Na. Edward Kondela
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetia saini hati ya makubaliano na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) ili kufanya utafiti utakaosaidia kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi hivyo kusaidia ongezeko la wawekezaji katika Sekta ya Uvuvi.
Utiliaji saini wa makubaliano hayo yamefanyika leo (12.05.2022) jijini Dar es salaam baina ya Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ismael Kimirei na Mkurugenzi Mtendaji wa OIA katika Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi, ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki mara baada ya kushuhudia makubaliano hayo amesema yana lengo la kutathimini kiwango cha samaki kinachoweza kupatikana katika eneo la bahari na itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika hapa nchini.
Waziri Ndaki amefafanua kuwa kazi ya kutathimini kiwango cha samaki kilichopo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ina gharama kubwa na kwamba inahitaji fedha nyingi na rasilimali zingine ili kuweza kufanya kazi yenye matokeo mazuri.
“Tuna matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo sisi kama nchi tuna matarajio makubwa sana.” Amesema Mhe. Ndaki.
Waziri Ndaki ameongeza kuwa bado sekta ya uvuvi inachangia pato dogo kwa taifa hivyo utafiti huo utasaidia nchi kuwa na mipango ya uhakika juu ya uvunaji wa rasilimali za uvuvi na kushawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei akafafanua juu ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kubainisha kuwa utafiti huo utafanyika kwa kushirikisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI) ili kutimiza malengo ya sekta ya uvuvi Tanzania Bara na Visiwani.
Dkt. Kimirei amesema makubaliano hayo yatawezesha muda wowote kuwasili kwa meli ya kufanya utafiti ili kuiwezesha nchi kupata takwimu ya aina, wingi na mtawanyiko wa samaki katika ukanda wa bahari ili nchi iweze kupata taarifa sahihi ya uwepo wa samaki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Mohamed Al Tooqi amesema utafiti huo utasaidia kuongeza thamani ya biashara katika Ukanda wa Bahari ya Hindi kwa Tanzania na kwamba wanatarajia huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano baina ya Tanzania na Oman katika shughuli mbalimbali zinazohusu Sekta ya Uvuvi.
Zoezi la utiaji saini wa hati ya makubalino baina ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) kwa ajili ya kufanya utafiti wa samaki katika ukanda wa Bahari ya Hindi limeshuhudiwa pia na Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti katika Sekta ya Uvuvi kwa Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ana matumaini na uhakika kazi itafanyika vizuri na kuleta matokeo ambayo nchi ina matarajio makubwa katika kukuza Sekta ya Uvuvi. (12.05.2022)
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Balozi wa Oman nchini Tanzania Dkt. Salim Al-Harbi na watafiti kutoka Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam, mara baada ya hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya utafiti wa Sekta ya Uvuvi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi baina ya TAFIRI na Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA). (12.05.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni