Nav bar

Jumanne, 10 Mei 2022

NDAKI AMSIMAMISHA KAZI MKANDARASI TANGA


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kumsimamisha kazi mkandarasi anayejenga miundombinu ya mnada wa Ndelema wilayani Handeni Mkoani Tanga kwa kushindwa kufanya kazi kwa wakati.

 

Waziri Ndaki ametoa agizo hilo leo (23.04.2022) mara baada ya kukagua kazi iliyofanyika katika ujenzi wa miundombinu ya mnada huo ambapo wakati anapita kukagua hakukuwa na kazi yoyote inayoendelea na mkandarasi hakuwepo kwenye eneo la ujenzi.

 

Pamoja na agizo hilo la kusitisha mkataba wa mkandarasi huyo, Waziri Ndaki pia ameagiza kusitishwa kwa malipo ambayo yalikuwa yapo kwenye mchakato kwa kuwa mkandarasi huyo hastahili kulipwa kutokana na kazi aliyoifanya. Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kumtafuta mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa wakati ndani ya siku 14 ili kazi hiyo iweze kuendelea.

 

Waziri Ndaki amesema serikali ilishatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya mnada huo inajengwa kwa lengo la kuwezeshwa wafugaji kuuza mifugo yao kwenye mazingira mazuri na kusaidia katika kuongeza ukusanyaji wa maduhuli. Hivyo amewasihi wakandarasi kuhakikisha wanafanyakazi zao kwa wakati kulingana na mikataba kwani serikali haitamvumilia mkandarasi mzembe.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchemba amesema kuwa mnada huo ni muhimu sana katika ukusanyaji wa maduhuli ya halmashauri hivyo ucheleweshwaji wa ujenzi wa miundombinu yake unakwamisha maendeleo ya mji wa handeni ambayo yangepatikana kupitia fedha ambazo zingekusanywa hapo.

 

Prof. Hezron Nonga ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, amesema kuwa mkandarasi huyo alishaandikiwa barua ya onyo kutokana na ucheleweshaji wake wa kazi lakini pia alishaitwa wizarani kwa lengo la kumtaka amalize kazi aliyopewa ya ujenzi wa miundombinu kwenye mnada wa Ndelema.

 

Katika ziara yake hiyo, Waziri Ndaki alitembelea Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga kukagua kazi zinazoendelea kufanyika kwa ajili ya maandalizi ya kuwapokea wafugaji kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro wakati alipotembelea Kijiji cha Msomera wilayani Handeni. Waziri Ndaki amewasihi wafugaji hao kuhamia kwenye Kijiji hicho kwa kuwa mazingira yanayoandaliwa na serikali ni mazuri kwa shughuli zao za mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akitembelea mnada wa Ndelema uliopo wilayani Handeni mkoani Tanga kwa lengo la kukagua kazi ya ujenzi wa miundombinu ya mnada huo, ambapo amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kumsimamisha mkandarasi anayejenga miundombinu hiyo na ndani ya wiki mbili atafutwe mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa wakati. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe. (23.04.2022)


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akitoa maelekezo kwa watendaji kutoka Wizara na Wilaya ya Handeni wakati wa ukaguzi wa kazi zinazoendelea kufanyika kwa ajili ya maandalizi ya kuwapokea wafugaji kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro wakati alipotembelea Kijiji cha Msomera wilayani Handeni. (23.04.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akikagua nyumba zilizojengwa kwa ajili ya makazi ya wafugaji watakaohamia katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha. (23.04.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiongea na moja ya familia katika Kijiji cha Msomera wakati alipotembela kijijini hapo kukagua kazi ya maandalizi ya kuwapokea wafugaji kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro inayoendelea kufanyika. Mhe. Ndaki amewasihi kuwapokea wafugaji wanaokuja vizuri na kuishi nao. (23.04.2022)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akisaini kitabu cha wageni wakati alipofiki kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni kabla ya kuanza ziara ya kikazi katika wilaya hiyo. (23.04.2022)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni