Nav bar

Jumamosi, 6 Aprili 2024

PROF. SHEMDOE AZINDUA BWENI LA WASICHANA CHUO LA LITA MOROGORO

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amezindua bweni la wanafunzi wa kike katika chuo cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Morogoro lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 216 lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 970 fedha za mapato ya ndani

Akizungumza baada ya kuzindua jengo hilo Aprili 06,2024,  Prof Shemdoe ameipongeza LITA kwa kufanikisha ujenzi huo kwa kutumia fedha za ndani ambapo kukamilika kwakwe kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na changamoto ya mabweni kwa wanafunzi katika kampasi hiyo

Prof. Shemdoe alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendela kufanya jitihada za makusudi katika kuboresha miundombinu katika kampasi zote nane za LITA ambazo kwa sasa kila kampasi inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukarabati wa majengo chakavu

“Bajeti ya mwaka 2024/2025 imezingatia sehemu ya vipaumbele muhimu vinavyolenga kutatua changamoto zilizopo kwa awamu ili kuiwezesha Wakala kuwa na uwezo wa kudahili na kutoa mafunzo bora kwa vijana na wafugaji, Wizara itaendelea kuwaunga mkono hasa kwa kuendelea kuchangia fedha za maendeleo.” Alisema Prof. Shemdoe

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa bweni hilo Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt Pius Mwambene,  amesema kuwa ujenzi huo umetumia miaka miwili hadi kukamilika ambapo kwa sasa wameanza kwa kujenga bweni la wanawake na kisha baadaye watahamia kwenye ujenzi bweni la wanaume

Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Wakala katika kutatua changamoto ya miundombinu ya kufundishia ambayo itawawezesha wanafunzi na watumishi kutekeleza majukumu yao wakiwa katika mazingira bora

“Bweni hili limetimiza takribani miaka miwili na sasa lipo tayari kutumika ambapo tumetumia shilingi 970,388,312 fedha ambazo zimetoka katika mapato ya ndani ya taasisi yetu, lakini pia pamoja na mafanikio haya zipo changamoto chache tuomba msaada ikiwemo uhaba wa usafiri ususani mabasi ili kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo nje ya kampasi zao” alisema Dkt. Mwambene

Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema Wakala inaendelea kujiandaa na utekelezaji wa mtaala mpya wa kufundishia ambao unatarajiwa kuanza kutumika mwaka mpya wa masomo mwezi octoba mwaka huu ambapo mpaka sasa wadau wawili wameshajitokeza kusadia

Amesema mtaala wa sasa unatarajiwa kufikia tamati mwezi april mwaka huu na kutoa nafasi ya kuhuisha mitaala mipya ambapo wadau waliojitokeza  katika kusaidia uhuishaji wa mitaala hiyo ni pamoja na  shirika la kilimo endelevu (Sustainable Agriculture Tanzania (SAT)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao cha 11 cha Baraza kuu la Wafanyakazi la Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) katika Kampasi ya Morogoro,  Aprili 06,2024

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene akitoa neno la utangulizi mara baada ya uzinduzi wa bweni la Wasichana na wakati wa kikao cha 11 cha baraza kuu la wafanyakazi wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) katika kampasi ya Morogoro , Aprili 06,2024

Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani,  Dkt. Angello Mwilawa akitoa neno la shukrani mara baada Uzinduzi wa Bweni la Wasichana na ufunguzi wa kikao cha 11 cha baraza kuu la wafanyakazi wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) katika kampasi ya Morogoro, Aprili 06,2024

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa tatu kutoka kushoto) akikata utepe ishara ya uzinduzi wa Bweni la wasichana lililopo kwenye Wakala ya mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Morogoro Aprili 06,2024