Nav bar

Jumatatu, 11 Novemba 2019

CHANGAMOTO ZA ZAO LA MWANI ZATAFUTIWA UFUMBUZI
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah jana (09.11.2019) amekutana na wabunge wa majimbo ya Ukanda wa Pwani jijini Dodoma kujadili jinsi ya kuendeleza na kuimarisha kilimo na biashara ya zao la mwani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo Katibu Mkuu Dkt. Tamatamah amesema zao la mwani limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wafugaji wadogo wadogo wa maeneo ambayo hapo awali walikuwa wakifanya shughuli za uvuvi na kilimo.

Aidha amesema baada ya mafanikio kuonekana kwenye ukuaji wa zao la mwani kampuni nyingi zimeanza biashara ya kulima na kusafirisha zao hilo nchi za nje.

Pamoja na hayo, imeelezwa kuwa kutokana na changamoto mbalimbali uzalishaji umeshuka na Tanzania sasa hivi ni nchi ya tatu, katika uzalishaji ambao umeshuka hadi kufikia tani 918 kwa mwaka 2018/2019 ukilinganisha na wastani wa tani 1,395 kwa mwaka 2017/2018, tani 1,197 kwa mwaka 2016/2017 na tani 1,500 kwa miaka ya 2000.

Aidha ametoa sababu za kushuka kwa uzalishaji wa zao la mwani ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ukosefu wa mitaji na wawekezaji makini, ununuzi wa mwani usiofuata utaratibu na kuleta migogoro baina ya wawekezaji na wazalishaji na kutokuwepo kwa soko la ndani.

Dkt. Tamatamah amewataka wabunge hao kutoka Ukanda wa Pwani kutoa maoni yatakayohakikisha biashara ya zao la mwani inafanyika kikamilifu kwa amani, uaminifu na kufuata sheria zilizopo ili wadau wote wanaojishughulisha kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo waweze kunufaika.

”Kwa upande wa serikali kupitia Wizara yetu tumechukua hatua mbalimbali kufanya tafiti zinazopunguza changamoto zilizopo na kuwajengea uwezo wakulima ikiwemo fursa za mikopo na kuongeza kasi kuwatafutia soko na kuona wakulima wa mwani wanaongeza kiwango cha ulimaji na uwezo wa ubunifu.” Amesema Dkt. Tamatamah.

Aidha amefafanua kuanzishwa kwa Dawati la Sekta Binafsi kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwakutanisha wakulima na wafugaji wadogo wadogo na taasisi za kifedha na imefanya vizuri na sasa kujikita zaidi kwenye zao la mwani.Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah akielezea umuhimu na faida za zao la mwani kwa namna ambayo limekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wafugaji wadogo wadogo wakati akifungua warsha ya wabunge kutoka ukanda wa Pwani kwenye ukumbi wa NBC jijini Dodoma ili zao hili liweze changia zaidi pato la Taifa. (09/11/2019Baadhi ya wabunge na wawakilishi wa wabunge kutoka katika ukanda wa Pwani wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Uvuvi ) Dkt. Rashid Tamatamah ( hayupo pichani) wakati akifungua warsha ya kujadili namna ya kuendeleza na kuimarisha kilimo na biashara ya zao la mwani katika ukumbi wa NBC jijini Dodoma. (9/11/2019)
Jumanne, 29 Oktoba 2019

VIWANDA VINAVYOTUMIA MALIGHAFI ZA MIFUGO KUTAMBULIWA ILI KUFIKIA UCHUMI WA KATISerikali imewataka maafisa mifugo wote nchini katika maeneo yao ya kazi kufuatilia idadi ya viwanda vinavyotumia malighafi ya mifugo ambavyo vinafanya kazi pamoja na ambavyo havifanyi kazi kufahamu changamoto zake ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi na viwanda hivyo vianze kufanya kazi kuendana na azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda Mwaka 2025.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha hayo jana (27.10.2019) katika Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo cha Rotiana Social Investment ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na baadhi ya mitambo yake kuharibika na vifaa vingine kudaiwa kuibiwa na baadhi ya watu waliokuwa wakikisimamia kiwanda hicho.

Prof. Gabriel amesema lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha inasimamia vyema azma ya serikali kuhakikisha viwanda vya malighafi za mifugo vinafanya kazi na kutaka maafisa hao wa mifugo kushirikiana na maafisa kutoka Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) katika kubaini changamoto mbalimbali zinazovikabili viwanda hivyo.

“Kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Manyara umuliki wa mitambo lazima uweze kufahamika kisheria umekaaje na kuhakikisha viwanda ambavyo vimekuwa vikichakata mazao ya mifugo vinafanya kazi ili mnyororo wa mazao ya mifugo uendelee kufanya kazi na kufikia uchumi wa kati 2025 kupitia viwanda.” Amesema Prof. Gabriel

Kuhusu kiwanda cha Rotiana Social Investment chenye eneo la Hekari 12,500 Prof. Gabriel ameutaka uongozi wa Mkoa wa Manyara kuendelea kufuatilia kwa kina umiliki wa ardhi wa eneo hilo kisheria kutokana na kiwanda hicho kutekelezwa baada ya kuibuliwa na Taasisi ya Ilaramatak Lorkornei na Stitching Her Groen Wout ya nchini Uholanzi na kufunguliwa kiwanda mwaka 2011 ambapo kwa sasa hakifanyi kazi.

Kiwanda hicho ambacho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe zaidi ya 300 kwa siku na pamoja na mifugo mingine wakiwemo mbuzi katibu mkuu huyo ametaka pia uongozi wa Mkoa wa Manayara kufuatilia kwa kina umiliki wa mitambo hiyo kisheria na hatimaye kiwanda hicho kiweze kufanya kazi baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Bibi Mary Kisyoki ambaye amewahi kuwa mmoja wa viongozi wa Shamba la Rotiana linalomiliki kiwanda cha Rotiana Social Invetment ameshukuru uongozi wa Mkoa wa Manyara na TCCIA katika kufuatilia kiwanda hicho kilichotelekezwa ambapo amesema kupitia serikali ya awamu ya tano ataendelea kusimamia ukweli ambao amekuwa akiusimamia katika kulinda mali za kiwanda hicho zinasimamiwa vyema na hatimaye kiweze kufanya kazi.

Amesema katika kipindi chote mara baada ya kiwanda hicho kusimama kufanya kazi amekuwa akihakikisha mali za kiwanda hazizidi kuibiwa au kuharibiwa na baadhi ya watu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Manyara Bibi Mwanahamisi Hussein ametoa wito kwa makatibu wenzake wa mikoa na wilaya kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali na sekta binafsi na kujikita kuangalia fursa na changamtoto zilizopo ili kuweza kuzitatua zikiwemo za wafugaji na kuhakikisha jamii inapata faida kutokana na yale wanayosimamia.

Aidha ameishuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweza kufuatialia masuala mbalimbali kwa kuweza kufanyia kazi yale ambayo yamekuwa yakifikishwa katika wizara hiyo likiwemo la kutekelezwa kwa kiwanda cha Rotiana Social Investmant suala ambalo amekuwa akilisimamia ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafahamika umiliki wake na hatimaye kiweze kufanya kazi.


Sehemu ya kuhifadhia nyama baada ya mifugo kuchinjwa kwenye kiwanda cha Rotiana Social Investment kilichopo Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ambacho kwa sasa hakifanyi kazi baada ya kutelekezwa.(27/10/2019 

katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akizungumza  na baadhi ya viongozi alioambatana nao kukagua kiwanda cha Rotiana Social Investment baada ya kutelekezwa. (27/10/2019)

SERIKALI YAELEKEZA KUKAMILIKA KWA UJENZI WA KIWANDA ILI KUKUZA SOKO LA MIFUGO NCHINI


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameuelekeza uongozi unaosimamia ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kinachojengwa katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa kiwanda hicho mapema mwanzoni mwa mwaka 2020 ili kiweze kuleta tija kwa taifa na wafugaji wanaoishi katika Mkoa wa Arusha, mikoa ya jirani na nchi ya jirani ya Kenya.

Prof. Gabriel amesema hayo jana (24.10.2019) mara baada ya kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho akiwa pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido na kukuta tayari ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 90 ambapo mitambo mbalimbali imeanza kufungwa katika kiwanda ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 kwa siku na mbuzi takriban Elfu Mbili kwa siku.

Katibu mkuu huyo ametoa wito kwa wadau wa mifugo kujipanga vizuri namna ya kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho ili wafugaji na wafanyabiashara waweze kuuza mifugo katika kiwanda hicho ambacho kitaongeza ajira na kukuza sekta ya mifugo nchini.

Awali akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Longido kabla ya kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea maoni ya namna ya kudhibiti vitendo vya kutorosha mifugo mipakani hali inayochangia kuikosesha serikali mapato ambapo elimu imesisitizwa kwa watu wanaoishi mipakani.

Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inazidi kuchukua maoni ya namna ya kuhakikisha vitendo vya utoroshaji wa mifugo hususan katika mpaka wa Namanga ambao ni kati ya mipaka ya nchi za Tanzania na Kenya vinadhibitiwa ili kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei pamoja na kusimamia viwanda vya kusindika nyama kikiwemo cha Eliya kinachotarajia kukamilika mapema mwaka 2020 kinapata mifugo ya kutosha kutoka Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani ili kusindika nyama katika kiwanda hicho.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kinachojengwa katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 na mbuzi takriban Elfu Mbili kwa siku. Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kukamilika Mwezi Februari Mwaka 2020 ambapo kwa sasa ujenzi umekamilika kwa Asilimia 90. (24.10.2019)


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoani Arusha pamoja na jeshi la polisi nchini mara baada ya kikao cha namna ya kudhibiti utoroshaji wa mifugo katika mpaka wa Namanga uliopo katika wilaya hiyo ambao ni moja ya mipaka kati ya Tanzania na Kenya. (24.10.2019)

 

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Bw. Jumaa Mhina mara baada ya kuhitimisha kikao cha namna ya kudhibiti utoroshaji wa mifugo katika mpaka wa Namanga. (24.10.2019)

 

NAIBU WAZIRI ULEGA AHUDHURIA MKUTANO WA MAWAZIRI WA AU MJINI ADDIS ABABANaibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega yuko nchini Ethiopia ambapo anahudhuria mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wanaohusika na Kilimo, mifugo, uvuvi, mazingira, maji na Maendeleo Vijijini.

Mkutano huo ulioitishwa na Kamisheni ya Afrika kupitia Shirika lake la kusimamia Maendeleo ya Rasilimali za Wanyama Barani Afrika (AU-IBAR), unafanyika kwa siku mbili mjini Addis Ababa ambapo mbali na mambo mengine mkutano huo utapokea ripoti na maazimio mbalimbali kutoka kwa wataalam wa sekta hizo kujadili na kuyapitisha ili waweze kupeleka Halmadhauri Kuu ya AU kwa maamuzi na utekezaji.

Moja ya mikakati, ripoti na maazimio na mapendekezo yanayotarajiwa kujadiliwa na kuridhiwa na baraza hilo la mawaziri wa AU wa sekta ya mifugo, uvuvi, kilimo, mazingira na maji ni;
1. Ripoti ya miaka miwili ya Tathmni ya Azimio la Malabo (Malabo Declaration) lenye lengo la kuondoa njaa katika bara ka Afrika ifikapo Mwaka 2025.

2. Ripoti ya Tathnimi ya kuwasiliana na Majanga ya asili kama mafuriko na ukame.

3. Ripoti ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi.

4. Juhudi za nchi wanachama kuzuia matumizi ya bidhaa za plastiki.

5. Mkakati wa kupanda mazao yenye viini lishe vya kutosha.
6. Mkakati wa kukabiliana na upotevu wa mazao ya mimea na samaki baada ya kufunga (Post harvest Loss)

7. Mkakati wa kupambana na magonjwa na vimelea sugu kwa mifugo.

8. Mpango wa kuanzisha maabara za kupima ubora wa chakula katika bara la Afrika.

9. Mpango wa pamoja wa kuwa na kusimamia na kuweza katika wazo la uchumi wa bahari (Blue economy).

10. Mpango mkakati wa miaka 10 kuendeleza uvuvi mdogo mdogo (small scale fisheries)

11. Mpango mkakati wa miaka 10 wa kuendeleza sekta ya ukuzaji viumbe maji.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mheshimiwa balozi Bi. Josefa Correia Sacko-mkuu wa Kamisheni ya Afrika ya Kilimo na maendeleo vijijini, ambapo zaidi ya washiriki 300 kutoka nchi 49 za bara la Afrika wanahudhuria wakiwepo wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kama FAO, WWF, Benki ya Dunia na NEPAD.Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akifuatilia hoja mbalimbali katika kikao kinachoendelea Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.


Naibu Waziri wa Mifugo Mhe. Abdallah Hamis Ulega akijadili jambo na baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo kutoka Tanzania:  Kutoka kushoto: Pamela (Afisa Kitengo cha Hali ya HewaAU-IBAR Ethiopia, Dkt. Claude John Mosha, Mkurugenzi Mstaafu Usalama wa Chakula-TBS,  na Dkt. Paul Onyango Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Uvuvi