Nav bar

Alhamisi, 22 Septemba 2022

SERIKALI YAKUSUDIA KUBORESHA MNYORORO WA THAMANI WA ZAO LA PWEZA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema  utafiti wa ufuatiliaji (traceability) wa zao la Pweza unaokwenda kufanyika wilayani Kilwa utasaidia kuongeza thamani ya zao hilo kwa wavuvi nchini.  


Aliyasema hayo  Septemba 19,2022 wakati akifungua  kongamano la kuunda mkakati wa ufuatiliaji wa kielektroniki  wa uvuvi wa pweza  lililofanyika katika hoteli ya Peacock, Jijini  Dar es Salaam, 


Alisema Serikali ya awamu ya sita inafanya jitihada kubwa ya kuweka mazingira safi na salama katika sekta ya uvuvi ili kuifanya iwe na mchango mkubwa kwa taifa.


''Utafiti huu utakuwa chachu ya kuongeza thamani ya zao la pweza na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye zao hilo kwa wingi'' alisema.


Alisema utafiti huo unakwenda sambamba na sera ya taifa ya uvuvi ambayo inasisitiza kulinda, kubainisha, kuendeleza na kuvua.


Waziri Mashimba alisema anaipongeza Taasisi ya Ufuatiliaji na Uhalalisho wa Mazao ya Bahari (SALT) katika kutafuta ufumbuzi wa matumizi endelevu wa mazao ya bahari.


Aidha Mhe. Ndaki alisema mazao ya bahari yanayopatikana nchini au kuzalishwa nchini ni salama ikiwemo uwepo wa maabara bora za kupima na kukagua mazao hayo.


''Tuna wataalamu wa kutosha ambao wanakagua samaki kabla na baada ya kuvuliwa, maeneo yote ya kuvulia mazao hayo ni salama'' alisema.


Alisema usalama huo ndio unafanya wawekezaji kuja nchini, ambapo hivi karibuni wamepatikana wawekezaji wawili wanaotaka kuwekeza katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na mwingine mkoani Tanga  


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Eston Paul aliipongeza SALT kwa kuja na wazo hilo, ambalo litakuwa chachu ya uwekezaji wa mazao ya bahari.


''Kilwa ndio kuna samaki wengi na wa kila namna, sasa kuna bandari kubwa inataka kujengwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia'' alisema.


Alisema uwepo wa mipango bora na ujio wa ufuatiliaji huo, utaifanya Kilwa kuwa moja ya eneo bora la uvuvi wa mazao ya bahari.


Pia, Mwakilishi wa SALT, Jenny Barker alisema umoja huo umekuwa ukishirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa matumizi endelevu wa mazao ya bahari.


''Tunajikita katika ufuatiliaji wa mnyororo wa usambazaji wa vyakula na miradi hiyo kutekelezwa na taasisi ya FishWise'' alisema.


SALT ni taasisi yenye ubia na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Packard Moore, Mfuko wa Hisani wa Walton, ambao unatoa ushauri kuhusiana na uzalishaji endelevu wa mazao ya bahari.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kongamano  la kuunda mkakati wa ufuatiliaji wa kielektroniki  wa uvuvi wa pweza  lililofanyika katika hoteli ya Peacock, Jijini Dar es Salaam, Septemba 19, 2022

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau walioshiriki kongamano la kuunda mkakati wa ufuatiliaji wa kielektroniki  wa uvuvi wa pweza mara baada ya ufunguzi wa kongamani hilo  lililofanyika kwenye hoteli ya Peacock, Jijini Dar es Salaam, Septemba 19,2022

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni