Nav bar

Jumanne, 30 Machi 2021

NDAKI: TUTABORESHA SEKTA YA MIFUGO KWA KUJENGA MAJOSHO 129

 SERIKALI imesema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 imepanga kuboresha sekta ya mifungo ikiwa ni pamoja na kujenga majosho 129, ili kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, aliyasema hayo jana jijini Dodoma, wakati wizara yake ilipokuwa kiwasilisha bajeti ya sekta ya mifugo kwenye kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo, mifugo na maji.

 

Alisema, Wizara hiyo imezamilia kufanya maboresho makubwa katika sekta ya mifugo ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo na kuchangia katika pato la taifa.

 

Ndaki, alisema moja katika eneo ambalo watalifanyia kazi ni kujenga majosho 129, mapya pamoja na kukarabati yaliyopo ili kusaidia wafugaji kupata huduma hizo katika maeneo yao,

 

“Tutahakikisha kuwa tunajenga majosho kwa ajili ya kuogeshea mifugo kila eneo lenye mifugo nchini lakini pia kukarabati majosho yote yalipo ili kuwezesha wafugaji kupata huduma za ugani katika maeneo yao”alisema

 

Alisema, pia eneo jingine ambalo watalifanyia kazi ni kuboresha eneo la malisho kwa ajili ya mifugo ili kuwa na malisho ya uhakika na kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

 

“Katika hili hivi sasa tumepunguza bei ya kukodisha maeneo ya malisho kwa kukodisha kwa Sh. 3,500 kwa heka kwa mfugaji atakaye hitaji eneo la malisho”alisema

 

Vile vile, alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha wamepanga kukusanya mapato katika sekta kiasi cha Sh. bilioni 50.

 

Awali akiwasirisha bajeti ya sekta ya mifugo mbele ya katimati hiyo, Katibu Mkuu Wizara mifugo na uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel alisema itasaidia kuongeza thamani ya mifugo.

 

Alisema, katika mipango ya bajeti ijayo wamepanga kuhakikisha kuwa wanawekeza katika kuboresha afya ya mifugo,pamoja na kutafuta masoko ya mazao ya mifugo.

 

“Katika kipindi hichi tutahakikisha kuwa tunatafuta masoko katika bidhaa za mazao ya mifugo kama vile nyama, ngozi , maziwa lakini pia kuongeza fursa nyingine ya matumizi ya vitu kama kwato, pembe na manyoya”alisema

 

Aidha, alisema kuwa tayari wamepata wawekezaji kutoka nchi ya Slovakia, ambao wapenga kuja kuwekeza kiwanda cha kutengeneza mbolea kwa kutumia manyoya, pembe pamoja na kwato.

 

Hata hivyo, alitoa wito kwa wafugaji kutumia fursa ya mitamba ya kisasa iliyopo katika Ranchi za taifa kufanya uhimilishaji ili kupata mifugo iliyobora itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuongeza pato la taifa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akizungumza wakati wa uwasilishaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ya Sekta ya Mifugo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29, 2021 bungeni Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul pamoja na Viongozi na watumishi wa wizara hiyo ya Mifugo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya mwaka 2021/2022 ya Sekta ya Mifugo kwa  kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo, mifugo na maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel, akiwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2021/22 ya Sekta ya Mifugo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye ni Mbunge wa  Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka, akiwaslisha hoja wakati wa uwasilishwaji wa  Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Kipindi cha Mwaka 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya 2021/22 ya Sekta ya Mifugo leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah akiwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya mwaka 2021/22 ya Sekta ya Uvuvi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.

Baadhi ya Viongozi katika Sekta ya Uvuvi wakifuatilia uwasilishwaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya 2021/22 ya Sekta ya Uvuvi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.




Alhamisi, 18 Machi 2021

MASHAMBA DARASA YA UFUGAJI SAMAKI KUANZISHWA KOTE NCHINI

Na. Edward Kondela

 

Serikali imesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 ina mpango wa kuanzisha vituo vya ukuzaji viumbe maji katika halmashauri 80 za wilaya ikiwa na lengo la kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na kituo hicho ambacho kitatumika kama shamba darasa kwa ajili ya kufundisha wananchi namna ya kufuga samaki.

 

Akizungumza jana (17.03.2021) wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji kinachozalisha vifaranga vya samaki cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema mkakati wa serikali kupitia vituo hivyo vitakavyokuwepo katika halshamauri zote za wilaya ni kuwa na samaki wengi wafugwao kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mabwawa na kufikia uzalishaji wa samaki wa asilimia 50 kwa njia ya kufuga na asilimia 50 wanaotokana na maji ya asili.

 

“Kupitia tasnia hii ya ukuzaji viumbe maji tunataka kuweka nguvu kubwa ili tuweze kuvuna rasilimali ya uvuvi iweze kusaidia lishe, ajira na kuondoa umasikini kwa wananchi, hivyo wizara inaweka mikakati ya kuhakikisha inafikia malengo yake kupitia tasnia hii.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Aidha, Waziri Ndaki amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina mpango wa kuhakikisha inavipa uwezo mkubwa na kuvikarabati vituo vyote vya ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini ili viweze kwenda sawa na uzalishaji wa vifaranga vya samaki kulingana na mahitaji yake.

 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu wa Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka jitihada mbalimbali za kuhakikisha inazalisha kwa wingi vifaranga vya samaki pamoja na kutoa elimu juu ya ufugaji wa samaki.

 

Amesema kamati hiyo itaangalia vyema bajeti ya wizara itakayowasilishwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2021/22 ili iweze kuwa na tija na kuleta matokeo chanya hususan katika tasnia ya ufugaji samaki kwa kuwa bado ni eneo jipya ambalo watu wengi wanahitaji kujifunza na kujiingiza katika ufugaji huo.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga amesema kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, katika kutekeleza majukumu yake kati ya mwaka 2010 hadi 2020 kimetoa mafunzo kwa wananchi 11,280 kutoka mikoa mbalimbali pamoja na kuzalisha vifaranga vya samaki aina ya sato zaidi ya milioni sita vilivyosambazwa maeneo mbalimbali nchini.

 

Katika ziara hiyo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhakikisha inakiboresha kituo cha Kingolwira kwa kufanya upanuzi wa baadhi ya majengo kwa ajili ya ukuzaji viumbe maji na kuiomba wizara izidi kufanya maboresho zaidi katika maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kufuatia ushauri mbalimbali uliotolewa na wajumbe hao.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto), akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma wakati walipokuwa wakipatiwa maelezo na mmoja wa wataalamu (hayupo pichani) juu ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato, wakati kamati hiyo ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (17.03.2021)

Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ikishuhudia moja ya mabwawa ya kufugia samaki wazazi aina ya sato mara baada ya kutembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ambapo wameridhishwa na namna kituo hicho kinavyofuga samaki hao na kutaka uwepo wa samaki wazazi ambao watatoa vifaranga bora vya samaki. (17.03.2021)

Muonekano wa sehemu ya vifaranga vya samaki aina ya sato vinavyozalishwa na kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, ambavyo vimekuwa vikisambazwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini. Kifaranga kimoja cha samaki aina ya sato kinauzwa Shilingi 100. (17.03.2021)

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (wa kwanza kulia) akipatiwa maelezo ya mafanikio na mikakati ya uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga wakati kamati hiyo ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (17.03.2021)

Mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji samaki aina ya kambale ambapo kituo hicho kipo katika mikakati ya kuanza kuzalisha vifaranga vya samaki hao ili kuongeza upatikanaji wake. (17.03.2021)




Jumanne, 16 Machi 2021

WAFANYABIASHARA WAPEWA SIKU 5 KUONDOA MIFUGO KATIKA MNADA WA KIZOTA

Wafanyabiashara wa mifugo katika Mnada wa Kizota Jijini Dodoma wametakiwa kuacha kuhifadhi mifugo yao inayokwenda machinjioni katika eneo la mnada kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.

 

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul leo (16.03.2021) wakati alipotembelea mnada huo kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika ambapo pia alikutana na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo.

 

Gekul amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa zipo taratibu za uendeshaji wa Minada ya Upili ambapo mifugo ikishanunuliwa inatakiwa kuchukuliwa na sio kutuzwa hapo ikisubiri kupelekwa machinjioni.

 

“Hivyo natoa siku tano kwa wafanyabiashara wote ambao mnatunza mifugo yenu hapa mkisubiri kuipeleka machinjioni kuhakikisha mnaitoa na kuitafutia eneo jingine kwa ajili ya kuitunza,” alisema Naibu Waziri Gekul.

 

Aidha, Naibu Waziri Gekul aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa wizara imeshatenga fedha zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuanza kuboresha miundombinu ya mnada huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ukuta unaozunguka mnada huo.

 

Vilevile ametoa rai kwa wananchi kutovamia eneo la mnada, kwani moja ya sababu iliyochelewesha kuanza kwa ujenzi wa ukuta huo ni migogoro iliyotokana na uvamizi wa ardhi. Pia amewataka viongozi katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kuhakikisha wanasimamia na kuchukua hatua mapema pale wanapoona mtu anavamia maeneo haya ya minada.

 

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema kuwa timu ya wataalam inayofanya uhakiki wa eneo hilo kutokana na uvamizi itakapomaliza kazi yake watahakikisha wanalipima eneo hilo kwa haraka.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika ambapo amewapa siku tano kuhakikisha wanaiondoa mifugo yao wanayoitunza kwenye mnada huo ikisubiri kwenda kuchinjwa. (16.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na watendaji wa mnada wa kizota, viongozi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma na viongozi kutoka WMUV wakati alipotembelea mnada Kizota kukagua shughuli zinazofanyika ambapo ameagiza ujenzi wa ukuta katika mnada huo uanze haraka. (16.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akikagua miundombinu iliyopo katika Mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika. (16.03.2021)



WACHUNAJI NGOZI WASIOZINGATIA TARATIBU KUFUTIWA LESENI

Serikali imesema itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafutia leseni wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Morogoro wanaotoboa ngozi za mifugo na kuifanya kukosa thamani licha ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.

 

Akizungumza (15.3.2021) mara baada ya kufanya ziara ya kukagua uzalishaji wa ngozi bora zinazohitajika katika soko, Kaimu Mkurugenzi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura alisema licha ya kufanyika mafuzo ya uchunaji bora wa ngozi lakini bado wapo watu wanaokiuka taratibu zilizowekwa.

 

Alisema mafunzo yaliyotolewa yamesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ngozi bora lakini Serikali haitawafumbia macho baadhi ya wachunaji wa ngozi wanaoendelea kutoboa ngozi kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo hasa katika viwanda vikubwa vya ngozi vilivyoanzishwa.

 

“Tulizitoa lesei hizi kwa sheria ya ngozi namba 18 ya mwaka 2008, lakini pia tulitoa mafunzo ya uchunaji wa ngozi ili kuzipa thamani ngozi mnazozalisha lakini kuna baadhi yenu bado wanafanya makosa kwa kutoboa ngozi, sasa makosa haya yakijirudia tutawafutia leseni” alisema Bura

 

Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imejidhatiti kwa kuanzisha na kufufua viwanda nchini ikiwemo kiwanda cha ngozi cha ACE Leather cha Morogoro na kiwanda cha ngozi kilichopo Moshi, hivyo kitendo cha kuendelea kutoboa ngozi hizo ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali.

 

Aidha, aliwataka wachunaji hao kuhakikisha wanaendelea kuzingatia sheria katika utendaji wa kazi zao sambamba na kutengeneza upya leseni zao ambazo zipo ukingoni kuisha muda wake wa kipindi cha mwaka mmoja ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

 

Mkaguzi mkuu wa nyama Bw. Joseph Kupa wa  Manispaa ya Morogoro amesema kuwa pamoja na mambo mengine wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria sambamba na magonjwa ya ngozi.

 

Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya wafugaji kuendelea kupiga chapa mifugo yao jambo linalosabisha ngozi kukosa thamani huku magojwa kama Exiima na Lab Skin ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakishambulia mifugo.

 

“Changamoto tunazopata mara nyingi ni mifugo inakuja hapa ikiwa imepigwa chapa na mingine imeshambuliwa na magonjwa ya ngozi sasa ikifika hapa inakuwa tayari haina thamani hata hatuwezi kuichuna kwa sababu haiwezi kununuliwa na inatokana na baadhi ya wafugaji kutokuwa na elimu yakutosha juu ya umuhimu wa ngozi” alisema Kupa

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa wachunaji wa ngozi katika machinjio ya manispaa ya Morogoro, Mapinduzi Ernest ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa elimu waliyowapa ambayo inawasaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ngozi bora na kuiomba Serikali kufikisha elimu kwa wafugaji juu ya upigaji chapa ili kupata ngozi bora.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura (katikati) akiangalia Ngozi kwenye kiwanda cha ACE Limited kilichopo mkoani Morogoro wakati wa ziara yao mkoani humo. Kulia ni Afisa Mifugo kutoka WMUV, Bi. Mariam Muchakila na kushoto ni Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. George Obol. (15.03.2021)

Mkaguzi wa Ngozi kutoka kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. Godson Shayla (wa tatu kutoka kushoto) akitoa maelezo kwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura(wa nne kutoka kushoto) ya namna ya kuchuna Ngozi na jinsi walivyopanga kutoa adhabu kwa yoyote atakayetoboa Ngozi wakati wa kuchuna Ngozi hizo kwenye Machinjio ya Manispaa ya Morogoro. (15.03.2021)

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura ( wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Machinjio ya Manispaa ya morogoro na wachunaji wa ngozi za Mifugo mara baada ya kukagua namna yanavyofanya uchunaji kwa kuzingatia sheria na kanuni katika Machinjio Iyo mkoani Morogoro. (15.03.2021)


GEKUL AITAKA TALIRI KUJIENDESHA KIBIASHARA

Na. Elibariki Mafole, Mpwapwa

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kujiendesha kibiashara ili iweze kukabiliana na changamoto zinazo ikabili.

 

Gekul ameyasema hayo leo (15.03.2021) wakati alipo tembelea kituo cha TALIRI na LITA Mpwapwa kwa lengo la kukagua kazi zinazofanywa na taasisi hizo.

 

Katika taarifa iliyosomwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TALIRI, Dkt. Jonas Kizima ilielezea changamoto wanazokabiliana nazo zikiwemo za upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi na uhaba wa rasilimali fedha kwa shughuli za kiutafiti. Lakini pia alizungumzia mikakati waliyonayo katika kukabiliana na changamoto hizo.

 

Kwa kuwa changamoto nyingi zinahitaji fedha ili kuzitatua ndipo Naibu Waziri Gekul akawaagiza TALIRI kujipanga vizuri ili sasa waweze kujiendesha kibiashara kwani kwa kufanya hivyo wataweza kutatua changamoto walizonazo badala ya kusubiri kupata fedha kutoka Serikalini.

 

Pia amewapa miezi mitatu kuhakikisha wanawalipa vibarua wanaochunga ng'ombe pamoja na walinzi mishahara yao ya miezi sita wanayodai.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri amemshukuru Naibu Waziri kwa maamuzi yake ya kitembelea taasisi hizo na kutatua tatizo la mishahara ya vibarua na walinzi.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Bw. Jonas Kizima amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri na watakwenda kuyafanyia kazi hasa suala la taasisi hiyo kujiendesha kibiashara.

 

Katika ziara yake hiyo Wilayani Mpwapwa, pia ametembelea wilaya ya Kongwa ambapo amatembelea Ranchi ya Kongwa, shamba la malisho la mfugaji Bw. Mnyonaki lililopo katika kijiji cha Msunjilile wilayani Kongwa na Machinjio ya kuku iliyopo katika kijiji cha Mbande wilayani Kongwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Viongozi na watumishi wa TALIRI na LITA Mwapwapwa pamoja na viongozi wa Wilaya wakati alipotembelea taasisi hizo kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika. (15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na wachungaji wa ng'ombe (waliosimama kushoto) wanaomilikiwa na taasisi ya TALIRI Mpwapwa wakati alipotembelea taasisi ya TALIRI na LITA Mpwapwa kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika. Waliosimama kulia ni Viongozi kutoka Wizarani, TALIRI, LITA na Viongozi wa Wilaya ya Mpwapwa. (15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi wilayani humo.(15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Viongozi wa NARCO na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Kongwa wakati alipotembelea Ranchi ya Kongwa kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika. (15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Mama Salma Kikwete (wa kwanza kulia) katika duka la nyama kwenye Ranchi ya Kongwa wakati alipotembelea Ranchi hiyo kukagua shughuli zinazofanyika. (15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na Bw. Mnyonaki (wa kwanza kushoto) ambaye ni mfugaji na mkulima wa malisho ya Mifugo katika kijiji cha Msunjilile Wilayani Kongwa wakati alipomtembelea kwa lengo la kuona shamba lake la malisho. (15.03.2021)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kutoka kushoto) akiangalia eneo la kuchinjia kuku katika machinjio ya kuku iliyojengwa katika kijiji cha Mbande Wilayani Kongwa wakati alipoitembelea Machinjio hiyo. (15.03.2021)






Ijumaa, 12 Machi 2021

SOKO LA SAMAKI WAFUGWAO NA MAJI YA ASILI KUSHINDANISHWA

 Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali imeweka lengo la kuhakikisha Sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji samaki inazalisha idadi kubwa ya samaki sambamba na samaki wapatikanao kwenye maji ya asili.

 

Akizungumza jana (10.03.2021) alipokuwa akikagua shughuli zinazofanywa na Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri Ndaki amesema tasnia ya ufugaji samaki imekuwa na mwitikio mkubwa kwa sasa kutokana na mahitaji ya soko la samaki kuongezeka hivyo jitihada nyingi zinafanyika kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki.

 

“Kwa sasa tasnia ya ufugaji samaki imekuwa ikitoa faida kubwa kwa wanaojishulisha na ufugaji hivyo natoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kufuga samaki  na pia na toa wito kwa vituo vyetu vya ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wa samaki kwa kuwa mahitaji ya vifaranga ni mengi.” Amesema Mhe. Ndaki

 

Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itahakikisha inaendelea kuviboresha vituo hivyo kwa kuboresha miundombinu ya uzalishaji vifaranga na kupanua uwezo wake ili viweze kwenda sambamba na mahitaji ya vifaranga kwa watu wanaofuga samaki.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema wizara ipo katika hatua mbalimbali ya kupata programu maalum ya simu ya mkononi itakayoweza kutumiwa na watu wanaotaka kufahamu mambo mbalimbali kuhusu ufugaji samaki na namna ya kupata vifaranga vya samaki kutoka katika vituo ambavyo vipo chini ya wizara.

 

Pia, Dkt. Madalla amemfahamisha Waziri Ndaki uboreshaji ambao unafanyika katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Kingolwira kwa kupanua shughuli za uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato na pia kituo kipo mbioni kuanza uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina kambale.

 

Kuhusu bei ya vifaranga vya samaki amesema kwa sasa vituo vya ukuzaji viumbe maji vilivyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi vinauza kifaranga kimoja cha samaki aina ya sangara kwa Shilingi 100 na vimekuwa vikiwarahisishia wahitaji wa vifaranga kuwafikishia popote walipo bila ya ulazima wa wao kufika katika vituo hivyo. 

 

Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Vumbe Maji Kingolwira Bw. Hamady Makorwa amesema mikakati ya kituo katika kuendeleza shughuli za uzalishaji ni kufikia uzalishaji wa vifaranga 600,000 kwa mwezi hivyo kituo kinahitaji mabwawa yasiyopungua 26 na sato wazazi wasiopungua 24,000 ambapo kwa sasa wapo 5,430.

 

Amefafanua kwa sasa vifaranga vya samaki vilivyopo katika kituo hicho ni 38,000 huku tayari wamepokea maombi ya vifaranga zaidi ya 180,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika kwa mara ya kwanza katika Kituo cha Uzalishaji Viumbe Maji cha Kingolwira lengo likiwa ni kuhakikisha tasnia ya ufugaji samaki inakuwa kwa uwepo wa idadi kubwa ya upatikanaji wa vifaranga vya samaki nchini vitakavyouzwa kwa bei nafuu zaidi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla juu ya vifaranga ambavyo viko tayari kusafirishwa kwa wahitaji ambavyo vinahifadhiwa katika matanki. Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiangalia vifaranga vya samaki aina ya sato ambavyo vimezalishwa na Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, na viko tayari kwa ajili ya kusafirishwa na kuwekwa kwenye mabwawa ili kuendelea kukuzwa na hatimaye kufikia ukubwa wa samaki unaotakiwa sokoni. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati), akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla (wa kwanza kulia) na Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ukuzaji Vumbe Maji Kingolwira Bw. Hamady Makorwa (wa kwanza kushoto), wakati Waziri Ndaki akipatiwa maelezo ya namna vifaranga vya samaki vinavyozalishwa katika kituo hicho kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla akizungumza wakati wa ugeni wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira (hawapo pichani). (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) wakijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla, wakati Waziri Ndaki alipokuwa akikagua maboresho ya miundombinu ya uzalishaji vifaranga vya samaki katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kituo hicho na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki kulingana na mahitaji ya soko. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka katika wizara hiyo Dkt. Nazael Madalla (anayemfuata), namna samaki wazazi aina ya sato wanavyozalisha mayai na njia wanazotumia wataalamu kutoka mayai hayo kwenye midomo ya samaki na kuyaweka katika hatua mbalimbali ili kupata vifaranga. Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (10.03.2021)




Alhamisi, 11 Machi 2021

WAZIRI NDAKI ANUSA UBADHILIFU MNADA WA PUGU, AUONYA UONGOZI NA KUMUONDOA ASKARI KAZINI

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemtaka Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU) Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kumuondoa kazini katika mnada wa Pugu, mkuu wa zamu na wenzake kwa tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi za idadi ya mifugo inayoingia mnadani.


Waziri Ndaki amesema hayo leo (10.03.2021) jijini Dar es Salaam, mara baada ya Waziri Ndaki kutembelea mnada wa Pugu ili kukagua namna watumishi wa umma wanaofanya kazi katika mnada huo wanavyohakikisha wanasimamia vyema mapato ya serikali.


Mara baada ya kukagua vitabu vya taarifa za mifugo katika mnada huo, waziri huyo akabaini dosari katika taarifa za Kikosi Maalum cha Kuzuia Wizi wa Mifugo na kumtaka mkuu wa kikosi hicho Kanda Maalum ya Dar es Salaam Inspekta Nyangogo Justine kumuondoa katika mnada huo Sajenti Ahmad na wenzake waliokuwa zamu jana (09.03.2021) kwa tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi za idadi ya mifugo inayoingia mnadani.


Kufuatia hali hiyo Waziri Ndaki amemtaka Mkuu wa Mnada wa Pugu Bw. Kerambo Samwel pamoja na viongozi wengine wa mnada katika vitengo mbalimbali kuhakikisha wanatunza vyema kumbukumbu za shughuli za mnada na kufanya kazi kwa uadilifu.


“Wewe mkuu wa mnada nawapeni tahadhari na kumbukumbu zenu, sitaki kuja kukuta vitu vya namna hii, na wewe askari huyo mwenzako nishamwambia mkubwa wenu sitaki kumuona hapa asirudi hapa pamoja na wenzake waliokuwa kwenye zamu jana hatuwezi kufanya kazi na watu wasio waaminifu.” Amesema Waziri Ndaki.  


Kuhusu malengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kuutaka Mnada wa Pugu kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni Tatu au zaidi ifikapo Juni 30 Mwaka 2021, licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali zilizoainishwa na Mkuu wa Mnada wa Pugu Bw. Kerambo Samwel, Waziri Ndaki amesema mnada huo unaweza kukusanya mapato mengi ya serikali endapo watumishi wa mnada watafanya kazi kwa uadilifu na kwamba makadirio hayo hata yapunguza.


“Makadirio yaliyowekwa sipunguzi chochote hata nukta nataka Tarehe 30 Mwezi Juni Mwaka 2021, makusanyo yenu yawe Shilingi Bilioni Tatu au zaidi hizo sababu zingine ambazo ni nyepesi sitaki kabisa haya ndiyo maelekezo yangu kwenu kila mtu anataka hela ila iwe kwa njia ambazo ni halali.” Amefafanua Mhe. Ndaki


Aidha, akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika Mnada wa Pugu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewahakikishia kuwa serikali ipo katika hatua za kuangalia upya tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kero kwao ili kuhakikisha inawatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwemo kupunguza au kuondoa tozo ambazo ni kero.


Pia, amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha mara wanapolipa tozo mbalimbali kuhakikisha wanapatiwa risiti za kieletroniki kwa kuwa ndiyo risiti ambazo zinatambulika na kubainisha kuwa fedha iliyolipwa imeingia serikali kuu.


Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itahakikisha katika mwaka wa fedha ujao 2021/22 itakarabati miundombinu ya Mnada wa Pugu ukiwemo ujenzi wa uzio pamoja na kuhakikisha maji yanapatikana katika mnada huo baada ya wananchi kulalamikia uwepo wa lambo la kunyweshea mifugo maji ambalo limekuwa halina maji kwa muda mrefu pamoja na mifugo kutoka nje ya mnada kwa kukosekana uzio mnadani hapo.


Awali akisoma taarifa ya Mnada wa Pugu, mkuu wa mnada huo Bw. Kerambo Samwel amesema Mnada wa Pugu ndiyo mnada mkubwa nchini na unafanya kazi siku zote saba za wiki na zaidi ya saa nane kwa siku ambapo shughuli kubwa ni kukagua afya ya mifugo inayoingia kutoka mikoani, kukagua afya ya mifugo inapoondoka kwenda machinjioni na kukagua uhalali wa vibali vyote vinavyotumika kusafirisha mifugo.


Bw. Samwel amebainisha shughuli nyingine ni pamoja na kutoa vibali kwa mifugo iliyonunuliwa kwenda machinjioni na kuhakikisha kuwa maduhuli ya serikali yamelipwa, kulinda maeneo ya mnada ikiwemo mipaka ya mnada na miundombinu ya mnada pamoja na kusimamia shughuli zote za biashara ya mifugo pamoja na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wa mifugo wana leseni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akikagua vitabu vya taarifa za mifugo inayoingia na kutoka katika Mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam. Aliyesimama kushoto ni mkuu wa mnada Bw. Kerambo Samwel na askari wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo katika mnada huo Sajenti Kasegezya. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akikagua miundombinu na shughuli mbalimbali katika Mnada wa Pugu jijini Dar es Salaam, ambapo ameahidi kuwa wizara itaufanyia ukarabati mnada huo katika mwaka ujao wa fedha 2021/22. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kutoka kulia) akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika Mnada wa Pugu jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua miundombinu ya mnada huo na kuwaarifu kuwa wizara inaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara hao kwa kuondoa tozo zenye kero. (10.03.2021)




TANGAZO


 

TAARIFA ZA UTEKELEZAJI MIFUGO, UVUVI ZATINGA BUNGENI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo  imewasilisha taarifa zake za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopo (2020/2021) na mikakati iliyojiwekea katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka ujao wa fedha (2021/2022) mbele ya kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.

 

Sekta ya Mifugo ndio ilikuwa ya kwanza kuwasilisha taarifa yake ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel alibainisha kuwa sekta yake iliidhinishiwa kiasi cha Shilingi bilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa fedha uliopo likiwa ni ongezeko la takribani asilimia 60 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita (2019/2020) ambapo sekta hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi 3.

 

“Mhe. Mwenyekiti fedha hiyo ndo tumeitumia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majosho 20 yaliyojengwa katika Halmashauri mbalimbali za wilaya, kujenga kliniki na maabara 10 za mifugo ambazo zitagharimu shilingi milioni 700 na tayari mchakato wa kuhamisha fedha umeshaanza” Amesema Prof. Ole Gabriel.

 

Prof. Ole Gabriel ameieleza kamati kuwa uwepo wa kliniki na maabara za mifugo utawasaidia wafugaji kupata huduma bora za afya ya mifugo kwenye maeneo yao na kuondokana na hali iliyopo hivi sasa ambapo wafugaji wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma hiyo huku pia akielezea namna Sekta hiyo ilivyofanikiwa kujenga mabwawa ya kisasa ya kunyweshea mifugo ya Kimokouwa lililopo wilayani Longido, Narakauo lililopo wilayani Simanjiro na Chamakweza lililopo wilayani Chalinze. .

 

“Lakini pia Mhe. Mwenyekiti tunaendelea na Ujenzi wa Kiwanda cha kuzalisha chanjo pale Kibaha ambacho mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 90 na fedha iliyotumika ni shilingi milioni 213 kati ya shilingi milioni 600 zilizotengwa na tayari vifaa vya maabara vimeshanunuliwa” Ameongeza Prof. Ole Gabriel.

 

Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walipata fursa ya kuchangia mambo mbalimbali yaliyopo kwenye taarifa hiyo ambapo Mbunge wa Viti Maalum (Manyara) Mhe. Yustina Rahhi aliishauri sekta hiyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa maafisa ugani hasa kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ambako ndipo wanapopatikana wafugaji wengi ushauri ambao Prof. Ole Gabriel aliupokea na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kukabiliana na changamoto hiyo.

 

Kwa upande wa taarifa ya sekta ya uvuvi iliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo, Jumla ya shilingi bilioni 13 zilitengwa ambazo zinajumuisha shilingi bilioni 6 zinazotokana na fedha za ndani na shilingi bilioni 7 zinazotokana na fedha za nje.

 

Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi wa Sera na Mipango (Uvuvi) Dkt. Andrew Komba amesema kuwa sekta hiyo mpaka sasa imetekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ujenzi na ukarabati wa mialo 13  ya kisasa ya kupokelea samaki, kuboresha masoko matatu ya samaki na  vituo vitano vya ukuzaji viumbe maji.

 

“Mhe. Mwenyekiti, Ujenzi wa bandari ya Uvuvi upo katika hatua za awali za upembuzi yakinifu lakini pia baada ya Serikali kuamua kutobinafsisha shirika la TAFICO tayari Serikali imeshaanza ukarabati wa miundombinu ya Shirika hilo” Amesema Dkt. Komba.

 

Aidha Dkt. Komba ameiambia kamati kuwa Sekta yake  ilipokea fedha za mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Uvuvi kusini mwa bahari ya Hindi (Swiofish) ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo (bilioni 6) zimetekeleza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba 3 za wafanyakazi mkoani Tanga na ujenzi wa maabara ya kisasa ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) iliyopo Kunduchi jijini Dar-es-salaam.

 

“Mhe. Mwenyekiti, hata hivyo kutokana na changamoto ya kutokuwepo kwa vituo vya kutosha vya ukuzaji viumbe maji, tumeanza mchakato wa ujenzi wa kituo kikubwa cha Ukuzaji viumbe maji pale Kunduchi ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo na kwa sasa ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na tayari Wakala wa Majengo nchini (TBA) wameshaanza kazi ya kusanifu miundombinu ya kituo hicho  kisha wao ndio watasimamia ujenzi huo” Amesema Dkt. Komba.

 

Akihitimisha taarifa zilizowasilishwa na sekta zote mbili (Mifugo na Uvuvi), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul mbali na kuishukuru kamati hiyo kwa maoni na mchango walioutoa wakati wa uwasilishwaji, ameahidi kufanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na wajumbe wa kamati ambapo aliwaomba kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwenye Wizara yake ili iendelee kuboresha sekta hizo hapa nchini.

 

“Hivi karibuni Mhe. Waziri aliagiza wapangaji waliokodisha vitalu afu hawavitumii wanyang’anywe vitalu hivyo ili wapewe wafugaji wengine wenye mahitaji navyo na huu ndo msimamo wa Wizara kwa sasa kwa hiyo waheshimiwa wajumbe wa kamati, ninawahakikishia Wizara yetu itaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ambayo awali yalikuwa ni changamoto kwa wafugaji au wavuvi” Amehitimisha Mhe. Gekul.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akifafanua moja ya hoja zilizowasilishwa na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Wizara yake kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na sekta yake kwa mwaka huu wa fedha (2020/2021) mbele ya kamati ya Kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji leo (09.03.2021) kwenye moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango (Uvuvi) Dkt. Andrew Komba akiwasilisha taarifa ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na sekta yake kwa mwaka huu wa fedha (2020/2021) mbele ya kamati ya Kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji leo (09.03.2021) kwenye moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.

Baadhi ya Watendaji wa Sekta ya Uvuvi wakifuatilia michango inayotolewa na wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya Sekta za Mifugo na Uvuvi kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.


Baadhi ya Watendaji wa Sekta ya Mifugo  wakifuatilia michango inayotolewa na wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji muda mfupi baada ya Sekta za Mifugo na Uvuvi kuwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa huu fedha (2020/2021) leo (09.03.2021) katika moja ya kumbi za bunge jijini Dodoma.