Na Mbaraka Kambona, Uvinza-Kigoma.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo wanatengeneza miundombinu mizuri na kuwapatia Wavuvi wanaoishi
kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na maeneo mengine vifaa vya kisasa
vya uvuvi ili viwasaidie kuongeza thamani ya zao la Dagaa na
kupunguza upotevu wa zao hilo baada ya kuvua.
Ulega aliyasema hayo wakati wa
ziara yake aliyoifanya katika vijiji vya Buhingu na Katumbi vilivyopo wilayani
Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 6 - 7, 2022.
Wakati akiongea na Wavuvi wa
vijiji hivyo kwa nyakati tofauti alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan
imedhamiria kukuza uchumi wa buluu na ndio maana inatengeneza miundo mbinu
mizuri ya kuchakata dagaa na mazao mengine ya samaki ili kuwaongezea thamani na
waweze kuuzika kwa bei nzuri na wananchi wafaidike na zao hilo.
"Tunataka tuone zao la
dagaa ambalo huku kigoma linazalishwa kwa wingi linainua maisha ya watu,
hatutaki kuona hata dagaa mmoja anapotea kwa kuharibika au kuoza, lengo letu ni
kuona ukanda wote huu wa Ziwa Tanganyika mnanufaika ipasavyo kupitia
dagaa", alisema.
Aliongeza kuwa wanawapatia
Wavuvi hao vifaa ikiwemo Boti, injini, nyavu, kamba na taa lengo likiwa ni
kufanya Uvuvi endelevu na kulifanya zao la Dagaa kuwa la kimkakati ili liwe
chachu ya maendeleo kwa wavuvi hapa nchini.
"Serikali kwa kushirikiana
na wadau wa maendeleo tunaendelea kutengeneza miundombinu mizuri ya kuchakata
dagaa na mazao mengine ya samaki katika maeneo mbalimbali kwa lengo la
kupunguza upotevu wa mazao hayo na kuyaongezea thamani ili yauzwe kwa bei nzuri
ndani na nje ya nchi", alifafanua.
Aidha, aliwataka wananchi
wanaoishi kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika kuendelea kutunza na
kuhifadhi mazalia ya samaki ili uvuvi katika eneo hilo uwe endelevu kwa manufaa
ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza,
Mhe. Hanaf Msabaha alisema kuwa kuna haja Serikali kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki Wilayani humo ili samaki waweze
kupatikana muda wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane ambao unatekelezwa Mkoani Kigoma, Bw. Lukindo Hiza alisema tayari wameshirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Uvinza kwa ajili ya kujenga Mwalo wa kisasa utakaosaidia kupunguza upotevu wa dagaa na wataweza kuwaongezea thamani ili wawauze kwa bei nzuri zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah
Ulega akizungumza na Wavuvi wa Kijiji cha Buhingu kilichopo Wilayani Uvinza,
Mkoani Kigoma alipofanya ziara katika Kijiji hicho mwishoni mwa wiki ikiwa ni
muendelezo wa maadhimisho ya miaka 10 ya Mradi wa Tuungane yaliyofanyika Mkoani
Kigoma Mei 5, 2022. Mradi huo wa Tuungane ambao unatekelezwa katika ukanda wa
Ziwa Tanganyika umejikita katika kutunza mazalia ya Samaki, kupunguza Uvuvi
haramu na kuwezesha wachakataji wa mazao ya Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah
Ulega akikagua taa za kufanyia uvuvi wa dagaa kabla ya kukabidhi vifaa vya
kuvulia dagaa kwa wavuvi katika Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani
Uvinza, Mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki. Vifaa alivyokabidhi Mhe. Ulega kwa
wavuvi vilitolewa na Mradi wa Tuungane ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho
ya miaka 10 ya Mradi huo yaliyofanyika Mkoani Kigoma Mei 5, 2022. Mradi huo wa
Tuungane ambao unatekelezwa katika ukanda wa Ziwa Tanganyika umejikita katika
kutunza mazalia ya Samaki, kupunguza Uvuvi haramu na kuwezesha wachakataji wa
mazao ya Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah
Ulega (katikati) akipatiwa maelezo na Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane, Bw. Lukindo
Hiza (wa tatu kutoka kulia) kabla ya kukabidhi vifaa vya kuvulia dagaa kwa
wavuvi wa Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma mwishoni
mwa wiki.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah
Ulega (katikati) akipatiwa maelezo na Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane, Bw. Lukindo
Hiza (wa tatu kutoka kulia) kabla ya kukabidhi vifaa vya kuvulia dagaa kwa
wavuvi wa Kijiji cha Katumbi kilichopo Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma mwishoni
mwa wiki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni