Nav bar

Jumanne, 22 Oktoba 2024

PROF. SHEMDOE AONGOZA TIMU YA WATALAAM KUTOKA TANZANIA MKUTANO WA IOTC BANGKOK, THAILAND

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe aongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa 13 wa Kamati ya Wataalam ya Vigezo vya Mgawanyo wa Mavuno ya Samaki aina ya Jodari na Jamii zake (13th Technical Committee on Allocation Criteria - TCAC13) ya Kamisheni ya Jodari ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Tuna Commission (IOTC) unaofanyika Bangkok, Thailand kuanzia tarehe 21 hadi 24 Oktoba 2024. 

Prof. Shemdoe ameongoza Timu hiyo ya wataalam akiwa ameongozana na Maafisa wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) akiwemo Dkt. Emmanuel Sweke, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA.

Katika kuhakikisha mgawanyo huo wa samaki unakuwa sawa kwa nchi wanachama, kamati hiyo ya IOTC iliundwa  katika kikao chake cha 14 kilichofanyika Busan, Korea tarehe 1 hadi 5 Machi, 2010 kwa lengo la "kujadili vigezo vya ugawaji kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali za Jodari katika Bahari ya Hindi na kupendekeza mfumo mzuri wa mgao.

 Aidha,  kwa takribani miaka 13 sasa Kamati hiyo imeendelea kujadili mfumo utakaowezesha usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za samaki aina ya Jodari na jamii zake kwenye Bahari ya Hindi.

Kwa kuzingatia mikakati ya Tanzania katika kukuza Uvuvi wa bahari kuu,Tanzania imepiga hatua kubwa  ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko na ufufuaji wa mashirika ya uvuvi (TAFICO na ZAFICO) na matarajio ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi kwa Ujumla wake.

Prof.Shemdoe amesema kuwa "Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu tumeendelea kutetea msimamo wetu  kama Nchi ya Mwambao inayoendelea (Developing Coastal State) wa haki yake ya msingi ya kupata kiasi cha samaki kinachostahili pindi ambapo mfumo wa ugawaji wa rasilimali za Jodari utakapopitishwa na kuanza kutumika." Alisema Prof.Shemdoe.

Vilevile, haki hii ya msingi imeainishwa katika Sura ya 16 ya Mkataba wa kuanzishwa kwa IOTC (IOTC Agreement) ya mwaka 1993, Mkataba wa Uhifadhi na Usimamizi wa Samaki wanaohama hama (Highly Migratory Fish Stocks and Highly Straddling Fish stocks), “United Nations Fish Stock Agreement - UNFSA) wa mwaka 2001 na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari (United Nations Convention on the Law of the Sea - UNCLOS) ya mwaka 1982.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DSFA Dkt. Emmanuel Sweke (Kushoto) Katika Mkutano wa IOTC nchini Bangkok,Thailand Jana tarehe 21 Oktoba 2024.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akifuatilia wasilisho  katika Mkutano wa IOTC unaoendelea nchini Bangkok Thailand Jana tarehe 21 Oktoba, 2024. Lengo la Mkutano huo ni kuhusu namna bora ya Kufanya mgawanyo wa Kiasi cha Samaki aina ya Jodari katika Bahari ya Hindi kwa nchi wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania.



Jumatatu, 21 Oktoba 2024

TANZANIA KUWA MWENYEJI MKUTANO WA JUKWAA LA TASNIA YA KUKU NA NDEGE WAFUGWAO KWA NCHI ZA SADC

Na. Stanley Brayton

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 17 Octoba, 2024 Serena Hotel jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza leo tarehe 11 Oktoba, 2024  jijini Dodoma, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdala Ulega, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Riziki Shemdoe, amesema lengo la mkutano huo ni kukuza fursa za ajira nje na ndani ya nchi pamoja na kujadili na kubadilishana uzoefu wa sekta hiyo  na nchi za SADC.

“mkutano huo utatoa nafasi kwa Tanzania kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo katika Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa hizo katika nchi za SADC na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za SADC katika Tasnia hiyo” amesema Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameshukuru uongozi wa awamu ya sita uliochini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele na kufungua fursa za wawekezaji katika sekta za uzalishaji ikiwemo Tasnia ya Kuku.

Vilevile, Prof. Shemdoe amesema tukio hilo litaambatana na maonesho ya kitaifa ya Tasnia ya kuku na ndege wafugwao yatakayofanyika 18-19 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar Es Salaam.

Prof. Shemdoe amesema, mgeni Rasmi katika mkutano huo ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko.

Aidha, Prof. Shemdoe amewakaribisha wadau wote wa ufugaji kuku na watanzania kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika matukio haya, kwani jukwaa hili na maonyesho haya ni bure na hayana gharama.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, kuhusu uwepo wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utafanyika tarehe 16 - 17 Oktoba, 2024 katika Hoteli ya Serena, Jijini Dar es Salaam na kufuatiwa na maonesho ya Kitaifa ya Tasnia ya kuku na ndege wafugwao yatakayofanyika Oktoba 18 -19, 2024 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ni katika Ukumbi wa Wizara - NBC, Oktoba 11, 2024, Dodoma





TANZANIA NA IRAN ZA SAINI HATI SABA ZA MAKUBALIANO ILI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Na. Stanley Brayton

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran zimesaini hati saba  za makubaliano ili kukuza diplomasia ya uchumi baina ya mataifa hayo mawili.

Hafla ya kusaini hati hizo za makubaliano imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Oktoba, 2024, katika mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Kilimo wa   Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh walishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini hati hizo lililohusisha Wizara za Kisekta, baadhi ya Taasisi za Umma na Taasisi binafsi. 

Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliohusisha Viongozi wa ngazi za juu za Serikali za nchi hizo, wakiwemo Mawaziri, Mhe. Balozi Kombo amemshukuru Mhe. Golamreza Nouri kwa jitihada zake za kuimarisha ushirikiano wa uwili na azma yake katika kuongeza maeneo ya ushirikiano yakiwemo Mifugo na Uvuvi,  biashara na  uwekezaji,   kilimo, nishati, ulinzi   na   usalama na elimu. Maeneo mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na Iran yatahusisha sekta ya afya, sayansi na teknolojia, na utamaduni. 

Hati hizo za makubaliano zilihusisha hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   na Wizara ya Kilimo ya   Jamhuri ya Kiislam ya   Iran, kuhusu ushirikiano katika sekta ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Mifugo na Uvuvi  ya Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Iran kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya ya wanyama; na hati ya makubaliano baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Michezo na Vijana ya Iran. 

Hati nyingine za Makubaliano zilisainiwa baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye ulemavu ya Tanzania na Wizara ya Ushirika, Kazi na Maendeleo ya Jamii ya Iran kuhusu ushirikiano katika kazi, ajira na usalama wa raia.Taasisi   za Serikali zilizotia saini   hati za makubaliano ni pamoja   na Kikosi cha Uokozi  na Zimamoto, chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, na Kitengo kinachoshughulikia masuala ya moto cha Iran, kuhusu ushirikiano katika huduma za zima moto na uokozi. 

Aidha katika hafla hiyo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilitia saini hati  ya makubaliano na Taasisi ya Uendelezaji  Biashara ya Iran kuhusu ushirikiano  katika kukuza na kutangaza biashara kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Kwa upande wa sekta   binafsi, Taasisi ya Biashara, Viwanda  na   Kilimo ya Tanzania ilisaini hati ya  makubaliano na Taasisi  ya Biashara,  Viwanda  na  Kiimo ya Iran kuhusu   ushirikiano katika uanzishwaji wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya nchi hizo mbili. 

Akitoa neno la shukrani   wakati wa kuhitimisha   kikao hicho, Naibu   Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano  wa Afrika Mashariki   anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb) amewashukuru Mawaziri, Viongozi wa Serikali na Sekta Binafsi pamoja na wadau wote kwa mchango wao katika kufanikisha mkutano huo wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, kwani umeziwezesha pande zote mbili kufikia malengo ili  kukuza  diplomasia na ushirikiano  wa kimataifa.

Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Iran, ulianza rasmi tarehe 16 Oktoba 2024, na ulitanguliwa na kongamano la biashara, kikao cha ngazi ya  Wataalam   na   Maafisa   Waandamizi   kutoka   Tanzania   na   Iran   kilichoandaa   agenda   za kuiamarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo pamoja na Kikao cha ngazi ya juu ya Viongozi wa nchi hizo wakiwemo Mawaziri, ambacho kiliidhinisha  na kutia saini Hati za Makubaliano ya pamoja kwa manufaa ya nchi hizo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (kulia aliyesimama), na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh (kushoto aliyesimama) wakionesha hati za makubaliano ya ushirikiano baada ya kuzisaini, ni katika Mkutano wa tano wa Tume ya pamoja ya kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran, ambayo umefanyika katika Ukumbi wa JNICC, Oktoba 19, 2024. Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (kulia aliyekaa na kusaini), akisaini hati za makubaliano ya ushirikiano na Iran, ambazo hati hizo zimehusisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, ni katika Hafla ya utiaji saini hati za makubaliano ya ushirikiano wakati wa Mkutano wa tano wa Tume ya pamoja ya kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiislam ya Iran, ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa JNICC, Oktoba 19, 2024. Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislaam ya  Iran, Mhe. Golamreza Nouri Ghezelcheh


Jumatano, 16 Oktoba 2024

NWM-DKT. BITEKO: ASILIMIA 55 YA KAYA NCHINI ZINAFANYA SHUGHULI ZA UFUGAJI KUKU

Na. Stanley Brayton

Naibu Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko amesema asilimia 55 ya kaya nchini zinafanya shughuli za ufugaji kuku uliopelekea ongezeko la uchumi jumuishi unaolenga kujenga kesho iliyo bora.

Amyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Serena Hotel Dar Es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Tasnia ya Kuku na Ndege wafugwao kwa Nchi za Kusini mwa Afrika.

“Tasnia hii imeajiri zaidi wanawake na vijana, vilevile inazalisha malighafi za viwanda, inachangia usalama wa chakula na lishe na upatikanaji wa fedha za kigeni” 

Aidha Dkt. Bitteko amesema lengo la mkutano huo ni kujadili na kubadilishana uzoefu kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na kubainisha fursa za kimkakati zinazohusu tasnia ya kuku na ndege wafugwao.

Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Ulega amesema kuwa kuku ni mifugo rafiki na mifugo hiyo haihitaji eneo kubwa katika kuitunza, inazaliana kwa haraka na haihitaji mtaji mkubwa hivyo mikakati ya uwekezaji katika Tasnia hiyo ili kuongeza ajira hususani kwa Vijana na Wanawake na kuhangia pato la taifa,

Aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya Mifugo na Uvuvi kipindi wanapofanya tafiti zinazohusu mifugo na uvuvi na mazao yake ili kuepusha kuleta taharuki kwa watumiaji wa bidhaa hizo.


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, akihutubia washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, akihutubia washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wa Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao ambalo limefanyika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (aliekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Mashirika ya Binafsi, ni katika Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao, lililofanyika katika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam. Wa pili kulia kwa waliokaa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega


Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (aliekaa katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na vijana wa mnyororo wa thamani katika Tasnia ya kuku kutoka nchi Tanzania (62), Msumbiji (10) na Shirikisho la Vyama vya Kilimo Kusini mwa Afrika SACAU (10) ambao wamepongezwa leo kwa mchango wao katika Tasnia hiyo, ni katika Jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege wafugwao, lililofanyika katika Hoteli ya Serena, Oktoba 16, 2024. Dar es Salaam. Wa pili kulia kwa waliokaa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega


Jumatano, 9 Oktoba 2024

DKT. MPANGO AZIPONGEZA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KWA UTEKELEZAJI MZURI WA SHUGHULI ZAKE

Na. Stanley Brayton

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amezipongeza Sekta za Mifugo na Uvuvi kwa utekelezaji mzuri wa shughuli zake ambazo zimelenga kukuza shughuli za ufugaji na uvuvi kwa kuendana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhudumia wananchi na kuwapa maisha Bora.

Akizungumza, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango leo Oktoba 8, 2024 katika Ziara yake wilayani Igunga, Mkoani Tabora, Dkt. Mpango amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya vizuri katika kuhakikisha mifugo bora inapatikana kwa wananchi kwa kutoa pembejeo bora kwa wafugaji na wavuvi, vilevile kutoa mikopo kwa wafugaji na wavuvi pamoja na kuwapatia mbegu bora za vifaranga vya samaki pamoja na madume Bora ya ng'ombe.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo imefanya mambo mengi sana kwa watanzania na ata katika Wilaya ya Igunga ikiwa ni kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi.

“tuna fursa ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, na ya utengenezaji wa mabwawa ya kufugia samaki pamoja na kutoa madume Bora ya ng'ombe kama mbegu”, amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, Mhe. Mnyeti amesema, Madume Bora ya ng'ombe yalishagawiwa katika baadhi ya wilaya, ikiwemo Wilaya ya Bahi, Serengeti na Bunda.

Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema mpango huo ni endelevu hapa nchini, na Wizara inampango wa kusambaza madume hayo Bora ya ng'ombe katika wilaya zote nchini Tanzania ila yaweze kupanda ng'ombe wa kienyeji na kupata ng'ombe wengine walio Bora.


Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, akimuuliza swali Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (hayupo pichani), ni lini Wizara italeta Madume Bora ya ng'ombe Wilayani Igunga, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, akijibu swali la Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpangoni (hayupo pichani), kuwa Wizara italeta Madume Bora ya ng'ombe 20 Wilayani Igunga baada ya wiki tatu, ni katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Picha ni wananchi wakimsikiliza Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora ya Oktoba 8, 2024, Igunga - Tabora


Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukene kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe Bora kwa watoto na mama wajawazito ili waweze pata Protini ya kutosha itakayowasaidia kukuza ufikiri wa mtoto na kusisitiza Maafisa kutoa elimu kuhusu lishe Bora ili jamii zielewe nini maana ya lishe bora na umuhimu wake, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora


Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, akisalimia wanakijiji wa Bukene na kutoa Salamu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ni katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora



 Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango (aliyeshika bomba la maji), akifungua maji kama Ishara ya Uzinduzi  na Upanuzi wa Mradi wa Maji kutoka ziwa Viktoria kwenda Bukene, ni katika Ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora, Wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti


Picha ni Washiriki mbalimbali wakiwemo wakazi wa Bukene na Maafisa mbalimbali na Viongozi wa Serikali wakiwa katika Ziara ya kikazi Mkoani Tabora ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, Oktoba 8, 2024, Nzega - Tabora





Jumanne, 1 Oktoba 2024

DKT. MHINA AIPA HEKO MRADI WA AgResults KWA UTEKELEZAJI MZURI

Na. Stanley Brayton

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina amepongeza utekelezaji wa Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa (AgResults Tanzania Dairy Productivity Challenge) kwa utekelezaji mzuri wa kukuza Sekta ya Mifugo, ususani katika kuboresha mahusiano mazuri kati ya wafugaji na maafisa wa malisho pamoja na maafisa Mifugo, na kutoa pembejeo kwa wafugaji na utoaji wa huduma za Ugani ili kukuza Sekta hii ya Mifugo. 

Akizungumza, katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa,  kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Mhina amesema anawapongeza maafisa wa Mradi wa AgResults kwani wametumia namna mbalimbali ili kuweza kuwafikia wafugaji wadogo na kuweza kuwapatia huduma mbalimbali za ugani, ikiwa ni pamoja na kutoa pembejeo za Mifugo.

“mradi huu umefika mpaka kwa wafugaji mbaimbali maeneo ya vijijini kiasi kwamba umetoa huduma kwa wafugaji na mifugo yako kwa kuboresha malisho pamoja utoaji chanjo”, amesema Dkt. Mhina

Aidha, Dkt. Mhina amesema ni wajibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha huduma zinawafikia wafugaji hadi vijijini, ikiwa ni pamoja na utoaji chanjo za mifugo na tiba kwa mifugo pamoja na pembejeo ili kuweza kuwapa huduma mbalimbali zitakazosaidia kuboresha mifugo na maisha ya wafugaji.

Vilevile, Dkt. Mhina amesema Wizara iangalie ni namna gani inaweza kuwafikia wafugaji Tanzania nzima ili kuhamasisha na kutoa mbegu Bora za madume ya ng'ombe kwa wafugaji na kuhakikisha matibabu ya mifugo yanapatikana kwa wakati.

Dkt. Mhina ametoa rai kwa maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi katika kuboresha huduma za mifugo, na kuhakikisha maziwa salama yanapatikana kwani asilimia kubwa ya watanzania hawanywi maziwa salama, na hii inatokana na maziwa mengi kuuzwa kienyeji, na mashirikiano hayo yatasaidia katika kuboresha usindikaji na utunzaji maziwa kwa njia ya usalama zaidi kiasi cha kutanua masoko nchini hadi nchi za nje.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina na ndiye Mgeni Rasmi, akitoa Hotuba fupi, katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma


Msimamizi wa Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa (AgResults Tanzania Dairy Productivity Challenge Project), Bi. Neema Mrema, akitoa Ripoti ya Utekelezaji wa Mradi wa AgResults, ni katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma


Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Stephen Michael, akitoa neno la Ukaribisho kwa washiriki, ni katika Kikao cha kufunga Mradi wa Utatuzi wa Changamoto za Uzalishaji wa Maziwa, uliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Mtumba, Octoba 01, 2024, Dodoma






Jumatatu, 30 Septemba 2024

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YATOA ELIMU YA KICHAA CHA MBWA KWA WANANCHI

Na.  Martha Mbena

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetaoa elimu kwa wananchi juu ya kichaa cha Mbwa Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 28.2024.

Akiongea na wakazi wa kitongoji cha Ng'walo gwa magole kata ya Bulemeji Wilayani hapo Leo (27.09.2024) Mkurugenzi Msaidizi wa afya ya jamii ya Veterinari kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Stanford Ndibalema amewataka wananchi kuzingatia chanjo ya kichaa cha Mbwa ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

"Huu ugonjwa unaweza kuzuilika iwapo tutaamua kuwachanja Mbwa wetu, hivyo kila mmoja wetu anaemiliki Mbwa anapaswa kumlinda Mbwa huyo dhidi ya ugonjwa huu", Amesema Dkt. Ndibalema.

Aidha, Dkt. Ndibalema amesisitiza umuhimu wa kuwaona wataalam wa Mifugo kwa ajili ya chanjo badala ya kusubiri chanjo ya bure inayotolewa na Serikali 

Baadhi ya wazazi na wanafunzi waliofikiwa Na elimu ya kichaa cha Mmbwa wanasema  elimu  imewasaidia kutambua dalili za Mbwa mwenye kichaa na matibabu ya mtu aliyeng'atwa na Mbwa.

Elimu hiyo imetolewa katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Misungwi zikiwemo Shule za msingi na sekondari pamoja na wataalam kutoka sekta ya Mifugo.








SERIKALI KUFANYA UTARATIBU WA KUWEZESHA UPATIKANAJI WA CHANJO ZA KICHAA CHA MBWA ZA KUTOSHA NCHINI

Na. Martha Mbena

Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya Kimataifa tayari imeanza kufanya utaratibu wa kuwezesha upatikanaji wa chanjo za kutosha ili Mbwa na paka wengi wapate Chanjo dhidi ya kichaa Cha Mbwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo  Ndug. Abdul Mhinte alipokuwa anafunga kilele Cha maadhimisho ya siku ya Kichaa Cha Mbwa Duniani yaliyofanyika Kitaifa Katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza Septemba 28.2024.

Mhinte amesema katika jitihada za kutokomeza ugonjwa huo Serikali inaratibu upatikanaji wa chanjo za kutosha kwa ajili ya kuchanja Mbwa na paka ambapo kwa kuchanja zaidi ya idadi ya 70% ya Mbwa na Paka kwa miaka mitano mfululizo tunaweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo Nchini.

"Pamoja na hatari kubwa ya ugonjwa huu, ni kwamba unaweza kuzuilika kwa asilimia mia Moja na tunaweza kutokomeza iwapo tutaweza kuwachanja Mbwa na Paka wetu na kuwatunza vizuri", amesema Mhinte. 

 Aidha, Septemba 28 kila mwaka ni siku ya kichaa cha Mbwa duniani ambapo kutokana na takwimu za Wizara ya Afya Tanzania, watu 1,500 hufariki kwa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa kila mwaka huku watu 60,000 hufariki kila mwaka kwa ugonjwa huo duniani. 

Pia Mhinte amesema lengo la siku hiyo ni kuongeza ufahamu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo na kujua namna ya kujikinga.

"Tunajua Mbwa na Paka ni wanyama muhimu katika maisha yetu lakini wanyama hawa kama hawatatunzwa vizuri pamoja na kuwakinga dhidi ya magonjwa wanageuka kuwa hatari kwa mwanadamu",amesema Mhinte.

 Pia, amesema mwanadamu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kung'atwa na Mbwa au Paka na kwa njia ya mate ya mnyama alieathirika na ugonjwa huo na kuweza kuambukizwa kwa mwanadamu.

Mh. Naibu katibu Mkuu amesema lengo la umoja wa mataifa ni kuhakikisha ugonjwa unatokomezwa duniani kote ifikapo 2030 kwa kutumia kauli mbiu ya "Breaking Rabies Boundaries" kama hamasa ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuchagua kufanya maadhimisho hayo Wilayani hapo.

Mhe. Samizi amesema ni jukumu la kila mmiliki wa Mbwa kumtunza Mbwa wake kwa kumpatia chakula, dawa na Chanjo zote na kumpenda Mbwa huyo ili kuhakikisha Mbwa  wahazuruli mitaani.

Kauli mbiu ya kutokomeza kichaa cha mbwa inakuja na jitihada za kuondoa vikwazo vya kuwezesha mbinu za kutokomeza ugonjwa huo zikiwemo matumizi ya teknologia katika kutokomeza ugonjwa, kuongeza uelewa kwa wananchi kupitia kampeni mbalimbali na kuunganisha wadau.





Ijumaa, 27 Septemba 2024

MNYETI AGAWA MADUME BORA YA NG’OMBE 40 KWA WAFUGAJI SERENGETI NA BUNDA

Na. Stanley Brayton

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amekabidhi madume bora 20 ya ng’ombe wa nyama kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Nyichoka Wilayani Serengeti na madume Bora 20 kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Mariwanda Wilayani Bunda, ili iwasaidie kuzalisha kizazi chenye uwezo wa kutoa nyama nyingi zaidi ya wale wa asili waliopo hapa nchini. 

Akikabidhi, madume hayo Bora ya Ng'ombe kwa vikundi vya wafugaji katika hafla fupi zilizofanyika leo Septemba 27, 2024 Wilayani Serengeti na Bunda mkoani Mara, Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mnyeti amesema kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikitekeleza mpango wake wa kuleta mabadiliko katika Sekta ya Mifugo, ambapo mpango huo umegusa nyanja mbalimbali za uzalishaji wa mifugo ili kuhakikisha ukuaji wa uhakika wa uzalishaji wa mifugo na mazao yake ili kukidhi ongezeko la soko la ndani na nje ya nchi.

“mpango huu unahusisha kuboresha mbari za mifugo, upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na kuhakikisha afya ya mifugo kwa kuwapatia wafugaji dawa za kuogeshea na kampeni ya chanjo”, amesema Mhe. Mnyeti

Aidha, Mhe. Mnyeti amesema hatua zingine zinazochukuliwa ni pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa kuwapatia maafisa ugani mafunzo rejea na vitendea kazi vikiwemo pikipiki kwa ajili ya usafiri wa kuwafikia wafugaji, kuongeza fedha kwa ajili ya utafiti pamoja na kujenga na kuboresha masoko ya mifugo.

Vilevile, Mhe. Mnyeti amesema asilimia 97 ya ng’ombe walioko hapa nchini ni wale wa asili, ila ng’ombe hawa wa madume Bora ni wavumilivu kwenye masuala ya magonjwa pamoja na uhaba wa malisho na maji, na uzalishaji wake wa nyama ni wa juu ukilinganisha na ng’ombe wengine wa asili, kwani wameboreshwa kwa kuingiza vinasaba vya mbegu yenye uzalishaji mkubwa kwa kuchanganya mbegu za ng’ombe wa asili na wale wenye uzalishaji wa juu kunazalisha ndama mwenye sifa zaidi ya wazazi wake kwani anakuwa na uzalishaji mkubwa kuliko yule wa asili na kwa upande mwingine anakuwa na uwezo wa kuvumilia mazingira magumu kuliko yule mwenye uzalishaji mkubwa asiye wa asili.

Mhe. Mnyeti ameongezea kwa kusema, Wizara imefanya hivyo kwa vikundi kadhaa vya wafugaji kwenye Halmashauri mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kutoa hamasa kwa wafugaji ili kubadilika na kufuga kibiashara kwa kuwa na ng’ombe wenye tija.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Msaidizi  Uzalishaji Mifugo, Bw. Simon Lyimo amesema Wizara ya Mifugo imejipanga vyema katika kutatua changamoto mbalimbali za wafugaji pamoja na mifugo.

