Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea na hatua mbalimbali za ununuzi wa Meli Nane (8) za Uvuvi katika Bahari Kuu kama alivyoagiza Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwahani, Mhe. Yahya Abdulwakil Ahmed ambaye alitaka kufahamu mkakati wa serikali wa kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya ununuzi wa meli nane za Uvuvi katika bahari kuu Novemba 1,2022.
Alisema, katika kutekeleza agizo hilo Serikali itanunua Meli Nane (8) kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) chini ya Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo-IFAD kwa awamu mbili ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 meli nne (4) na vifaa vyake zitanunuliwa. Meli hizo zitagawanywa Tanzania Bara Meli (2) na Zanzibar Meli (2).
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Mkataba baina ya Serikali na IFAD ununuzi wa meli hizo unatakiwa kukamilika baada ya kufanya Tathmini ya Athari za Kimazingira na Kijamii pamoja Upembuzi wa Kina wa uendeshaji wa meli za uvuvi. Hata hivyo taratibu za kufanya Upembuzi wa kina unaendelea.
Aidha akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kwahani, Mhe. Yahya Ahmed aliyetaka kufahamu kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishirikishwa katika hatua za awali za manunuzi ya meli hizo, Mhe. Ulega alisema ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar upo kwa kiasi kikubwa sana na jambo hili linaratibiwa na ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na ofisi ya makamu wa pili wa Rais upande wa Zanzibar, na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uchumi wa Buluu lakini na mashirika yetu vilevile ya TAFICO na ZAFICO yote yanafanya kazi hii kwa pamoja .
Mhe. Ulega alihitimisha majibu yake kwa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Lindi Mhe. Salma Kikwete aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali kwa mikoa miwili ya Mtwara na Lindi juu ya upatikanaji wa meli hizi kwa kuzingatia kule kuna samaki wengi sana ambapo alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha kwamba meli hizi kwanza zitamilikiwa na shirika letu la TAFICO kwa ubia na mashirika binafsi,
"kwa upande wa mikoa ya Lindi na Mtwara na sehemu zote ambazo shughuli za uvuvi zinafanyika serikali imekuja na mpango madhubuti wa kukopesha wavuvi ambapo boti zaidi ya mia na hamsini (150) zitakopeshwa nchi nzima katika maeneo ambayo shughuli za uvuvi zinafanyika" alisema Mhe. Ulega
Aliongeza kuwa tayari maelekezo na maombi mbalimbali yameshapokelewa ili harakati na utaratibu wa kuweza kuwapata wenye sifa za kukopa mikopo hii zifanyike na hatimaye waweze kupata mikopo isiyo na riba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni