Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul ameagiza kuandaliwa kwa mkakati shirikishi wa kupeleka chanjo kwa wafugaji kuanzia mwezi Februari Mwaka 2021 kupitia programu za chanjo ya magonjwa muhimu zitakazosimamiwa na wizara.
Akizungumza (12.12.2020)
wakati akifunga kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA)
kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka
2020, ambapo pia amezindua mchanganyiko wa chanjo tatu kwa ajili ya kuku kwenye
magonjwa ya mdondo, ndui na mafua ameagiza kuanzishwa kwa uchanjaji wa mifugo
ikiwa na lengo kuu la kuhakikisha wizara inasimamia chanjo ya magonjwa yote
ifikapo Mwaka 2022.
“Hizi programu zitasimamiwa
na wizara na siyo kuiachia halmashauri kwani wao hawana uwezo wa kutekeleza
majukumu haya muhimu, hivyo kwa kuwa wizara imeshatayarisha kalenda ya chanjo
na bei elekezi licha ya mapungufu machache yaliyopo ninamuelekeza Mkurugenzi wa
Huduma za Mifugo aende na aandae mkakati shirikishi na kupekeleka chanjo kwa
wafugaji kuanzia mwezi Februari, mwaka 2021.” Amesema Mhe. Gekul
Aidha, Naibu Waziri Gekul
amesema kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Mwaka 2003 serikali inapaswa
kuhakikisha ina madaktari wa mifugo katika mikoa na halmashauri kwa kutambua
kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo na ukosefu wa madaktari wa mifugo kwa mikoa 10
na halmashauri 77 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na halmashauri
husika itawasilisha mapendekezo ya ikama ya watumishi kwa Utumishi kwa ajili ya
kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka 2012/2022, lengo ikiwa ni kuhakikisha
watumishi hawa wanaajiriwa ili kusimamia vizuri tasnia ya wanyama.
Pia, Mhe. Gekul amesema kwa
kutambua kilio kikubwa cha watumishi waliojiendeleza kimasomo ambao
hawatambuliwi na mfumo wa utumishi kwa kuwa wizara haijaainisha sifa ya mafunzo
hitajiwa kwa watumishi wa sekta ya mifugo, tathmini itafanyika ili wizara
iainishe mafunzo hitajiwa kwa watumishi wa kada mbalimbali na kuwasilisha
utumishi na hivyo wale walio na sifa hitajiwa kufanyiwa marekebisho katika
mfumo wa kiutumishi ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi.
Kwa kuzingatia changamoto
zilizopo katika Sekta ya Mifugo nchini Naibu Waziri Gekul amesema atamshauri
Waziri wa Mifugo na Uvui Mhe. Mashimba Ndaki kuunda kikosi kazi kishirikishi
kwa ajili ya kuishauri wizara katika masuala muhimu na kumtaka Mkurugenzi wa
Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Msajili wa Baraza
la Vetarinari Tanzania, kuandaa andiko ili liwasilishwe kwa Waziri Ndaki kwa
ajili ya kupata ridhaa yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) anayemaliza muda wake Prof.
Dominick Kambarage amesema mfumo wa kusimamia watumishi na Sekta ya Mifugo ni
muhimu kuhakikiwa ili kuimarisha sekta hiyo ambapo Mwaka 2019 TVA na TAMISEMI
walianzisha mazungumzo kwa kina namna ya kusimamia sekta na watumishi.
Naye Msajili wa Baraza la
Veterinari Tanzania Dkt. Bedan Masuruli akizungumza kando ya kikao cha 38 cha
Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA), amesema baraza limejadili pia
maadili kwa wataalam mbalimbali wa mifugo ambao wameshindwa kutoa taarifa za
magonjwa kwa idara ya huduma za mifugo kila wiki na kila mwezi, hivyo
kulazimika kutoa onyo kali kwa wataalamu 9 juu ya utoaji wa taarifa.
“Tarehe 9 Desemba Mwaka 2020
baraza liliitisha kikao cha dharula kujadili maadili na kushuhudia karibu
asilimia 44 ya wataalamu hawatoi taarifa za magonjwa ya mifugo ambapo katika
wilaya 184, wataalamu 78 walikuwa wahatoi taarifa lakini baada ya kufanya
mahojiano ya awali, wataalamu 34 walibakia kutotoa taarifa ambapo 19 walifika
kwenye kikao na walipohojiwa wataalamu 9 walionekana hawana ushahidi wamepewa
onyo kali na kuhakikisha katika mwaka mmoja hawakosi kabisa kutoa taarifa za
magonjwa ya mifugo kila wiki na kila mwezi.” Amefafanua Dkt. Masuruli
Katika kikao hicho pia Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amezindua chanjo mpya ya kuku
inayotengezwa na wanasanyansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),
inayodhibiti magonjwa matatu kwa mara moja inayofahamika kwa jina la Tatumoja
imefanyiwa utafiti na kutengenezwa na wanasanyansi hao wakiongozwa na Prof.
Philemon Wambura na Dkt. Mirende Kichuki.
Chanjo hiyo ina mchanganyiko
wa chanjo tatu kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mdondo, ndui ya kuku na mafua
ya kuku na kwamba itakuwa na faida kwa kuweza kutunzwa na kutumika katika joto
la kawaida bila kuhitaji ubaridi wa jokofu.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akipatiwa maelezo na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka katika wizara hiyo Prof. Hezron Nonga kuhusu chanjo za mifugo zinazozalishwa hapa nchini na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), wakati alipotembelea mabanda ya wadau wa Sekta ya Mifugo nchini kabla ya kufunga kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020. (12.12.2020)
Naibu waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (wa pili kutoka kulia) akikata utepe kuashiria rasmi
matumizi ya chanjo inayofahamika kwa jina la Tatumoja kwa jina ya kudhibiti
magonjwa ya mdondo, ndui ya kuku na mafua ya kuku wakati akifunga kikao cha 38
cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha
kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020. (12.12.2020)
Muonekano wa chanjo
inayofahamika kwa jina la Tatumoja kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mdondo,
ndui ya kuku na mafua ya kuku ambayo imefanyiwa utafiti na kutengenezwa na
wanasanyansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakiongozwa na
Prof. Philemon Wambura na Dkt. Mirende Kichuki. Chanjo hii imezinduliwa na
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul wakati akifunga kikao cha 38
cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha.
(12.12.2020)
Naibu waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akizungumza wakati akifunga kikao cha 38 cha Chama cha
Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe
10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020, ambapo ameagiza programu ya chanjo ya
mifugo kote nchini ambayo itakuwa ikisimamiwa na kuanza mwezi Februari Mwaka
2021. (12.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul wakati alipotembelea mabanda ya wadau wa Sekta ya
Mifugo nchini kabla ya kufunga kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo
Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi
Desemba Mwaka 2020, alijionea dawa aina ya Paranex ambayo imekuwa ikizalishwa
hapa nchini kwa ajili ya kuogeshea mifugo na kusisitiza ni muhimu kwa serikali
kuendelea kuwalinda wadau wanaowekeza hapa nchini. (12.12.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam wa afya ya
wanyama baada ya kufunga kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo
Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi
Desemba Mwaka 2020. (12.12.2020)
Mwenyekiti wa Chama cha
Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) anayemaliza muda wake Prof. Dominick
Kambarage akizungumza wakati wa kikao cha 38 cha chama hicho kilichofanyika
Mkoani Arusha na kusisitiza baadhi ya maboresho katika sera mbalimbali ili
kukuza sekta ya mifugo na wataalamu wa afya ya wanyama nchini. (12.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni