Na Mbaraka Kambona, Dar es Salaam
Serikali imewataka baadhi ya
wafugaji wenye mtindo wa kuongeza unga katika Maziwa kuacha kufanya hivyo kwani
sio tu inaharibu biashara ya maziwa katika soko la ndani ya nchi bali hata soko
la nje.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alitoa onyo hilo alipotembelea
Banda la Maonesho la Bodi ya Maziwa lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya
bidhaa za Viwanda yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl.
Nyerere jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Prof. Gabriel alisema
wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa kitendo hicho ni kibaya,
wanajidanganya wao wenyewe na wasipo jirekebisha wataishia pabaya.
“Bodi endeleeni kutafuna wale
wote ambao wanachakachua maziwa kadri iwezekanavyo na sheria ichukue mkondo
wake na hatutakuwa na huruma yeyote kwa sababu wanaharibu taswira nzima ya
biashara ya maziwa ndani na nje ya nchi,” alisema Prof. Gabriel
Aliongeza kwa kusema kuwa
Wafugaji wajue kwamba Serikali ina vipimo ambavyo vinaweza kutambua maziwa
yaliyowekwa unga na hivyo aliwataka wale wote wanaojihusisha na uhalifu huo
kuacha kufanya hivyo kwani watakaokutwa sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Prof. Gabriel aliitaka
Bodi ya Maziwa kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongezeka na wawahamasishe
Watanzania kadri iwezekanavyo walau ndani ya miaka mitano ijayo wazidi walau
lita zaidi ya 100 kwa mwaka kwani kwa sasa unywaji upo kwenye lita 54 jambo
ambalo ni aibu kwa nchi yenye ng’ombe milioni 33. 4 na inazalisha lita za
maziwa bilioni 3.01 huku kukiwa na viwanda vya kuchakata maziwa 99.
“Bodi fanyeni kazi ya ziada,
msifanye kazi kwa mazoea, wekeni sayansi kwenye kazi yenu na pia pimeni elimu
mliyoitoa imeeleweka kiasi gani ili wale wanaofanya vizuri muwapongeze na wale
wanaokosea muwaadhibu kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuifanya tasnia iwe
bora zaidi,” aliongeza Prof. Gabriel
Aliongeza kuwa anaamini
tasnia hiyo ya maziwa itaendelea kusimamiwa vizuri sana na itachangia vizuri
katika uchumi wa kati ambao Dkt. John Pombe Magufuli ameshafanya kazi ya ziada
kuipeleka nchi katika uchumi wa kati miaka mitano kabla, hivyo anaamini nchi
itaendelea kupanda kiuchumi na zao la maziwa ni muhimu likaendelea kuimarishwa
ili litoe mchango unaohitajika katika kukuza pato la taifa.
“Bodi ya Maziwa hakikisheni
ubora wa maziwa unakuwepo na yapatikane kwa wingi kwa ajili ya kujenga afya
bora kwa watumiaji,” alifafanua Prof. Gabriel
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Temeke, Godwin Gondwe alisema katika Wilaya ya Temeke na Mkoa wa Dar es Salaam
watahakikisha wanaendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa kupitia michezo
mbalimbali na wamejipanga hivi karibuni wanatarajia kufanya tamasha kubwa
ambalo litatumika kuchagiza pia unywaji wa maziwa nchini.
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Maziwa, Noely Byamungu alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanajenga utamaduni
kwa jamii kupenda kunywa maziwa na wameanza na kundi la wanamichezo lakini kuna
mpango mkakati wa kitaifa wa kuwafikia Watoto mashuleni.
“Mpango wa kitaifa unalenga
kukuza utamaduni wa unywaji wa maziwa kwa Watoto wadogo na kwa kufanya hivyo
kutasaidia kujenga jamii inayopenda kunywa maziwa, hivyo tunawaomba Waandishi
wa Habari mtusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa ili
tuwe na jamii inayopenda kunywa maziwa kwa afya,” alisema Byamungu
Aliongeza kwa kusema kuwa
katika kutekeleza mpango huo Bodi itashirikisha wadau tofautitofauti ikiwemo
Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Wizara ya Mifugo na
Uvuvi ili kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongozeka lakini pia wafugaji
wazalishe na waweze kupata masoko ya uhakika.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (watatu kutoka kushoto)
akiwapigia makofi kuwapongeza wacheza sarakasi wakati akiongoza vikundi
mbalimbali vya mazoezi vilivyoshiriki mbio za taratibu (Jogging) katika bonanza
la maziwa lililofanyika jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020. Washiriki hao
walikimbia takriban kilomita 5 kutoka Uwanja wa Taifa mpaka kwenye Viwanja vya
Maonesho ya Mwl. Nyerere (Sabasaba) kwa kupitia njia ya Police Changombe.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati aliyevaa Miwani)
akimsikiliza kwa makini mmoja wa Maafisa wa Kampuni ASAS alipotembelea banda la
Kampuni hiyo lililopo katika Maonesho ya bidhaa za Viwanda yanayofanyika katika
Viwanja vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi, Masoko na Uzalishaji, Stephen Michael cheti cha ushiriki wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Bonanza la Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkahidhi Naibu
Mkurugenzi, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Latifa Khamis
cheti cha ushiriki katika bonanza la maziwa lililofanyika katika Viwanja vya
Mwl. Nyerere jijiji Dodoma Disemba 6, 2020.
Mmoja wa washiriki wa Bonanza
la Maziwa akifurahia moja ya bidhaa ya maziwa inayozalishwa na Kampuni ya Asas
katika bonanza hilo lililofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere
(Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Maziwa, Noely Byamungu (kulia) akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe
muda mfupi baada ya kumalizika kwa Bonanza la Maziwa lililofanyika katika
Viwanja vya Mwl. Nyerere (sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akionesha kuvutiwa na moja ya
bidhaa inayozalishwa na Wajasiriamali kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
alipotembelea Banda la chuo hicho katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda
yanayofanyika katika Viwanja Maonesho vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) Dar es Salaam
Disemba 6, 2020.
Kaimu Msajili wa Bodi ya
Maziwa, Noely Byamungu (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo
na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) alipotembelea
banda la Maonesho la Bodi hiyo katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda
yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (sabasaba) jijiji Dar es Salaam
Disemba 6, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe wakati wakiagana baada ya kumalizika kwa Bonanza la Maziwa lililofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam Disemba 6, 2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni