Na Mbaraka Kambona, Dodoma
Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi
nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kuishauri Serikali namna bora ya
kuboresha na kuendeleza Sekta ya mifugo na Uvuvi ili ziweze kutoa mchango wa
kutosha katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza Pato la taifa na uchumi wa mtu
mmoja mmoja.
Waziri Mkuu (Mst) wa Awamu ya Nne wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda aliyasema hayo kwa
Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi waliotembelea
nyumbani kwake jijini Dodoma Jana jioni (Disemba 3, 2020) kwa lengo la
kujifunza na kubadilishana utaalamu kuhusu masuala ya ufugaji, uvuvi na
kilimo.
Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa nchini kuna Ng’ombe
wengi zaidi ya milioni 30, Mbuzi zaidi ya milioni 20 na mifugo mingine
mbalimbali vyote hivyo kama vikisimamiwa vizuri vinaweza kusaidia kukwamua
wananchi kutoka katika lindi la umasikini hasa ikizingatiwa watu wengi
wanaojishughulisha na ufugaji ni wafugaji wadogowadogo ambao vilevile ndio
wakulima katika maeneo ya vijijini.
“Kwa hili lazima niseme ukweli bado panahitajika
kazi kubwa sana, lakini napata faraja kwa sababu Rais wetu John Pombe Magufuli
katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/ 2025 unaona dhamira ipo kubwa ya
namna ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo, uvuvi na kilimo
hivyo nyie Wataamu nadhani ndio kipindi muafaka sasa kwa kusaidia nchi
kimawazo,” alisema Pinda
“Pia nafarijika kwa kuamua kufanya mkutano wenu wa
kujadili masuala ya kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mazao ya mifugo
hapa Dodoma hivyo nina hakika kabisa baada ya mkutano wenu mtatoka na vitu
vikubwa ambavyo baadae vitakuwa msaada kwa ushauri kwa upande wa Serikali,”
aliongeza Pinda
Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa anatamani sana Wataalamu
hao wakaweka mifumo mizuri ya kuwavuta vijana wanaomaliza elimu zao kujiingiza
katika sekta ya ufugaji, uvuvi na kilimo ili waweze kupata nafasi ya kutambua
kwamba sekta hizi ni fursa kubwa inayoweza kuleta mabadiliko makubwa sana
katika uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wataamu wa Mifugo Tanzania
(TSAP), Dkt. Daniel Komwihangilo alisema wao kama wataalamu wa mifugo na uvuvi
wamefaidika sana na ziara hiyo na wameweza kuona kwamba kumbe mambo
yanawezekana kinachohitajika ni juhudi na uvumilivu katika kuanzisha jambo
lolote.
“Kikubwa tulichojifunza hapa ni kwamba mifugo inaweza
kufugwa kwa tija kama utazingatiwa ushauri, sayansi ya ufugaji na tekinolojia
kama ambazo Mhe. Pinda anazitumia, hivyo kama kuna mtu anataka kufanya
anavyofanya sio swala la kuanza leo na hapo hapo uone matokea hapana mambo haya
yanahitaji muda na kuzingatia ushauri wa Wataalamu,” alisema Dkt. Komwihangilo
Wataalamu hao wa mifugo wamekutana jijini Dodoma katika
Kongamano la siku 3 kuanzia Disema 2- 4, 2020 kwa lengo la kujadiliana namna
bora ya Kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mifugo na uvuvi ili sekta
hizo ziweze kuwa na tija kubwa kwa nchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni