Nav bar

Jumatatu, 29 Juni 2020


HALMASHAURI ZASHAURIWA KUIGA MACHINJIO YA ILALA.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel amezishauri Halmashauri zote nchini ambazo zinafanya shughuli za ufugaji  kuiga mfano wa Machinjio ya kisasa ya Ilala ili nao waone haja ya kuwa na  machinjio ya kisasa yatakayosaidia kuboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la halmashauri zao.

Profesa Ole Gabriel alitoa rai hiyo ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26, 2020 alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Manispaa ya Ilala waliokuja kutembelea Machinjio ya Dodoma ili kujifunza namna ambavyo machinjio hayo yanavyoendeshwa.

Akiongea na Wataalamu hao, Prof. Ole Gabriel alisema itapendeza kama kila halmashauri ikawa na machinjio ya kisasa kwani yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri hizo na kuachana na kukimbizana kila siku na waendeshaji wa machinjio yaliyopo sasa ambayo hayana viwango ambavyo vinatakiwa.

“Niwaombe Makatibu Tawala wa Mikoa waliangalie hili, waone uwezekano wa kujenga machinjio ya kisasa yatakayosaidia kuboresha mazingira ya biashara yatakayochagiza kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri,”alisema

Aliongeza kuwa sio lazima Halmashauri zijenge Machinjio wao wenyewe, wanaweza kuingia ubia na sekta binafsi na wakajenga machinjio ya kisasa wakawa wanauza nyama katika soko la ndani na nje ya nchi, kodi ya Serikali ikawa inalipwa na wateja wakaendelea kupata huduma nzuri.

Prof. Ole Gabriel aliendelea kusema kuwa biashara ya nyama sio ndogo huku akifafanua kuwa kwa sasa wastani wa kilo milioni 2.6 za nyama zinaliwa nchini kila siku na hivyo aliwahimiza maafisa biashara kuelimisha jamii kuhusu zao la nyama ili watu wale nyama kwa wingi.

“Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) mahitaji ya kidunia kwa mtu mmoja anatakiwa kula kilo 50 kwa mwaka, lakini sisi Watanzania bado wastani wetu wa kula nyama kwa mtu bado upo chini sana, kwa sasa tumefikia kilo 15 kwa mwaka, bado kiasi ni kidogo sana,” alieleza

“Maafisa biashara tumieni taaluma zenu kuelimisha umma kuhusu zao la nyama ili watu wale nyama, watu wakila nyama kwa wingi itachagiza biashara ya machinjio na ndipo hasa uwekezaji pia utakwenda vizuri,” alisisitiza

Aidha, aliipongeza Halmashauri ya Bahi kwa jitihada wanazoendelea nazo za kujenga machinjio ya kisasa jambo ambalo litaboresha biashara ya machinjio na kuongeza pato la Halmashauri hiyo.

Akielezea kuhusu machinjio ya Dodoma, Prof. Ole Gabriel alisema kabla machinjio hayo hayajachukuliwa na Serikali ng’ombe waliokuwa wanachinjwa kwa siku ni kati ya 40 mpaka 50 lakini toka machinjio hiyo irudishwe serikalini namba ya ng’ombe wanaochinjwa imepanda kufikia 150.

Aliendelea kueleza kuwa mikakati waliyonayo kuhusu machinjio hayo ni kuendelea kuiboresha kufikia kuwa Machinjio ya Mfano kwa Afrika Mashariki, Ukanda wa Nchi za SADC na hata ikiwezekana Afrika.

Aidha, Prof. Ole Gabriel alisema kuwa anaamini ziara hiyo ni katika  kutambua jitihada za Wizara na hivyo aliwahakikishia wataalamu hayo kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana na Manispaa ya Ilala kuhakikisha mipango yao inafanikiwa na machinjio hiyo iweze kufanya kazi zake kama walivyokusudia.

Naye Afisa Masoko wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu hiyo ya Wataalamu, Ando Mwankuga alisema machinjio ya Ilala ni mradi wa kimkakati katika kuboresha mazingira ya biashara ya machinjio ambayo itawawezesha kuwa na nyama za viwango zitakazouzika  hata  nje ya nchi.

“Lengo la mradi ni kuongeza mapato ya Manispaa, tunaamini mradi ukikamilika na kuanza kazi tutapunguza utegemezi kwa Serikali,” alisema

Alisema machinjio hiyo ambayo ni kubwa na ya kisasa inategemewa kuanza kufanya kazi Disemba, 2020 na watakuwa wanachinja   ng’ombe 1500 na mbuzi 1000 kila siku.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akisisitiza jambo wakati akiongea na timu ya wataalam kutoka manispaa ya Ilala (hawapo pichani) waliokuja kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma Juni 26,2020. Kulia ni Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga, kushoto niKaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya mifugo na Uvuvi Bw. Abdallah Temba. 



Afisa Mipango wa Manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga akieleza lengo la Ziara yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) walipomtembelea ofisini kwake mapema Juni 26,2020. 



Baadhi ya wajumbe kutoka Manispaa ya Ilala wakiwa katika kikao wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma. Juni 26,2020. 



Ijumaa, 26 Juni 2020

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI MHE. LUHAGA MPINA AFANYA UTENGUZI WA KAIMU MSAJILI WA BODI YA MAZIWA.

MADAKTARI WA MIFUGO WATAKIWA KUHUISHA TAARIFA ZAO.



Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt.Bedan Masuruli amewataka Madaktari wa Mifugo nchini kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari wa mifugo  kabla ya  Julai 1, 2020.

Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Juni 26, 2020, Dkt. Masuruli amesema ni muhimu wataalam kuhuisha majina yao ili baraza liweze kufahamu wako wapi, wanafanya nini na wanatoa huduma gani.

"Nasisitiza madaktari wote wa mifugo ambao hawajahuisha taarifa zao kwenye daftari la usajili wa madaktari wafanye hivyo kuanzia leo hadi kufikia Juni 30, 2020 kwani kuanzia Julai mosi tunaanza kusimamia Sheria" amesema Dkt. Masuruli.

Hata hivyo Dkt. Masuruli amesema wanafanya haya yote ili kuboresha huduma kwa wafugaji wote nchini na watatoa vitambulisho kwa wataalam wote ili wafugaji waweze kuwatambua.

 Amesema kuwa wamejipanga kusambaza wataalamu wa mifugo kwenye ngazi za msingi ili kuwa karibu na wananchi na kuwashauri namna ya kuipatia kinga mifugo hiyo na kuleta tija katika ufugaji wao.

Aliongeza kuwa ili kufikia adhima hiyo ni lazima wataalamu wote wa ngazi ya msingi kusajiliwa, kujiandikisha na kujiorodhesha katika daftari ili kusaidia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujua ubora wa wataalamu walionao katika maeneo yote na kusaidia wananchi  kuongeza tija katika  sekta ya ufugaji.


Tumeongeza muda ili wataalum waweze kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari kabla ya Julai 1 wawe tayari wamejisajili, na kwa ambaye hata fanya hivyo sheria za usajili zitachukua mkondo wake,alisisitiza

“Baada ya kuhuisha taarifa zao,  wataalamu watapatiwa vitambulisho maalum ili kusaidia wafugaji na wananchi kutambua kuwa ni mtaalamu aliyekidhi viwango hivyo, mwananchi anaweza kupatiwa huduma kwa kupata ushauri, kinga na namna ya kuboresha ufugaji ili kufikia mafaniko makubwa, aliongeza

Dkt.Masuruli amesema kuwa Wataalamu hao  watatakiwa kuwasilisha Wizarani taarifa za magonjwa ya mifugo inayosumbua katika maeneo yao ili kusaidia serikali kuandaa mpango kazi wa kutatua changamoto zilizoshindikana kutatuliwa na wataalaum hao.

Aidha, amesisitiza kuwa lengo kuu la kusogeza huduma hizo kwa wananchi ni kutaka kuhakikisha wanapatiwa huduma bora zinazokidhi viwango na itasaidia kubaini magonjwa yanayojitokeza katika mifungo ya wananchi wanao wahudumia na kuwasaidia kwa ukaribu.

“Natoa wito kwa vituo vyote vya afya ya wanyama kuanzia Julai Mosi, 2020 kuweka mpango wa muda wa miezi mitatu kupata hadubini katika vituo hivyo ili kusaidia kujua magonjwa katika mifugo ya wananchi wao wanao wahudumia, alifafanua.

Dkt.Masuruli ameongeza kuwa   ili wananchi waweze kunufaika na ufugaji wanahitaji wataalamu wa mifugo kuwa karibu na wafugaji ili kuwasaidia kuwapatia huduma bora itakayokidhi viwango na kuleta tija kwa asilimia kubwa na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) lengo ni kuwataka madaktari wa mifugo kuhuisha majina yao kwenye daftari la usajili kabla ya Julai mosi 2020 

Jumanne, 23 Juni 2020

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI MHE. LUHAGA MPINA AFANYA UTEUZI.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina amemteua Prof. Malongo Richard Mlozi kuwa Mwenyekiti  wa Bodi ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo Tanzania(LITA) na amewateua wafuatao kuwa Wajumbe wa Bodi ya LITA. Kupata orodha ya wajumbe walioteuliwa bofya hapa

MAGUFULI APONGEZA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa jitihada kubwa ilizozichukua katika kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wake ambazo zimesaidia kuboresha na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi na moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma, Rais Magufuli alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wake Wizara ya mifugo imechukua hatua kadhaa ambazo zimesaidia nchi kufikia mafanikio makubwa.

Rais Magufuli akitaja baadhi ya maeneo ambayo Wizara imeyashughulikia na kupata mafanikio, alisema kuwa katika kipindi hicho serikali iliongeza eneo la ufugaji kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2005 hadi kufikia hekta milioni 5 mwaka 2020. Jambo ambalo amelitaja kuwa limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Serikali kupitia Wizara imejenga mabwawa mapya ya kuogeshea ng’ombe 104, imesambaza chanjo na dawa za Mifugo nchi nzima, huku idadi ya ng’ombe waliohimilishwa imeongezeka kutoka laki moja na elfu tano (105,000) mwaka 2015 hadi kufikia laki tano kumi na nne elfu na mia saba (514,700).

Aliongeza kuwa serikali imeimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, kwa kuanzisha kanda kuu tatu (3) za Ziwa Victoria, Tanganyika na Pwani ikiwa ni pamoja na kudhibiti zana haramu za uvuvi.

“Nakumbuka kuna wakati nilimuona Mhe. Mpina alikuwa anatembea na rula kwenye Migahawa kupima urefu wa Samaki, hiyo ilikuwa ni katika hatua za kuhakikisha tunapata mafanikio haya ambayo tumeyapata”, alisema Rais Magufuli.

Aliendelea kusema kuwa Wizara imehamasisha na kufanikiwa kuongeza idadi ya Wafugaji wa Samaki kutoka laki moja themanini elfu na mia nane arobaini na tatu (180,843) mwaka 2015 hadi kufikia laki mbili sitini elfu mia nne sabini na nne (260,474) mwaka 2020.

“Katika kipindi hiki tumeongeza idadi ya Mabwawa kutoka 220,545 hadi kufikia 260,445 na kuongeza vizimba vya samaki kutoka 109 hadi 431, na uzalishaji wa Vifaranga vya Samaki vimeongezeka kutoka milioni nane na tisini elfu (8,090,000) hadi Vifaranga milioni kumi na nne laki tano thelathini na moja elfu mia nne themanini na saba (14,531,487)”, aliongeza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa sambamba na mafanikio hayo serikali imeongezea mtaji kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kiasi cha Shilingi Bilioni Mia Mbili na nane kupitia Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Pia serikali imeipatia TADB Dola za Kimarekani Milioni 25 sawa na Shilingi Bilioni 57.8 ili kuendesha Mfuko wa dhamana.

“Hii ina maana kuwa kwa miaka mitano iliyopita Serikali imeipa TADB Shilingi Bilioni 324.8 kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya kiasi cha shilingi bilioni 166.9 kwa Riba nafuu”, aliongeza Rais Magufuli

Kutokana na hatua hizo, Rais Magufuli alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana ambapo Sangara kwenye ziwa Victoria wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi kufikia tani 816,964 mwaka 2020.

“Kufuatia hatua hizo, urefu wa Sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16 hadi kufikia sentimeta 25.2 jambo ambalo limefanya samaki wetu kuanza kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika soko la Ulaya na nyinyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge ndege zimeanza kuja Mwanza na kubeba Samaki wetu kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi”, alisisitiza Rais Magufuli.

 “Kwa kuzingatia hilo mauzo ya samaki nje ya nchi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi bilioni 692 mwaka 2019”, alieleza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alisisitiza kuwa mafanikio hayo sio mambo madogo ni hatua muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ambao kwa sasa upo katika hatua nzuri ya kufikia uchumi wa kati ifikipo mwaka 2025.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli Akizungumza wakati akitoa hotuba yake ya kulifunga Bunge la kumi na moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 16, 2020 jijini Dodoma.








MHE. MPINA ATEUWA WAJUMBE WA BARAZA LA VETERINARI TANZANIA.

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mb) kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 4(1) cha sheria ya veterinari Na.16 ya mwaka 2003 amewateuwa wajumbe wa Baraza la Veterinari Tanzania. kwa kuona majina ya wajumbe waliochaguliwa, bofya hapa

Jumatatu, 22 Juni 2020

UHUISHAJI WA MAJINA YA MADAKTARI KWENYE DAFTARI LA USAJILI.

Madaktari wafuatao wanatakiwa kuhuisha  majina yao kwenye daftari la usajili wa madaktari wa mifugo kabla ya tarehe 25/06/2020. kupata orodha ya madaktari ambao hawajahuisha majina yao, bofya hapa

Ijumaa, 19 Juni 2020

WADAU WA TASNIA YA NDEGE WAFUGWAO WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTATUA KERO ZAO.


Wadau wa tasnia ndogo ya ndege wanaofugwa wameipongeza Serikali kwa kutatua kero za kisera ambazo zilikuwa zikidumaza tasnia hiyo.  

Hayo yamesemwa na Katibu wa chama Kikuu cha Wadau wa Tasnia ya Kuku (PAT), Manase Mrindwa katika kikao cha Wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma Juni 18,2020.

Akiongea kwenye kikao hicho Mrindwa alisema kuwa bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021   imetoa majibu kwa kero zao kwa kuondoa kodi kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga yanayotoka nje ya nchi, imepunguza tozo kwenye vyakula vya mifugo vinavyosafirishwa nje ya nchi na kupunguza  tozo kwenye mayai yanayosafirishwa nje ya nchi.

“Unafuu huu wa tozo tunategemea utaiinua tasnia hii ya ndege wanaofugwa hapa Tanzania, alisema Mrindwa.

Pamoja na pongezi hizo Mrindwa alieleza changamoto zilizowakumba kufuatia mlipuko wa maradhi ya Korona ambazo zimechangia kupungua kwa ulaji wa bidhaa za kuku kutokana na mdororo wa biashara uliopelekea kufungwa kwa baadhi ya shughuli za biashara ikiwemo mahoteli, migahawa, vyuo, shule na kusitishwa kwa shughuli zinazoleta mikusanyiko ya watu.

"Kudumaa kwa biashara zinazohitaji mazao ya kuku, kupungua kufuga kuliathiri viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo, uingizaji wa bidhaa za kuku kutoka nje zilisitishwa, wafugaji waliokopa kwenye taasisi mbalimbali za kifedha walipata shida katika marejesho." Aliongeza Mrindwa

Aidha, Mrindwa alisema kuwa  kufuatia kupungua kwa changamoto ya mlipuko wa maradhi ya Korona  shughuli za kibiashara zimeanza kurejea katika hali yake jambo ambalo litasaidia kuimarisha biashara hiyo huku akitaja shughuli ambazo zimeshaanza kurejea kama vile usafiri wa anga, utalii, uzalishaji katika viwanda, mashamba ya kuku wazazi ambayo yameanza kupokea vifaranga vya kuku na kuanza kuingia nchini virutubisho vya kutengenezea vyakula vya mifugo.

Aliongeza kuwa  kwa sasa wafugaji  wameanza kuongeza na kuimarisha shughuli zao za ufugaji hivyo kupelekea kuwa na changamoto ya  ongezeko la mahitaji ya vifaranga wa nyama na wa mayai. 


"Serikali iendelee kujadiliana na nchi jirani hususani Kenya na Zambia ili shughuli za mipakani ziweze kufanyika kama awali na usumbufu wa madereva na ucheleweshwaji wa mizigo uishe ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za mifugo ili biashara iweze kuimarika zaidi, alisisitiza Mrindwa.


Katika hatua nyingine, Wadau hao wamekiri kujifunza namna ya kuweka  mkakati wa  kuimairisha ulaji wa nyama ya kuku na mayai hapa nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza dawa za kuku na uwekezaji katika maghala na kuiomba serikali kuendelea na mchakato wa kuzalisha soya ya kutosha kwa mahitaji ya vyakula vya mifugo.

"Hivi sasa kwa wastani Mtanzania mmoja anakula mayai 75 kwa mwaka wakati kiwango cha FAO ni kula mayai 200 kwa mwaka, pia Mtanzania anakula kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati FAO inapendekeza kula kilo 45 kwa mwaka." Alifafanua Mrindwa.



Wadau wa tasnia ndogo ya ndege wanaofugwa wameipongeza Serikali kwa kutatua kero za kisera ambazo zilikuwa zikidumaza tasnia hiyo.  

Hayo yamesemwa na Katibu wa chama Kikuu cha Wadau wa Tasnia ya Kuku (PAT), Manase Mrindwa katika kikao cha Wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma Juni 18,2020.

Akiongea kwenye kikao hicho Mrindwa alisema kuwa bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021   imetoa majibu kwa kero zao kwa kuondoa kodi kwenye mayai ya kutotolesha vifaranga yanayotoka nje ya nchi, imepunguza tozo kwenye vyakula vya mifugo vinavyosafirishwa nje ya nchi na kupunguza  tozo kwenye mayai yanayosafirishwa nje ya nchi.

“Unafuu huu wa tozo tunategemea utaiinua tasnia hii ya ndege wanaofugwa hapa Tanzania, alisema Mrindwa.

Pamoja na pongezi hizo Mrindwa alieleza changamoto zilizowakumba kufuatia mlipuko wa maradhi ya Korona ambazo zimechangia kupungua kwa ulaji wa bidhaa za kuku kutokana na mdororo wa biashara uliopelekea kufungwa kwa baadhi ya shughuli za biashara ikiwemo mahoteli, migahawa, vyuo, shule na kusitishwa kwa shughuli zinazoleta mikusanyiko ya watu.

"Kudumaa kwa biashara zinazohitaji mazao ya kuku, kupungua kufuga kuliathiri viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo, uingizaji wa bidhaa za kuku kutoka nje zilisitishwa, wafugaji waliokopa kwenye taasisi mbalimbali za kifedha walipata shida katika marejesho." Aliongeza Mrindwa

Aidha, Mrindwa alisema kuwa  kufuatia kupungua kwa changamoto ya mlipuko wa maradhi ya Korona  shughuli za kibiashara zimeanza kurejea katika hali yake jambo ambalo litasaidia kuimarisha biashara hiyo huku akitaja shughuli ambazo zimeshaanza kurejea kama vile usafiri wa anga, utalii, uzalishaji katika viwanda, mashamba ya kuku wazazi ambayo yameanza kupokea vifaranga vya kuku na kuanza kuingia nchini virutubisho vya kutengenezea vyakula vya mifugo.

Aliongeza kuwa  kwa sasa wafugaji  wameanza kuongeza na kuimarisha shughuli zao za ufugaji hivyo kupelekea kuwa na changamoto ya  ongezeko la mahitaji ya vifaranga wa nyama na wa mayai. 


"Serikali iendelee kujadiliana na nchi jirani hususani Kenya na Zambia ili shughuli za mipakani ziweze kufanyika kama awali na usumbufu wa madereva na ucheleweshwaji wa mizigo uishe ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za mifugo ili biashara iweze kuimarika zaidi, alisisitiza Mrindwa.


Katika hatua nyingine, Wadau hao wamekiri kujifunza namna ya kuweka  mkakati wa  kuimairisha ulaji wa nyama ya kuku na mayai hapa nchini, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza dawa za kuku na uwekezaji katika maghala na kuiomba serikali kuendelea na mchakato wa kuzalisha soya ya kutosha kwa mahitaji ya vyakula vya mifugo.

"Hivi sasa kwa wastani Mtanzania mmoja anakula mayai 75 kwa mwaka wakati kiwango cha FAO ni kula mayai 200 kwa mwaka, pia Mtanzania anakula kilo 15 za nyama kwa mwaka wakati FAO inapendekeza kula kilo 45 kwa mwaka." Alifafanua Mrindwa.



Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Gabriel Bura akiongea na Wadau wa Tasnia Ndogo ya Ndege wafugwao (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa NBC jijini Dodoma. (18.06.2020) 



Wadau wa Tasnia ndogo ya ndege wafugwao wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura (hayupo pichani) kwenye kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC jijini Dodoma. 18.06.2020) 



Mkurugenzi Msaidizi, vyakula na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (wa pili kutoka kushoto), Bw.Rogers Shengoto akiongea na baadhi ya wadau wa Tasnia ndogo ya Ndege wafugwao Mara baada ya kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa NBC jijini Dodoma. (18.06.2020) 




WATUMISHI WA SEKTA YA UVUVI WAASWA KUWA NA UADILIFU KATIKA UTUMISHI WA UMMA.




Watumishi wa sekta ya Uvuvi wameaswa kuwa na uadilifu katika utumishi wa Umma hasa katika kuzingatia sheria,Kanuni na Taratibu za Nchi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alipokua akifungua kikao cha Mafunzo ya maadili ya Utumishi wa Umma, yaliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper leo tarehe 18/06/2020.

Dkt. Tamatamah amewasisitiza watumishi kuwa wazalendo katika kazi na kufuata maelekezo yote ya utumishi wa umma na sheria za Nchi.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha watumishi kutambua majukumu yao ya kiutumishi pamoja na maadili ya utumishi wa umma.

"Mtumishi anapaswa kujua misingi yake ya kazi katika utumishi na kuepuka kuchukua na kupokea rushwa katika kuwaudumia wananchi," alisema Dkt. Tamatamah.

Naye Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma Bwana kutoka TAKUKURU, Joseph Kasongwa Mwaiselo amewaeleza watumishi madhara ya rushwa kwa serikali, na kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakikumbatia rushwa na kudhani kuwa itawaongezea kipato.

Mwaiselo amesema madhara ya rushwa serikalini ni pamoja na kupunguza ukuaji wa uchumi kwa sababu ina haribu uwekezaji katika uchumi na pia rushwa inapunguza uwezo wa serikali kugharamia huduma za kijamii ikiwamo Afya na Elimu.

Aidha, akinukuu maneno ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipo wasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2016/2017, Mwaiselo amesema "Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uzembe, uvivu, na kukwepa wajibu wetu".

Watumishi wametakiwa kuacha rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na watumushi wanapaswa kupendana na kuacha majungu ambayo yanasababisha kukosekana kwa haki.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Alex Mfundo amewasihi watumishi kuhakikisha wanafuata maadili ya utumishi wa umma na amewapongeza watumishi kwa kuitikia wito katika mafunzo hayo.

Katika mafunzo hayo, watumishi wameelekezwa juu ya masuala ya maadili ya utumishi wa umma pamoja na mwongozo kuhusu ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, 2020.



Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya uvuvi (aliyekaa katikati) Dkt Rashid Tamatamah akipata picha ya pamoja na watumishi wa sekta ya uvuvi mara baada ya kufungua kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi wa umma, Nje ya ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma leo tarehe 18/06/2020. 



Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma Bwana Joseph Kasongwa Mwaiselo kutoka ofisi ya Takukuru, akitoa mafunzo kwa watumishi wa sekta ya uvuvi na kuonyesha Madhara ya rushwa kwa serikali, katika kikao cha mafunzo ya maadili ya utumishi  wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma leo tarehe 18/06/2020. 




Ijumaa, 5 Juni 2020

BARAZA LA VETERINARI LAONYA MADAKTARI ‘FEKI’ KUHUDUMIA MIFUGO




Baraza la Veterinari nchini Tanzania limewataka watu wote ambao hawana sifa za Udaktari wa Mifugo kuacha mara moja kuhudumia na kutibu Mifugo huku likionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kwenda kinyume na Sheria.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala katika Mkutano wa 45 wa Baraza hilo ulilofanyika jijini Dodoma Mei 4, 2020.

Akiongea na Vyombo vya Habari mara baada ya Mkutano huo, Profesa Kazwala alisema kuwa kutokana na fani hiyo ya Udaktari wa Mifugo kuingiliwa na watu wasiokuwa na sifa Baraza limeamua kuandaa vitambulisho na beji vitakavyowatambulisha Madaktari hao pindi wanapokwenda kutoa huduma kwa wafugaji.

“Wale wote wanaojiingiza katika fani hii bila kuwa na vyeti vya kitaaluma wajue kuwa kuna sheria namba 16 ya Veterinari ya mwaka 2003 ambayo inakataza mtu ambaye hajasomea taaluma ya Udaktari wa mifugo kufanya kazi ya kuhudumia na kutibu mifugo, atakayekutwa na kosa hilo sheria itachukua mkondo wake” alisema  Profesa Kazwala

Alisisitiza kuwa kuanzia sasa wafugaji wanapaswa kujua kuwa wataalamu wa mifugo watakuwa na vitambulisho vitakavyokuwa vinatolewa na Baraza hilo na kuwataka kuwakataa watu watakaokuwa wanakwenda kutaka kutibu mifugo yao bila kitambulisho.

“Huko nyuma hatukuwa na vitambulisho, kukosekana kwa vitambulisho kulipelekea watu wasio na sifa kujiingiza katika kazi ya tiba ya mifugo na kuchafua sifa za fani yetu”,alisema Profesa alifafanua

Kufuatia changamoto hiyo, Profesa Kazwala alisema mkutano huo umekubaliana na kupitisha maamuzi kuwa wataalamu wa mifugo wawe na vitambulisho ambavyo vitasaidia  kuzuia na kuwaondoa watu wasio na sifa ya udaktari wa mifugo.

Aliongeza kuwa watahakikisha wakaguzi wa mifugo wanapita kila mara kwa wafugaji kukagua mifugo yao na kufuatilia kama kuna watu kama hao ambao wanaendelea kuvunja sheria.

Profesa Kazwala ametoa wito kwa wafugaji na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Baraza hilo kuwakataa watu hao wasio na vitambulisho huku akiwasisitiza hata hao madaktari watakaokuwa na vitambulisho wanapokwenda kutibu mifugo yao kuweka kumbukumbu zao vizuri ikiwemo namba ya usajili ya mtaalamu huyo ili kama likitokea tatizo lolote litakalo sababishwa na mtaalamu huyo iwe rahisi kumtambua.

Aidha, Profesa Kazwala amewaeleza wananchi kuwa huduma za mifugo zinaendelea kuboreshwa nchini na kuanzia sasa vituo vyote vinavyotoa matibabu ya wanyama lazima viwe na vifaa vya kuchunguza mifugo kwa maana ya Darubini ili kutoa vipimo sahihi vya Sampuli zitakazokuwa zinachukuliwa kutoka kwa mifugo.

Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania, Prof. Rudovick Kazwala akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari Tanzania uliofanyika jijini Dodoma. (04/06/2020) 




Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akifafanua jambo mbele ya vyombo vya habari katika mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari Tanzania uliofanyika jijini Dodoma. (04/06/2020) 



Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari, Profesa Rudovick Kazwala (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha Picha ya pamoja na wajumbe wa baraza hilo mara baada ya kumaliza Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari uliofanyika jijini Dodoma Mei 4, 2020


Jumatano, 3 Juni 2020

NAIBU WAZIRI ULEGA AAGIZA KUKAMILIKA KANUNI, KUSIMAMIA SHERIA YA UVUVI WA BAHARI KUU




Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu kufanya maandalizi ya kupata kanuni bora za kusimamia Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na watendaji wa mamlaka hiyo Mjini Unguja Visiwani Zanzibar akifuatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame Ali Ussi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ulega aliwataka watendaji hao kuunda kanuni bora zitakazoenda sambamba na mfumo wa biashara kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anataka kuona namna ukanda wa bahari unavyosaidia kuinua uchumi wa taifa.

“Jumla ya vipengele vyote vya sheria takriban 104 tumevifanyia kazi na vipengele kama 23 ambavyo havijaguswa lakini vingine vyote vimeguswa kuendana na uchumi wa bahari ili kuwa na mchango kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla katika kufanya maboresho ya uvuvi na bahari kuu, rai yangu kwa mamlaka mmefanya kazi nzuri kwa utengenezaji wa sheria lazima kwenda mbio sasa ndani ya miezi miwili tuwe tumepata kanuni zitakazoenda sambamba na biashara ya leo bila kuathiri maslahi mapana ya taifa letu.” Alisema Ulega

Aliongeza kuwa matumizi ya sheria hiyo yatakayoenda sambamba na kanuni bora za utekelezaji wake zitakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji kwa raia kutoka nje ya nchi kuja na meli zao hapa nchini na kufanya shughuli za uvuvi na wengine kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa samaki kwa kuwa Ukanda wa Pwani ya Bahari Hindi bado hakuna uwekezaji wa kutosha wa viwanda hivyo.

 Aidha, aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ilivyoboresha mazingira kwenye maziwa na mito hali iliyopelekea ndege za mizigo kubeba minofu ya samaki kutoka katika uwanja wa ndege wa Mwanza na kusafirisha kwenda nje ya nchi.

 Pia, Naibu Waziri Ulega alifafanua kuwa wakati watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu wanaandaa kanuni za kusimamia sheria hiyo watambue kuwa ushirikiano ni muhimu katika utekezaji huo na kutokuwa na mvutano wowote kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein wanataka kuona mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi.

 “Lazima mfanye kazi pamoja mshirikiane msiwe na aina yoyote ya mvutano, lazima mfanye kazi nzuri ya kushirikiana lazima taifa letu linufaike, Tanzania kwanza, tunaenda kufungua uvuvi wa bahari kuu tunaenda kufungua uchumi wa bluu tunataka uvuvi utoke kuchangia Asilimia 1.9 katika pato la taifa kusiwe na jambo la kunyoosheana vidole.” Alifafanua Ulega

Ulega akizungumza katika kikao hicho alisema ni muda muafaka kwa wavuvi hapa nchini kuondakana na uvuvi wa kuwinda bali uendane na teknolojia ya kisasa kufahamu maeneo mahsusi kwa ajili ya uvuvi ili kupunguza gharama kwa kutengwa vituo maalum vya kutolea taarifa ya maeneo yenye samaki na umbali wa kufikia maeneo hayo.

Alibainisha kuwa ni lazima uwepo mfumo wa kitaaalamu kwenye vyombo vyao vya uvuvi ili mvuvi anapotoka pwani kwenda baharini kuvua awe na uhakika wa mahali anapokwenda kuvua samaki na kuwataka watendaji hao kulifanyia kazi suala hilo haraka ili kufikia malengo ya wavuvi kunufaika zaidi kupitia sekta hiyo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, akiwa katika ziara maalum visiwani Zanzibar alitembelea kituo cha utotoaji wa vifaranga vya samaki, majongoo na kaa eneo la Maruhubi Mjini Unguja, ambapo alisema ipo miradi midogomidogo itakayoweza kutumika ikiwemo ya uvuvi wa samaki, majongoo na kaa ambayo ina soko kubwa duniani.

Ulega alisema uzalishaji wa bahari ndio nguzo kuu ya kukuza uchumi kwa wakaazi wa Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Tanzania baada ya kufanikiwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye maji baridi hivyo mapinduzi makubwa yanaelekezwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye bahari.

 “Serikali imeamua kwa dhati bahari yetu iweze kutunufaisha na kuwa na mchango chanya wakati wa kuhamia katika uvuvi wa bahari kuu na jamii iweze kufuga na kukuza kipato katika viumbe ambavyo vinauzika na kuhitajika duniani kama kaa na majongoo bahari ambao wanahitajika katika mataifa ya nje ya nchi yetu na wamekuwa wakiuzwa kwa bei kubwa.”

Ulega alisema, juhudi hizo zinaendana na mikakati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo itakayoinua jamii ya Ukanda wa Pwani kupitia miradi hiyo midogo.

"Tunafanya haya yote kwa ajili tunapata vyanzo vingi vya mapato vitakavyosaidia uchumi wa nchi pamoja na wananchi ambayo itatusaidia Tanzania kukuza maendeleo yake kwa haraka, kama ni utalii tunapongeza viongozi wetu wakuu kwa kusimamia haya na elimu hii iende mbali zaidi uzalishaji viumbe maji kwenye bahari unaweza kusababisha kuinuka kama taifa na kufanya vizuri zaidi kiuchumi na kuinua pato la taifa.”

Aliongeza kuwa licha ya kuelekea mpango wa uvuvi katika bahari kuu tayari miradi kama hiyo imeleta mageuzi makubwa katika maji baridi kwa maana ya maeneo ya maziwa na mito kwa upande wa Tanzania Bara.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame Ali Ussi, alisema, Zanzibar inaendelea na mpango wa uchumi wa bahari, kwa kuwa una nafasi kubwa ya kuingiza mapato ya haraka pamoja na kuwanufaisha wananchi wengi.

“Tunaelekea kwenye uchumi wa bluu unaohitaji kutunza mazingira ya bahari, ninawashauri watanzania sehemu zote za pwani watunze maeneo ya bahari kwa kutunza maeneo ya mazalia ya samaki yakiwemo matumbawe.” Alisema Ussi

Pamoja na hayo, alisema kuwa miradi hiyo ya uzalishaji wa samaki imekuwa na nafasi kubwa katika kukuza mazingira ya bahari ambayo tayari sehemu kubwa ya maeneo yanayotegemewa kwa uvuvi yameshaathirika.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha sekta ya uvuvi inazidi kunufaisha zaidi taifa na mvuvi mmoja mmoja na kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (kushoto) akiwa ameshika jongoo bahari alipotembelea kituo cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar.

Aliyevaa tai nyekundu ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020) 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akishuhudia kaa, alipotembelea kituo cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar.

Akiambatana na  Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi






Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyevaa koti jeusi) akipata maelezo ya ufuatiliaji wa meli zinazoingia katika maji ya Tanzania kwenye Bahari ya Hindi mara baada ya kutembelea ofisi za  Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu visiwani Zanzibar. (02.06.2020) 



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyesimama) akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (hawapo pichani) katika ofisi za mamlaka hiyo Visiwani Zanzibar, aliyekaa kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020)