Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

TALIRI WEST KILIMANJARO KUWA KITIVO CHA UBORA UZALISHAJI MBUZI, KONDOO.


Ni kufuatia matokeo mazuri ya utekelezaji wa mradi wa ECF

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Wizara yake inakusudia kukifanya kituo cha Utafiti wa Mifugo kanda ya Kaskazini cha West Kilimanjaro kuwa kitivo cha Ubora kwenye uzalishaji wa mbuzi na kondoo walioboreshwa kwa ajili ya kuwapa wafugaji nchini ili waweze kufuga kwa tija.

Prof. Mushi amesema hayo leo Machi 05, 2024 baada ya kufika kwenye kituo hicho kilichopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) ambapo ameweka wazi nia ya Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kiwango cha nyama bora inayouzwa nje kupitia kituo hicho.

"Kama mnavyotambua nchi yetu kwa sasa imeongeza kasi katika kusafirisha nyama nje ya nchi na zaidi ya asilimia 90 ya nyama tunayopeleka huko ni ya mbuzi na kondoo hivyo tuna kila sababu ya kuongeza uzalishaji wa wanyama hao" Ameongeza Prof. Mushi.

Aidha Prof. Mushi amemuelekeza Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Leonard Marwa na timu yake ya wataalam kuongeza jitihada kwenye utafiti wa mbari, magonjwa, lishe na utunzaji wa mifugo kwa ujumla ili kukifanya kituo hicho kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbuzi na kondoo bora watakaokidhi soko la ndani na nje ya nchi.

"Sisi kama Wizara tunaona huu ndo wakati muafaka wa kuifanya nchi yetu kuwa kinara kwenye uzalishaji wa mbuzi na kondoo wengi na sio kwa idadi tu bali kwa ubora pia kwa sababu wataalam tunao, ardhi nzuri tunayo na hali nzuri ya hewa tunayo" Amesisitiza Prof. Mushi.

 Prof. Mushi amesema kuwa kituo hicho pia kitatumiwa na vijana wanaoshiriki programu ya "Jenga kesho iliyo bora kwa wajasiriamali wanawake na vijana upande wa sekta ya mifugo" (BBT-LIFE) ambapo watapata sehemu ya kununua mbari za mbuzi na kondoo bora na ujuzi wa namna ya kuzalisha wanyama hao.

Hatua hiyo ya Serikali kukifanya kituo hicho kuwa kitivo cha ubora kwenye uzalishaji wa mbuzi na kondoo nchini inatokana na mafanikio yaliyopatikana kwenye utekelezaji wa mradi wa ECF ambapo Serikali ilipeleka jumla ya mbuzi na kondoo 465 ili kuzalisha mbegu itakayosambazwa kwa wafugaji nchini.


Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Mifugo kanda ya kaskazini cha West Kilimanjaro Dkt. Leonard Marwa (kushoto) akimueleza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi kuhusu utekelezaji wa mradi wa ECF muda mfupi baada ya Prof. Mushi kufika kituoni hapo leo Machi 05, 2024 mkoani Kilimanjaro.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi akimuangalia mmoja wa ndama wa mbuzi waliozalishwa kupitia mradi wa ECF kwenye kituo cha Utafiti wa Mifugo kanda ya Kaskazini cha West Kilimanjaro muda mfupi baada ya kufika kituoni hapo leo Machi 05, 2024 mkoani Kilimanjaro.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni