Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema kwa kushirikiana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wameanza kufanya kazi kwa kasi kubwa ili kufahamu vipaumbele vya wizara hiyo, ambavyo vinapaswa kujumuishwa katika bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Akizungumza mjini Arusha
mwishoni mwa wiki (12.12.2020) na baadhi ya watumishi wa Kituo cha Taifa cha
Uhilimilishaji (NAIC) mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho,
Mhe. Gekul amesema kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwao kumshauri Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kwa mambo ambayo yatakuwa na
tija kwa taifa na kuyapa vipaumbele.
“Tunakimbia kasi ili
tunapoelekea kwenye bajeti tuweke vitu vyenye kipaumbele kwamba sasa kwa jinsi
sekta hii inavyokwenda tutakuwa kwenye nafasi pia ya kumshauri mheshimiwa rais
kwamba tunachoona sasa kinavyoendelea hiki hakikubaliki na hiki kingine
kinakubalika na tunadhani tukipe kipaumbele ili mwisho wa siku mambo yaende
vizuri.” Amesema Mhe. Gekul
Aidha, Mhe. Gekul amewataka
wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii na kutoendekeza uzembe huku akivitaka
vitengo vya masoko na kukusanyia takwimu vya kituo cha NAIC kuongeza
mawasiliano ili kutoa taarifa za mbegu za ng’ombe bora zinazozalishwa katika
kituo hicho ili kufahamu namna mbegu hizo zinavyoleta tija na namna wafugaji
wanavyozipokea na pia kufahamu matokeo yake.
Pia, amesema kwa kufanya
hivyo kutasaidia kuboresha utendaji kazi wa kituo na kuonekana kwa matokeo
chanya kwa uzalishaji wa mbegu hizo ili zilete tija na kuboresha maisha ya
watanzania, wafugaji na kukuza pato la taifa.
“Pale tunapohitaji mpaboreshe
ndugu zangu naomba mpaboreshe mheshimiwa rais wetu ana imani kubwa sana na
nyinyi wataalamu kwa sababu ndiyo mnaotekeleza ilani kwa vitendo, niwaombe hili
la masoko mlifanyie kazi kubwa sana hili likishafanyika hata uzalishaji
utaongezeka, tutakuza uchumi wetu, tutatoa ajira na maisha ya watanzania
yatakuwa yameboreka.” Amefafanua Mhe. Gekul
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amemwambia
naibu waziri huyo kuwa kwa sasa kituo cha NAIC kinazalisha zaidi mbegu bora za
ng’ombe kuliko idadi ya mbegu zinazopelekwa sokoni.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa
kwa kituo hicho kuhakikisha wanatumia vyema madume ya mbegu ambayo yamenunuliwa
kwa gharama kubwa na serikali kwa ajili ya kuzalisha mbegu ambazo zimekuwa
zikiwekwa kwenye mji wa mimba wa ng’ombe jike kwa njia ya uhimilishaji ili
kuboresha kosaafu za ng’ombe.
Prof. Nonga amefafanua kuwa
kwa sasa kituo cha NAIC kimekuwa kikijiendesha kwa gharama kubwa ilhali
hakipeleki mbegu nyingi sokoni kutokana na uhitaji mdogo, ambapo amesema agizo
la Mhe. Gekul la kuimarishwa kwa vitengo vya masoko na kukusanyia takwimu vya
kituo hicho ni muhimu ili kuwafikia wahitaji wengi wa mbegu hizo na kutoa
elimu.
Awali akisoma taarifa fupi ya
kituo cha NAIC kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul,
Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Paul Mollel amesema kituo kimefanikiwa kusambaza
mbegu bora za ng’ombe sehemu mbalimbali za nchi kuanzia Mwaka 2016 hadi sasa
walau dozi Elfu 30 hadi Elfu 50, ambapo mikoa inayochukua mbegu nyingi ni
Kilimanjaro na Arusha akitolea mfano kwa mwaka 2019 Arusha ilichukua takriban
dozi Elfu 12 na Mkoa wa Kilimanjaro dozi Elfu Tatu huku mikoa mingine ikichukua
kidogo.
Katika ziara hiyo ya siku
moja Mkoani Arusha, Naibu Waziri Gekul ametembelea pia Kampuni ya Shazain
inayohusika na ufugaji wa samaki na na uzalishaji wa vifaranga vya samaki
ambapo amesema kwa sasa wizara inawekeza katika ufugaji wa samaki ikilenga azma
ya serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo kutoa ajira
Elfu 45 kupitia ufugaji huo.
Mhe. Gekul amemtaka
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. ZainaAli Bhimani kuendelea kushirikiana na
wizara pia kuwasaidia wafugaji wadogo elimu juu ya ufugaji wa samaki ili
watanzania wengi waweze kujitokeza kufuga na hatimaye taifa kuwa na mazao mengi
ya samaki yanayotokana na ufugaji ili kutosheleza hitaji la taifa la ongezeko
la samaki wa kufuga na kutoa ajira.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amekuwa katika ziara za mwanzo katika maeneo yanayogusa sekta za mifugo na uvuvi, mara baada ya kuteuliwa na hatimaye kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli kushika wadhifa huo akimsaidia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Shazain
Bw. ZainaAli Bhimani namna kampuni yake inavyozalisha vifaranga vya samaki.
Mhe. Gekul amefanya ziara ya kikazi katika kampuni hiyo iliyopo jijini Arusha
kujionea namna inavyozalisha vifaranga vya samaki na ufugaji wa samaki.
(12.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akishuhudia namna vifaa vya kisasa vinavyotumika
kuhesabu mbegu za ng’ombe mara baada ya kutolewa kwa ng’ombe dume wakati
alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC)
kilichopo jijini Arusha. (12.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akiangalia kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuhifadhia
mbegu za ng’ombe wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Taifa cha
Uhimilishaji (NAIC) kilichopo jijini Arusha. Pembeni yake ni Mkurugenzi wa
Huduma za Mifugo kutoka katika wizara hiyo Prof. Hezron Nonga. (12.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha
Uhimilishaji (NAIC) Dkt. Paul Mollel namna mashine maalum inavyotoa taarifa juu
ya mbegu za ng’ombe mara baada ya kufanyiwa uchunguzi na mashine hizo. (12.12
2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Shazain
Bw. ZainaAli Bhimani namna kampuni yake inavyozalisha vifaranga vya samaki.
Mhe. Gekul amefanya ziara ya kikazi katika kampuni hiyo iliyopo jijini Arusha
kujionea namna inavyozalisha vifaranga vya samaki na ufugaji wa samaki.
(12.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni