Wadau wa TAFICO wametakiwa kujadili na kutoka na mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi hususani vitakavyotumika katika ujenzi wa meli ya uvuvi itakayomilikiwa na shirika hilo kwa niaba ya serikali.
Hayo yamesemwa na Kaimu
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Bw. Emmanuel Bulayi leo tarehe
01/10/2020 wakati akifungua kikao cha wadau hao kilichowahusisha washiriki
kutoka kampuni za uvuvi, TDB, THA, DMI, FETA, TAFIRI, TASAC, Menejimenti ya
TAFICO, Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu na wawakilishi wa Idara ya Uvuvi.
Bw. Bulayi amesema serikali
ilishatiliana saini na serikali ya Japan mkataba wa kuanza utekelezaji wa
Programu ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii utakaosaidia ununuaji wa vifaa vya
uvuvi ikiwa ni pamoja na meli moja ya uvuvi.
“Kwa kuwa taratibu za awali
zilishakamilika ambapo tayari mkandarasi kwa ajili ya kununua vifaa hivyo
ameshapatikana CROWN AGENT kutoka Japan, kinachosubiriwa ni sisi kutoka na
mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi tunavyotaka vinunuliwe na mkandarasi
huyo,” alisema Bw. Bulayi.
“Serikali katika suala hili
imeona ni vema wadau wakashirikishwa ili na wao waweze kutoa ushauri wao
kutokana na uzoefu walionao ili vifaa hivyo vitakapoagizwa viweze kukidhi
mahitaji kama ilivyokusudiwa hivyo ni muhimu majadiliano haya yatakapokamilika,
orodha ya vifaa hivyo iweze kujulikana,” aliongeza Bw. Bulayi.
Naye Kaimu Meneja Mkuu
TAFICO, Bi. Esther J. Mulyila amesema lengo la kikao hicho ni kujadili aina ya
vifaa vya uvuvi vitakavyonunuliwa kwa ajili ya meli ya uvuvi, majokofu kwa
ajili ya kuhifadhia samaki na mtambo wa kuzalishia barafu.
Bi. Mulyila amesema TAFICO
kwa sasa itatekeleza majukumu yake pamoja na miradi 10 yenye thamani ya bilioni
89.8 itakayokuwa inatekelezwa kwa awamu, ambayo itashirikisha wadau.
Miradi hii imegawanyika
katika maeneo matatu, kwanza ni miradi ya uvuvi kwa kutumia meli za aina 3 za
uvuvi (kwa ajili ya uvuvi wa maeneo matatu ya bahari), mradi wa mtambo wa kuzalisha
barafu, mradi wa majokofu ya kuhifadhia samaki, mradi wa viwanda vya uchakataji
samaki, miradi ya ukuzaji viumbe maji (uzalishaji wa vifaranga vya samaki,
uzalishaji wa vyakula vya samaki, ufugaji wa samaki kwenye vizimba na ufugaji
wa samaki kwenye mabwawa).
Serikali inaendelea na
mchakato wa ufufuaji wa shirika lake la TAFICO ambapo imepata msaada kutoka
serikali ya Japan wa Yen Milioni 200 takriban shilingi za kitanzania Bilioni
4.2 kupitia Programu ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii.
Miongoni mwa vifaa
vitakavyonunuliwa kupitia programu hiyo ni pamoja na meli moja ya uvuvi,
majokofu ya kuhifadhia samaki, na mtambo wa kuzalisha barafu. Serikali ya Japan
itanunua, itasafirisha, itasimika mitambo katika eneo la Ras Mkwavi na
kufundisha juu ya matumizi ya mitambo hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi,
Bw. Emmanuel Bulayi akifungua kikao (kwa niaba ya
Katibu Mkuu Uvuvi) cha kujadili vigezo mbalimbali vitakavyowezesha kupatikana
mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi vya TAFICO vitakavyonunuliwa kupitia
ufadhili wa serikali ya Japan. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu TAFICO, Bi. Esther
J. Mulyila na kushoto kwake ni Mhadhiri Mwandamizi – UDSM, Bw. Paul Onyango akifuatiwa
na Meneja Mkuu Mstaafu TAFICO, Bw. Francis R. Nkoka. (01.10.2020)
Kaimu Meneja Mkuu TAFICO, Bi.
Esther Mulyila (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa kikao cha kujadili
vigezo mbalimbali vitakavyowezesha kupatikana mapendekezo ya aina ya vifaa vya
uvuvi vya TAFICO vitakavyonunuliwa kupitia ufadhili wa Japan. Kushoto kwake ni Mkurugenzi
wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akifuatiwa na Mhadhiri Mwandamizi –
UDSM, Bw. Paul Onyango. (01.10.2020)
Wadau wakisikiliza mada
katika kikao cha kujadili vigezo mbalimbali vitakavyowezesha kupatikana
mapendekezo ya aina ya vifaa vya uvuvi vya TAFICO vitakavyonunuliwa kupitia
ufadhili wa Japan. (01.10.2020)
Picha ya pamoja ya Mkurugenzi
wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi na washiriki wa kikao cha kujadili
vigezo mbalimbali vitakavyowezesha kupatikana mapendekezo ya aina ya vifaa vya
uvuvi vya TAFICO vitakavyonunuliwa kupitia ufadhili wa Japan. (01.10.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni