Nav bar

Jumatano, 29 Aprili 2020

TUTAHAKIKISHA WAFUGAJI WOTE WANAFUGA KISASA NA KWA TIJA- DKT. MRUTTU




Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Hassan Ally Mruttu  amewataka wafugaji mkoani Pwani  kufuga kisasa na kwa tija huku wakichukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona. 

Akiongea wakati wa Mafunzo elekezi na uhamasishaji  kwa ajili ya kupandisha ng'ombe kwa njia ya chupa (uhimilishaji) kwenye kijiji cha Mkwalia kitumbo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga jana ( 22/04/2020) Dkt. Mruttu amesema lengo la Mafunzo hayo ni kutaka wafugaji kufuga kisasa na kupata Mifugo iliyo bora na mizuri ili kuwezesha wafugaji kufaidika na Mifugo yao.

"Ni jukumu la Wizara  kuhakikisha wafugaji wote nchini wanapata mbegu bora kwa njia ya uhimilishaji ili kupata Mifugo iliyo bora." Alisema Dr. Mrutu.

Aidha ametoa wito kwa wataalam wa Mifugo kuwa tayari wakati wowote kuwasaidia wafugaji pindi wanapotaka kupandikiziwa mbegu bora kwenye Mifugo yao.

Naye Mtafiti wa Mifugo, Bi. Neema Urassa kutoka taasisi ya utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) alielimisha wafugaji juu ya kufuga kibiashara kwa kukubali kuboresha Mifugo yao kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji ng'ombe. 

Aliongeza kuwa Uzalishaji wa ng'mbe bora na bidhaa zake utachangia katika kukidhi mahitaji ya lishe bora ya kaya na  upatikanaji wa malighafi za viwanda. 

Aidha, alisisitiza kuhusu uongezaji thamani wa bidhaa na mazao ya ng'ombe na kuongeza kuwa utaratibu wa uvunaji ng'ombe kwa wakati utamfanya mfugaji kuona tija na thamani ya Mifugo katika kuchangia uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.

" ili kukidhi mahitaji ya walaji na kupata soko lenye faida kubwa ni vyema kuzingatia masuala ya usafi unaokidhi viwango vya uzalishaji, usindikaji na ufungashaji wa mazao  na bidhaa zitokanazo na ng'ombe ikiwa ni pamoja na wanyama hai, maziwa, nyama, samli ngozi na samadi" alisema Bi. Urassa.

Kwa upande wake afisa Mifugo kutoka kituo cha Uhimilishaji Arusha NAIC  Bw. Juma Athumani alisema lengo kuu ya kukagua Mifugo ni kujua kama wana mimba, usalama wa vizazi vyao na kuwatenga wasio na mimba kwa ajili ya zoezi la uhimilishaji kwa njia ya chupa.

" Ni muhimu kwa mfugaji kuchagua mbegu anayotaka kwa Mifugo yake ikiwa ni pamoja na mbegu kwa ajili ya ngo'mbe wa nyama tuu na mbegu kwa ajili ya  maziwa na nyama." Amesema Bw. Juma Athumani.

Hata hivyo Mfugaji wa kijiji cha Mkwalia kitumbo wilayani Mkuranga mkoani Pwani Bw. Yakobo Onina aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuona umuhimu wa kuwaletea elimu ya ufugaji kibiashara na Uhimilishaji wilayani hapo kwani wamehamasika kupandisha Mifugo yao kwa njia ya chupa na kuonyesha utayari wa kutumia njia hiyo na kuendelea kufuga kibiashara.



Afisa Mfawidhi kituo cha Uhimilishaji Kanda ya Mashariki, Bw. Anzigari Balaka (katikati) akijibu maswali ya Bi.Imelda Kamunyu kuhusu Uhimilishaji mara baada kupima mimba na kuangalia usalama wa  vizazi vya mifugo kwa ajili ya maandalizi ya kufanya uhimilishaji kwa Mifugo itakayokuwa haina mimba na isiyo na shida ya kizazi kwenye kaya ya  Bw. Yakobo Onina kijiji cha Mkwalia kitumbo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. (22/04/2020) 



Wafugaji wa kijiji cha Mkwalia kitumbo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Hassan Ally Mrutu akitoa elimu kwa wafugaji hao juu ya ufugaji bora wenye tija na Uhimilishaji. (22/04/2020) 




Mtafiti wa Mifugo Bi. Neema Urassa (wa kwanza kulia) Mfugaji Bw. Mohammed Soa wataalam wa Mifugo Bw. Michael Mwinama (wa kwanza kushoto) na Juma Mohammed (wa pili kutoka kushoto) wakiongea na kumuelimisha mfugaji uyo namna ya kufuga kibiashara na  uhimilishaji na faida zake  kwenye kijiji cha Kondomwelanzi wilaya ya mkuranga mkoani Pwani. (22/04/2020) 




Wataalam wa Mifugo wakichagua na kuangalia ngo'mbe wanaofaa kwa ajili ya kupandikizwa/ uhimilishaji kwa mmoja wa wafugaji Bw. Toephil Mayega wa kijiji cha Kondomwelanzi, Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani (22/04.2020) 



Mtafiti wa Mifugo Bi. Neema Urassa akitoa elimu na kuhamasisha wafugaji kufuga kisasa na kibiashara lengo likiwa ni kuwasaidia wafugaji kupata Mifugo mizuri na iliyo bora ili kuweza kufaidika na Mifugo yao kwenye kijiji cha Kondomwelanzi Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani (22/04/2020) 




"NARCO ijiandae kuwa kitovu cha kuuza mifugo na bidhaa zake baada ya CORONA" Prof. Ole Gabriel



 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) kwa kushirikiana wadau wengine wa sekta ya Mifugo kuhakikisha Nchi inakuwa na Mifugo ya kutosha na yenye afya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya bidhaa zitokanazo na mifugo wakati huu wa janga la Ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid 19) na hata mara baada ya janga hilo kuisha.

Prof. Elisante Ole Gabriel aliyasema hayo mapema leo (18.04 2020) mchana alipofanya ziara katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera lengo likiwa ni kukagua utekelezaji marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II ili kutenga eneo lililopendekezwa  kuhamishia wananchi waishio ndani ya Ranchi hiyo.

"Wakati huu wa hili janga la Corona mahitaji ya nyama Afrika na duniani ni makubwa sana na yanaweza kuongezeka maradufu mara baada ya janga hili kuisha hivyo ni lazima tujipange ili kuhakikisha tunakuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo duniani na NARCO mnapaswa kujitokeza kifua mbele kuwa hilo mnaliweza na lipo ndani ya uwezo wenu" Aliongezea Prof. Ole Gabriel.

Alisisitiza katika kutekeleza hilo NARCO wanapaswa kutafakari vizuri na  kuchagua ranchi moja ya kimkakati kati ya 14 zilizopo hapa nchini ambayo watawekeza kwa dhati ili waweze kunenepesha ng'ombe wengi watakaosafirishwa nje ya nchi zenye mahitaji makubwa ya mifugo na bidhaa zake kwa sasa.

"Lakini pia katika kuelekea kwenye uchumi wa kati unaotegemea  viwanda 2025 ni lazima NARCO iainishe ranchi tano za mfano ambazo wananchi na wadau mbalimbali watafika kwa ajili ya kujifunza juu ya ufugaji wa kisasa na pia zitumike kama shule hata kwa wanaokodisha ranchi nyingine ili nao wafike kujifunza namna ya ufugaji bora utakaolenga kuzalisha mifugo itakayowawezesha kunufaika kiuchumi" Alisisitiza Prof.Ole Gabriel.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa marekebisho ya upimaji wa ramani ya Ranchi ya Mwisa II, kiongozi wa timu ya wataalam wanaofanya kazi hiyo Bw. Fikiri Mwasenga alisema kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 30 kuanzia hivi sasa na mpaka sasa tayari timu hiyo imeshakamilisha kumega maeneo ya vitongoji vitatu ambavyo ni Butera, Bionza na Rwenzige na kazi ya kupima maeneo mawili yaliyobaki inaendelea ili kuweza kukamilisha maeneo yote matano yaliyopendekezwa kutengwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hatua yake ya upimaji wa maeneo hayo ya ranchi ya Mwisa II kwani hatua hiyo itaondoa na kumaliza kabisa migogoro iliyokuwepo baina ya wakulima na wafugaji waliopo kwenye maeneo ya ranchi hiyo.

Ranchi ya Mwisa II ni miongoni mwa ranchi 14 zilizopo chini ya hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) ambapo ina ukubwa wa hekta 133,000 na inatajwa kuwa ranchi kubwa kuliko zote hapa nchini.


Kaimu Meneja  Mkuu wa hifadhi ya ranchi za taifa (NARCO) CPA Masele Mipawa akitoa ufafanuzi juu ya namna walivyoanza kutekeleza agizo la kuweka alama za kuonekana kwenye ranchi hizo wakati wa kikao baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel, viongozi wa Wilaya ya Muleba na timu ya wataalam wanaoendelea na zoezi la kurekebisha ramani ya ranchi ya Mwisa II leo (18.04.2020). 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (Katikati) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bw. Emmanuel Shelembi (Kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Ruyango leo (18.04.2020) huku wakitekeleza agizo la Wizara ya afya, la kusimama mita moja baina ya mtu mmoja na mwingine ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona. 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (Wa pili kutoka kushoto) akiwa kwenye  maombi mafupi ya kuliombea taifa dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona muda mfupi kabla ya kuanza kukagua josho la mifugo lililopo mnada wa awali wa Buzirayombo uliopo Wilaya ya Chato Mkoa wa Geita leo (19.04.2020)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato na wakala wa majengo (TBA) leo (19.04.2020) kwenye eneo la mnada wa wa awali wa Buzirayombo unapotarajiwa kufanyika ujenzi wa majengo ya kisasa ya mnada wa upili

Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa mapema leo (19.04.2020)  akifafanua hatua ambazo mpaka sasa ofisi yake imefikia kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya mnada wa Upili wa Buzirayombo unaotarajiwa kuanza kabla ya mwezi Julai mwaka huu.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati), Meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jeffa (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Leonard Mwaisabula wakielekea kwenye josho la mifugo lililopo ndani ya mnada wa awali wa Buzirayombo wakati wa ziara yake ya kukagua eneo hilo la mnada leo (19.04.2020)