Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

​SERIKALI KUTAFUTA ARDHI KWA AJILI YA UWEKEZAJI WA MUUNGANO WA UMOJA WA MAZIWA KILIMANJARO

Katibu Mkuu Wizara ya  Mifugo na uvuvi (Sekta ya Mifugo) Tixon Nzunda, amesema Serikali  itafanya mpango wa kutafuta ardhi kwa ajili ya  Muungano wa umoja wa maziwa Mkoani Kilimanjaro(JE) ili waweze kuzalisha  kwa tija. 


Hayo amesema jana  tarehe 27 aprili, 2022 Wilaya Hai Mkoani humo, wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha Maziwa cha Nronga Women  na kutembelea duka la pembejeo za Mifugo la Muungano wa Umoja wa vyama vya Maziwa Mkoa wa Kilimanjaro (JE).


Amesema  ni vema Serikali ya Wilaya na Mkoa zihakikishe zinawapatia eneo la kuwekeza  kikundi cha wanawake cha Nronga pamoja na Muungano wa umoja wa maziwa mkoa wa Kilimanjaro (JE)  ambao unaongozwa na wanawake kwa ajili ya uwekezaji wa Kiwanda cha kusindika Maziwa .


Nzunda  alisema Serikali iko mbioni kuondoa baadhi ya kodi kwenye bidhaa za  Maziwa  ili wasindikaji, ikiwa ni pamoja na ushirika huo wa Muungano wa Umoja wa vyama vya maziwa mkoa wa Kilimanjaro (JE) waweze kuzalisha na kusindika Maziwa kwa tija bila vikwazo vya mlundikano wa kodi.


Aidha, Katibu  Mkuu Nzunda aliwataka Maafisa  Mifugo kutembelea vyama vya ushirika vya maziwa na kuvijengea uwezo na misingi ya kisheria ya uzalishaji maziwa ili viweze kuzalisha maziwa hayo kwa  tija.


"Takribani Miezi mitatu sasa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) imeandaa Mpango Mkakati wa kuibadilisha (Transform) Sekta ya Mifugo ili iweze kuchangia katika Pato la Taifa, na moja ya eneo lililopewa kipaumbele ni pamoja na tasnia ya maziwa". Alisema Nzunda.


Aidha, aliupongeza  Muungano wa Vyama vya Maziwa mkoa wa Kilimanjaro (JE) kwa kuwezesha wanachama  kupata huduma za ugani kwa kuanzisha duka lenye thamani ya zaidi ya sh10 milioni, pamoja na kuanzisha kiwanda cha kuchakata chakula cha Mifugo.


Mwenyekiti wa Muungano wa umoja wa vyama vya maziwa  mkoa wa Kilimanjaro (JE) Nancy Mwanasikidi, amesema changamoto wanayokabiliana nayo ni uwepo wa wafanyabiashara  wanaouza maziwa bila kuzingatia sheria na taratibu za maziwa hali inayopelekea umoja huo kushindwa kujiendeleza.


Amesema uuzwaji holela wa maziwa mitaani unapelekea ushirika huo kudorola kutokana na wao kushindwa kujiendesha kutokana na kuwepo kwa kodi nyingi.


"Ushirika unakusanya Maziwa lita 200 kwa siku lakini mfanyabiashara wa maziwa ambaye halipi kodi yoyote anaweza  kukusanya lita 1000 ambazo anauza bila kufuata taratibu na sheria za usindikaji, jambo ambalo linapelekea ushirika kudorola"


Mwenyekiti huyo alisema kuwa sheria za uuzaji wa maziwa yaliyosindikwa zikisimamiwa vizuri tasnia hiyo ya Maziwa itakua na wafugaji watanufaika pamoja na vyama vya ushirika vya maziwa vitakua kwa kasi.


Meneja Mradi wa Tanzania Milk processing Project (TMPP) kutoka  HEIFER International, Mark Tsoxo, amesema shirika hilo limefikia kaya za wafugaji zipatazo 1,022,000, kwa kuwapatia elimu  juu ya ufugaji bora, na  namna bora ya kutafuta  masoko ya maziwa pamoja na umuhimu wa kuwa kwenye vyama vya ushirika.


Tsoxo alisema kuwa kuna  vyama vya ushirika 119, na kwamba shirika hilo la Heifer Internationa limeviwezesha vyama 109 vya Ushirika  ambavyo vimeweza kuongeza ukusanyaji wa maziwa kutoka  lita 14,600 kwa siku hadi kufikia lita 16,7000.


Awali Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda alipata fursa ya kuvikabidhi (Canes 80) Vifaa vya kukusanyia na kutunzia Maziwa kwa vikundi  vya Ushirika 14 na Vikundi Vidogo vidogo 6,  ambapo Pikipiki moja ilikabidhiwa kwa kikundi cha MUARA FRESH MILK ambapo vifaa hivyo pamoja na Pikipiki vimetolewa Msaada na Shirika la Heifer International Tanzania kwa Vikundi hivyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw.Tixon Nzunda,akionyesha kadi ya Pikipiki aliyokabidhiwa Mwenyekiti wa Kikundi cha MUARA FRESH Milk Bw. Jonathan Mrema Jana tarehe 27/04/2022 Wilayani Hai.Wengine ni Mark Tsoxo, Meneja wa  HEIFER International na Neema Masawe Mwanakikundi kutoka MUARA FRESH MILK.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wa Pili kutoka Kushoto  akimsikiliza kwa Makini "boiler operater" wa kiwanda cha Nronga Women, wa kwanza kutoka Kulia Bw.Godlove Masawe akimweleza katibu Mkuu Mifugo jinsi maziwa yanavyocheshwa mara yanapofika kiwandani hapo jana tarehe 27/04/2022.Kutoka kulia ni Hellen Usili, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Nronga Women,Mark Tsoxo Meneja wa Heifer Internationa Tanzania na Christopher Mgonja Meneja wa Kiwanda cha Nronga Women.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wa kwanza kutoka kulia,akihutubia wanaushirika wa Muungano wa Umoja wa Vyama vya Maziwa Mkoani Kilimanjaro jana tarehe 27/04/2022 Kabla hajagawa vifaa vya kutunzia na kukusanyia Maziwa (Canes).Wengine ni Mark Tsoxo, Meneja wa Heifer international Tanzania.Lengo la ziara hiyo ni kukagua utendaji kazi wa Muungano wa Umoja wa vyama vya Maziwa Mkoani Kilimanjaro.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akiwashukuru Muungano wa Umoja wa vyama vya Maziwa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuanzisha duka la Pembejeo za Mifugo jana tarehe 27/04/2022 Wilayani Hai.Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kuona jinsi Muungano wa Umoja wa vyama vya Maziwa Mkoani Kilimanjaro unavyofanyakazi.Wengine kutoka kulia ni Wema Masawe kutoka HEIFER International na John mrema msimamizi wa duka hilo la Pembejeo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi  (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda akisaini kitabu cha Wageni mara baada ya kufika  katika Kiwanda cha kusindika Maziwa Cha NRONGA WOMEN Wilayani Hai-Kilimanjaro tarehe 27/04/2022. Lengo la ziara hiyo ni kukagua utendaji kazi wa Vikundi vya Muungano wa Umoja wa vyama vya  Maziwa mkoani Kilimanjaro.Kulia ni Mark Tsoxo Meneja Kutoka HEIFER International.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni