwa kujihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki kwani
kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata kipato na lishe bora.
“Naomba
Watanzania watembelee kituo hiki ili waweze kujifunza kwa vitendo namna ya
kuchimba mabwawa makubwa na kufugaji samaki ili kujiongezea kipato na lishe
bora kwa ajili yao na Watoto wao,” alisema Dkt. Madalla
Kaimu
Katibu Tawala anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Mkoani Ruvuma Deogratius
Sibula alisema kuwa Ruhila kimekuwa kituo muhimu sana kwa mikoa ya Nyanda za
Juu Kusini kwa sababu wafugaji wengi wanategemea kituo hicho kupata vifaranga
vya samaki kwa ajili ya kufuga.
“Katika
Mkoa wa Ruvuma kuna Wafugaji wa Samaki takriban Elfu nne (4000) na kuna mabwawa
ya Samaki zaidi ya Elfu Sita (6000) na wote wamekuwa wakitegemea kituo hiki kwa
ajili ya kupata mbegu na kupata elimu ya ugani, hivyo ni kituo muhimu sana
katika kuchagiza ongezeko la ufugaji wa samaki na upatikanaji wa lishe bora kwa
Wananchi,” alisema Sibula
Naye,
Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ruhila, Emmanuel Maneno alisema kuwa baadhi ya
Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakabiliwa na Utapiamlo hivyo fursa ya uhakika
ya kuondokana na tatizo hilo ni kufuga samaki ambao watawahakikishia kupata
lishe bora na kipato cha kujikimu kimaisha.
Maneno
aliongeza kuwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina mazingira mazuri ya kufuga
samaki kwa sababu hali ya hewa ni nzuri, maji yapo ya kutosha lakini pia
malighafi kwa ajili ya kutengenezea chakula cha samaki inapatikana kwa urahisi
na hivyo kufanya gaharama za ufugaji wa samaki kuwa chini.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia - aliyevaa koti) akieleza
jambo wakati akiangalia moja ya Mabwawa ya kufugia Samaki alipotembelea Kituo
cha Kutotolesha Vifanga vya Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma Februari
6, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji
(WMUV), Dkt. Nazael Madalla.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akinawa maji ya Ziwa Nyasa alipotembelea Kituo
cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Nyasa kilichopo Mbamba bay, Wilayani
Nyasa, Mkoani Ruvuma Februari 6, 2021. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Idara
ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla.
Afisa Mfawidhi, Kituo cha kutotolesha
Vifaranga vya Samaki cha Ruhila, Emmanuel Maneno (wa kwanza kushoto) akimueleza
jambo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah
(katikati) alipotembelea Kituo hicho kilichopo Mkoani Ruvuma Februari 6, 2021.
Wa kwanza Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji WMUV), Dkt.
Nazael Madalla.
Mkurugenzi, Idara ya
Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla (wa kwanza kushoto) akifafanua
jambo kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah
(wa tatu kutoka kushoto) alipotembelea Kituo cha kutotolesha Vifaranga vya
Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma Februari 6, 2021.
Hongereni Sana wizara
JibuFuta