Doria zilizofanyika katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria zimesaidia kupunguza vitendo vya uvuvi haramu, biashara ya samaki wachanga na utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kwa asilimia 80.
Hayo yamesemwa leo
(06.02.2023) Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Abdallah Ulega wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Mhe.
Dkt. Oscar Kikoyo aliyetaka kujua ni kiwango gani Vikosi Kazi (Task Forces)
zimepunguza tatizo la uvuvi haramu katika Ziwa Victoria kwa kipindi cha miaka
mitatu iliyopita.
Naibu Waziri Ulega amesema
kuwa katika kipindi cha miaka mitatu (3)
kuanzia 2017/2018 - 2019/2020, Kikosi Kazi kilifanya doria na operesheni katika
maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Ziwa Victoria. Utekelezaji wa doria hizo
uliwezesha kukamatwa kwa zana haramu zilizokuwa zikitumika katika shughuli za
uvuvi ikiwemo nyavu za Makila, Makokoro, Nyavu za Timba (Monofilament) na nyavu za dagaa. Pia, vifaa vilivyokuwa vinatumika
kwenye uvuvi haramu na utoroshaji wa mazao ya uvuvi ikiwemo injini za boti
pamoja na gari.
Katika kipindi cha miaka
mitatu (3) 2017/2018-2019/2020 Kikosi Kazi kilifanya kazi katika maeneo
mbalimbali ya Ukanda wa Ziwa Victoria. Matokeo ya doria hizo yaliwezesha
kukamata zana haramu zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uvuvi ikiwemo
Nyavu za Makila 28, 867, Makokoro 532, Nyavu za Timba (Monofilament) 262, Nyavu za dagaa 257, pamoja na injini 10 na gari 5.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia
Sekta ya Uvuvi inaandaa Mkakati wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi unaolenga
kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi. Mkakati huo una
vipaumbele vya muda mrefu na muda mfupi. Utekelezaji wa mkakati huo
utashirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Vyombo vya Ulinzi
na Usalama, Jamii za Wavuvi na Wadau wengine wa Sekta ya Uvuvi wakiwemo NGOs na
CBOs.
Aidha, Sekta ya Uvuvi imeanzisha
vituo vya doria (16) katika Ukanda
wa Ziwa Victoria ikiwemo maeneo ya mipakani ili kuimarisha shughuli za Ulinzi
na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi na kudhibiti mianya ya utoroshaji wa mazao
ya uvuvi kwenda nje ya nchi. Vituo hivyo viko katika Mkoa wa Mwanza vituo (3), Mkoa wa Simiyu (1), Mkoa wa Mara (3), Mkoa wa Geita (1) na
Mkoa wa Kagera (8).
Vilevile, kwa sasa Serikali
inaendelea kutoa elimu kwa wavuvi ili kuondokana na matumizi ya zana haramu
ambazo zinatishia kupungua kwa samaki katika maji ya asili. Hivyo, nitoe wito
kwa wavuvi, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni za Uvuvi za mwaka
2009 pamoja na marekebisho yake.
Pia Naibu Waziri Ulega
amesema kuwa uvuvi haramu husababisha kupungua kwa samaki wazazi na hivyo
kusababisha kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria. Aidha, amesema kuwa
serikali itaendelea kufanya doria zitakazosaidia kudhibiti uvuvi haramu ambapo
amewataka wataalam wanaoshiriki doroa hizo kuwa waadilifu na waaminifu katika
kutekeleza kazi hiyo. Haya ameyasema akijibu maswali ya nyongeza ya Mhe. Dkt. Oscar
Kikoyola.
Vilevile Naibu Waziri Ulega alijibu maswalli ya Mbunge wa Jimbo la Ukerewe aliyetaka kujua ni lini mikopo ya zana za kisasa za uvuvi zikiwemo boti itatolewa, ambapo alisema serikali ya Awamu ya sita imejizatiti katika kuondoa uduni na kero ya wavuvi ya kutumia vyombo hafifu, hivyo kuamua kuwapatia vyombo vya uvuvi vya kisasa na tayari taratibu za kupata zana hizo zimekamilika na tayari zipo boti takribani 160 za kisasa zitakazogawiwa kwa wavuvi waliotimiza vigezo vilivyowekwa na serikali. Pia serikali imetoa fedha takribani bilioni 20 kwa ajili ya ufugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji wa samaki aina ya sato na walengwa ni vikundi vya vijana na wanawake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni