Nav bar

Jumatano, 3 Juni 2020

NAIBU WAZIRI ULEGA AAGIZA KUKAMILIKA KANUNI, KUSIMAMIA SHERIA YA UVUVI WA BAHARI KUU
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu kufanya maandalizi ya kupata kanuni bora za kusimamia Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na watendaji wa mamlaka hiyo Mjini Unguja Visiwani Zanzibar akifuatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame Ali Ussi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ulega aliwataka watendaji hao kuunda kanuni bora zitakazoenda sambamba na mfumo wa biashara kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anataka kuona namna ukanda wa bahari unavyosaidia kuinua uchumi wa taifa.

“Jumla ya vipengele vyote vya sheria takriban 104 tumevifanyia kazi na vipengele kama 23 ambavyo havijaguswa lakini vingine vyote vimeguswa kuendana na uchumi wa bahari ili kuwa na mchango kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla katika kufanya maboresho ya uvuvi na bahari kuu, rai yangu kwa mamlaka mmefanya kazi nzuri kwa utengenezaji wa sheria lazima kwenda mbio sasa ndani ya miezi miwili tuwe tumepata kanuni zitakazoenda sambamba na biashara ya leo bila kuathiri maslahi mapana ya taifa letu.” Alisema Ulega

Aliongeza kuwa matumizi ya sheria hiyo yatakayoenda sambamba na kanuni bora za utekelezaji wake zitakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji kwa raia kutoka nje ya nchi kuja na meli zao hapa nchini na kufanya shughuli za uvuvi na wengine kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa samaki kwa kuwa Ukanda wa Pwani ya Bahari Hindi bado hakuna uwekezaji wa kutosha wa viwanda hivyo.

 Aidha, aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ilivyoboresha mazingira kwenye maziwa na mito hali iliyopelekea ndege za mizigo kubeba minofu ya samaki kutoka katika uwanja wa ndege wa Mwanza na kusafirisha kwenda nje ya nchi.

 Pia, Naibu Waziri Ulega alifafanua kuwa wakati watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu wanaandaa kanuni za kusimamia sheria hiyo watambue kuwa ushirikiano ni muhimu katika utekezaji huo na kutokuwa na mvutano wowote kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein wanataka kuona mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi.

 “Lazima mfanye kazi pamoja mshirikiane msiwe na aina yoyote ya mvutano, lazima mfanye kazi nzuri ya kushirikiana lazima taifa letu linufaike, Tanzania kwanza, tunaenda kufungua uvuvi wa bahari kuu tunaenda kufungua uchumi wa bluu tunataka uvuvi utoke kuchangia Asilimia 1.9 katika pato la taifa kusiwe na jambo la kunyoosheana vidole.” Alifafanua Ulega

Ulega akizungumza katika kikao hicho alisema ni muda muafaka kwa wavuvi hapa nchini kuondakana na uvuvi wa kuwinda bali uendane na teknolojia ya kisasa kufahamu maeneo mahsusi kwa ajili ya uvuvi ili kupunguza gharama kwa kutengwa vituo maalum vya kutolea taarifa ya maeneo yenye samaki na umbali wa kufikia maeneo hayo.

Alibainisha kuwa ni lazima uwepo mfumo wa kitaaalamu kwenye vyombo vyao vya uvuvi ili mvuvi anapotoka pwani kwenda baharini kuvua awe na uhakika wa mahali anapokwenda kuvua samaki na kuwataka watendaji hao kulifanyia kazi suala hilo haraka ili kufikia malengo ya wavuvi kunufaika zaidi kupitia sekta hiyo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, akiwa katika ziara maalum visiwani Zanzibar alitembelea kituo cha utotoaji wa vifaranga vya samaki, majongoo na kaa eneo la Maruhubi Mjini Unguja, ambapo alisema ipo miradi midogomidogo itakayoweza kutumika ikiwemo ya uvuvi wa samaki, majongoo na kaa ambayo ina soko kubwa duniani.

Ulega alisema uzalishaji wa bahari ndio nguzo kuu ya kukuza uchumi kwa wakaazi wa Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Tanzania baada ya kufanikiwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye maji baridi hivyo mapinduzi makubwa yanaelekezwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye bahari.

 “Serikali imeamua kwa dhati bahari yetu iweze kutunufaisha na kuwa na mchango chanya wakati wa kuhamia katika uvuvi wa bahari kuu na jamii iweze kufuga na kukuza kipato katika viumbe ambavyo vinauzika na kuhitajika duniani kama kaa na majongoo bahari ambao wanahitajika katika mataifa ya nje ya nchi yetu na wamekuwa wakiuzwa kwa bei kubwa.”

Ulega alisema, juhudi hizo zinaendana na mikakati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo itakayoinua jamii ya Ukanda wa Pwani kupitia miradi hiyo midogo.

"Tunafanya haya yote kwa ajili tunapata vyanzo vingi vya mapato vitakavyosaidia uchumi wa nchi pamoja na wananchi ambayo itatusaidia Tanzania kukuza maendeleo yake kwa haraka, kama ni utalii tunapongeza viongozi wetu wakuu kwa kusimamia haya na elimu hii iende mbali zaidi uzalishaji viumbe maji kwenye bahari unaweza kusababisha kuinuka kama taifa na kufanya vizuri zaidi kiuchumi na kuinua pato la taifa.”

Aliongeza kuwa licha ya kuelekea mpango wa uvuvi katika bahari kuu tayari miradi kama hiyo imeleta mageuzi makubwa katika maji baridi kwa maana ya maeneo ya maziwa na mito kwa upande wa Tanzania Bara.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame Ali Ussi, alisema, Zanzibar inaendelea na mpango wa uchumi wa bahari, kwa kuwa una nafasi kubwa ya kuingiza mapato ya haraka pamoja na kuwanufaisha wananchi wengi.

“Tunaelekea kwenye uchumi wa bluu unaohitaji kutunza mazingira ya bahari, ninawashauri watanzania sehemu zote za pwani watunze maeneo ya bahari kwa kutunza maeneo ya mazalia ya samaki yakiwemo matumbawe.” Alisema Ussi

Pamoja na hayo, alisema kuwa miradi hiyo ya uzalishaji wa samaki imekuwa na nafasi kubwa katika kukuza mazingira ya bahari ambayo tayari sehemu kubwa ya maeneo yanayotegemewa kwa uvuvi yameshaathirika.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha sekta ya uvuvi inazidi kunufaisha zaidi taifa na mvuvi mmoja mmoja na kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (kushoto) akiwa ameshika jongoo bahari alipotembelea kituo cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar.

Aliyevaa tai nyekundu ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020) 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akiwa ameshika jongoo bahari alipotembelea kituo cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar. (02.06.2020) 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyevaa koti jeusi) akipata maelezo ya ufuatiliaji wa meli zinazoingia katika maji ya Tanzania kwenye Bahari ya Hindi mara baada ya kutembelea ofisi za  Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu visiwani Zanzibar. (02.06.2020) Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyesimama) akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (hawapo pichani) katika ofisi za mamlaka hiyo Visiwani Zanzibar, aliyekaa kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020) 
Jumatatu, 1 Juni 2020

SERIKALI YATEKELEZA KWA VITENDO ILANI YA UCHAGUZI KWA WAVUVI

Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha awamu ya kwanza imeweka mikakati mizuri na kuthubutu kuhakikisha wavuvi wanaanza kuaminika na kukopeshwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezungumza hayo katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, wakati akikabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kutoka TADB kwa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Bukasiga na kufafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameweka mazingira ya kufanya wavuvi waweze kuaminika na taasisi za kifedha na kupewa mikopo ili kujiimarisha katika shughuli zao.

“Hii benki tangu ianze ina miaka mitano sasa na katika miaka mitano ya Dkt. John Magufuli imewakopesha watanzania katika nyanja za kilimo, mifugo na uvuvi zaidi ya Shilingi Bilioni 170 na tangu uhai wa taifa hili wavuvi wameanza kuaminika na kukopeshwa pesa.” amesema Mhe. Ulega

Ameongeza kuwa wavuvi walikuwa wanaonekana ni watu wa kuhamahama lakini kwa uthubutu, uzalendo na utayari wavuvi wanaanza kuaminika na kuhamasishwa kujiunga katika vikundi vya ushirika na kupatiwa mikopo ya masharti nafuu ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ibara ya 27 na msimamo wa Rais Dkt. John Magufuli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine akizungumza katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kwa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Bukasiga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha barafu, amesema wameweza kutekeleza upatikanaji wa mkopo huo baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati ya kuhakikisha inatekeleza uvuvi uwe wa kisasa utakaoonesha fursa zaidi.

Akitoa neno la shukran kwa niaba ya wanachama wa kikundi cha Bukasiga makamu mwenyekiti wa chama hicho Bw. Jumbula Lugola amesema wanashukuru kwa mkopo huo kwa kuwa shughuli zao za uvuvi zitabadilika na kufanyika kisasa zaidi kwa kuwa CCM imeweka mkakati mzuri ili kuhakikisha wavuvi wanaufaika kupitia mikopo.

Ameongeza kuwa kwa juhudi za Rais Magufuli hatimaye wameweza kupatiwa mkopo na TADB wa Shilingi Milioni 200 na kumuahidi Rais Magufuli kuwa mkopo waliopatiwa watahakikisha wanautumia vyema ili uwanufauishe pia watanzania wengine.


Picha ya pamoja: Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyevaa koti jeusi) akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwemo Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo Bw. Steven Michael (wa tatu kutoka kushoto) ambaye ameongoza dawati lake kufanikisha mikopo ya wavuvi kutoka TADB. (31.05.2020) 

SERIKALI YATAKA MIKOPO YA TADB KUWA CHACHU KWA WAVUVI KUANZISHA VIWANDA VIDOGO
 Serikali imesema inataka kuona uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi kupitia mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuyaongezea thamani mazao yanayotokana na sekta za mifugo na uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezungumza hayo (30.05.2020) katika Kijiji cha Kanyala kilichopo Halmashauri ya Buchosa iliyopo Wilaya Sengerema Mkoani Mwanza, wakati wa kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 uliotolewa na TADB kwa Chama cha Ushirika cha Zilagula ambacho pia kimepata mkopo wa Shilingi Milioni Tano kutoka katika mfuko wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Mhe. Ulega amesema licha ya vyama vingine vya Kasalazi na Soswa ambavyo kila kimoja kimepata pia mkopo wa halmashauri wa Shilingi Milioni Tano, ili wafugaji na wavuvi waweze kunufaika na mikopo kupitia ushirika wao, wizara itakuwa msimamizi kwa vyama vitakavyokidhi sifa za kupata mikopo kutoka TADB.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaenda kuwa msimamizi namba moja wa vyama vya ushirika tena kwa barua hivyo niwatakeni uongozi wa mkoa, halmashauri na ushirika wekeni taarifa zenu vizuri. Tunataka viwanda vidogo vidogo vya wafugaji na wavuvi vikiwemo vya kukausha dagaa, minofu ya samaki na kutengeneza kayabo nzuri ili mpeleke bidhaa hizo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.”  Amesema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amevitaka vyama hivyo vitatu vilivyopata mikopo waitunze mikopo hiyo kwa kuifanyia kazi na hatimaye kuirejesha, kikiwemo Chama cha Zilagula kilichopata mkopo kutoka TADB, kwa kuwa fedha zilizotolewa na benki hiyo zinamilikiwa na watanzania kwa asilimia mia moja  ili watanzania wengine pia waweze kunuifaika na mikopo hiyo na kutoa rai kwa wavuvi kuendelea kujiunga katika vyama vya ushirika wakati akikabidhi hati ya kuandikishwa kwa vyama vya Sangara-Nyakaliro na Gembare vilivyopo Halmashauri ya Buchosa.

Amewataka pia watendaji wa serikali kutoa elimu kwa vyama vya ushirika namna ya kuitumia vyema mikopo wanayopata ili waweze kuirejesha kwa wakati pamoja na kuwaongoza ili waweze kupata mikopo mikubwa zaidi kwa kuwa utoaji mikopo kwa vyama vya ushirika vya wafugaji na wavuvi ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kutaka kuona wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo hapa nchini.

“Watendaji wakati mwingine vyama vya ushirika havikosei kufikia hatua mbaya ya kukosa mikopo ni muhimu elimu itolewe na watendaji kwa wafugaji na wavuvi msiwaache hawa watu wa ushirika waliopatiwa mikopo kwa kuwapatia elimu na kuwaongoza hatua kwa hatua ili waweze kulipa marejesho ya mikopo waliyopatiwa.” Amefafanua Mhe. Ulega

Vilevile, Naibu Waziri Ulega amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kujiepusha na ubadhilifu wa fedha za mikopo hiyo kutoka TADB, huku akitoa rai kwa wavuvi kuwa na uchumi endelevu na hatimaye kuwa walinzi wa rasilimali za uvuvi kupitia vyama vyao vya ushirika kwa kuwa azma ya serikali ni kuona Tanzania inaongoza kwa kusafirisha minofu ya samaki kwenda nje ya nchi na mchango wa samaki katika pato la taifa unaongezeka kutoka Asilimia 1.7 hadi Mbili ya sasa na kufikia Asilimia Tano na kuendelea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka mikakati mizuri na benki hiyo iliyowezesha kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanakuwa na sifa za kupatiwa mikopo ili kujiendeleza katika sekta hizo.

“Tuliomba kwanza vyama hivi vikae katika ushirika kwa sababu tuliamini ule umoja wao utatupatia njia kuhakiksha mikopo inalipwa kwa kuwaweka katika mfumo ulio rahisi, wizara pia iliweka mazingira ya kubadilisha mitumbwi kuwa na namba na kufahamika ili benki iweze kuwa na taarifa sahihi ya mitumbwi ya wahusika wanaopatiwa mikopo pamoja na kuweka mazingira ya wavuvi kuwa na mifumo rasmi ya kuweka na kutoa pesa ili benki iweze kujua historia na kutoa mikopo kulingana na historia ya waombaji.” Amebainisha Bw. Justine

Bw. Justine ameongeza kuwa TADB inatoa mikopo hiyo na nia yao ni kuona wafugaji na wavuvi wengine wengi wananufaika na mikopo hiyo na kuwataka kufanya biashara zao kwa kuweka kumbukumbu zao vizuri ili wanufaika waweze kufikia hatua ya kuwa na viwanda vidogo vidogo.

Aidha, amesisitiza kwa vyama vya ushirika vilivyopata mkopo kutoka TADB kuhakikisha vinalipa mikopo hiyo kwa wakati ili watanzania wengine wenye uhitaji wa kupata mikopo hiyo waweze kupata na kukuza biashara zao.

Kuhusu Dawati La Sekta Binafsi lililo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambalo limekuwa likifanya kazi kubwa katika kuhakikisha wafugaji na wavuvi wanaunganishwa na taasisi mbalimbali za kifedha, Mratibu wa dawati hilo Bw. Steven Michael amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha matokeo chanya yanaonekana likiwemo tukio la Chama cha Ushirika cha Zilagula kupatiwa mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kutoka TADB.

Bw. Michael amesema wamefanya kazi kubwa kuhakikisha vyama vya ushirika wanaviunganisha na taasisi za kifedha pamoja na halmashauri mbalimbali nchini na kufuatilia mara kwa mara kwa kuwa wao wanafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wadau wa mifugo na uvuvi na taasisi hizo kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Zilagula Bw. Joram Yuda amesema wanaishukuru serikali kwa kuwa wavuvi wameanza kuaminika na taasisi za kifedha kwa kuwapatiwa mikopo ili kujiendeleza katika sekta hiyo, huku Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Gembare Bw. Hassan Muhenga ameishukuru pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TADB kwa kuhakikisha wanasimamia maono ya Rais Dkt. John Magufuli ya wkupatiwa mikopo.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na wananchi mara baada ya kuwasili katika kijiji cha Kanyala kilichopo Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kwa ajili ya kutoa mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Halmashauri ya Buchosa kwa vikundi vya ushirika vya wavuvi. (30.05.2020) 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na baadhi ya wananchi na vikundi vya ushirika wa wavuvi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa vikundi hivyo kutoka TADB na Halmashauri ya Buchosa na kutaka mikopo hiyo iwe chachu kwa wavuvi kuanzisha viwanda vidogo vidogo. (30.05.2020) Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TADB Bw. Japhet Justine (aliyevaa miwani) kwa namna benki yake ilivyowezesha kutoka mkopo wa Shilingi Milioni 100.7 kwa Chama cha Ushirika Zilagula kilichopo Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza. (30 05.2020Walioshika mfano wa hundi: Kutoka kushoto, Mkurugenzi Mkuu wa TADB Bw. Japhet Justine, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Zilagula Bw. Joram Yuda na Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi Bw. Steven Michael .Ijumaa, 29 Mei 2020

"WATANZANIA TUNYWE MAZIWA YA HAPA NCHINI"-ULEGA
Watanzania wametakiwa kuwa wazalendo kwa kunywa maziwa yanayotengenezwa hapa nchini ili kuendeleza uchumi wa viwanda na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya wiki ya maziwa  Mkoani Dodoma kwa njia ya kielectronic 

"Ninaomba Sana na ninawasisitiza watanzania lazima tuwe na wivu wa maendeleo kwa ajili ya Taifa letu, lazima tuwe na uzalendo wa Taifa letu" Ulega

Pia ameongezea na kusema kuwa Mhe. Raisi wetu Dr John Joseph Pombe Magufuli ametupa Ari kubwa Sana ya uzalendo kwa kupenda vya kwetu.

Imeelezwa kuwa sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa hapa nchini inachangia kwa asilimia saba (7%) huku asilimia thelathini (30%) ikitokana na sekta ndogo ya maziwa hivyo asilimia 1.2% ya Pato zima la Taifa inatokana na sekta ya maziwa.

Mhe. Ulega amesema  Katika mwaka 2017/2018 kulikua na jumla ya viwanda (76,) lakini hivi Sasa tunajumla ya viwanda (99) kwa hivyo tunazidi  ongezeko la viwanda vidogo,vya Kati na vikubwa 20 katika Taifa letu.

Naye Kaimu msajili wa bodi ya maziwa Dr Sophia Mlote amesema bodi ya maziwa imefanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kuhakikisha tasnia ya maziwa inakua kwa kiasi kikubwa

Maadhimisho ya wiki ya maziwa yanakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo "wiki ya maziwa 2020 chagua viongozi Bora kwa maendeleo ya tasnia ya maziwa"


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega akifungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kielekitroniki 2020 yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma. Maadhimisho haya ni ya 23 kufanyika tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho haya mwaka 1997 yakiwa na lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kutoka wastani wa Lita 49 kwa mtu kwa mwaka hadi kufika Lita 200 kwa mtu kwa mwaka. 


Kaimu msajili wa bodi ya maziwa bi Sophia Mlote akitoa Taarifa ya tasnia ya maziwa katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya maziwa, na wadau wakimsikiliza kwa makini,maadhimisho hayo yalifanyika katika ukumbi wa treasure square  tarehe 28/05/2020

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dkt. Felix Nandonde kwa niaba ya Katibu Mkuu (M) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega kwenye Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kielekitroniki yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma. 


Katibu Tawala Mkoa Ndugu, Maduka  Kessy akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.Abdallah Ulega mara baada ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa kwa njia ya Kielekitroniki jijini Dodoma,

Jumanne, 26 Mei 2020

MAAZIMIO YA MKUTANO WA MAWAZIRI WA KILIMO, USALAMA WA CHAKULA, KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (SADC jijini Dsm, (22.05.2020)
* Mkutano umetoa miezi mitatu kwa kila mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kufanya tathmini ya madhara ya ugonjwa wa Covid - 19 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

* Mkutano umeweka mikakati ya usalama wa chakula na lishe katika ukanda wa SADC licha ya changamoto mbalimbali.

* Mkutano umeazimia mikakati ya kulinda magonjwa yanayovuka mipaka yanayohusu mimea na wanyama na kuathiri kilimo na mifugo.

* Mikakati imewekwa kutathmini namna wavuvi wanavyoathirika na ugonjwa wa Covid - 19.

* Mikakati imewekwa kwa shughuli za uvuvi katika ukuzaji viumbe kwenye maji hususan kwa nchi zizisizokuwa na maji ya asili (maziwa, bahari na mito).

* Mkutano umeweka mikakati ya nchi wanachama wa SADC kujilinda na ugonjwa wa covid - 19.Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) (kulia), akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye ni mwenyekiti wa maafisa waandamizi wa SADC katika sekta hizo, wakiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza kwa mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) akizungumza na mawaziri 11 kati ya 16 wakati wa mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) Baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Tanzania, wakifuatilia mkutano wa mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) akionyesha ishara ya kuwaaga mawaziri 11 kati ya 16 wa SADC (hawapo pichani) walioshiriki  mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference'. (22.05.2020) 
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (Mb) ambaye pia Mwenyekiti wa Mawaziri wa Kilimo, Usalama wa Chakula, Kilimo, Mifugo na Uvuvi akiwa na baadhi ya maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Kilimo ambao wamehudhuria mkutano wa SADC kwa njia ya video 'video conference' jijini Dar es Salaam. (22.05.2020) Ijumaa, 22 Mei 2020

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUTHAMINI SOKO LA NYAMA.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wafanyabiashara wanaouza nyama nchini kutopandisha bei ya nyama kipindi hiki cha sikukuu ya Eid El Fitr  ili kuhakikisha kila mwananchi anapata kitoweo hicho.Akizungumza (18.05.2020) jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mhe.Ulega amemtaka pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Bw. Jumanne Shauri ndani ya siku saba kuhakikisha wanawapeleka wafanyabiashara wanaofanya biashara katika machinjio ya vingunguti kujionea eneo jipya lililotengewa na Manispaa ya ilala.Mhe. Ulega amebainisha hayo wakati akikagua ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa katika eneo la vingunguti katika Manispaa ya Ilala, ambapo amesisitiza wafanyabiashara wa nyama wanapaswa kuuza nyama kwa bei ya kawaida kulingana na hali ilivyo ili kuhakikisha watu wote wanapata kitoweo hicho.Aidha amesema imekuwa ni kawaida kwa wafanyabiashara wa Nyama kupandisha bei kipindi cha sikukuu kinapofika hali inayosababisha  wananchi kutopata nyama kulingana na bei kuwa juu."Serikali ya awamu ya tano inatengeneza uchumi endelevu hivyo katika kuhakikisha hili wafanyabiashara wa nyama wanatakiwa kuchangamkia fursa ya sikukuu ya Eid El kuuza nyama kwa bei ya kawaida na sio ya kuwaumiza wananchi," amesema Mhe. Ulega.Kuhusu mradi wa machinjio ya kisasa ya vingunguti ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 ya ukamilikaji wake, Mhe. Ulega amesema mradi huo unaogharimu kiasi cha Sh.Billioni 12.4 ambao unalengo la kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, mikoa mingine na nchi za nje kupata nyama itakayokuwa bora na yenye kuandaliwa vizuri kutokana na jengo hilo."Wizara yangu ndiyo inashughulikia masuala ya mifugo natoa pongezi kwa serikali kwa hatua hii ya kufikisha jengo hili katika kiwango cha juu kwani kiwanda pekee kinachotusaidia kwa sasa kipo Mwanza, Chobo Investmest hivyo kupitia kiwanda hiki naamini tutaongeza nguvu katika uuzaji wa nyama." Ameongeza Mhe. UlegaHata hivyo Mhe. Ulega amesema uwekezaji wa mradi huu utailipa serikali katika hatua zote ikiwemo kiuchumi na kijamii pindi shughuli za mnada zitakapoanza kufanyika katika jengo hilo.Naibu waziri huyo amesema Tanzania bado ina fursa nyingi katika mifugo na serikali tayari ina mikakati mizuri ya kuhakikisha sekta hii inazidi kukua siku hadi siku na kutoagiza nyama nje ya nchi."Bado tuna fursa nyingi katika kuhakikisha nyama inapatikana kwa wingi na tutaacha ununuaji wa nje ya nchi pindi mradi huu utakapokamilika na tutahakikisha sisi ndio tunawapelekea watu wa  nchi nyingine" amesema Mhe. UlegaAmesema eneo hilo litachinja ng'ombe takriban 1,500 na mbuzi 1000 kwa siku moja pindi itakapokamilika hivyo upandishaji holela wa bei ya nyama kwa vipindi vya sikukuu hautakuwepo tena kutokana na nyama kupatikana kwa urahisi zaidi.Pia amesema kwa wafanyabiashara wa machinjio hayo wanaofanya biashara, tayari wamepatiwa eneo ambalo watajengewa na kufanya shughuli zao karibu na eneo hilo kama kawaida."Najua kuna watu wanajiuliza kuhusu wakinamama na vijana wanaofanya kazi hapa, Manispaa ya Ilala imeshawatafutia eneo na ni zuri lipo karibu na machinjio haya ya kisasa litawapa fursa ya kuendelea kufanya shughuli zenu, ninamuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuwapeleka wafanyabiashara na kuliona hilo eneo." amesema UlegaWakati huo huo Mhe. Ulega amempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa hotuba yake aliyotoa juzi ambapo wafugaji na wavuvi wamempongeza kwani bila kutoka kwao hawawezi kupata kipato.Pia amesema maono ya Rais Magufuli ni ya kizalendo, Kiutu na kuwainua wananchi wake hivyo watendaji katika nyanja mbalimbali wanapaswa kutomuangusha ili kuifikisha nchi katika uchumi wa juu.Kwa Upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama nchini, Bw. Imani Sichalwe amesema kupitia mradi huo wafugaji watapata masoko makubwa na kutoingiliwa na madalali ambao kwa asilimia kubwa walikuwa wanawapunja.Amesema ni wakati wa wafugaji kujipanga na kuanza kufuga kisasa kwa kuongeza ubora na kuwaongezea thamani mifugo yao.


"Wafugaji wataunganishwa moja kwa moja na watu wa mradi hivyo hawatawatumia tena madalali, kinachotakiwa wafugaji wanenepeshe mifugo yao iwe tayari kwa kuuza," amesema Bw. Sichalwe

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) akisikiliza kwa makini maelekezo ya ramani ya jengo la machinjio ya Vingunguti Wilaya ya Ilala mkoani Dar es salaam. (18/05/2020) 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) atembelea machinjio ya Vingunguti Wilaya ya Ilala jijini dar es salaam. (18/05/2020) lengo likiwa ni pamoja na kuimiza ukamilishwaji wa mradi huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) atembelea machinjio mpya inayojengwa Vingunguti Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam.


UKIFUGA KISASA HUWEZI KULALA NJAA. - MRUTTU

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Mruttu amesema wafugaji wakifuga kisasa kwa kunenepesha na kuvuna mifugo yao ni rahisi kupata masoko ndani na nje ya nchi kwani watu wengi wanategemea bidhaa za ng'ombe.Ameyasema hayo wakati akiongea na  wafugaji kwenye kijiji cha Nkerenge Wilaya ya  Misenyi Mkoani Kagera, (12/05/2020) Dkt. Mruttu amesema faida kuu za kufuga kwa mkakati ni pamoja na kupata masoko ya uhakika kutokana na  ng'ombe atakuwa akijiuza na sio kutafuta mnunuzi kwani  muonekano wake tuu utamvutia mnunuzi." Biashara ya mifugo ni nzuri na inafaida sana kwani mfugaji hawezi kulala njaa hata siku moja, inamuwezesha mfugaji kuvuna, kuuza na kufanya mambo ya maendeleo." Amesema Dkt. MruttuAidha Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti Tanzania (TALIRI) Bi. Neema Urassa amehimiza wafugaji kuendelea kuwekeza kwenye lishe bora ya ng'ombe na kufuga kwa kufuata kanuni bora za ufugaji ili kupata faida zaidi na kuwataka wafugaji wanaofuga kwa kutumia mfumo huria kufuga ng'ombe katika eneo kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya ng'ombe na malisho." Hii itachochea uwezo wa ng'ombe kuzalisha mazao bora ya Nyama, maziwa, ngozi na bidhaa zitokanazo na usindikaji wa mazao hayo  kupata soko la uhakika" Amesema Bi NeemaHata hivyo Bi. Neema ameongeza kuwa ng'ombe ni kama kiwanda kwani ana uwezo wa kula na kutunza chakula (nyasi na vyakula vingine) na kuvibadilisha kuwa nyama, maziwa, ngozi na mbolea kwa ajili ya matumizi ya binadamu." Kinyesi cha ng'ombe ni chanzo cha nishati ya bayogesi kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani na kuwa faida hizi zote zinampatia mfugaji uwezo wa kuongeza pato la kaya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.Naye Mtafiti kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Atupele Mohammed amewapongeza wafugaji kwa kukubali na kutumia fursa ya uhimilishaji kwani kwa kufanya hivyo kasi ya uzalishaji wa mifugo yenye ubora itaongezeka."Wafugaji mmeonyesha mfano mzuri kwa mamna mnavyozingatia kanuni za afya kwa kuwa, karibu kila kaya imeweka maji na sabuni kwa ajili ya kusafisha mikoni kwa kila mtu anayeingia na kutoka katika maboma yenu." Amesema Bi. AtupelePia Bi Atupele  amewaeleza kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi inajali afya na suala zima la kujikinga na maambukizi ya virusi vya korona hivyo imetoa vitakasa mikono kwa kila kaya iliyoshiriki katika mafunzo.Aidha Mfugaji wa  kijiji cha Nkerenge Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera ambaye pia amepata fursa ya kuhimilisha ng'ombe zaidi ya sitini  ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na  Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hiyo kijijini kwao na  kuiomba Wizara hiyo kuwasaidia kupata madawa na chanjo kwa wakati, kupatiwa elimu, wataalam wa malisho, na kuanzisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa  ng'ombe ambao utamsaidia Mfugaji kupata maziwa, kuuza na kuweza kuendesha maisha yake.

Mfugaji wa kijiji cha Nkerenge kata ya Mtukula Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera Bw. Majid Kayondo ambae pia alipata fursa ya kuhimilisha mifugo yake ameishukuru Wizara ya mifugo na Uvuvi na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kuwafikia na kuwahamashisha juu ya ufugaji bora na wenye tija. Aidha ameiyomba serikali kuwajengea Barabara ya kuingia mnadani, kupatiwa madawa kwa wakati, kupatiwa elimu ya malisho na kurudisha utaratibu wa kopa ng'ombe lipa ng'ombe. (12/05/2020) 

Zoezi la Uhamasishaji na uelimishaji wa wafugaji ukiendelea kwenye boma la Bw. Majid Kayondo Kata ya Mtukula  kutoka kwa watafiti wa wizara ya mifugo na Uvuvi leo Mkoani Kagera. (12/05/2020)