Nav bar

Alhamisi, 17 Septemba 2020

WATENDAJI WA SHAMBA LA LANGWILA WATAKIWA KUZINGATIA TARATIBU ZA UPANDAJI MALISHO.

Mkufunzi Mkuu wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gilla amesema ni vema kufanya kilimo cha malisho ya mifugo kwa mzunguko katika eneo moja kwa muda usiozidi miaka mitano ili kuzalisha kwa wingi na kupunguza kiwango cha magugu.

 

Dkt. Gilla alisema hayo wakati wa ziara ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye shamba la malisho la Langwila lililopo mkoani Mbeya walipotembelea kujionea shughuli zinazoendelea shambani hapo.

 

"Tusibuni namna ya kuotesha malisho bali twende kwa utaratibu unaotakiwa na hii itasaidia kupata muda wa kurutubisha ardhi na kupata malisho yaliyo bora," Alisema Dkt. Gilla

 

Hata hivyo Dkt. Gilla amesema ili kuweza kuwa na mbegu bora ni vyema kuvuna kwa wakati, kuchakata na kuhifadhiwa vizuri ili kuepuka kuoza kwa mbegu na kuwa na utaratibu wa kuhakikisha ubora wa mbegu za malisho.

 

Aidha, alishauri kupitia Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo isaidie kutengeneza duka la malisho pembezoni mwa Barabara kuu ili kujitangaza na kusaidia watu kupata huduma kwa ukaribu zaidi na kuweza kuongeza pato la shamba na taifa kwa ujumla.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Amos Zephania alisema ili uzalishaji uwe bora na wa tija ni vyema wafugaji wakapewa elimu ya upandaji na ulimaji wa malisho kwa vitendo ili kuongeza ufanisi zaidi.

 

"Tunahitaji kutumia miundombinu yetu vizuri ili kuweza kujipatia fedha za kuendesha shamba letu kwa kukodisha matrekta kwa wakulima," Alisema Bw. Zephania

 

Aliongeza kuwa mikataba ya kukodisha matrekta kwa wakulima iandaliwe kwa kuonyesha idadi za ekari zilizokodishwa na kwa kiasi kilichopendekezwa.

 

"Mashamba yasikodishwe kwa kufikiria tuu bali ni vyema kuwasiliana, kupata mwongozo na ni vyema pia Katibu Mkuu Mifugo alifahamu hili ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima," Alisisitiza Bw. Zephania

 

Naye Meneja wa shamba la Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander aliwashukuru watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kufanya ziara shambani kwao na kupokea yale yote waliyofundishwa na kuelekezwa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Steven Michael akichangia hoja wakati wa ziara ya kutembelea shamba la malisho la Langwila mara baada ya kutembelea stoo iliyojazwa mbegu za malisho na kushauri kuangalia namna bora zaidi ya kuhifadhi mbegu hizo. (16.09/2020)

Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Emmanuel Mayage akikagua faili la kumbukumbu ya manunuzi ya vifaa kwenye shamba la malisho ya mifugo Lagwila, mkoani Mbeya walipotembelea shambani hapo. (16.09.2020)

Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Andrew Ponda (katikati) akiwakumbusha watumishi wa shamba la Langwila juu ya ujazaji wa fomu za opras na umuhimu wake walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Ephron Sanga (kushoto) akipata maelezo ya namna ya kukusanya malisho, kuyafunga kwenye marobota na kuhifadhi kwa ajili ya kuuza. (16.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt. Edwin Chang'a (wa nne kutoka kulia) akiwatembeza watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho wakati wa ziara yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifigo na Uvuvi, Bw. Israel Kilonzo akifungua kikao cha kujadili namna wanaweza kusaidia shamba la malisho Langwila kufanya vizuri zaidi ikiwa ni pamoja na ushirikiano baina yao, walipotembelea shamba hilo lililopo mkoani Mbeya na kuona shughuli zinazoendelea. (16.09/2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiangalia ndama katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ndama mara baada ya kuzaliwa ambapo hupewa huduma na uangalizi wa karibu. (16.09.2020)

Meneja wa shamba la malisho ya mifugo Langwila, Bw. Datus Ngerera Alexander akieleza namna mashine ya kukatia nyasi inavyofanya kazi kwa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi walipotembelea shamba hilo mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Mtunza Kumbukumbu Msaidizi kutoka Wizara ya mifugo na Uvuvi, Bi. Nsia Kileo akichangia mada kwenye kikao kifupi kilichofanyika kwenye shamba la malisho Langwila mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa shamba la mbegu za malisho ya mifugo Lagwila walipotembelea kujifunza na kujionea mazingira na shughuli zinazofanywa katika shamba hilo. (16.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole, Dkt.  Edwin Peter Chang'a akiongea na watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) walipotembelea kituo hicho wakati wa ziara yao mkoani Mbeya. (16.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya mifugo na Uvuvi wakielekea kuangalia jengo kwa ajili ya Kiwanda kidogo cha uchakataji wa Maziwa ambalo bado lipo kwenye ujenzi kwenye kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole (TALIRI) mkoani Mbeya. (16.09/2020)

MAFUNZO YA WAPANGA MADARAJA NA WAKAGUZI WA NGOZI YAFANYIKA KWA KANDA YA MASHARIKI

 

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura akifungua Mafunzo ya Wapanga Madaraja na Wakaguzi wa Ngozi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Elisante Ole Gabriel, katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam. Lengo la Mafunzo hayo ni Kuwajengea uwezo wa kiutendaji wakaguzi na wapanga madaraja ya Ngozi hapa nchini. (16.09.2020)

Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya Wapanga Madaraja na Wakaguzi wa Ngozi Kanda ya Mashariki wakifuatilia kwa makini hotuba ya ufunguzi iliyokuwa ikitolewa na Mgeni rasmi hayupo katika picha. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam leo. (16.09.2020)

Mshauri wa Masuala ya Ngozi hapa nchini, Bw. Emmanuel Muyinga akichangia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya Wapanga Madaraja na Wakaguzi wa Ngozi yaliyofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam. Bw. Muyinga ameipongeza Wizara kwa kufanya maamuzi ya uteuzi na usajili wa wakaguzi wa Ngozi. (16.09.2020)

Washiriki wa Mafunzo ya Wapanga Madaraja na Wakaguzi wa Ngozi kutoka Kanda ya Mashariki, Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga wakiwa katika Picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam leo. (16.09.2020)


SIKU YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI
 

SAUTI YETU WIKI HII

 


Jumatano, 16 Septemba 2020

WARSHA YA KUKUSANYA MAONI YA MAANDALIZI YA MPANGO KAZI WA KITAIFA KWA AJILI YA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO WA HIARI WA KUENDELEZA SEKTA YA UVUVI MDOGO NCHINI YAFANYIKA MKOANI KIGOMA.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Merisia Mparazo akifungua warsha ya kukusanya maoni ya Maandalizi ya Mpango Kazi wa Kitaifa kwa ajili ya Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi Mdogo nchini kwa muktadha wa kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umasikini. Warsha hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) mkoani Kigoma leo. (16.09.2020).

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Maandalizi ya Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi Mdogo nchini, Alhaj Yahya Mgawe akishiriki kusimamia zoezi la ukusanyaji wa maoni ya Mpango huo kwenye warsha iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) mkoani Kigoma leo. (16.09.2020).

Sehemu ya washiriki (wadau wa sekta ya Uvuvi) wa warsha ya kukusanya maoni ya Maandalizi ya Mpango Kazi wa Kitaifa kwa ajili ya Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi Mdogo nchini kwa muktadha wa kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umasikini wakifuatilia kwa makini maelekezo ya wataalam wa Uvuvi kwenye warsha iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo Uvuvi (FETA) mkoani Kigoma leo. (16.09.2020).

Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Emanuela Mawoko (mwenye tisheti ya bluu), akisimamia zoezi la kukusanya maoni ya Maandalizi ya Mpango Kazi wa Kitaifa kwa ajili ya Utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi Mdogo nchini kwa muktadha wa kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umasikini. Warsha hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) mkoani Kigoma leo. (16.09.2020).
 

SIKU YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI


 

WATAALAM WA MIFUGO WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO.

 Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Hezron Nonga amewasihi watumishi wa umma kuwa wazalendo kwa kutimiza wajibu wao na kuwatia moyo kwamba wapo hapo kwa makusudi ya Mwenyezi Mungu.

 

Prof. Nonga amesema hayo katika shamba la kuzalisha mitamba Saohill Mkoani Iringa wakati wa majadiliano ya namna watakavyoboresha na kufanya shamba hilo kuzalisha zaidi na kupata mafanikio makubwa.

 

"Kutotimiza yale mnayopaswa kufanya ni dhambi kama dhambi zingine na tukiendelea kuwaza hasi hatutakuwa wazalendo na wala hatutaendelea,” Alisema Prof. Nonga.

 

Prof. Nonga amesisitiza kutengenezwa kwa programu nzuri itakayosaidia kujua magonjwa ya mifugo ili kusaidia kutoeneza magonjwa kwa mifugo mingine na kuwa na utaratibu wa kuchanja mifugo kila mara.

 

"Tuwe na mikakati ya kutambua magonjwa ili kusaidia katika udhibiti wa magonjwa na vifo pamoja na uongozi mzuri ili kusaidia shamba kuendelea," alisisitiza Prof. Ezron Nonga.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Stephen Michael amewataka watumishi hao kujitathmini na kuona ni wapi wametoka na wanapoelekea katika uzalishaji, uboreshaji na uendelezaji wa shamba la Saohill na sio kufanya mambo kwa makadirio ambayo husababisha kuendelea kushuka kwa uzalishaji katika shamba hilo.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Fraksed Mushi amewakumbusha watumishi wa shamba la mitamba Saohill kufuata sheria, na kusisitiza kuwa likizo ni muhimu na lazima kwa kila mtumishi kwani ni haki kisheria.

 

"Likizo za uzazi kwa mwanamke ni siku 84 na kwa upande wa mwanaume ni siku tano (5)," alimalizia Bw. Mushi.

 

Aidha, watumishi katika shamba la Saohill wamewashukuru watumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwaelimisha na kuwapa uelewa kwenye mambo ambayo walikuwa hawayajui na kukumbushwa baadhi ya maadili wanayopaswa kuyaishi  kwenye utumishi wa umma.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga awaasa wafanyakazi kuwa wazalendo na kufanya yale wanayopaswa kufanya kwenye ofisi za shamba la Saohill walipoenda kutembelea na kujifunza mambo mbalimbali kwenye shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Steven Michael akifungua mjadala wa watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wafanyakazi wengine wa shamba la Saohill kwenye ofisi za shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiangalia baadhi ya mashine zinazotumika kwenye shamba ya Saohill kwa ajili ya kukatia, kukusanya na kufunga malisho kwenye karakana ya shamba hilo Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya mifugo na Uvuvi wakipima uzito wa marobota ya malisho ya mifugo kwa kuyabeba walipotembelea shamba la Mifugo la Saohill Mkoani Iringa. (15.09.2020)

Baadhi ya malisho ya Mifugo   waliyovunwa na kufungwa kwenye marobota 1,200 katika shamba la Saohill tayari kwa kubebwa na kwenda kuhifadhiwa. (15.09.2020)

Mabanda kumi na mbili ya madume yanayofahamika kama NAIC 2 yenye uwezo wa kuweka madume 24, yapo katika shamba la Saohill Mufindi Mkoani Iringa. Lengo lilikuwa ni kuhifadhi madume ila hadi sasa hakuna mfugo wowote unaoishi huko. (15.09.2020)