Serikali kupitia Wizara ya
Mifugo na Uvuvi imetumia shs. Milioni 249.27 kununua Mizani 82 ambayo itatumika
kupima uzito wa mifugo wakati wa biashara katika minada ili kuifanya biashara
hiyo kuwa na tija zaidi kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Mashimba Ndaki aliyasema hayo katika hafla fupi ya kupokea mizani 82
iliyofanyika jijini Dar es Salaam Februari 6, 2023.
"Mizani inawekwa katika
minada ili kuleta ushindani wa wazi wa bei kulingana na uzito wa mnyama, ni
jukumu letu kuhakikisha mifugo tunayoiuza minadani inapimwa na tunajua uzito
wake, ili tuweze kupata faida ya mifugo yetu," alisema Mhe. Ndaki
Alisema kwa muda mrefu
biashara ya mifugo nchini imekuwa ikifanyika kwa kukisia na kuangalia umbo la
mfugo na si uzito halisi na hivyo kuifanya biashara kutokuwa na tija
inayotarajiwa huku akibainisha kuwa lengo la Serikali ni kufunga mizani hiyo
katika minada yote nchini lakini kwa kuanzia wameanza na hiyo 82.
"Jambo hili limekuwa
halina tija kwa wafugaji kwa kuwa bei inayouzwa hailingani na uzito wa mnyama,
hivyo huchangia kudhoofisha kipato cha wafugaji,"alifafanua
Alibainisha kuwa kwa kutambua
changamoto hiyo na nyingine zinazoikabili Sekta ya Mifugo, Wizara iliamua kuja
na mpango wa mabadiliko ili kuifanya sekta kutoka katika kufanya shughuli zake
kienyeji na kuziboresha na kuwa za kibiashara.
"Mwaka huu wa fedha
2022/2023 tulitenga kiasi cha Shs.Milioni 249.27 kwa ajili ya kununua mizani 82
na tayari mizani hiyo yote imenunuliwa," alibainisha
Aidha, aliwataka wasimamizi
wa minada kuhakikisha mifugo yote inayouzwa inapimwa na kumbukumbu za mifugo
iliyouzwa na uzito wake zinawekwa.
"Pia hakikisheni mizani
iliyonunuliwa na Serikali inatunzwa, endapo kutatokea uharibifu wa makusudi ili
kuzuia zoezi hili la kupima mifugo, wahusika watawajibika," alisisitiza
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa
jiji la Dar es Salaam, Amani Mafuru alisema kwa muda mrefu mifugo iliyokuwa
ikifika katika minada biashara imekuwa ikifanyika kwa makisio lakini Wizara
ikaona umuhimu wa kuwepo kwa mizani hiyo.
"Hii itafanya biashara
iwe ya uhakika hakuna mtu anayepunjwa, mfugo ukipimwa uuzwe kwa bei ambayo
mfanyabiashara alitarajia na mnunuzi anunue kwa bei tarajiwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akikata utepe ishara ya upokeaji na uzinduzi wa mizani 82 ikiwa ni moja ya mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo wakati wa hafla fupi iliyofanyika Jijini Dar es salaam, Februari 06, 2023
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na wafugaji, pamoja na wafanyabiasha wa mifugo ( hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya upokeaji na uzinduzi wa mizani za kupima uzito wa Mifugo ikiwa ni moja ya mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 06, 2023
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni