Nav bar

Jumatano, 23 Desemba 2020

ZECO YAPEWA SIKU 14 KUKAMILISHA UKARABATI WA BWAWA LA KIMOKUWA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ameipa Kampuni ya ZECO yapewa siku 14 kukamilisha ukarabati wab wawa la Kimokuwa litakalotumika kwa ajili ya matumizi ya kunyweshea mifugo na matumizi ya binadamu.

 

Prof. Gabriel ametoa maelekezo hayo leo (22.12.2020) wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ukarabati wa mradi huo unaotekelezwa katika kijiji cha Kimokuwa, wilayani Longido, mkoani Arusha.

 

“Mwanzoni kampuni hii ilianza kazi vizuri lakini mwishoni imekuwa na matatizo kwani usimamizi wao wa mradi sio mzuri kitu ambacho kimesababisha umaliziaji wa mradi kuwa na mapungufu,” alisema Prof. Gabriel.

 

Pia amemtaka mkandarasi kujiridhisha kwenye kingo za bwawa hilo walizoziweka kwani ikitokea zikabomoka hatua kali zitachukuliwa dhidi ya kampuni hiyo.

 

Kutokana na mapungufu aliyoyaona amempa mkandarasi siku 14 kuhakikisha anakamilisha mradi. Kutokana na kuwepo kwa mapungufu hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul hataupokea mradi huo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

 

Prof. Gabriel amewasihi wakandarasi wazawa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa umakini ili waendelee kuheshimika na kupewa kazi na serikali kwani fedha zinazotolewa za miradi zinatoka kwa wananchi walipa kodi. Hivyo amewataka wafanye kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia viwango.

 

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Bw. Simba amempogeza Katibu Mkuu Gabriel kwa uamuzi wake wa kukagua maendeleo ya mradi huo kabla ya kukabidhiwa kwa mapungufu yaliyopo hata uongozi wa wilaya ulishayabaini. Lakini pia amemsihi mkandarasi kuhakikisha anayafanyia kazi mapungufu yote yaliyoainishwa katika ukaguzi huo ili wafugaji na jamii kwa ujumla iweze kupata huduma hiyo ya maji.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimokuwa, Bw. Kileli Olendere amesema Katibu Mkuu yupo sahihi kuamua kutomleta Naibu Waziri kuja kukabidhiwa bwawa hilo kwani ukarabati wake bado haujakamilika hivyo ni vema mkandarasi kwanza akamilishe kazi zinazotakiwa ndipo mradi ukabidhiwe kwa viongozi pamoja na wananchi.

 

Zephania Umbuli ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya ZECO Construction amesema ameyapokea maelekeo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Gabriel na ameahidi kuyatekeleza ndani ya siku 14 walizopewa.

 

Ukarabati wa bwawa hili la Kimokuwa unaogharimu milioni 511.9 ulitakiwa kukamilika Novemba 25. 2020 lakini mkandarasi aliomba kuongezewa muda mpaka Decemba 10. 2020. Kutokana na mapungufu yaliyoainishwa amepewa siku 14 mpaka Januari 06, 2021 kuhakikisha anakamilisha kazi vinginevyo hatua za kimkataba zitaanza kuchukuliwa.




Katibu Mkuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelekezo wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ukarabati wa bwawa la kunyweshea maji mifugo na matumizi ya binadamu la Kimokowua lililopo wilayani Longido, mkoani Arusha. (22.12.2020)

Bwawa la Kimokuwa linaloendelea kukarabatiwa na Kampuni ya ZECO Construction kwa ajili ya kunyweshea maji mifugo na matumizi ya binadamu lililopo katika Kijiji cha Kimokuwa, wilaya ya Longido, mkoani Arusha. (22.12.2020)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akionyesha moja ya mapungufu aliyoyabaini wakati wa ukaguzi wa mradi wa ukarabati wa bwawa la Kimokowua lililopo wilayani Longido, mkoani Arusha. (22.12.2020)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni