HOTUBA ZA WAZIRI NA TAARIFA MBALIMBALI



HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI MHESHIMIWA DKT. TITUS MLENGEYA KAMANI (MB) ALIYOITOA KUMKARIBISHA WAZIRI MKUU – MGENI RASMI KUTOA HOTUBA YAKE KATIKA MKUTANO WA WADAU WA MIFUGO ULIOFAYIKA MWANZA, TAREHE 5 - 7 SEPTEMBA, 2014


Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri,
Mhe. Injinia Evarist Welle Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya,         
Mhe. Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,
Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa,
Waheshimiwa Meya wa Majiji, Miji na Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri,
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri,
Wawakilishi wa Mashirika ya Serikali, yasiyo ya Serikali na Sekta Binafsi,
Wafugaji,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
 Asalaam Aleykum, Tumsifu Yesu Kristu, Bwana Asifiwe

1.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha leo hapa Mwanza kwenye mkutano huu wa wadau wa mifugo tukiwa na afya njema. Nitumie nafasi hii kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuitisha mkutano huu na kwa kukubali kwako kutufungulia na kisha kuwa Mwenyekiti wa mkutano huu. Aidha, nachukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Mkoa na wananchi wa Mwanza kwa kukubali kuwa wenyeji wetu na kwa mapokezi mazuri waliyotupatia. Nipende pia kuwashukuru washiriki wote kwa kukubali wito wa kuja kwenye mkutano huu muhimu.
2.    Mheshimiwa Waziri Mkuu, Uzalishaji wa mazao ya mifugo nchini bado ni mdogo kwani inakadiriwa kuwa kila Mtanzania anakula wastani wa kilo 11 za nyama, lita 45 za maziwa na mayai 72 kwa mwaka. Ulaji huo, haujafikia viwango vya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ambavyo ni kilo 50 za nyama, lita 200 za maziwa na mayai 300 kwa mtu kwa mwaka. Inakisiwa kwamba mifugo tuliyonayo nchini inazalisha chakula (nyama, maziwa na mayai) yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 20. Kama ingekuwa chakula hicho kinaagizwa kutoka nje ya nchi, kiasi hicho cha fedha kisingepatikana kutoka kwenye bajeti yetu ambayo ni shilingi trilioni 19.
3.    Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na uchangiaji huo katika chakula, sekta ya mifugo katika mwaka 2013/2014 ilichangia asilimia 4.4 katika pato la Taifa. Sekta hii ingeweza kuchangia zaidi kama changamoto zinazoikabili zingetatuliwa hivyo ni vyema sekta hii ya mifugo ikasaidiwa kutatua changamoto zilizopo ili iweze kuwa endelevu na kuchangia zaidi katika afya na kipato cha watanzania na uchumi wa nchi kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa katika mkutano huu tutajadili kwa kina na kutoa mapendekezo kuhusu tufanye nini ili sekta ya mifugo ichangie zaidi katika uchumi wa Taifa.
4.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mkutano huu unafanyika katika kipindi ambacho sekta ya mifugo na hasa wafugaji wa asili, wakiwa na changamoto nyingi. Ninaamini yale yote yatakayojadiliwa hapa yataleta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hii muhimu katika uchumi wa Taifa. Sekta ya mifugo ina changamoto nyingi zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Naomba nitaje baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo.
Nyanda Duni za malisho
5.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, Tatizo la upatikanaji wa malisho hapa nchini linaendelea kuongezeka hasa wakati wa kiangazi ambapo malisho hupungua kwa kiasi kikubwa. Tatizo hilo limesababisha maafa makubwa hasa kwa wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.  Wafugaji wanaohama wamekuwa wakiongezeka kutoka maeneo yenye mifugo mingi na kwenda katika mikoa ya kusini ambako maeneo mengi yanatumika kwa kilimo. Hali hii imesababisha kuwepo kwa migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Kwa mfano, migogoro ya wafugaji na wakulima Mkoani Morogoro (Kilosa na Mvomero) na Mkoa wa Pwani (Ikwiriri – Rufiji).
Uhaba wa Maji kwa Mifugo
6.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, Sambamba na tatizo la malisho, upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo limekuwa pia ni tatizo kubwa. Katika kipindi cha kiangazi maji hukauka hata katika baadhi ya mabwawa na malambo na kufanya wafugaji kuhangaika na kuhama ili kunywesha mifugo yao. Pamoja na juhudi za Wizara za kuchimba malambo mapya na kukarabati yaliyopo, bado malambo haya hayatoshi kutokana na wingi wa mifugo. Ujenzi na ukarabati wa malambo nchini unahitaji rasilimali fedha nyingi ili kuipatia mifugo maji ya kutosha.

Magonjwa ya Mifugo
7.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, Magonjwa ya mifugo pia ni eneo ambalo linatakiwa kutengenezewa mikakati ya kudumu ili iendelee kuwa na afya na kuzalisha kwa tija. Magonjwa yanayoathiri mifugo kwa kiasi kikubwa (asilimia 70) ni yale yanayoenezwa na kupe. Serikali imejitahidi kujenga na kukarabati majosho na pia kununua dawa za kuogesha mifugo lakini bado magonjwa hayo yanatishia ustawi wa mifugo hapa nchini. Kati ya mwaka 2010/2011 na 2013/2014 Serikali ilitumia shilingi bilioni 4.2 kama ruzuku kununua na kusambaza lita 252,138 za dawa ya kuogesha mifugo.
8.     Wizara imeanza kutenga Maeneo Huru ya Magonjwa ya Mifugo ili kuzuia ueneaji wa magonjwa katika maeneo maalumu kwa lengo la kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo. Katika kuendeleza azma hiyo, Wizara imeimarisha miundombinu ya Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo cha Kanda ya Kusini na kutoa mafunzo kwa wataalamu wake. Hata hivyo, hili ni eneo moja tu na inatakiwa kutenga maeneo ya kutosha nchini ili kuweza kuhudumia mifugo ya kutosha.
Uzalishaji na Usambazaji wa Teknolojia za Mifugo
9.     Mheshimiwa Waziri Mkuu, idadi ya mifugo bora hasa ng’ombe wa maziwa na wa nyama walionenepeshwa ni ndogo sana na hivyo bidhaa za maziwa na nyama hazitoshelezi na kusababisha kuagizwa nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji. Idadi ya ng’ombe wa maziwa imeongezeka kutoka 605,000 mwaka 2009 hadi 720,000 mwaka 2013 na kuchangia kiasi cha asilimia 30 cha maziwa yanayozalishwa nchini. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na nchi jirani ya Kenya ambayo ina ng’ombe wa kisasa wa maziwa zaidi ya milioni 4. Aidha, takriban ng’ombe 175,000 walinenepeshwa katika mwaka 2013/2014, kiasi ambacho ni kidogo sana ikilinganishwa na idadi ya ng’ombe ya milioni 22.8.
10.Mheshimiwa Waziri Mkuu, teknolojia ya uhimilishaji inatumika kuzalisha na kupata ng’ombe wa kisasa wanaozalisha maziwa na nyama zaidi. Wizara imeendelea kuimarisha Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC – Usa river Arusha) pamoja na vituo vya kanda vya uhimilishaji 6 vya Kanda ya Ziwa (Mwanza), Mashariki (Kibaha), Kati (Dodoma), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kusini (Lindi), Kanda ya Magharibi (Mpanda) na Sao Hill. Hata hivyo, elimu ya kutosha inahitajika kutolewa kwa wafugaji katika suala la uhimilishaji.
Upatikanaji wa Masoko ya Mifugo na Bidhaa zake
·        Mifugo
11.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, masoko ya mifugo na bidhaa zake ndani na nje ya nchi ni suala muhimu kwa maendeleo ya sekta hii ya mifugo. Idadi ya mifugo iliyouzwa minadani imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka ng’ombe 857,208, mbuzi 682,992 na kondoo 122,035  mwaka 2009/2010 hadi ng’ombe 1,215,541, mbuzi 960,199 na kondoo 209,292 mwaka 2013/2014. Ongezeko hilo bado ni dogo ukilinganisha ni idadi yote ya mifugo iliyopo ambayo inatakiwa kuvunwa kwa asilimia 25 kila mwaka. Mauzo ya mifugo minadani yanaendelea kuongezeka kutokana na kuimarisha miundombinu ya minada. Hata hivyo, minada mingi iko katika hali isiyo ya kuridhisha na inahitaji kuimarishwa zaidi ili ifanye kazi kwa ufanisi. Uuzaji wa mifugo nje ya nchi bado ni kidogo sana kwani soko linalotegemewa ni, Comoro na nchi jirani ambazo mahitaji yao yanabadilika mara kwa mara.
·        Zao la Nyama
12.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, mahitaji ya nyama kwa ajili ya soko la nje yameendelea kukua lakini tumeshindwa kuyafikia kutokana na kukosekana kwa machinjio na viwanda vya kuchakata nyama zinazokidhi viwango vya kimataifa. Kwa mfano, katika mwaka 2012 nchi ya Misiri na Zambia zilihitaji tani 50,000 kwa mwaka wakati uwezo wetu ni tani 23,000. Soko la nyama linaweza kuwa la uhakika na kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni kama tungekuwa na machinjio na viwanda vikubwa vya kusindika nyama. Hivyo, ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ruvu ukikamilika utaongeza mauzo ya nyama bora ndani na nje ya nchi. Aidha, ufugaji wa ngombe wa nyama kisasa ni muhimu ili kuongeza upatikanaji wa nyama bora kwa ajili ya masoko maalumu na kuuza nje ya nchi. Hata hivyo, ufugaji huu unahitaji raslimali kubwa ambazo zimekuwa vigumu kupatikana kutokana na masharti magumu ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.
·        Zao la Maziwa
13.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, uzalishaji wa maziwa umeendelea kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa wingi wa mifugo. Hata hivyo, ukusanyaji wa maziwa hayo kwa ajili ya masoko ya ndani na usindikaji umekuwa kidogo sana kutokana na miundombinu hafifu ya ukusanyaji na usindikaji. Kwa sasa tunavyo viwanda 74 vyenye uwezo wa kusindika lita 403,000 lakini vinazalisha lita 139,800. Aidha, unywaji wa maziwa nchini bado ni mdogo na hivyo ni muhimu kupanua soko la ndani ili kuongeza uzalishaji, usindikaji wa maziwa na ajira. Programu inayoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ya Unywaji wa Maziwa Shuleni, kupitia Bodi ya Maziwa Tanzania inatakiwa kupanuliwa ili kuongeza wigo wa soko la maziwa la ndani.
·        Zao la Ngozi
14.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, Zao la ngozi ni zao la mifugo muhimu ambalo likiendelezwa lina mchango mkubwa kwa wafugaji na uchumi wa Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, zao hili linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubora hafifu na makusanyo madogo ya ngozi kutokana na ufugaji usiozingatia kanuni bora za ufugaji ambazo ni aina duni za mifugo, lishe duni kwa mifugo, umri mkubwa wakati wa kuchinjwa, upigaji chapa ovyo katika maeneo muhimu ya ngozi, mikwaruzo itokanayo na miiba au vitu vyenye ncha kali na kupiga viboko. Aidha, elimu duni, mapungufu katika ujuzi wa utendaji kazi kwa wachunaji na wawambaji na kukosekana kwa mbinu za ujasiriamali kwa wafanyabiashara wa ngozi na hali mbaya ya miundo mbinu ya machinjio, makaro ya kuchinjia, mabanda ya kukaushia na maghala ya kuhifadhia ngozi vinachangia pia katika kupunguza ubora  na thamani ya ngozi kwa siku za karibuni tatizo la utoroshwaji wa ngozi nje ya nchi, kupungua kwa uwezo wa viwanda vya kusindika ngozi, bei isiyotabirika ya ngozi zilizosindikwa kwa kiwango cha wet blue na  ushindani usio wa haki wa bidhaa hafifu za ngozi (plastiki na mitumba) zinazoingizwa kutoka nje zimeendelea kudumuza tasnia ya ngozi nchini.
Usimamizi hafifu wa Sheria za Mifugo na Kanuni
15.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, ubora wa mifugo, mazao yatokanayo na mifugo, pembejeo na huduma za mifugo husimamiwa na sheria 10 za mifugo pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali.  Usimamizi mzuri wa sheria huongeza ubora wa bidhaa za mifugo na hivyo kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi. Kutozingatiwa kwa sheria na kanuni zake kumesababisha bidhaa na huduma nyingi za mifugo kuwa duni na hivyo kusababisha bidhaa na mazao ya mifugo yanayozalishwa kuwa na ubora hafifu.
16.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, sekta hii pia inasimamiwa na sheria nyingine ambazo usimamizi na utekelezaji wake unawataka wadau kulipa tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeendelea kusababisha malalamiko kutoka kwa wadau. Kwa mfano, wadau wa maziwa wanalalamikia matakwa ya sheria zaidi ya kumi (10) ambazo zipo katika mamlaka mbalimbali kisheria na zinasimamia shughuli zinazofanana katika tasnia ya maziwa. Changamoto iliyopo ni jinsi ya kupunguza mzigo wa tozo na kodi zinatozwa na mamlaka mbalimbali kwenye zao lile lile.
17.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, ili kuleta mapinduzi katika sekta ya mifugo, changamoto hizi na zingine ambazo hazikutajwa hapa, zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi. Wizara kwa kushirikiana na wadau wake wanatakiwa kushirikiana kwa karibu ili kupanga mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto zilizopo.
18.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, baada ya kueleza changamoto hizo, napenda kukuarifu kuwa kwa sasa sekta ya mifugo inaingia katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa – BRN. Bado tunaendelea na maandalizi stahiki ili kuanza kutekeleza mpango huo. Ni matumaini yangu kuwa katika mpango huo sekta hii itaendelea kwa kasi zaidi ili kuongeza ajira, kuongeza kipato na kupunguza umasikini kwa wananchi wa Tanzania.
19.  Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwisho, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na wewe Mhe. Waziri Mkuu kwa kuhimiza maendeleo katika sekta ya mifugo. Hali hiyo ikiendelea sekta hii itakua kwa haraka na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania kwani, Sekta hii imeajiri watanzania wengi.
20.  Baada ya kusema haya Mhe. Waziri Mkuu, kwa heshima sasa naomba utufungulie mkutano na hatimaye uongoze majadiliano.


AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA


       



HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI MHE. DKT . TITUS MLENGEYA KAMANI (MB) WAKATI WA UZINDUZI WA JENGO LA OFISI YA TAASISI YA UTAFITI WA MIFUGO TANZANIA (TALIRI) NALIENDELE, MTWARA TAREHE 2 AGOSTI, 2014.
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara;
Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Lindi;
Makaibu Wakuu wa Wizara ;
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu COSTECH;
Wakurugenzi wa Taasisi za Utafiti wa Mifugo na Uvuvi;
Wataalamu wa mifugo na Uvuvi;
Viongozi na Wananchi wa Nalindele.
Waandishi wa Habari.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana
Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuweza kukutana leo katika hafla hii fupi na muhimu ya kufanya uzinduzi wa jingo la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo Kituo cha Naliendele hapa Mtwara. Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru ninyi nyote mliotenga muda wenu wa kuja kujumuika nasi hapa leo.
Ndugu Mkuu wa Mkoa ,Wageni waalikwa na Wananchi; Sekta za Mifugo na Uvuvi ni muhimu  kutokana na mchango wake katiak kuwapatia wananchi lishe bora, ajira na hivyo kuchangia kuondoa au kupunguza umasikini pamoja na kukuza uchumi wa Taifa. Kwa mwaka 2013/2014Sekta ya Mifugo ilikua kwa asilimia 3.8 na kuchangia katika  pato la Taifa kwa asilimia 4.4. Tanzania inakadiriwa  kuwa na ng’ombe milioni 22.8, mbuzi milioni 15.6 na kondoo milioni 7.0. vilevile wapo kuku wa asili 35.5, kuku wa kisasa milioni 24.5 na nguruwe milioni 2.01. ulaji wa mazao ya mifugo kulingana na viwango vya mataifa (FAO, 2011) ni kilo 50 za nyama, lita 200 za maziwa na mayai 300 kwa mtu kwa mwaka. Kwa upande wa nchio yetu viwango vya ulaji wa mazao hayo kwa sasa nui wastani wa kilo 12 za nyama, lita 45 za maziwa na mayai 75 kwa mtu kwa mwaka. Viwango hivi ni vidogo sana ukilinganishwa na mapendekezo ya FAO. Jitihada za makusudi zinatakiwa kuwekwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wanahamasishwa kutumia mazao ya mifugo kwa lengo la kuboresha afya zao ili hatimaye tuweze kukaribia viwango vinavyopendekezwa kimataifa.
Ndugu Mkuu wa Mkoa ; Serikali inajizatiti katika kufikia Azimio la Maputo la kutenga karibu asilimia 10 ya GDP yake kwa utafiti ambapo tathimini ya mwaka 2012/2013  inaonesha tunafikia karibu asilimia 8 ukichanganya fedha zote zinazotolewa na Serikali na Wadau wa Maendeleo.

Katika kuimairisha na kuendeleza utafiti Serikali imeweka na inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuendeleza utafiti ikiwemo kuwepo kwa Sera, sharia , kanuni na miundo ya Asasi zinazosimamia na kuendesha utafiti kote nchini kupitia chombo kikuu kinachoratibu cha COSTECH kwa kushirikiana na Wizara husika. TALIRI ambayo imeanzishwa chini ya sharia namba 4 ya mwaka 2012 kuanziaq mwaka huu 2014/2015 itakuwa ianjiendesha chini ya usimamizi na ushauri wa bodi yake ambayo nimeiteua hivi karibuni. Hivyo naiagiza bodi ya TALIRI kuanza kazi mara moja kusimamia na kuelekeza Taasisi hii itekeleze majukumu yaliyokusudiwa na kuweza kujiendesha kisasa na kuleta tija. Mnatakiwa kuhakikisha kuwa mnatumia fursa zote zilizopo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Ndugu wananchi; napenda pia kusisitiza na kuelekeaza vityuo vyote vya utafiti chini ya mwavuli wa TALIRI ambavyo vimetamkwa kwa majina katika sharia na vinginevyo vitakavyoanzishwa kutokana na sharia hii vifanye kazi kwa ubunifu wa gharama nafuu lakini wenye matokeo ya haraka ili kufanya secta ya mifugo iwe kiongozi wa uchumi hapa nchini katika muda mfupi ujao. Bodi inayosimamia TALIRI  lazima kuhakikisha inaimarika, inakua haraka na kutoa matokeo mazuri ya kiutafiti katika viwango vya kiamtaifa. Mikakati ya kuboresha miundombinu ya kusomesha wataalamu waliobobea  wenye shahada za juu za PHD waongezeke na miundo mbinu na maabara kuwa za kisasa hadi zifikie viwango  vya kushiriki katika mafunzo ya postgraduate MSc  na PhD zikiwa kama Deemed universities ‘’
Ndugu mkuu wa mkoa ,Wageni waalikwa na wananchi ;  Kazi ya ujenzi wa ofisi ya TALIRI Naliendele ambayo leo nina lizindua ni katika mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya uchunguzi wa CCM ya 2010-2015 kama ilivyoainishwa  katika ibara ya 38 katika vifungu (e) na(h) vya ilani hiyo kama ifuatavyo:
1.       Kuendeleza elimu kwa wafugaji ili wajue kuwa mifugo waliyonayo ni mali ambayo inaweza kuvunwa katika umri na uzito muafaka unaokidhi mahitaji ya soko , ili kuwaondolea umaskini wao  badala ya kuridhika na wingi wa mifugo iliyo duni na maisha ya kuhamahama .
2.       Kuimarisha utafiti wa mifugo kwa kuboresha na kuhifadhi kosaafu za mifugo ya mifugo ili kuongeza uzalishaji na tija
Serikali imeendelea kudhihirisha utashi wa kisiasa (political will) kwa vitendo kwa kuimarisha utafiti wa mifugo na tafiti nyingine .Kupitia mpango huu serikali imegharimia ujenzi wa jingo hili la TALIRI Naliendelee ambapo limegharimu shilingi 470,821,600/=. Aidha serikali inaendelea naku gharamia ukarabati wa maabara ya Uhawilishaji wa viini tete (embryos) kutumia teknolojia za “embyo transfer” zinazojumuisha (MOET/OPIVF-Multiple ovulation and Embryo Transfer; Ovum Pick-up InVitro fertilization) katika vituo vyake kuanzia na TALIRI Mpwapwa. Nichukue fursa hii kuwapongeza TALIRI kwa kubuni na kuanza kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya kutumia teknolojia hii ambayo imeanza kuenea na kutumika duniani kama njia za kusambaza”genomes” zenye sifa kwa wingi na haraka. Matumizi ya teknolojia hizipamoja na nyingine kama “Clonining” zinaweza kupunguza urefu wa muda wa kuzaliana kwa mifugo- “Generation Interval” ambayo ni kubwa kuliko ilivyo ka mazao ya kilimo ya muda mfupi. TALIRI lazima mjipange kujenga uwezo wa wataalamu wenu kuweza kufanya utafiti na kutumia teknolojia hizi na kuwafundisha ndani nan je ya nchi na kuzieneza kwa wafugaji nchini badala ya kuendelea kuzisikia tu kila siku kwenye taarifa na matarajio yenu.
Ndugu Mkuu wa Mkoa; nimetaarifiwa kuwa taliri mnaendelea na ujenzi wa mtambo wa kuchakata maziwa katika kituo cha TALIRI  Uyole na inaendelea kukamilisha ujenzi wa maabara ya utafiti wa nyama ya ng’ombe katika kituo cha TALIRI Mabuki. Napenda kuwapongeza kwa juhudi hizo na kuwaagiza mzikamilishe mapema ili ziweze kutumika na kutoa matunda yaliyokusudiwa. Tafutebni fedha kutoka vituo vingine nje ya vituo vya kawaida kwa kuandika na kuwasilisha maandiko ya miradi maeneo mbalimbali hususani katika mifuko ya kimataifa inayotoa fedha kwa tafiti mbalimbali. Kwa upande wa serikali Wizara yangu itaendelea kuwaombea na kusisitiza Serikali iendelee kugharamia mafunzo ya watafiti wa mifugo katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kupata wataalamu mahiri katika sekt6a pana ya utafiti, uzalishaji na afya ya mifugo na samaki.
Ndugu Mkuu wa Mkoa; kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto ya kuwepo uunganisho mdogo baina ya utafiti, mafunzo na ugani. Napenda kuchukua fursa hii kuiagiza TALIRI kuanzisha na kuendesha kitengo imara cha usamabazaji teknlojia (technology transfer) katika vituo vyenu kwa kuwa na “Communication and Documentation Center”  mbele tu  za ofisi zenu ambazo zimekuwa chanzo cha kupata taarifa zote za teknolojia zilizokuwa zimekwisha  iva na tayari kwenda kwa watumiaji. Nchini India chini ya mwavuli wa India  Agriculture Research Institute (ICAR) KILA Taasisi ya Utafiti ina kitengo imara cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma (Communication and Technology Transfer) mbali na taratibu mlizozizoea za siku ya Wakulima/Wafugaji katika vituo vyenu na tafiti za nje nza kushirikisha wadau.
Kwa upande wa wananchi wa Mkoa Mtwara na Mikoa yote  nchini natoa wito wajenge taratibu na tabia za kufika au kuwasiliana mara kwa mara na vituo vya Taasisi ya Utafiti  wa Mifugo na Uvuvi nchini ili waweze kujifunzza, kuona na kuchukua teknolojia bora zinazoweza kuboresha ufugaji na uvuvi/ ufugaji viumbe kwenye maji ili waweze kuongeza tija na kipato kinachotokana na matumizi ya teknolojia zinazozalishwa kwenye vituo vyetu vya utafiti.  Elimu hutafutwa,  hivyo nawaomba wananci nao waongeze udadisi ili ufugaji wao uwe na tija.
Ndugu Mkuu wa Mkoa; pamoja na mafanikio ya utafiti na jitihada za Serikali kuumarisha utafiti wa mifugo bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali. Mojawapo ya cha changamoto hizi ni pamoja na wananchi wanaozunguka mashamba na vituo vya utafiti kuvamia ardhi iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti. Wananchi katika maeneo yanayozunguka vituo kama vile TALIRI Kongwa , Mpwapwa, Mabuki, Tanga na kituo kidogo cha Mnima Wilayani Newala wamekuwa na tabia ya kuingia kinyume na utaratibu kwenye mashamba haya kwa nia ya kutaka kulima, kuchunga na hata kujenga na hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu na mazingira. Napenda kuchukua fursa hii kuagiza wananchi wote waliopo jirani na vituo vyetu vya utafiti kuheshimu sharia na taratibu zilizowekwa wanapotaka kutumia maeneo  yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Ndugu Mkuu wa Mkoa ; napenda kuhutimisha hotuba yangu kwa kutoa shukrani  zangu za dhati na za Wizara yangu kwa ushirikiano uliopo na unaoendelea na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)  ambayo Serikali iltoa fedha kupitia kwao na yenyewe kutoa fedha kugharamia uimarishaji wa miundombinu ya uatafiti, ujenzi wa miundombinu mipya ya utafiti pamoja na kusomesha watyafiti kwa lengo la kuimarisha na kuboresha utafiti nchini. Pamoja na Taasisis hizo wizara yangu inashauri na kuomba COSTECH kujumuisha Wakala zetu za mafunzo FETA na LITA kuimarisha uwezo na miundombinu ya utafiti ili nazo ziweze kufanya utafiti kutumia wataalamu waliobobea ambao wanazidi kuongezeka kadri Serikali inavyozidi kusomesha.
Nimalize kwa kuwasihi tena wananchi wa Mikoa hii ya Mtwara la Lindi waendelee kushirikiana kna vituo vya utafiti vilivyopo katika ukanda huu wa Kusini ikiwemo TALIRI  Naliendele ili wajipatie maarifa na ujuzi unaotokana na jitihada zinazofanywa na wataalamu wetu. Ninawathibitishia tena kwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kuimariosha shughuli za utafiti kwa lengo kuhakikisha kuwa ufugaji na uvuvi unakuwa wa tija na unamkomboa mfugaji na mvuvi kutoka katiak lindi la umasikini.
Maada ya maelezo haya napenda kutamka kuwa “jingo la ofisi ya TALIRI Naliendele limezinduliwa rasmi”
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.



HOTUBA ILIYOTOLEWA NA KAIMU MKURUGENZI MKUU WA TALIRI DKT. RASHID MSANGI, TAREHE 02/08/2014 WAKATI WA UFUNGUZI WA JENGO LA UTAFITI WA MIFUGO MTWARA NALIENDELE
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Jengo hili la ofisi ya taasisi ya utafiti wa mifugo Naliendele unalozindua leolimegharimu jumla ya shillingi 470,500,000 kati hizo Tume ya   Sayasi na teknolojia (COSTECH) ilichangia jumula ya shilingi 370,500,000 na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilichangia jumla ya shilingi 100 milioni.Tunapenda kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia COSTECH kwa kutoa fedha hizi ambazo zimewezesha ujenzi wa jengo hili. Jengohili ambalo unalizindua leo litaongeza na kuimarisha kazi za utafiti katika kituo hiki.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mpaka sasa serikali kupitia COSTECH inaendelea kufadhili miradi mitano  ya  utafiti ikiwemo utafiti wa kuku,malisho, nguruwe na ng’ombe wa nyama iliyopo TALIRI  Mpwampwa , Kongwa na Uyole. Aidha COSTECH inaendelea kugharamia ukarabati wa miundombinu ya utafit ikiwemo ukarbati wa maabara ya baiteknolojia (biotecknology) nalishe ya mifugo, Kwa upande mwingine maabara za lishe ya mifugo (animal nutrition laboratory) na baitecknolojia zilizokarabatiwa bado zinahitaji vifaa kuziwezwsha kufanya kazi zilizokusudiwa. Vilevile COSTECH inagharamia mafunzo ya watafiti walioajiriwa na TALIRI waliopo masomoni katikachuo kikuucha Sokoine cha kilimo (SUA) .Tunaishukuru serikali na Tume ya Taifa ya Sayansi na Tecknolojia kwa uwezehaji huo. Aidha tunaomba COSTECH iwezeshe kupata vifaa vya maabara illi ziweze kufanya kazi zilizokusudiwa.
 Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
 Taasisi inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufuwa vitendea kazi na rasilimali watu na fedha. Watafiti wamekuwa wanaandika miradi mbalimbali kwa wadau wa maendeleo ya ndani na nje ili kuweza kuongeza fedha za utafiti na ununuzi wa vitendea kazi. Aidha  Taasisi inakubaliwa na uhaba wa nyumba za watumishi ,lakini pia hata ambazo zipo ni chakavu na zinahitaji kukarabatiwa ,taasisi imekuwa ikitenga fedha zamaendeleo kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zake, ingawa fedha hazitoshi.
Moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Taasisi ya utafiti wa MifugoTanzania kwa ujumla wake ni uvamizi wa maeneo ya aridhi ambapo wananchi wanaoishi karibu na mashamba ya Taasisi wanakwenda kinyume cha sharia kwa ajili ya kulima, kuchunga, hata kujenga. Hali hii, inasababisha watafiti kushidwa kutekeeza majukumu yao ya kitaaluma ikiwemo kusimamia mipango ya udhabiti wa magonjwa ya mifugo na tafiti za uendelezaji wa malisho bora. Aidha, usalama wa watumishi wa taasisi unahatarishwa zaidi pale ambapo migogoro imepelekea ugomvi. Naomba wananchi walio karibu na mashamba ya taasisi kuwa ni vema kutii sheria na utaratibu zinazohusu matumizi ya rasilimali za umma yakiwemo mashamba ya TALIRI, kwani faida zinazipatikana ni Kwa ajili ya manufaa ya watanzania wote. Aidha, taasisi inawaomb waheshimiwa wabunge na madiwani, kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya kuheshimu mipaka halali ya mashamba ya serikali na taasisi zake.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Baada yakusema hayo machache, napenda kukushukuru tena Kwa kukubali kufika Kwa ajili ya shughuli hii.nawatakia wageni wetu wote hafla njema
Ahsanteni sana.



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI





Telegram:Mji Mtwara
Simu: 0732333118
Fax : 0732333118
Barua pepe: vicmtwara@gmail.com
           





                                               
In reply please quart:



 


Kituo cha huduma za mifugo
Kanda ya kusini,
s.l.p 186,
Mtwara



 


                  




                                                                                                    02/08/2014
Kumb. Na.
ADM.20/ZVC/MT/VOL.lll/450

TAARIFA FUPI YA KITUO CHA HUDUMA ZA MIFUGO CHA KANDA YA KUSINI (ZVC MTWARA): KWA WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI, MH. DR. TITUS MLENGEYA KAMANI (MB)

Salaam
Mh. Waziri,

Naomba kwa niaba ya idara ya huduma za mifugo na watumishi wote wa kituo cha huduma za mifugo kanda ya kusini; ninakushukuru kwa kuweza kufika katika kituo na kuahirisha majukumu mengine uliyonayo kitaifa.

Utangulizi

 Kituo cha huduma za mifugo cha kanda ya kusini (ZVC Mtwara) kimeanzishwa mwaka 2012 kutokana kugawanywa kwa kituo cha uchunguzi wa magonjwa ya mifugo cha kanda ya kusini (VIC Mtwara) kufuatia kuundwa kwa wakala wa maabara ya mifugo Tanzania (TVLA). Hivyo kituo hiki kwa sasa kinafanya kazi zote zilizokuwa zikifanya na VIC Mtawra isipokuwa utambuzi wa magonjwa ya wanyama ambayo kwa sasa inafanywa na wakala.

Mh. Waziri, kihistoria VIC Mtwara ilizinduliwa mwaka 1982 na Hayati Baba wa Taifa, Mwl, Julius Kambarge Nyerere ikiwa ni mpango wa serikali wa kuingiza na uendelezaji wa mifugo kanda ya kusini. Kituo hiki kilikuwa kikihudumia mikoa mitatu yaani Lindi, Mtwara na Ruvuma. Baadhi ya kazi za iliyokuwa VIC Mtwara ni:
1.     Uchunguzi na ufuatiliaji wa magonjwa mbalimbali ya mifugo kwa ajili ya kubaini kimaabara
2.     Kiusimamia uzuiaji wa magonjwa ya mifugo kwa kushirikiana na halmashauri zote za wilaya, miji, wafugaji binafsi, wafanyabiashara za mifugo na wadau wote wa sekta ya mifugo kwa ujumla.
3.     Kufanya utafiti wa magonjwa ya mifugo.
4.     Upimaji wa kimaabara wa samuli za wanyama.
5.     Udhibiti wa usalama wa biashara za mifugo, wanyama porina mazao yanayotokana na wanyama.
6.     Kuchunguza na kufuatilia magonjwa ya mifugo yanayoathiri pia binadamu kama vile Kimeta, Mafua ya ndege na Kifua Kikuu, Kichaa cha Mbwa na Ugonjwa wa Kuharibu Mimba.
7.     Kusambaza chanjo za mifugo, kufuatilia na kusimamia ufanisi wa chanjozote za magonjwa muhimu kiuchumi na kijamii katika kanda ya kusini.
8.     Kutoa ushauri wa mafunzo ya muda mfupiya uzuiaji na udhibiti wa magonjwa ya wanyama kwa wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo kwa kushirikiana na wizara na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo.
9.     Upimaji wa ubora wa dawa za kuogeshea mifugo.
10. Ukusanyaji wa ushuru wa biashara ya mifugo katika masoko ya upili (hayajaanzishwa katiak kanda yetu.).

Mh. Waziri, baada ya kuanzishwa kituo cha huduma za mifugo cha kanda (ZVC Mtwara) kimeendelea na majukumu yote ya iliyokuwa VIC isipokuwa upimaji wa sampuli za maabara na ubora wa dawa za kuogesha mifugo ambazo zipo TVLA au taasisi zingine za serikali.

Kwa sasa kituo chetu mbali ya kufanya kazi hizo juu, chini ya idara ya huduma za mifugo ya wizara yako, ZVC ina majukumu mengine kama vile
       I.            Kusimamia kituo cha uhimilishaji wa ng’ombe kilichopo Lindi Manispaa.
    II.            Kushirikiana na taasisi za kitafiti kama vile TALIRI, SUA, NIMRI, TVLA, TFDA, TANAPA, TAWIRI na nyingine nyingi.
 III.            Kusimamia miradi iliyowekwa na wizara katika kanda.
IV.            Kusimamia ustawi wa wanyama kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na wadau wote mifugo.

Mafanikio
Mh. Waziri kituo kimeendelea kuwa ni tegemeo na kimbilio la matatizo mengi ya wafugaji na jamii. Kwa mfano:
       I.            Tumeweza kubaini na kuweza kuudhibiti ugonjwa wa Sotoka ya mdbuzi na kondoo kwa kuubaini kimaabara na kufuatilia uchanjaji wa mifugo katika maeneo ambayo yalikuwa hayajaathirika.
    II.            Pia ugonjwa wa mdondo/kideri kwa kuku wa asili umeweza kupungua kwa kiwango kikubwa kutokana na uelewa wa wafugaji juu ya matumizi ya chanjo dhidi ya mdondo ikiwa ni pamoja na I2
 III.            Kupitia mradi wa wizara wa kutokomeza kichaa cha mbwa tumefanikiwa kuzuia vifo vya wanyama na binadamu katika halmashauri zinazopitiwa na mradi.
IV.            Tumeweza kufuatilia vifo vya ng’ombe katika jeshi la magereza mkoani Lindi na kudhibiti.
   V.            Pia tumeweza kudhibiti ugonjwa hatari wa kuku katika banda la utafiti wa kuku TALIRI Naliendele.
VI.            Tumefanikiwa kutoa ushauri wa kiutaalamu katiak jeshi la polisi na mahakama juu ya wafugaji au mfugaji aliposhitaki wezi wa mifugo .
VII.            Tumeweza kufuatilia, kuchukua sampuli na kuwasilisha maabara kwa utambuzi wa milipuko ya magonjwa ya homa ya mapafu ya ng’ombe na ugonjwa wa kuoza miguu au midomo.
VIII.            Baadhi ya watumishi wameweza kujiendeleza kitaaluma na kupitia mmiradi ya wizara.
IX.            Vilevile kituo kina baadhi ya watumishi ambao wameweza kutoa machapisho ya kisayansi katika majarida ya kisayansi ya kimataifa.
   X.            Pamoja na kugawanyika VIC,ZVC Mtwara na TVLA katika kituo  hiki tumeendelea kufanya kazi kwa pamoja na bila ya kuelezwa hakuna anayeweza kuuona mgawanyiko katika shughuli zetu.

Pamoja na mafanikio haya juu kituo kinakumbana na changamoto nyingi kama ifuatavyo:
       I.            Uhaba wa watumishi. Kwa sasa kituo kina jumla ya watumishi watano tu  VO-2, LFO-2 na dereva mmoja. Kituo kinahitaji kuongezwa watumishi kama ifuatavyo VO-1, LFO-2, Mhasibu 1, Mnunuzi 1, PS -1 na dereva 1.
    II.            Kituo kinahitaji kuwa na ofisi nje ya maabara na miundombinu ya kuhifadhi chanjo lakini bado hakijafanikiwa kupata fedha za ujenzi wa ofisi ijapokuwa katika bajeti iliyopita tumeweza kuweka katiak bajeti ya maendeleo.
 III.            Gari tunalo moja la mradi wa kichaa cha mbwa ambalo limekuwa likitumika katika ofisi zetu mbili (TVLA na ZVC Mtwara). Hivyo likienda safari kituo kinabaki bila usafiri.
IV.            Ucheleweshwaji wa malipo ya fedha za matumiziya ofisi unaotokana na mfumo mpya wa malipo katika hazina. Hili husababisha kituo kushindwa kutumia fedha katika shughuli zake. Mfano OC ya mwezi Mei haijalipwa kutokana na matatizo ya mfumo TISS ijapokuwa hazina ndogo ilikuwa imeshaziingiza kwa malipo.

Mh. Waziri ili kupunguza changamoto za kituo, na hususani bajeti finyu inayotolewa ya OC kati ya milioni 16 na milioni 26 kwa mwaka; baadhi yetu watumishi tumekuwa tukiandika miradi na kufanikisha fedha kiasi cha shilingi milioni mia moja ishini na moja (mil. 121) katiak miaka miwili iliyopita. Pamoja na hilobado kituo kinaomba utusaidie tuweze kufanikisha yafuatayo:
       I.            Ujenzi wa ofisi kama utakavyozindua leo hapa taliri tunakadiria shilingi milioni mia tatu sabini zinaweza kufanikisha hilo.
    II.            Kupata gari moja au mawili zaidi aina ya landcuiser station wagon kwa kuwa shughuli zetu zinahitaji kusafiri mara kwa mara.
 III.            Wizara iendelee kuajiri watumishi wa sekta mifugo hapa kituoni na hata katika halmashauri.

Mwisho japo si kwa umuhimu tunaomba upokee taarifa hii na tunakukaribisha sana uzidi kufanya ziara kama hii mara kwa mara wakati mwingine.

Wako katika ujenzi wa Taifa letu na ninayoheshima kuwasilisha.

Dr. Albano Oscar Mbyuzi
Afisa Mfawidhi
Kituo cha huduma za mifugo kanda ya kusini
ZVC Mtwara.






HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI MHESHIMIWA DK. TITUS MLENGEYA KAMANI (MB) KWENYE UZINDUZI WA MFUMO WA KITAIFA WA UTAMBUZI NA UFUATILIAJI MIFUGO ULIOFANYIKA KATIKA VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI MTONGANI, MLANDIZI WILAYA YA KIBAHA, JULAI 22, 2014.

Mheshimiwa Mwamtumu Mahiza, Mkuu wa Mkoa wa Pwani;
Mheshimiwa Diana Templelman, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Chakula na Kilimo (FAO);
Mhreshimiwa Minoru Homma, Mwenyekiti wa Development Partners - Agricultural Working Group;
Mheshimiwa Halima Kihemba , Mkuu wa Wilaya ya Kibaha;
Mheshimiwa Abuu Juma, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini;
Mheshimiwa Mansuli Ally Kisebengo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha;
Mheshimiwa Kasongo Kirendu, Makamu Mwenyekiti wa Hlmashauri ya Wilaya ya Kibaha;
Mheshimiwa Fatma Shari, Diwani wa Kilangalanga;
Wakurugenzi wa Wizara na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya mliohudhuria;
Dr. Helmut Karb, Mkandarasi wa ADT-UBK toka Ujerumani;
Wenyeviti wa Vyama vya Wafugaji, Asasi na Wadau wengine wa Mifugo.
Waandishi wa Habari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika siku ya leo tukiwa na afya tele. Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa hafla hiikunialika kuwa Mgeni Rasmi kwenye Uzinduzi wa Mfumo wa Kitaifa wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Kibaha kupitia Mkuu wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha pamoja na wadau wengine waliochangia kwa namna moja au nyingine katika kuandaaa na kufanikisha shughuli hii muhimu kwa mustakabali wa uchumi wan chi yetukupitia biashara ya mifugo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali kubwa ya mifugo. Kulingana na takwimu zilizopo, idadi bya mifugo nchini inakadiriwa kuwa na ng’ombe milioni 22.8, mbuzi milioni 15.6 na kondoo milioni 7.0. vilevile wapo kuku wa asili 35.5, kuku wa kisasa milioni 24.5 na nguruwe milioni 2.01. rasilimali ya mifugo hii tuliyonayo inatosheleza soko la ndani ya nchi na tunaweza kuuza ziada nje ya nchi. Tanzania tunauza wastani wa tani 353 za nyama ya mbuzi na kondoo kwa mwaka yenye thamani ya US$ 1,343,960 katika soko la Mashariki ya kati tu na hatujaingia la Asia ya mbali na Ulaya ambako moja ya masharti ni kuwa na mfumo wa utambuzi wa mifugo unaofanya kazi. Uchumi wa mifugo unategemea sana upatikanaji wa soko la uhakika kwa mifugo na mazao yako. Nchi nyingi duniani ambamo mifugo inachangia katika uchumi ni kutokana na masoko makubwa ya mifugo. Soko zuri la  
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Ndugu Wafugaji, mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ni nyenzo muhimu na yalazima katika ufugaji kwa sasa dunianikote ili kuwezesha kukubalika katika masoko ya kimataifa. Pamoja na hayo ni nyenzo inayosaidia kukabilian na magonjwa ya mifugo, wizi wa mifugo, uhamishaji au usafirishaji holela wa mifugo na hivyo kuepusha migogororo baina ya wafugaji na wakulima pamoja na watumiaji wengine wa ardhi.
Mfumo wa utambuzi na ufuatiliaji mifugo kwa tafsiri rahisi ni utaratibu unaotuwezesha kuwa na alama katika mifugo katika mifugo na kuweka kumbukumbu za matukio muhimu katika maisha ya mifugo yetu. Utaratibu wa kuweka kumbukumbu ndio usajili wa mifugo, wafugaji na matukio muhimu ya mifugo yetu. Mfano kuzaliwa, vifo, kupotea, kuhama au kusafirisha, chanjo au matibabu mengine ili kuhifadhi kumbukumbu zote hizi nilizotaja na nyingine nyingi unahitajika mfumo wa kompyuta uliojengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli hiyo. Kwa bahati nzuri Tanzania tumepata msaada wa Dola za Kimarekani 475,000 sawa na Tsh. 781,375,000/= kutoka kwa wnzetu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambao walitusaidia kuujenga Mfumo kupitia wazabuni wa Kampuni za Kijerumani zilizoitwa UBK na ADT. Nimearifiwa kwamba mfumo huu wa kompyuta umekamilika na sasa umeanza kufanya kazi katika Wilaya za mfano za Kibaha, Bagamoyo na Mheza ambapo jumla ya ng’ombe 5,845 wametambuliwa.
Ndugu wafugaji, Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuattiliaji Mifugo Na 12 ya mwaka 2010 (Sura 184) na pia Waziri waMaendeleo ya Mifugo na Uvuvi chini ya Sheria hii alitoa kanuni zza kuwezesha utekelezaji wa sheria hii kupitia Tangazo la Serikali namba 362 (G.N. 362)
Sharia hii na kanuni zake zinatumika  kwa pamoja na sheria nyingine chini ya Wizara yangu ambazo nazo zinalenga kuboresha uzalishaji wa mifugo na soko lake. Sheria hizi  ni pamoja na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo (Animal Diseases Act  2003), Sheria ya Tasnia ya Nyama (Meat Industry Act, 2006), Sheria ya Nyanda za malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo Na. 13 ya mwaka 2010 na Sheria ya Ngozi (Sheria Na.18,2008).
Ndugu wafugaji, utekelezaji wa Mfumo huu baada ya kuuzindua leo hautakuwa jambo la hiyari au utashiau utashi wa mfugaji bali ni lazima kwa mujibu wa Sheria na Kanuni. Hivyo, napenda kuchhukua fursa hii kuwashauri na kuwaelekeza wafugaji wote katika maeneo ambayo Waziri nitatangaza kuwa ya Utambuzi wa Mifugo(Compusory Livestock Identification Areas) washiriki katika kutambua na kusajili mifugo yaona wawe tayari kuchangia katika ununuzi wa vifaa vya utambuzi wa mifugo hiyo. Serikali kupitia Wizara yangu pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa itasimamia na kuratibu utekeleza wa Mfumo kwa faida ya wafugaji na maendeleo ya sekta kwa ujumla.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Ndugu Wafugaji, Ili usimamizi na utekelezaji wa mfumo huu uwe endelevu katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara yangu inazishauri mamlaka hizi kufufua na kutumia mifuko ya Maendeleo  ya Mifugo (Livestock Development Fund LDF). Mfuko huo utawezesha kuwa na fedha za mzunguko za kununulia vifaa vya utambuzi na kuchangia gharama za nyingine za  uendeshaji. Napenda nichukue nafsi hii kuwapongeza  Halmashauri za Wilaya za Karagwe na Ngara Mkoani Kagera kwa tafsiri sahihi ya kifungu cha 24Kifungu Kidogo cha 2 cha Sheria ya Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ambacho kimetamka kwamba wanufaika na mfumo huu wachangie gharama ambapo walitaka wafugaji wao kuchangia. Hivyo  Mamlaka za Serikali mza Mitaa  nyingine nchini hazina budi kuiga mfano huu.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Wananchi, Ili ufuatiliaji wa mifugo na mazao yake katika mnyororo wa thamani wa mifugo nuwezekane kupitia huu. Hapana budi wadau wanaohusika kuanza ufugaji, wasafirishaji, waendesha minada, waendesha machinjio na Maafisa Ugani pamoja na wasimamizi wa Kanzidata ya Mfumo (TANLITS Database) watimize majukumu yao kama yale ya kutambua mifugo, kutoa taarifa ya mifugo inapozaliwa, kufa, kuchinjwa au kusafirishwa.
Ndugu wafugaji na wananchi, mwisho napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Kimataifa (FAO), kwa msaada wa kugharamia ujenzi wa mfumo huu. Aidha, shukrani hizi ziwaendee Washirika wetu wa Maendeleo (Development Partners) waliokuwa wakichangia katika  Mfuko wa ASPP Busket Fund (Irish Aid, IFAD, JAICA na Benki ya Dunia), Mradi wa EAAPP (Benki ya Dunia) na Serikali kwa kugharamia unu nuzi wa wa vifaa vya utambuzi na usajili wakati wa ujenzi wa mfumo huu.
Vilevile napenda nishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Watendaji wa Wizara yangu, Wafugaji na Wananchi wa Mlandizi kwa kuandaa hafla hii.
Napenda kutambua nafasi na ushiriki wa taasisis mbalimbali kwenye ujenzi wa Kanzidata ya Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugozikiwemo;  Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambao wametuwezesha kupata takwimu mbalimbali za maeneo na ramani, Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa na Wakala wa Serikali Mtandao kwa ushauri na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa mawasiliano ya mtandao. Aidha nalipongeza Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO)LILILOSHIRIKI Katika hatua za awali za uanzishwaji wa mfumo kwa kuwezesha mijadala ambayo hatimaye ilizaa mfumo huu. Pia Benki ya Rasilimali (TIB) ambayo imeonesha nia ya kushiriki kwa kuhamasisha wale wanaotaka kuwekeza katika ufugaji kuzingatia matakwa ya kuwa na mfumo huu.
Ndugu wananchi, natoa wito kwa Taasisi nyingine za Kitaifa na Kimataif kuendelea kushirikiana na Wizara yangu kuimarisha na kuboresha zaidi  mfumo huu ili uweze kukidhi mahitaji ya Nchi nzima naviwango vya Kimataifa.
Pamoja nanyi narejea tena kusisitiza kauli mbiu ya uzinduzi wa mfumo huu; “SAJILI MIFUGO YAKO KWA UHAKIKA WA SOKO NA UDHIBITI WA WIZI WA MIFUGO NA MIGOGORO”
Baada ya kusema hayo napenda kutangaza kuwa Mfumo wa Kitaifa wa Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo Mifugo Umezinduliwa Rasmi.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

















VIKAO VYA WAKUU WA IDARA/VITENGO NA WATENDAJI WAKUU WA WIZARA

Kila wiki siku ya  Jumatatu ni siku ya kufanya Kikao cha Wakuu wa Idara na Vitengo wa wizara kuanzia saa nne kamili asubuhi. Kama unahitaji kumuona katibu Mkuu Naibu Katibu Mkuu, Mkuu wa Idara au Kitengo, hakikisha unamuona kabla ya saa za kikao .  


BARAZA LA WAFANYAKAZI 

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilifanya Kikao cha Baraza hilo katika ukumbi wa ST Gaspar pale Dodoma mapema mwezi juni 2011 tarehe 16 na 17 /06 na kutoa Maazimio ambayo sasa yanatekelezwa . Watumishi wote walishiriki katika uchaguzi wa uongozi mpya wa TUGHE hapa Wizarani na RAAWU kwa upande wa Utafiti kule Mpwapwa ambapo ndipo ilipo Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Mifugo Mpwapwa. Wakuu wa Idara na Vitengo wamepewa dokezo la kukumbushwa utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa pale Dodoma dokezo la tarehe 11/10/2011 na Katibu wa Baraza .

HOTUBA YA BAJETI  2011/12

Hotuba ya bajeti ya wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imechapishwa kwenye gazeti la Uhuru na Habari leo tarehe 28/07/2011, pia inapatikana kwenye mtandao wa wizara http://www.mifugo.co.go.tz/  


MAANDALIZI YA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA KWA WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI  YATAFANYIKA VIWANJA VYA SABASABA BARABARA YA KILWA -  DAR-ES-SALAAM KUANZIA TAREHE 1 - 12/12/2011

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inapenda kuwajulisha Wadau na Wananchi kuwa itashiriki kwenye maonyesho tajwa hapo juu, yatakayofanyika kuanzia tarehe 1 - 12 /12/2011. Wadau wote wanakaribishwa, ambapo baadhi ya wadau watakuwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, kwa wale ambao hawatashiriki moja kwa moja waje waone wenzao hatua waliyopiga mbinu ,utaratibu na utendaji wao wa kazi. (KUONA NI KUAMINI) Hakuna lisilo wezekana Vilevile mtapata fursa ya kuelezewa na Wizara ni huduma gani ambazo ikiwa ni Idara au Vitengo vya Mifugo na Uvuvi hufanya katika kuendeleza Sekta hizo muhimu katika maisha ya Mtanzania,  nini jukumu la Wizara katika kutekeleza Sera Mipango na Mikakati mbalimbali ambayo imeandaliwa  na Wizara. Aidha Wadau watakuwepo kuonyesha matokeo ya Sera, Mipango Mikakati mbalimbali ambapo wataeleza na kuonyesha wamenufaika vipi na usimamizi na ufuatiliaji huo wa Wizara katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuendeleza sekta hizo mbili kwa ujumla. 

Wote Mnakaribishwa

WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI.

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, imegawanyika kwenyeSekta kuu mbili  yaani Sekta ya
 •  Mifugo 
 • Uvuvi 
 • zile za Mtanbuka
Sekta ya Mifugo ina Idara zifuatazo:
 1. Huduma za Mifugo.,
 2. Uzalishaji, Masoko na Matumizi ya ardhi kwa mifugo,
 3. Utafiti Mafunzo,Ugani Utanmbuzi na ufuatailiaji wa Mifugo.
 4. Maabara Kuu ya Mifugo
 5. Baraza ka Vetenary
 6. Taasisi ya Taifa ya Utafiti Mpwapwa
Sekta ya Uvuvi ina Idara zifuatazo
 1. Maendeleo ya Uvuvi
 2. Uzalishaji Viumbe kwenye Maji.
Idara za Mtambuka
 1. Sera na Mipango
 2. Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu.
Viengo Mtambuka
 1. Fedha
 2. Sheria
 3. Ukaguzi wa Ndani
 4. Manunuzi
 5. Mawasiliano Serikalini.
Kila Idara au Kitengo kina Mkuu wa Idara/Kitengo Je unahitaji kuwasiliana na Mkuuwa Idara au Kitengo tuma barua yako ya maombi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi tuma maswali yako kabla ili yamfikie mhusika ayajibu kwa uhakika nawe utakabidhiwa.

"TUSHIRIKIANE KATIKA KUENDELEZA WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI"