Nav bar

Alhamisi, 12 Mei 2022

NDAKI AKUTANA NA WAFANYABIASHARA YA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona, Dodoma


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekutana na Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE) kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto wanazokabiliana nazo Wafanyabiashara hao katika shughuli zao za kila siku.


Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma Mei 10, 2022, Wafanyabiashara hao waliwasilisha kero na changamoto mbalimbali kwa Waziri huyo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi utakaosaidia kuwapunguzia madhila wanayopata katika biashara hiyo.


Wakati akiwasilisha taarifa ya Umoja huo, Katibu wa UWAMIMATE, Bw. Elias Mjanja alitaja jumla ya kero 12 ambazo zimekuwa ni kikwazo kwao katika ufanyaji wa  biashara hiyo.


Alizitaja kero hizo ni pamoja na utitili wa tozo, leseni za usafirishaji mifugo hai, mifugo isiyo na ubora sokoni, miundombinu chakavu minadani, uwepo wa madalali kwenye minada, kushamili kwa uuzaji wa nyama kiholela.


Kero nyingine ni kodi kubwa kwenye vifaa vya buchani, faini zinazotozwa na Bodi ya Nyama katika ukaguzi bucha, vibali kwa wauzaji wa mifugo minadani, faini kwa wainua mifugo kwenye magari, changamoto ya kituo cha TRA kilichopo Dumila kuhusu mashine za EFD na ushirikiano kati ya Wadau na Wizara.


Akitolea maelekezo kero hizo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema Wizara imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali katika kutatua kero hizo ikiwemo kuanza kukarabati na kujenga minada katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.


Aliongeza kwa kusema Wizara yake itaendelea kushughulikia kero hizo ili biashara ya mifugo na mazao yake iendelee kuwa na tija kwa Wafanyabiashara hao na nchi kwa ujumla.


"Biashara yenu inahusu moja kwa moja Wizara yetu, tunataka mtoke kwenye kulalamika kuhusu kero na changamoto na muende mbali zaidi kimaendeleo na mnufaike", alisema Ndaki


Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Bw. Tixon Nzunda aliwasihi Wafanyabiashara hao kuwa pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo waendelee kutii Sheria wakati changamoto hizo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi akiongeza kuwa milango ya Wizara ipo wazi wakati wote wanapopata changamoto wasisite kuwasiliana na Wizara ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo kwa pamoja.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Uongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE) alipokutana na Umoja huo kwa lengo la kusikiliza kero zao. Mhe. Ndaki alikutana na viongozi wa umoja huo  jijini Dodoma Mei 10, 2022.

Pichani ni sehemu ya washiriki wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE) kilichofanyika jijini Dodoma Mei 10, 2022.


Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE), Bw. Elias Mjanja akieleza kwa ufupi kuhusu kero wanazokabiliana nazo kwenye shughuli zao za kila siku katika kikao baina ya Umoja huo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki kilichofanyika jijini Dodoma Mei 10, 2022.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (kushoto) akifafanua jambo katika kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na Uongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara ya Mifugo na Mazao yake Temeke (UWAMIMATE) kilichofanyika jijini Dodoma Mei 10, 2022.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni