Nav bar

Alhamisi, 11 Machi 2021

WAZIRI NDAKI ANUSA UBADHILIFU MNADA WA PUGU, AUONYA UONGOZI NA KUMUONDOA ASKARI KAZINI

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemtaka Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Wizi wa Mifugo (STPU) Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kumuondoa kazini katika mnada wa Pugu, mkuu wa zamu na wenzake kwa tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi za idadi ya mifugo inayoingia mnadani.


Waziri Ndaki amesema hayo leo (10.03.2021) jijini Dar es Salaam, mara baada ya Waziri Ndaki kutembelea mnada wa Pugu ili kukagua namna watumishi wa umma wanaofanya kazi katika mnada huo wanavyohakikisha wanasimamia vyema mapato ya serikali.


Mara baada ya kukagua vitabu vya taarifa za mifugo katika mnada huo, waziri huyo akabaini dosari katika taarifa za Kikosi Maalum cha Kuzuia Wizi wa Mifugo na kumtaka mkuu wa kikosi hicho Kanda Maalum ya Dar es Salaam Inspekta Nyangogo Justine kumuondoa katika mnada huo Sajenti Ahmad na wenzake waliokuwa zamu jana (09.03.2021) kwa tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi za idadi ya mifugo inayoingia mnadani.


Kufuatia hali hiyo Waziri Ndaki amemtaka Mkuu wa Mnada wa Pugu Bw. Kerambo Samwel pamoja na viongozi wengine wa mnada katika vitengo mbalimbali kuhakikisha wanatunza vyema kumbukumbu za shughuli za mnada na kufanya kazi kwa uadilifu.


“Wewe mkuu wa mnada nawapeni tahadhari na kumbukumbu zenu, sitaki kuja kukuta vitu vya namna hii, na wewe askari huyo mwenzako nishamwambia mkubwa wenu sitaki kumuona hapa asirudi hapa pamoja na wenzake waliokuwa kwenye zamu jana hatuwezi kufanya kazi na watu wasio waaminifu.” Amesema Waziri Ndaki.  


Kuhusu malengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kuutaka Mnada wa Pugu kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni Tatu au zaidi ifikapo Juni 30 Mwaka 2021, licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali zilizoainishwa na Mkuu wa Mnada wa Pugu Bw. Kerambo Samwel, Waziri Ndaki amesema mnada huo unaweza kukusanya mapato mengi ya serikali endapo watumishi wa mnada watafanya kazi kwa uadilifu na kwamba makadirio hayo hata yapunguza.


“Makadirio yaliyowekwa sipunguzi chochote hata nukta nataka Tarehe 30 Mwezi Juni Mwaka 2021, makusanyo yenu yawe Shilingi Bilioni Tatu au zaidi hizo sababu zingine ambazo ni nyepesi sitaki kabisa haya ndiyo maelekezo yangu kwenu kila mtu anataka hela ila iwe kwa njia ambazo ni halali.” Amefafanua Mhe. Ndaki


Aidha, akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika Mnada wa Pugu, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewahakikishia kuwa serikali ipo katika hatua za kuangalia upya tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kero kwao ili kuhakikisha inawatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwemo kupunguza au kuondoa tozo ambazo ni kero.


Pia, amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha mara wanapolipa tozo mbalimbali kuhakikisha wanapatiwa risiti za kieletroniki kwa kuwa ndiyo risiti ambazo zinatambulika na kubainisha kuwa fedha iliyolipwa imeingia serikali kuu.


Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itahakikisha katika mwaka wa fedha ujao 2021/22 itakarabati miundombinu ya Mnada wa Pugu ukiwemo ujenzi wa uzio pamoja na kuhakikisha maji yanapatikana katika mnada huo baada ya wananchi kulalamikia uwepo wa lambo la kunyweshea mifugo maji ambalo limekuwa halina maji kwa muda mrefu pamoja na mifugo kutoka nje ya mnada kwa kukosekana uzio mnadani hapo.


Awali akisoma taarifa ya Mnada wa Pugu, mkuu wa mnada huo Bw. Kerambo Samwel amesema Mnada wa Pugu ndiyo mnada mkubwa nchini na unafanya kazi siku zote saba za wiki na zaidi ya saa nane kwa siku ambapo shughuli kubwa ni kukagua afya ya mifugo inayoingia kutoka mikoani, kukagua afya ya mifugo inapoondoka kwenda machinjioni na kukagua uhalali wa vibali vyote vinavyotumika kusafirisha mifugo.


Bw. Samwel amebainisha shughuli nyingine ni pamoja na kutoa vibali kwa mifugo iliyonunuliwa kwenda machinjioni na kuhakikisha kuwa maduhuli ya serikali yamelipwa, kulinda maeneo ya mnada ikiwemo mipaka ya mnada na miundombinu ya mnada pamoja na kusimamia shughuli zote za biashara ya mifugo pamoja na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wa mifugo wana leseni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akikagua vitabu vya taarifa za mifugo inayoingia na kutoka katika Mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam. Aliyesimama kushoto ni mkuu wa mnada Bw. Kerambo Samwel na askari wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo katika mnada huo Sajenti Kasegezya. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akikagua miundombinu na shughuli mbalimbali katika Mnada wa Pugu jijini Dar es Salaam, ambapo ameahidi kuwa wizara itaufanyia ukarabati mnada huo katika mwaka ujao wa fedha 2021/22. (10.03.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kutoka kulia) akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika Mnada wa Pugu jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua miundombinu ya mnada huo na kuwaarifu kuwa wizara inaendelea kuboresha mazingira ya wafanyabiashara hao kwa kuondoa tozo zenye kero. (10.03.2021)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni