Nav bar

Jumanne, 26 Januari 2021

MAUAJI YA MKULIMA YAWE MWANZO NA MWISHO, FUATENI SHERIA, WAZIRI MKUU KITETO IKO SALAMA." WAZIRI NDAKI

Na. Edward Kondela


Serikali imewataka wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye maeneo wasiyoruhusiwa, kuondoka mara moja na kuwataka wafuate sheria, taratibu na kanuni za nchi ambapo wakulima na wafugaji wanatakiwa kuwa kwenye maeneo waliyotengewa kisheria bila kuingiliana.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo (24.01.2021) akiwa katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara kutatua mgogoro wa matumizi ya ardhi uliojitokeza hivi karibuni kati ya wakulima na wafugaji katika ukanda wa malisho ya mifugo wa vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri, mgogoro ambao umesababisha kifo cha mkulima Bw. Emelian Malima miaka 45 anayedaiwa kuuwawa na wafugaji (20.01.2021) katika eneo la ukanda wa malisho ya mifugo.


Akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika vijiji hivyo, Waziri Ndaki amesema serikali imekuwa ikitenga matumizi bora ya ardhi maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Kiteto na kwamba maeneo ya wakulima yametengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo pekee na maeneo ya wafugaji yametengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo  na wote wanalindwa na sheria. 


“Wilaya ya Kiteto ilishatenga maeneo ya wakulima na wafugaji na maeneo hayo ya wafugaji wanakaa wafugaji na mifugo yao na maeneo ya wakulima wanakaa wakulima na kulima mazao yao, hakuna mtu anayeruhusiwa kuingilia eneo la wenzake sisi wakulima haturuhusiwi kuingilia maeneo ya wafugaji na wafugaji haturuhusiwi kuingilia maeneo ya wakulima.” Amesema Waziri Ndaki


Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Wilayani Kiteto ambayo Waziri Wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefuatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Manyara ikiongozwa na mkuu wa mkoa huo Mhe. Joseph Mkirikiti, Waziri Ndaki amewataka wakulima walioingilia eneo la malisho ya mifugo katika vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri vilivyopo kata za Loolera na Lengatei na kufanya shughuli za kilimo watoke eneo hilo kwa kuwa wanachangia migogoro inayotokana na wakulima hao kuingilia eneo la malisho.     


Kuhusu kifo cha mkulima Bw. Emelian Malima miaka 45 anayedaiwa kuuwawa na wafugaji katika eneo hilo la malisho, Waziri Ndaki ametaka tukio hilo liwe la kwanza na mwisho na kumhakikisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Wilaya ya Kiteto iko salama na itaendelea kuwa salama.


“Hicho kifo tulichokisikia ni cha kwanza na mwisho hatutamtetea mtu na ndiyo maana watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa na mahakama itatenda haki pia ninamhakikishia Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyenielekeza kuja hapa kuwa Wilaya ya Kiteto iko salama.” Amesema Mhe. Ndaki


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti amewataka wakulima kuheshimu amri ya mahakama kwa kuacha kulima kwenye ukanda wa malisho katika Wilaya ya Kiteto, kwa kuwa wamekuwa wakirudi na kukutwa na hatia huku wakiiomba mahakama kuwaruhusu waondoke baada ya kuvuna jambo ambalo limekuwa likijirudia mara kwa mara.


Aidha, amesema uongozi wa kijiji ndiyo wenye mamlaka kupitia mkutano mkuu kugawa maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya kilimo na kubainisha amekuwa akipewa taarifa na baadhi ya wakulima kuwa wamegaiwa maeneo na wenyeviti wa vijiji ambao wamekuwa hawafuati utaratibu ambapo Mhe. Mkirikiti amewataka watu wote ambao wamepewa maeneo ya kilimo kinyume na utaratibu kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ili kujua hatma yao na kutaka viongozi waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.


Pia, amepiga marufuku baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uwakala wa ardhi katika Wilaya ya Kiteto na kuwauzia watu wanaotoka nje ya wilaya hiyo maeneo ya malisho ya mifugo kwa kuwadanganya kuwa ni maeneo ya kilimo.


Baadhi ya wananchi waliopatiwa nafasi kuzungumza katika mkutano huo wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti na wananchi wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa malisho Wilayani Kiteto, wamesema mgogoro uliojitokeza kati ya wakulima na wafugaji unatokana na ukinzani wa baadhi ya vijiji kuingiliana na kila kijiji kuainisha matumizi tofauti ya ardhi ya kijiji.


Katika kuhakikisha wanaendeleza shughuli za kilimo Katika Wilaya ya Kiteto, uongozi wa Mkoa wa Manyara na wilaya hiyo umeainisha nia yao ya kuwatafutia maeneo ya kilimo na kuacha kufanya shughuli za kilimo katika ukanda wa malisho ya mifugo kwenye vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri vilivyopo Kata za Loolera na Lengatei.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Joseph Mkirikiti (aliyevaa kofia nyeusi) akifafanua jambo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama upande wake wa kulia) juu ya mgogoro wa matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji katika ukanda wa malisho uliyopo Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara. (24.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa malisho ya mifugo katika vijiji vya Amei, Loolera, Lesoit na Lembapuri vilivyopo kata za Loolera na Lengatei kwenye Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, ambapo Waziri Ndaki amewataka wakulima kuondoka katika ukanda huo.  (24.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiangalia mazao yaliyopo kwenye shamba la mmoja wa wakulima waliovamia maeneo ya ukanda wa malisho ya mifugo katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, hali mbayo imekuwa ikisababisha mgogoro wa matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. (24.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyenyoosha mkono) akiwa katika eneo ambalo inadaiwa wafugaji walimuua Bw. Emelian Malima miaka 45 ambaye alikuwa akifanya shughuli za kilimo katika ukanda wa malisho ya mifugo katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, ambapo Waziri Ndaki amechukizwa na kitendo hicho cha wananchi kujichukulia sheria mkononi na kutaka iwe mwanzo na mwisho. (24.01.2021)


NGURUWE WENYE THAMANI YA MILIONI 370 WAMEKUFA KWA HOMA, SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUDHIBITI

Na Mbaraka Kambona,


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioikumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivi karibuni unadhibitiwa, huku akisema kuwa tangu ugonjwa huo uanze mpaka sasa umeshasababisha vifo vya Nguruwe 1500 wenye thamani ya shilingi milioni 375.


Ndaki aliyasema hayo Januari 23, 2021 jijini Dodoma alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuudhibiti ugonjwa huo uliokumba Mikoa ya Kanda ya Ziwa. 


Alisema kuwa vifo hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja kwa wafugaji kwa sababu kipato hicho kilichopotea ilikuwa wakipate wafugaji huku akiwataka wafugaji hao kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya serikali ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa kwa haraka.


Aliongeza kuwa  ugonjwa huo unaosababishwa na virusi unahama kutoka kwa nguruwe pori na  Ngiri na unasambaa kupitia  njia ya Maji, Damu au Kinyesi.


Ndaki alisema kuwa Halmashauri zilizoathirika mpaka sasa ni Mbogwe, Kyerwa, Geita, Sengerema, Kahama na Misungwi na alibainisha kuwa serikali imeshachukua hatua kadhaa za kudhibiti ugonjwa huo.


Alisema kuwa mpaka sasa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ikiwemo kuweka karantini za mifugo hiyo ili kudhibiti ugonjwa huo usisambae zaidi.


“Tumeongeza Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Wataalamu kutoka Chuo cha Sokoine (SUA) na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwenda kuungana na wataalamu wa Halmashauri ili kuongeza nguvu ya kudhibiti ugonjwa huo,” alisema Ndaki

Ndaki alisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha wanazingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu ikiwemo kupulizia dawa za kuua wadudu Kupe katika mabanda ili kuzuia ugonjwa huo usisambae zaidi.


“Niwaombe wananchi waache kula nyama ya Nguruwe, hatua hizi tunazochukua lengo lake ni kudhibiti ugonjwa usiendelee kuleta madhara zaidi katika maeneo mengine,”alisema Ndaki


Aidha, Ndaki amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi katika maeneo yaliyoathirika kuhakikikisha wanasimamia kikamilifu karantini zilizowekwa na wataalamu ili ugonjwa huo kuzuiwa kusambaa katika maeneo mengine  huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili hatua hizo zinazochukuliwa na serikali ziweze kuzaa matunda.


Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga alisema kuwa ili ugonjwa huo usisambae zaidi ni muhimu wafugaji kuhakikisha kuwa mifugo yao inakuwa katika mabanda wakati wote na kuacha kusafirisha mifugo na mazao yake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kabla ya kupimwa na Daktari. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)  kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti ugonjwa wa homa ya Nguruwe kwenye Mkutano uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakichukua matukio katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (hayupo pichani) kuhusu ugonjwa wa homa ya Nguruwe uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga (kushoto) akifafanua jambo kwa  Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ugonjwa wa homa ya Nguruwe katika Mkutano uliofanyika jijini Dodoma Januari 23, 2021. Kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.


MWONGOZO WA UTOAJI WA CHANJO ZA MIFUGO NCHINI WAZINDULIWA, KULINDA AFYA YA MNYAMA

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amezindua mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, wenye lengo la kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama.


Waziri Ndaki amebainisha hayo (22.01.2021) jijini Dodoma wakati akizindua mwongozo huo baada ya hivi karibuni kuagiza kusimamishwa kwa muda, utoaji wa chanjo unaofanywa na halmashauri nchini kupitia kampuni walizoingia nazo mikataba, baada ya kubaini chanjo kutolewa kiholela kwa mifugo bila kuwepo utaratibu sahihi na kusababisha madhara kwa mifugo na hasara kwa mfugaji.


Kufuatia hali hiyo, Waziri Ndaki amesema katika kuhakikisha mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, unakuwa na tija kwa taifa ametaka kuwepo kwa haki na wajibu kwa wadau wote wa mifugo ili kuelewa vyema haki na wajibu huo katika kusimamia mwongozo huo na kufikia matokeo chanya katika kuboresha afya ya mifugo. 


“Mambo ya msingi kabisa kwenye jambo hili ni afya ya mifugo, afya ya mifugo ilikuwa hatarini ni kweli utaratibu wanafanya halmashauri lakini hauko wazi sana, ndiyo maana tukasema sasa ni muhimu kuwa na mwongozo huu kutuelekeza nini cha kufanya, chanjo ikifanywa vizuri kwa usahihi bila makosa tuliyokuwa tunayaona tunaweza kuwa na ng’ombe wenye afya bora na njema.” Amesema Waziri Ndaki


Aidha, amesema mwongozo huo ambao umeshirikisha wadau zaidi ya thelathini wakati wa kuundaa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kupokea maoni ya wadau sehemu ambazo mwongozo utaonekana kuwa na mapungufu ili kuurekebisha na kuufanya uwe bora zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha afya ya mifugo nchini inalindwa na mfugaji kutopata hasara ya mifugo yake kufa au kupata madhara mengine yoyote baada ya kuchanjwa.


Katika kuhakikisha kuwa serikali inaendeleza mahusiano mazuri na sekta binafsi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema wizara itahakikisha inaandaa mazingira mazuri ya kuwa pamoja na sekta binafsi ili kufanya kazi pamoja ambayo itakuwa na tija kwa taifa na wafugaji kwa ujumla.


“Sekta binafsi nipende kuwahakikishieni kwamba sisi tutafanya kazi na sekta binafsi vizuri kabisa tusiwe na mashaka ni vile tuliona kasoro, lakini niwaombeni sekta binafsi hasa wale mlio vizuri katika jambo hili la chanjo msiwe na wasiwasi hata mkiingia mikataba na halmashauri ili mradi muwe na sifa na vigezo ndiyo maana ya sisi tukatoa mwongozo ili tufanye kazi pamoja.” Amefafanua Waziri Ndaki


Pia, amewataka viongozi wenzake wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mamlaka za serikali za mitaa, watoa huduma za afya ya mifugo na sekretarieti za mikoa wazingatie maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini na kutoa maoni au kuuliza maswali sehemu ambazo zitakuwa na utata ili kuhakikisha mwongozo huo unatekelezwa kama ambavyo umezingatiwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.


Ameitaka pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa nakala za kutosha za mwongozo huo kwa wadau wa sekta ya mifugo kote nchini na pia kuwataka wadau kupata nakala laini kupitia tovuti ya wizara hiyo, www.mifugouvuvi.go.tz.


Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Mukunda amesema mkoa huo utahakikisha yale yote ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatamani yatokee katika Sekta ya Mifugo mkoa uko tayari kuyasimamia ili yalete tija kwa taifa na wafugaji na kuiomba wizara kuangalia ikama ya wataalamu wa afya ya mifugo na pia wale waliopo katika ngazi za juu kuwa na utaratibu wa kufika katika maeneo ya chini ya wafugaji.


“Ili pia mwongozo huu uweze kufanya vizuri ikama ya wataalamu wa mifugo bado haitoshi hivyo ni vyema wataalamu waliopo katika ngazi za juu waweze kuwafikia pia wafugaji wa chini na tunataka kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kitovu cha kuzalisha nyama na maziwa kwa wingi.”  Amesema Mhe. Mukunda


Ameongeza kuwa Sekta ya Mifugo kwa sasa imekuwa ikirasimishwa rasmi na kuifanya iheshimishe watu wanaofanya shughuli za mifugo kwa kuwa imekuwa na tija kubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.


Katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema serikali bado inahakikisha inafanya jitihada mbalimbali za kupata masoko zaidi ya mazao ya mifugo yenye ubora ambayo yanachochewa na uwepo wa chanjo bora na mifugo kupatiwa chanjo hiyo kwa njia sahihi na pia kutoa angalizo kwa halmashauri nchini kuhakikisha zinakuwa na miundombinu bora kwa ajili ya kuogeshea mifugo.


“Wenzangu niwaombe popote huu waraka ulipo ukatusaidie ili malalamiko ya mnada umeharibika au wilaya nzima kutokuwa na josho, hayo malalamiko yafike mwisho kupitia mapato mbalimbali ambayo halmashauri wamekuwa wakipata yakiwemo ya minada iliyopo kwenye wilaya hizo, wanapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kuyakarabati.”  Amefafanua Mhe. Gekul  


Akizungumzia mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini Bw. Jeremiah Wambura amesema tasnia ya maziwa nchini ikisimamiwa vyema inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa pato la taifa na kuhamasisha uwepo wa viwanda vingi vya kuchakata maziwa nchini.


Hivyo ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia vyema namna ya kuisimamia tasnia ya maziwa ili iwe na tija zaidi kwa taifa pamoja na kuongeza wingi wa maziwa ambayo yanaweza kutumika majumbani pamoja na kuchakatwa viwandani.


Mara baada ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, wenye lengo la kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuanzia sasa mwongozo huo unaweza kutumika na huduma ya chanjo kuendelea kutolewa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimkabidhi Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini kati ya sekta binafsi na umma katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma ambapo Waziri Ndaki amesema mwongozo huo unalenga kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama. (22.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wadau wa sekta ya mifugo (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini kati ya sekta binafsi na umma. Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma. (22.01.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Mukunda, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini kati ya sekta binafsi na umma katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma. (22.01.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini Bw. Jeremiah Wambura mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini kati ya sekta binafsi na umma katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma. (22.01.2021)

Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini. Waliosimama ni baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo, na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyekaa katikati), Mkuu wa Wilaya ya Bahi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mwanahamisi Mukunda (wa pili kushoto waliokaa), Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul ( wa pili kulia waliokaa), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto waliokaa) na mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mifugo kutoka Shirika la Kilimo na Chakula Duniani – Tanzania (FAO) Dkt. Niwael Malamsha. (22.01.2021)

MHE. NDAKI ATEMBELEA SHAMBA LA MFUGAJI JOSAM NTANGEKI LILILOPO KWENYE RANCHI YA KIKURURA WILAYANI KARANGWE, MKOA WA KAGERA.

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akitoa maelekezo mara baada ya kufika kwenye shamba la Mfugaji anayefahamika kwa jina Josam Ntangeki lililopo kwenye ranchi ya Kikukurura wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera jana (19.01.2021). Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Bw. Noeli Byamungu (wa kwanza kulia).
Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Bw. Noely Byamungu (katikati) akimweleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kutoka kulia) juu ya namna Bodi inavyompa ushirikiano Mmoja wa wawekezaji wa Ng'ombe wa Maziwa waliopo kwenye ranchi ya Kikulula Bw. Josam Ntangeki (wa pili kutoka kushoto), baada ya Mhe. Mashimba kutembelea ranchi hiyo jana (19.01.2021).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na katibu Mkuu wa wizara hiyo (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel wakikagua moja ya ng'ombe waliopo kwenye kitalu cha Mwekezaji Josam Ntangeki muda mfupi baada ya kufika kwenye ranchi ya Kikulula iliyopo Wilayani Karagwe mkoa wa Kagera jana (19.01.2021)

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) muda mfupi baada ya kufika kwenye shamba la mwekezaji wa ndani Bw. Josam Ntangeki lililopo kwenye Ranchi ya Kikurura wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera jana (19.01.2021)

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA UVUVI WA KATA YA MIGOLI MKOANI IRINGA

 

Afisa Uvuvi Mwandamizi (WMUV), Hamidu Njegite (aliyesimama katikati) akiwaeleza wadau wa uvuvi wa kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya  Iringa faida za kuunda ushirika wakati wa Mafunzo rejea kwa wadau hao, yaliyokuwa pia na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya wavuvi. Mafunzo hayo yanafanyika katika mwalo wa Migoli na Chapuya, kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa. (18/01/2021)

Diwani wa kata ya Migoli, Mhe. Benitho Kayugwa (aliyevaa suti nyeusi) akifungua Mafunzo rejea ya wadau wa uvuvi wa kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya  Iringa yaliyokuwa pia na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya wavuvi. Mafunzo hayo yanafanyika katika mwalo wa Migoli na Chapuya, kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa. (18/01/2021)

Mkufunzi Mwandamizi (WMUV), Bi. Kresensia Mtweve (aliyesimama katikati) akiwaeleza wadau wa uvuvi wa kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya  Iringa jinsi ya kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi wakati wa Mafunzo rejea kwa wadau hao, yaliyokuwa pia na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya wavuvi. Mafunzo hayo yanafanyika Chapuya, kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa. (18/01/2021)
Afisa Mfawidhi kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu, Bw. Godbless Msuya (aliyesimama katikati) akiwaeleza wadau wa uvuvi wa kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya  Iringa jinsi ya kutunza rasilimali za uvuvi wakati wa Mafunzo rejea kwa wadau hao, yaliyokuwa pia na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya wavuvi. Mafunzo hayo yanafanyika katika mwalo wa Migoli na Chapuya, kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa. (18/01/2021)

Afisa Ushirika kutoka halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bi. Neema Lema (aliyesimama katikati) akiwaelimisha wadau wa uvuvi wa kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya  Iringa namna ya kuanzisha vyama vya Ushirika wakati wa Mafunzo rejea kwa wadau hao, yaliyokuwa pia na lengo la kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya wavuvi. Mafunzo hayo yanafanyika katika mwalo wa Migoli na Chapuya, kata ya Migoli, Wilaya ya Iringa, mkoani Iringa. (18/01/2021)

MAAFISA MIFUGO RUDINI KAZINI - GEKUL

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amewataka Maafisa Mifugo kote nchini kurudi kazini na kushirikiana kwa ukaribu na Chama cha Wafugaji nchini kushughulikia changamoto mbalimbali za wafugaji tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo Wafugaji wengi bado wameendelea kukosa huduma kwa wakati.


Mhe. Gekul ameyasema hayo leo (14.01.2021) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kwenye ukumbi wa hoteli ya Royal Village jijini Dodoma ambapo alisema kuwa Wizara haitamvumilia Afisa Mifugo ambaye hatotimiza wajibu wake ipasavyo kwa kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wafugaji hali inayosababisha watu wengi kukata tamaa kwenye shughuli za ufugaji.


"Mfugaji anampigia simu mtaalam na kumsubiri kwa saa kadhaa bila kupata msaada wowote wa kitaalam mpaka mifugo inakufa, kwa kweli hilo sisi hatuwezi kukubali kuona likiendelea" Alisema Mhe.Gekul.


Mhe. Gekul alisifu jitihada za Chama Cha Wafugaji nchini kwa jitihada mbalimbali ambazo imeendelea kuzifanya ili kuboresha mazingira ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Benki ya Posta ili iweze kuwasaidia kupata bima kwa mfugaji mmoja mmoja.


"Nawasihi muendelee na jitihada za kuzungumza na taasisi nyingine za fedha ili wafugaji wote nchini waweze kufikiwa na huduma mbalimbali zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa mafanikio makubwa" Alisema Mhe. Gekul.


Aidha amebainisha kuwa Wizara yake itaendelea kutoa huduma bora kwa wafugaji wote nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu utoaji wa chanjo za mifugo na kujenga majosho katika maeneo mbalimbali ili kuikinga mifugo na maradhi mbalimbali.


"Sekta ya Ufugaji ni sekta inayogusa maisha ya kila siku ya mwananchi aliyepo hapa nchini kupitia mazao yake kama vile Nyama, Maziwa, Ngozi n.k. hivyo tunatambua ni kiasi gani tunao wajibu wa kuhakikisha tunaiboresha ili iweze kukidhi mahitaji ya wakati uliopo na unaokuja" Aliongeza Mhe. Gekul.


Mhe. Gekul alimuagiza Mwenyekiti wa Chama hicho kuhakikisha Bw Jeremiah Wambura kuhakikisha wanakiimarisha na kushusha mfumo wake mpaka kwenye ngazi ya kata, vijiji na mitaa hasa kutokana na wafugaji wengi hapa nchini kutofahamu Sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia ya ufugaji kwa ujumla.


"Hali hii ndo imesababisha baadhi ya wafugaji kutoa rushwa kwa baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu hata kama wanakuwa hawajafanya kosa lolote" Alisisitiza Mhe. Gekul.


Katika hatua nyingine Mhe. Gekul amepiga marufuku uwepo wa madalali wa mifugo maarufu kwa jina la "Garagaja" kwa sababu uwepo wao unasababisha wafugaji kushindwa kuuza na kununua mifugo yao kwa bei stahiki.


"Ninawaagiza Maafisa Mifugo wote nchini kurudi kazini na mkae na Viongozi wa Chama Cha Wafugaji ili muweze kuwahudumia wafugaji wetu kwa ukaribu kabisa tofauti na hali ilivyo sasa". Alisisitiza Mhe. Gekul.


Katika hatua nyingine Mhe. Gekul amewaagiza wafugaji wote nchini kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli nyingine ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara.


"Ni lazima tutimize wajibu wetu kwa kutopeleka mifugo yetu kwenye maeneo yaliyotengwa kwa shughuli nyingine za kiuchumi kwa sababu mbali na kusababisha migogoro kufanya hivyo pia ni kosa kisheria na sisi kama Wizara hatutawatetea pindi mkifanya hivyo" Alisisitiza Mhe. Gekul.


Amebainisha kuwa Wizara zote zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi na kukuza uchumi wa nchi hivyo wadau wa kila upande wanapaswa kutimiza wajibu wao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akifafanua jambo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Kikao kazi cha  Chama Cha Wafugaji nchini kilichofanyika leo (14.01.2021) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma .
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (Kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji nchini Bw Jeremiah Wambura wakijadili jambo wakati wa kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Chama Cha Wafugaji nchini wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.
Baadhi ya wawakilishi kutoka benki ya Posta wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.
Katibu wa Chama cha Wafugaji nchini Bw Joshua Lugaso (wa kwanza kulia), baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (kulia kwake) wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati akizindua  kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) kwenye hoteli ya Royal Village jijini Dodoma.


Alhamisi, 14 Januari 2021

KIKAO KAZI CHA KUANDAA MWONGOZO WA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA UVUVI KWENYE MAJI MADOGO NA MAENEO OEVU NCHINI


Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa kikao kazi cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma. 14/01/2021


Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi, Bi. Merisia Sebastian Mparaza akieleza lengo la kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini wakati wa kikao hichi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi leo kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma. 14/01/2021

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismail Kimirei akichangia mada wakati wa kikao cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini wakati wa kikao hichi jijini Dodoma. 14/01/2021

 


Mkurugenzi wa Idara  ya Utafiti, Mafunzo na Ugani  Sekta ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha akichangia hoja kwenye kikao kazi cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye ukumbi wa Chuo cha mipango jijini Dodoma leo 14/01/2021


Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi, Bw. Amosi Machilika ( wa pili kutoka kulia mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha kuandaa mwongozo wa kusimamia Rasilimali za Uvuvi kwenye maji madogo na maeneo oevu nchini mara baada ya kikao hichi kwenye ukumbi wa  Chuo cha mipango jijini Dodoma. (14/01/2021)


WALIOKAIDI MKATABA WA NARCO KIKAANGONI NDANI YA SIKU KUMI

Na. Edward Kondela


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ametoa siku kumi kwa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kubaini na kuwanyang’anya maeneo, wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa ambao wamebadili matumizi ya ardhi kinyume na makubaliano ya mikataba yao.


Waziri Ndaki amebainisha hayo jana (12.01.2021) wakati alipotembelea Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kufanya mkutano wa hadhara na baadhi ya wawekezaji, wakulima na wafugaji, ambao wanafanya shughuli zao katika ranchi hiyo na kubaini kuwa baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu na NARCO kwa ajili ya kufuga na kulima malisho ya mifugo wamekuwa wakikodisha maeneo hayo kwa wakulima na wafugaji kinyume na mkatabata.


“NARCO siku kumi nadhani zinawatosha kubaini watu wanaojiita wawekezaji, waliobadilisha matumizi ya ardhi ambayo siyo kufuga wala malisho wanyang’anywe maeneo kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu wa mkataba kati yao na NARCO, na mimi nitafuatilia nitapenda kupata taarifa mmepata wangapi na wangapi wamenyang’anywa kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu waliokubaliana.” Amesema Mhe. Ndaki


Waziri Ndaki amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Mbarali kuwa wamekuwa wakikodishwa maeneo ya ranchi hiyo na wawekezaji kwa shilingi elfu ishirini kwa hekari moja kwa ajili ya kilimo na madebe kumi ya nafaka baada ya mavuno kwa kila hekari moja, huku wafugaji wakilipa takriban shilingi milioni mbili kwa hekari moja katika kipindi cha miezi minne kwa ajili ya kulisha mifugo yao kwenye maeneo ya wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu na NARCO kwa mkataba wa kufuga au kulima malisho ya mifugo.


Amefafanua kuwa mkataba wa NARCO na wawekezaji kwa ajili ya kufugia mifugo na kulima malisho hauruhusu wawekezaji kukodisha eneo kwa mtu mwingine kwa ajili ya shughuli zozote kwa kuwa maeneo ya ranchi za taifa ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).


Kuhusu deni la zaidi ya Shilingi Bilioni Sita ambalo NARCO inawadai wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa NARCO kufikia Tarehe 15 Mwezi Februari Mwaka 2021 saa saba mchana awe amepata taarifa ya wawekezaji waliolipa madeni yao pamoja na ambao bado hawajalipa, kabla ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi.


“Wawekezaji wote ambao tunawadai hapa Usangu na kwenye ranchi zingine wote walipe pesa ya NARCO tulipokubaliana kwenye mkataba tulikubaliana mtalipa pesa, mlipe madeni yenu ifikapo tarehe 15 mwezi februari saa saba mchana muwe mmelipa madeni yenu tunataka NARCO ijiendeshe kibiashara, lakini sioni tukielekea kwenye kujiendesha kibiashara na moja ya matatizo yanayotufanya tusifike huko ni kulea watu wa namna hii.” Amefafanua Mhe. Ndaki.


Ameongeza kuwa wale ambao hawatakuwa wamelipa hadi kufikia muda huo wanyang’anywe maeneo hayo ili wapatiwe watu wengine ambao wataweza kulipa kwa mujibu wa mkataba ili NARCO iweze kufikia malengo yake na kulalamika kuwa NARCO imechelewa kuchukua hatua kwa watu ambao wamekuwa na madeni ya siku nyingi.    


Amesema kuwa wizara imefanya tathmini juu ya madeni hayo na kuagiza yalipwe katika viwango na tozo mpya zilizowekwa kwa sababu imejiridhisha kwamba kwa gharama hizo NARCO itaweza kujiendesha na kuhudumia vizuri ranchi zake.


Kwa mujibu wa taarifa ya NARCO iliyotolewa na Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Bw. Masele Mipawa, maeneo ya vitalu katika ranchi za taifa yanayokodishwa kwa wawekezaji yamegawanywa katika viwango vitatu, ambapo kiwango cha chini ni Shilingi 3,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta 1 hadi 2000, kiwango cha kati ni Shilingi 5,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta kuanzia hekta 2001 hadi 5000 na kiwango cha juu ni Shilingi 7,500/= kwa hekari moja kuanzia eneo lenye hekta zaidi ya 5001.


Aidha Waziri Ndaki, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia namna ya kukodisha maeneo ya ranchi za taifa kwa wakulima ambao wanaweza kulima malisho ya mifugo ili kuondokana na migogoro ya wakulima kupata maeneo kwa ajili ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi.


Amesema ni muda muafaka kwa wizara kuangalia namna wananchi wanavyoweza kutumia maeneo hayo kwa ajili ya tija kwa taifa badala ya kusubiri wawekezaji ambao baadhi yao wamekuwa wakienda kinyume na makubaliano ya mikataba na kuwafanya wananchi wanaoishi karibu na ranchi za taifa kukosa maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kiuchumi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema atahakikisha anasimamia maelekeo yote yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki likiwemo la wawekezaji kulipa madeni ya vitalu walivyokodishwa ili Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inayomiliki maeneo hayo iweze kujiendesha kibiashara kama moja ya malengo ya kampuni hiyo kupitia maeneo yake.


Katika mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wakulima, wafugaji na wawekezaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali, Bibi Uliya Mahenge amemuomba Waziri Ndaki kuwapatia wakulima maeneo kwenye ranchi za taifa ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo huku wakilipa kodi ya serikali ya maeneo hayo watakayokidishwa kama ambavyo wafugaji wanavyopatiwa vitalu kwa ajili ya kufugia mifugo kwenye ranchi hizo.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya ambapo katika ziara hiyo alikuwa na lengo la kufahamu changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu ambayo ni moja ya ranchi zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyesimama), akizungumza na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Reuben Mfune. (12.01.2021)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia), akielekezwa jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wa kikao na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo ili kutambua changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu na kuzitafutia ufumbuzi. (12.01.2021)

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Masele Mipawa akitoa taarifa ya madeni ya wawekezaji waliopatiwa vitalu kwenye ranchi za taifa zilizopo maeneo mbalimbali nchini wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Bw. Mipawa amesema NARCO inawadai wawekezaji zaidi ya Shilingi Bilioni Sita. (12.01.2021)

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel na baadhi ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao kwenye Ranchi ya Usangu iliyopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, pamoja na baadhi ya wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo. Waziri Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya kwa kuwataka wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa kuheshimu mikataba waliyoingia na kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). (12.01.2021)



 

WAKAGUZI WA NGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA UZALISHAJI WA NGOZI BORA

Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura amewataka wakaguzi wa zao la Ngozi wa Kanda ya Mashariki kusimamia ubora wa Ngozi zinazozalishwa.

 

Bura ameyasema hayo leo (12.01.2021) wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wakaguzi wa Ngozi wa Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yanayofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House jijini Dar es Salaam.

 

Wakaguzi hao wa Ngozi wametakiwa kusimamia uzalishaji wa zao hilo katika hatua zake zote ili kupata Ngozi zinazofaa kusindikwa katika viwanda.

 

Aidha, wakaguzi hao wametakiwa kutumia sheria namba 18 ya mwaka 2008 inayolenga kuboresha zao la ngozi ili wadau waweze kuzalisha ngozi bora inayokidhi mahitaji ya viwanda vyetu na hatimaye kuwa na tija ya uzalishaji wa zao hilo.

 

Bura amesema uzalishaji wa ngozi za ng’ombe na mbuzi kwa siku ni vipande 31,000 lakini ni asilimia 10 tu ya ngozi zinazopelekwa viwandani hufaa kwa ajili ya kusindikwa, na asilimia 90 hazifai kutokana na kukosa ubora unaofaa kwa ajili ya kusindikwa.

 

“Hivyo baada ya kupata mafunzo haya ni matarajio ya wizara kuwa mtakwenda kulisimamia nyema zao hili la Ngozi ili kuhakikisha Ngozi yote inayozalishwa inakuwa bora,” alisema Bura.

 

Hapa nchini vipo viwanda viwili tu vyenye uwezo wa kusindika ngozi hadi hatu ya mwisho ambavyo ni Moshi Leather Industry chenye uwezo wa kusindika futi za Mraba elfu 15,000 kwa siku na Himo Tannery and Planter Ltd chenye uwezo wa kusindika futi za mraba 10,000 kwa siku.

 

Uwezo wa usindikaji wa viwanda vyote viwili kwa siku ni sawa na vipande 1000 vya ngozi ya ng’ombe na 9000 vya ngozi ya mbuzi, hivyo bado kuna uhitaji wa viwanda vya kusindika Ngozi na vilivyopo kuongeza uwezo wake wa kusindika zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura (kulia aliyesimama) akifungua mafunzo ya siku mbili ya Wakaguzi wa Ngozi kutoka Hamashauri na Manispaa za Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yenye lengo la kuwajengea uwez, yanayofanyika katika ukumbi Mvuvi Huose Jijini Dar es Salaam (12.01.2021)


Mshiriki wa Mafunzo ya wakaguzi wa ngozi, Bw. Severine Munishi kutoka Halmashauri ya Malinyi akichangia mada ya Sheria ya Ngozi katika mafunzo ya kikao cha wakaguzi wa Ngozi yanayofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es salaam. (12.01.2021)

Picha ya pamoja ya Washiriki wa Mafunzo ya siku mbili ya Wakaguzi wa Ngozi na Wawezeshaji nje ya Jengo la Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)

Mtaalam wa Ngozi Mstaafu, Bw. Emmanuel Muyinga akiwasilisha mada ya Sheria ya Ngozi namba 18 ya mwaka 2008 kwa Washiriki wa Mafunzo ya Ngozi ya siku Mbili toka Halmashauri na Manispaa za Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)

Afisa Mifugo Mkuu kutoka Idara ya Uzalishaji na Masoko (WMUV), Bw. Edson Kilyenyi akitoa maelezo mafupi ya kuwakaribisha washiriki wa Mafunzo ya wakaguzi wa Ngozi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi afungue mafunzo hayo, yanayofanyika katika ukimbi wa wa Mvuvi House Jijini Dar es Salaam. (12.01.2021)



Jumanne, 12 Januari 2021

GEKUL ATEMBELEA WAKALA YA MAABARA YA VETERINARI KIBAHA MKOANI PWANI

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul moja ya chanjo wanazozalisha alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo cha kutengeneza chanjo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021. Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul moja ya chanjo wanazozalisha alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo cha kutengeneza chanjo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021.


Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha TANCHOICE, Selo Luwongo (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa tatu kutoka kushoto) mbuzi waliochinjwa na kuhifadhiwa katika chumba chenye baridi kali kwa ajili ya kusafirishwa kuuzwa nje ya nchi. Gekul alitembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021.

Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha TANCHOICE, Selo Luwongo (wa pili kutoka kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa pili kulia) maroli yaliyopakiwa minofu ya nyama ya mbuzi zaidi ya Tani 40 kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi alipotembelea Kiwanda hicho Januari 11, 2021. Kulia ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (katikati) alipotembelea Kituo cha Wakala hiyo kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Januari 11, 2021. Kushoto ni Kaimu Msajili, Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.


 

Jumapili, 10 Januari 2021

FETA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA KUZALISHA WATAALAM KUIMARISHA UVUVI WA BAHARI KUU

 Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuongeza kasi ya kuzalisha Wataalam watakaokuwa na uwezo wa kuendesha Meli za uvuvi wa bahari kuu zitakazonunuliwa na Serikali ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi kupitia uchumi wa bluu.

 

Gekul alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika ofisi za Wakala hiyo zilizopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.

 

Alisema kuwa mpango wa serikali katika miaka hii mitano chini ya uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ni kununua meli nane zitakazotumika kwenye shughuli za uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni muhimu kuongeza kasi ya kutoa wataalam ambao wataweza kuziendesha meli hizo pindi zitakapofika.

                                   

Aliongeza kuwa mwishoni mwa mwaka huu meli ya kwanza itakuja, huku akisema kuwa haitapendeza kama vyombo hivyo vitakuja halafu pasiwepo na vijana watakaohusika na kuviendesha. 

 

“Nchi inawategemea mtoe wataalam watakaosaidia kuendesha meli hizo zitakazoletwa kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu, tunaomba mkatuzalishie wataalam ambao hatutapata upungufu wa wataalam wa kuendesha vyombo hivyo,” alisema Gekul

 

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani alisema kuwa wameshaingia mkataba wa maridhiano wa viwango vya mafunzo na utoaji vyeti kwa wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi wa mwaka 1995 na hivyo itasaidia kuweza kutoa vyeti kwa Manahodha wa Meli, Maafisa wa Meli, Mabaharia na Waangalizi wa Meli zitakazofanyakazi katika uvuvi wa bahari kuu.

 

“Huwezi kuajiriwa kule kama hauna cheti cha kukutambulisha, hivyo kupitia maridhiano haya sasa Mabahari watapatikana kutoka katika chuo hiki,” alisema Dkt. Mzighani

 

Dkt. Mzighani aliongeza kuwa kwa Afrika vyuo vinavyotoa mafunzo kwa Wataalam hao vipo Afrika ya Kusini na Misri, huku akisema ni wakati mzuri sasa kupitia mafunzo yatakayotolewa hapa nchini kuongeza ajira kwa vijana na kupata fedha za kigeni kupitia watu kutoka nchi nyingine watakaokuja kusoma katika chuo hicho.

 

Aidha, Dkt. Mzighani alisema pamoja na mipango na mikakati mizuri waliyonayo katika kuboresha huduma zao bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya gharama za uendeshaji wa vyuo vya uvuvi, hivyo ameiomba serikali iwaongezee nguvu ili waweze kutoa wataalam wazuri watakaokwenda kulisaidia Taifa kukuza na kuimarisha uchumi wa bluu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akiwapa chakula Samaki alipotembelea Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki. Kulia kwake ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala hiyo, Dkt. Semvua Mzighani.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Dkt. Semvua Mzighani (kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.

Nahodha Mkuu, Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Kampasi ya Mbegani, Nikasi Mbandi (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul ramani inayoonesha maeneo ya uvuvi na kina chake katika Bahari ya Hindi alipotembelea Wakala hiyo iliyopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.



Jumamosi, 9 Januari 2021

GEKUL AMPA MKURUGENZI ILALA SIKU 7 KUMLIPA MKANDARASI

Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha kuwa ndani ya siku 7 anamlipa Mkandarasi anayejenga Machinjio ya Vingunguti shilingi bilioni 5 anazodai ili aweze kukamilisha ujenzi huo.

 

Gekul alitoa agizo hilo alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam Januari 8, 2021.

 

Alisema kuwa hali za machinjio nyingi kwa sasa sio nzuri, Wanyama wanachinjwa katika mazingira machafu na sio salama kwa walaji huku akisema machinjio hayo ya Vingunguti yatakuwa mkombozi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

 

“Kwa hiyo Mkurugenzi hakikisha ndani ya siku 7 kuanzia leo tarehe 8 unamlipa Mkandarasi ili kazi hii ikamilike kama ambavyo Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli alivyoagiza,” aliagiza Gekul

 

Gekul aliendelea kusisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo ni lazima uende sambamba na ununuzi wa magari kwa ajili ya kubebea nyama na kuzisambaza katika mabucha yaliyopo jijini Dar es Salaam kwani haitapendeza kuwepo kwa machinjio hayo mazuri halafu nyama ziwe zinabebwa kwenye pikipiki.

 

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha machinjio hayo yanapata Wanyama wazuri na salama kwa ajili ya walaji, wataboresha mnada wa machinjio ya Pugu ili wanyama watakaokuwa wanapelekwa hapo wawe na viwango vya kuchakatwa katika machinjio hayo.

 

Aidha, aliwapongeza Mkurugenzi na Mkandarasi kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kukamilisha ujenzi huo na kuwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili ukamilike kama inavyotarajiwa.

 

Naye, Msimamizi wa ujenzi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa, Mhandisi, Efraim Phanuel alisema kuwa endapo watalipwa kiasi hicho cha pesa wanachodai kama alivyoagiza Naibu Waziri watakamilisha ujenzi huo mapema mwezi wa pili mwaka huu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul (katikati) akikagua risiti ya mteja aliyemkuta akitoka na mbuzi katika mnada wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam alipotembelea mnada huyo Januari 8, 2021. Kulia ni Kaimu Msajili, Bodi ya Nyama, Imani Sichwale.


Mhandisi Efraim Phanuel akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul michoro inayoonesha muonekano wa  machinjio ya Vingunguti utakavyokuwa baada ya kukamilika kwake alipotembelea machinjio hayo Januari 8, 2021.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Msimamizi wa Ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti, Mhandisi EfraimPhanuel (hayupo pichani) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hayo Januari 8, 2021. Kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri.