Nav bar

Alhamisi, 17 Novemba 2022

SERIKALI IMEJIPANGA KUONGEZA THAMANI ZAO LA DAGAA

Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inatarajia kujenga vichanja 80 vya kukaushia dagaa (Drying Racks), kununua mitambo minne (4) ya umeme ya kukaushia dagaa (Electric Drier) na Solar Tents 15 katika Halmashauri za Kilwa, Mafia, Pangani na Bagamoyo kuanzia mwaka wa fedha 2023/24.  


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi, ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwapatia vifaa vya kisasa wananchi wanaofanya shughuli za kukausha dagaa, Novemba 08, 2022.


Akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalum Mhe. Maryam Mwinyi aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa haraka wa kuwasaidia wanawake wanaojihusisha na ukaushaji wa dagaa, Mhe. Ulega alisema mpango wa Serikali ni kutangaza zao la dagaa kuwa ni zao la biashara ili kuvutia taasisi za fedha kuwakopesha wanawake wanaokausha dagaa. Pia, tunashauri wanawake wanaokausha  dagaa kutumia fursa ya fedha za halmashauri kwa ajili ya kupata mikopo.


Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kufungua soko la dagaa kimataifa ili kutoa fursa zaidi kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya dagaa.


Alisema Wizara itaendelea kuwahamasisha na kuwaunganisha Wajasiriamali wa sekta ya uvuvi ili waweze kupata mikopo nafuu kupitia TADB itakayowawezesha kununua zana bora na za kisasa za kuendesha uvuvi endelevu, biashara yenye tija ya mazao ya uvuvi na matumizi ya vifaa vya kisasa vya kukaushia dagaa.


Vilevile Naibu Waziri Ulega akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nchinga Mhe. Salma Kikwete aliyetaka kufahamu mpango Serikali kwa wanawake wanajishughulisha na zao la mwani kwa kuwapatia vifaa, alisema katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya kununua vifaa vya kuzalisha mwani ikiwemo kamba na kujenga maghala ya kuhifadhi mwani. Lengo ni kuongeza uzalishaji wa zao la mwani kutoka tani 3,500 hadi kufikia tani 10,000 kwa mwaka.


Aidha akijibu swali ya nyongeza la Mbunge wa viti maalum Mhe. Mwantumu Zodo aliyetaka kufahamu siku Serikali itapeleka vichanja vya kukaushia dagaa, Mhe. Ulega alisema  katika mwaka wa fedha 2022/23 baada ya kukamilisha taratibu zote za kitaalam ambazo  zilikuwa zikitukwamisha tutakwenda kutekeleza ahadi hii ya serikali kwa uhakika kabisa.


Mhe. Ulega alihitimisha majibu yake kwa kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum Mhe. Dkt. Alice Kaijage aliyetaka kufahamu siku mradi wa kuwainua wavuvi utafika katika wilaya za Mkuranga na Kibiti ambapo alisema Wilaya za Mkuranga na Kibiti ni miungoni mwa Wilaya zitakazonufaika na mradi huo vilevile zitafaidika na mradi mkubwa wa blue economy ambapo kutajengwa maghala ya kuifadhia samaki , masoko pamoja na vichanja.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni