Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

WAFUGAJI WILAYANI HANDENI WAHIMIZWA KUFUGA KIBIASHARA

Wafugaji wa Wilaya ya Handeni wamehimizwa kufuga biashara ili waweze kuongeza kipato katika familia zao kutokana na shughuli za ufugaji wanazofanya.

 

Hayo yamesemwa (29.04.2022) na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani, Bi. Felista Kimario wakati wa mafunzo yaliyotolewa kwa wafugaji hao katika vijiji vya Mkata, Mazingara, Gendagenda na Kwasunga wilayani Handeni mkoani Tanga ambapo wizara ya Mifugo na Uvuvi upande wa Sekta ya Mifugo imeendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafugaji hao.

 

Bi. Kimario amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuhakikisha wafugaji wanafuga kibiashara na kukuza kipato chao. Wafugaji wengi bado wamekuwa wakiendelea na ufugaji wa mazoea hali inayosababisha wafugaji hao kuwa na mifugo mingi ambayo haiwasaidii sana katika kuongeza kipato katika familia zao na taifa kwa ujumla.

 

“Elimu tunayoitoa hapa itawasaidia wafugaji hawa kuelewa nini maana ya ufugaji wa kibiashara, umuhimu wa uanzishaji wa mashamba ya malisho kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la malisho, udhibiti wa magonjwa ya mifugo, matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji huduma za ugani (M-KILIMO), umuhimu wa mashamba darasa, umuhimu wa wafugaji kujiunga kwenye ushiriki na matumizi ya hereni za kielektroniki,” alisema

 

Bi. Kimario aliongeza kuwa wafugaji wanapopata elimu hii pamoja na mada nyingine na wakaifanyia kazi ni lazima kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo. Wafugaji wanatakiwa kuamua kubadilika na kufuga kulingana na ushauri wanaopatiwa na wataalam ili wafuge kwa tija.

 

Naye Selemani Nyauba ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwasunga amesema kuwa kupitia elimu hii wameweza kuelewa umihimu wa upandaji wa malisho kwa wafugaji kitu ambacho kitasaidia kuondokana na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hususani wakulima wakati malisho ya asili yanapokosekana. Hivyo amewasihi wafugaji kuona namna ya kuanza kutekeleza hili. Vilevile kuhusu suala la hereni za kielektroniki amesema kuwa ni jambo zuri ambalo litasaidia sana kupunguza tatizo la kesi za wizi wa mifugo ambazo zilikuwa zikiripotiwa ofisini kwake.

 

Aidha, ameiomba wizara kuendelea na utaratibu huo wa kuwatembelea wafugaji na kuwapatia elimu kwa kuwa inawasaidia kujifunza mambo mengi sana yanayohusu ufugaji wa kisasa.

 

Naye Hamza Masimba ambaye ni mfugaji katika Kijiji cha Gendagenda wilayani humo ameishukuru wizara kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kufahamu mambo mengi kuhusu ufugaji ambayo mengi walikuwa hawayafahamu. Aidha, kutokana na mafunzo hayo wametambua kuwa ni muhimu sana kuwatumia wataalam wa mifugo walionao pamoja na Mfumo wa M-KILIMO katika kutatua changamoto za ufugaji wanazokutana nazo.


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani, Bi. Felista Kimario akitoa maelezo ya awali kwa wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda kabla ya mafunzo kuanza ambapo aliwaeleza wafugaji malengo ya wizara kupitia mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na utoaji elimu kuhusu uboreshaji wa kosaafu za mifugo, kilimo cha malisho na mfumo wa M-Kilimo unaotumika kutoa huduma za ugani. Mafunzo hayo yamefanyika kwenye Ofisi ya Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni mkoani Tanga. (29.04.2022)


Afisa Mifugo Mkuu, Bi. Mary Yongolo akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuwa na mashamba darasa wakati wa mafunzo ya wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni mkoani Tanga yaliyofanyika kwenye ofisi za Kijiji hicho.  (29.04.2022)


Afisa Mifugo Mkuu, Bw. Sebastian Shilangalila akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa M-Kilimo kwa ajili ya utoaji huduma za ugani kwa wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni wakati wa mafunzo yaliyofanyika kwenye ofisi za Kijiji hicho. (29.04.2022)


Daktari wa Mifugo wa Wilaya ya Handeni, Dkt. Key Amiri akiwasilisha mada kuhusu udhibiti wa magonjwa ya mifugo wakati wa mafunzo kwa wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni yaliyofanyika katika Ofisi za Kijiji hicho. (29.04.2022)


Afisa Ushirika wa wilaya ya Handeni, Bw. Fratern Minde akiwasilisha mada kuhusu umihimu wa wafugaji kujiunga kwenye ushirika wakati wa mafunzo yaliyofanywa kwa wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni mkoani Tanga. (29.04.2022)


Picha ya pamoja ya Watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Halmashauri ya Handeni na baadhi ya wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda wilayani Handeni mkoani Tanga mara baada ya kumalizika kwa mafunzo yaliyotolewa kwa wafugaji hao yaliyofanyika kwenye ofisi za Kijiji hicho. (29.04.2022)


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani, Bi. Felista Kimario (wa pili kutoka kulia) akizungumza na Katibu Tawala Wilaya ya Handeni, Bw. Mashaka Mgeta (katikati) kabla ya kwenda kutoa mafunzo kwa wafugaji wa Kijiji cha Gendagenda kilichopo wilayani humo. Wengine ni Watendaji kutoka Sekta ya Mifugo na Halamshauri ya Wilaya ya Handeni. (29.04.2022)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni