Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka Wafugaji kuachana na tabia ya kufuga kuku
kwa mazoea badala yake wafuge kibiashara ili kujikwamua kiuchumi.
Naibu waziri amesema
hayo Septemba 21 leo, wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya wafugaji
wa kuku Mkoa wa Dar es Salaam. Wafugaji hao wametoka wilaya za Ilala,
Kinondoni, Kigamboni, Temeke na Ubungo.
Alieleza Ulega ni watu
wachache wanaofuga kuku kibiashara, lakini waliobaki wanafanya shughuli
kama sehemu ya maisha yao, hali inayosababisha kutofanikisha malengo ya kukuza
uchumi.
“Nataka mfuge
kibiashara, hatutaki mfuge kuku kimazoea. Watu watambue ufugaji kuku ni
biashara kama zingine na ni fursa ya kujikwamua kimaisha,”amesema Ulega
Amesema ufugaji wa
kuku sehemu mojawapo itakayowakomboa wanawake na vijana kuondokana na
changamoto ya ajira ambayo imekuwa kilio kwa watu mbalimbali.
Ulega amesema nyama ya
kuku inapendwa kila mahali na kila mtu hususani kwenye miradi mikubwa ya
maendeleo inatumika kama kitoweo chao .
“Ni vyema wafugaji
wakaiona fursa hii, kwa kuzalisha kwa wingi kuku. Tunataka watu wazalishe
kuku wa kutosha ili nyama yake ishuke bei.
“Sasa hivi baadhi ya
watu kula kwao nyama ya kuku hadi kuwe na shughuli fulani au sherehe jambo
ambalo halileti picha nzuri hasa kwa karne hii ya uchumi wa viwanda
unaosimamiwa na Rais John Magufuli,”amesema.
Aliendelea kueleza
Ulega kuwa, ifikapo 2020 nataka ugonjwa wa mdondo uwe wa kihistoria, na ifike
mahala tusiagize chanjo kutoka nje bali tuzalisha wenyewe.
"Dozi moja ya
mdondo kwa sasa inauzwa Tshs elfu 20 ambayo ni sawasawa na wastani wa kuku
zaidi ya 300", alisema Mhe. Ulega
Ulega amewataka
washiriki wa mafunzo hayo, kujiskia kuwa huru kupata ufafanuzi au kuuliza
maswali yoyote kwa Wataalamu kuhusu Sekta ya ufugaji na changamoto zake
na njia za kukabiliana nazo.
Awali ya yote Naibu
Waziri alisema, ni muhimu wataalamu wangu Washirikiane na Halmashauri ili kuona
ni namna gani wafugaji wetu wanaojiunga na Vyama vya Ushirika iwe njia rahisi ya
kujipatia mikopo.
"Nia yetu sisi
tunataka benki ziwe rafiki kwa wafugaji wadogo wadogo na vileville mfugaji aweze kukopesha kirahisi kupitia Ushirika. Alisema
" Nataka mtumie
muda huu kujadiliana na kupata mafunzo, watu wapewe vipeperushi vya ratiba ya
uchanjaji wa dawa, " alielekeza Ulega
"Ni matarajio ya
Serikali kuwa, baada ya mafunzo haya, maarifa ya wafugaji wetu wa kuku
yataongezeka, idadi ya vijana na wanawake wanaoingia kwenye tasnia hii
itaongezeka, hivyo kupanua soko la uhakika la kuku na mazao yake, alimalizia
kusema.
Kaimu Mkurugenzi wa
Utafiti Mafunzo na Ugani Dkt Angelo Mwilawa amesema mafunzo hayo yameshirikisha
wafugaji wa wilaya hizo na lengo ni kuwajengea uwezo.
Mmoja wafugaji
akizungumza kwa niaba ya wenzake, Eva Nyella, amesema “ Tulikuwa tunafuga tu,
bila kujua nini cha kufanya, fursa zilizopo lakini mafunzo haya yatatusaidia.
Hili ni jambo kubwa tunaahidi tutakuwa wafugaji bora.
DKT. ANGELO MWILAWA MKURUGENZI WA UTAFITI, MAFUNZO NA UGANI AKIONGEA MACHACHE NA KUMKARIBISHA MGENI RASMI
MGENI RASMI MHE. NAIBU WAZIRI AKISOMA HOTUBA FUPI WAKATI WA UFUNGUZI WA MAFUNZO YA KUKU JIJINI DAR ES SALAAM
WAFUGAJI NA
WATAALAMU WAKIMSIKILIZA MGENI RASMI HAYUPO PICHANI
PICHA YA PAMOJA MGENI RASMI AKIWA NA WAFUGAJI NA WATAALAMU KUTOKA WIZARANI |