“tumechukua hatua mbalimbali za kuiboresha mifugo ili wafugaji waweze kupata mifugo bora na kufuga kwa tija”, amesema Bw. Lyimo

Naye, Kiongozi wa wafugaji Kanda ya Nyanza ambayo inajumuisha Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga, Bw. Kikuri Mnikokostantine ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Mhe. Abdallah Ulege (Mb), kwa kuwapatia madume Bora ya ng'ombe na kuomba kuongezewa tena kama ikimpendeza Mheshimiwa Rais na Waziri mwenye dhamana.

Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (aliyeshika nyaraka ya Buluu), akikabidhi mdume bora 20 ya ng'ombe kwa wafugaji wa kijiji cha Nyichoka, ni katika Hafla fupi iliyofanyika Septemba 27, 2024, Serengeti - Mara


Picha ni madume Bora 20 ya ng'ombe, yaliokabidhiwa kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Nyichoka na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, Septemba 27, 2024, Serengeti - Mara


Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, akizungumza na wanavikundi wa ufugaji ng'ombe (hawapo pichani), ni katika Hafla fupi ya kukabidhi Madume Bora 20 ya ng'ombe kwa vikundi vya wafugaji katika kijiji cha Nyichoka, Septemba 27, 2024, Serengeti - Mara






Jumatano, 25 Septemba 2024

PROF. SHEMDOE ASHIRIKI UVUNAJI SAMAKI MRADI WA KISOKO

Na. Stanley Brayton

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, ameshiriki shughuli za uvunaji wa samaki aina ya Sato katika Vizimba vilivyopo eneo la Kisoko ili kushuhudia  hali ya Samaki hao ikiwemo ukubwa wake na shughuli za uuzaji wa Samaki hao ulivyofanyika katika eneo hilo.

Akizungumza, leo Septemba 25, 2024 mkoani Mwanza alipotembelea eneo hilo la Mradi wa Ukuzaji Samaki kwa njia ya Vizimba, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Shemdoe amesema samaki hawa walikuwa wadogo sana, ila leo hii wanavunwa wakiwa wakubwa kiasi cha kwamba wanafaa kuingia sokoni na kuliwa.

"hii mbegu ya samaki ilikuwa ndogo sana na haishikiki, ila leo hii tunavuna ikiwa kitu ambacho tunakiona hapa kwa mara ya kwanza, na hii yote ni Shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha ili ziweze kutumiwa na Vijana hawa wa Jenga Kesho Iliyo Bora - BBT katika uzalishaji huu wa bidhaa za uvuvi" amesema Prof. Shemdoe

Aidha, Prof. Shemdoe alisema Tarehe 30 Januari mwaka huu Mhe. Rais alizindua Mradi huu ambao ulikuwa na vizimba 222 na Boti 160 ambazo zimekopeshwa katika maeneo ya ziwa Viktoria na Bahari ya Hindi, na kutokana na mkopo huo, leo hii kinaonekana kilichopatikana ambacho ni uwepo wa Samaki wengi na wakubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Imani Kapinga, amesema lengo la Mradi huu ilikuwa ni kufikisha gramu 300, ila ni habari njema kuwa kuna samaki wenye gramu 400 hadi 500, kiasi kwamba malengo yamevukwa.

Vilevile Dkt. Kapinga amesema, mvuno wa leo ni wa Kikundi kimoja kati ya vikundi 12 vilivyopo hapa eneo la Kisoko, ila vikundi vingine vitaendelea kuvuna kuanzia mwezi wa kumi na moja hadi wa tatu mwakani. 

Naye, Afisa Maendeleo ya Biashara Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TAD, Bw. Samson Siyengo amesema Mkoa wa Mwanza umenufaika kwa kiasi kikubwa kwani zaidi ya Bilioni 4 zimetolewa kwa Vijana wa Jenga Kesho Iliyo Bora waliopo Mwanza.

Mnufaika wa Vizimba ambaye pia ni Katibu wa Kikundi kilichovuna samaki leo, Kikundi cha Vijana Nguvu Kazi, Bw. Pius Mtenya ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya  Mheshimiwa Abdallah Ulega kwa kuwapa Mkopo husio na Riba ili waweze kufanya shughuli za ukuzaji viumbe maji ili waweze kujipatia kipato.

Vilevile, Bw. Mtenya Amesema katika uvunaji wa leo wanataraji kupata jumla ya tani 19.8, katika vizimba 6, ikimaanisha kila kizimba kitatoa tani 3.3, na hii inaonyesha ni jinsi gani watakavyopata faida kutokana na Mradi huu.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe (wa kwanza kushoto), akiwa ameshikiria Samaki aina ya Sato waliovunwa kwenye Vizimba, ni mara baada ya kushiriki shughuli za uvunaji Samaki hao, uliyofanyika eneo la Mradi wa Kisoko, Septemba 25, 2024, Mwanza








Alhamisi, 19 Septemba 2024

TANGA YAJIPANGA KUONGEZA UZALISHAJI WA SAMAKI

Na Edward Kondela

Mkoa wa Tanga unajikita kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki na mazao mengine ya baharini, ili kuzinufaisha jamii zake kupitia shughuli hizo zinazohusiana na Uchumi wa Buluu.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Balozi Dkt. Batilda Burian, ameyasema hayo (18.09.2024) kwenye mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa ajili ya kujadili masuala ya uhifadhi wa bahari kwa vizazi na maendeleo ya sekta hiyo Mkoani Tanga.

Amesema uvuvi ni moja ya sekta muhimu mkoani humo, hususan kwenye wilaya za Tanga, Pangani, Mkinga na Muheza ambapo takwimu zinaonesha kuwepo jumla ya wavuvi 13,336 na vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa 1,922. 

Mhe Balozi Dkt. Burian ametoa mfano kuwa, mwaka 2023/2024 samaki waliouzwa mkoani humo walikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 47.208, zilizowezesha ukusanyaji ushuru uliofikia takriban Shilingi Milioni 951.7 huku wakulima wa mwani wakifikia 5,300.

Ameongeza kuwa uzalishaji wa zao hilo la baharini umefikia tani 3,000 kwa thamani ya takribani Shilingi bilioni 5, kiasi kinachotarajiwa kuongezeka kufikia tani tani 5,000.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, amemtaja Mhe Balozi Dkt. Batilda Burian kuwa ni ‘Champion’ wa ulinzi wa rasilimali za bahari na mazao yake, kutokana na jitihada mbalimbali anazozifanya katika sekta hiyo Mkoani Tanga.

Amebainisha kuwa mkuu huyo wa mkoa amekuwa akifanya kampeni mbalimbali za kuhakikisha rasilimali za bahari hususan samaki wanazaliana kwa wingi kwa kupiga marufuku na kusimamia matukio ambayo yanaashiria uvunjifu wa sheria katika Sekta ya Uvuvi.

Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kutoa elimu na kuhakikisha wadau wa sekta hiyo wanaendelea kufanya shughuli kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu za nchi lengo likiwa kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa kupitia Sekta ya Uvuvi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh ametoa wito kwa Sekretarieti za Mikoa kusimamia halmashauri kutekeleza sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi, kupitia sera, sheria na kanuni za uvuvi, kuandaa miongozo ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi na mazingira yake, kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya uvuvi.

Amesema endapo hayo yatasimamiwa vyema rasilimali za uvuvi zitakuwa na tija kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na kuifanya Sekta ya Uvuvi kuwa endelevu na kubadili mtazamo juu ya jamii ya wavuvi na wote wanaojishughulisha na mazao ya uvuvi.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wametoa maoni yao juu ya kuendeleza rasilimali za uvuvi wakitaka elimu zaidi kutolewa kwa wadau wa uvuvi ya namna ya kutunza rasilimali za uvuvi na mazao ya uvuvi kwa ujumla na kuendelezwa kwa kampeni mbalimbali za kudhibiti uvuvi haramu.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede (kulia kwake) na baadhi ya viongozi kutoka katika wizara hiyo na ofisi ya mkuu wa mkoa huo, baada ya Mhe. Balozi Dkt. Burian kutembelewa ofisini kwake na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Mhede, kabla ya kushiriki mkutano wakujadili namna ya kukuza rasilimali za uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu, kilichohusisha baadhi ya viongozi na wadau wa Sekta ya Uvuvi Mkoa wa Tanga. (18.09.2024)