Nav bar

Alhamisi, 12 Mei 2022

TAASISI NA WIZARA ZATAKIWA KUSHIRIKIANA KUKABILI UTAPIAMLO

 Wizara na Taasisi zinazohusiana na masuala ya lishe nchini zimetakiwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya Utapiamlo kuhakikisha jamii na Taifa linakuwa salama.


Akizungumza katika mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu Mpango wa Pili Jumuishi wa Masuala ya Lishe wa Kitaifa kwa Menejimenti ya Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Ukumbi wa Wizara hiyo Mei 10, 2022 Jijini Dodoma Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Lishe kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo Kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha alisema mpango huo unaanza utekelezaji wake mwaka 2021-2022/ 2025-2026 hivyo kama sekta ya mifugo ina sehemu ya kufanya kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa.

Alisema kwamba vipaumbele katika mpango huo ni Utapiamlo wa chini na wa kuzidi, utapiamlo utokanao na virutubishi na madini kwa kuzingatia makundi yote ndani ya jamii akisema kuwa afya bora huanzia ngani ya familia hadi Taifa huku akisema kwamba bado ipo changamoto kubwa ya lishe hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Kwa takwimu za mwaka 2018 zinasema asilimia ya watoto 32 ya watoto wa Tanzania wana udumavu, ukondefu watoto zaidi ya 500,000 nchini wanakabiliwa na ukondefu wakati asilimia 45 ya kina mama walio umri wa kuzaa wanakabiliwa na ukosefu wa damu na asilimia 28 ya kina mama wanakabiliwa na uzito uliokithiri ndiyo maana tumekaa kuona namna gani sekta za lishe zinaaweza kutusaidia,”Alisema Mratibu huyo.

Pia alihimiza sekta binafsi kuzalisha bidhaa za vyakula na dawa zenye ubora unaozingatia lishe bora kama hatua ya kushirikiana na Serikali kutatua changamoto ya utapiamlo pindi mlaji wa mwisho anapotumia bidhaa hizo badala ya kudumaza afya za walaji.

“Sekta binafsi zina mchango mkubwa sana katika suala la lishe kwa sababu wao ndiyo wazalishaji wa bidhaa za vyakula au dawa kwahiyo sisi tunashirikiana nao kwa karibu maana tunataka watengeneze vyakula au bidhaa zinazosaidia kukabili hii changamoto na zizingatie makundi muhimu ya chakula na katika mpango huu wa pili tunategemea sana watusaidie,”alisisitiza Bi. Debora.

Aidha akitaja mikoa inayoongoza kwa utapiamlo licha ya kuwa na kiwango  kikubwa cha uzalishaji wa chakula alitaja kuwa ni mikoa  saba ikiwemo ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Iringa ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watoto wana udumavu unaoathiri hata uwezo wao kimasomo.

Kwa upande wake  Mkurugenzi  Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Devotha Gabriel alibainisha kwamba kuendelea kupungua kwa udumavu kumetokana na utekelezwaji wa mpango wa kwanza huku akisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo waratibu hivyo iko tayari kushiriki kikamilifu katika jitihada hizo.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu hiyo muhimu itakayowajengea uwezo sekta hiyo.

“Kama Wizara tumejipanga kutekeleza vipaumbele vya sekta ya mifugo inayochangia kwa kiasi kikubwa katika suala la lishe na niwahimize watanzania kuzingatia ulaji wa mlo kamili tuache kula kwa mazoea pia wale samaki, nyama kwa aina zake ambazo zinashauriwa kiafya na kunywa maziwa  kwa wingi maana ni azima ya Serikali kila mtanzania awe na afya bora aweze kufanya shughuli zake na kuchangia pato la Taifa,” alihitimisha Dkt. Mhina.


Mkurugenzi wa Utawala na usimamizi wa rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Devotha Gabriel (wa pili kutoka kushoto, mratibu kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha (wa pili kutoka kulia), pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kupata mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe, Mei 10, 2022 mtumba Jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu Sekta ya Mifugo, Dkt. Charles Mhina ( kulia) akiongea wakati wa mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe kwa menejimenti ya Sekta ya Mifugo (hawapo pichani)  kwenye ukumbi wa Wizara hiyo mtumba Jijini Dodoma Mei 10, 2022. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Devotha Gabriel.


Mratibu wa mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha akitoa mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe kwa menejimenti ya Sekta ya Mifugo (hawapo pichani) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) kwenye ukumbi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mtumba Jijini Dodoma. Mei 10, 2022.


Mkurugenzi Msaidizi Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Nishe, Sekta ya Mifugo, Dkt. Nyamizi Bundala akichangia hoja wakati  mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe kwa menejimenti ya Sekta ya Mifugo iliyotolewa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) kwenye ukumbi wa Wizara hiyo mtumba Jijini Dodoma Mei 10, 2022.


Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Devotha Gabriel akiishukuru Menejimenti ya Sekta ya Mifugo (hawapo pichani) kwa kutenga muda wao na kuweza kusikilizia mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID) kwenye ukumbi wa Wizara hiyo mtumba Jijini Dodoma. Mei 10, 2022.


Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya kuongeza uelewa kuhusu lishe wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo  iliyotolewa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya kimataifa (USAID) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU) wakisikiliza kwa makini mafunzo hayo kwenye ukumbi  wa Wizara  mtumba Jijini Dodoma. Mei 10, 2022


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni