Nav bar

Jumanne, 16 Machi 2021

WACHUNAJI NGOZI WASIOZINGATIA TARATIBU KUFUTIWA LESENI

Serikali imesema itawachukulia hatua kali ikiwemo kuwafutia leseni wachunaji wa ngozi katika machinjio ya Manispaa ya Morogoro wanaotoboa ngozi za mifugo na kuifanya kukosa thamani licha ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.

 

Akizungumza (15.3.2021) mara baada ya kufanya ziara ya kukagua uzalishaji wa ngozi bora zinazohitajika katika soko, Kaimu Mkurugenzi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Bw. Gabriel Bura alisema licha ya kufanyika mafuzo ya uchunaji bora wa ngozi lakini bado wapo watu wanaokiuka taratibu zilizowekwa.

 

Alisema mafunzo yaliyotolewa yamesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ngozi bora lakini Serikali haitawafumbia macho baadhi ya wachunaji wa ngozi wanaoendelea kutoboa ngozi kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo hasa katika viwanda vikubwa vya ngozi vilivyoanzishwa.

 

“Tulizitoa lesei hizi kwa sheria ya ngozi namba 18 ya mwaka 2008, lakini pia tulitoa mafunzo ya uchunaji wa ngozi ili kuzipa thamani ngozi mnazozalisha lakini kuna baadhi yenu bado wanafanya makosa kwa kutoboa ngozi, sasa makosa haya yakijirudia tutawafutia leseni” alisema Bura

 

Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imejidhatiti kwa kuanzisha na kufufua viwanda nchini ikiwemo kiwanda cha ngozi cha ACE Leather cha Morogoro na kiwanda cha ngozi kilichopo Moshi, hivyo kitendo cha kuendelea kutoboa ngozi hizo ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali.

 

Aidha, aliwataka wachunaji hao kuhakikisha wanaendelea kuzingatia sheria katika utendaji wa kazi zao sambamba na kutengeneza upya leseni zao ambazo zipo ukingoni kuisha muda wake wa kipindi cha mwaka mmoja ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

 

Mkaguzi mkuu wa nyama Bw. Joseph Kupa wa  Manispaa ya Morogoro amesema kuwa pamoja na mambo mengine wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria sambamba na magonjwa ya ngozi.

 

Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya wafugaji kuendelea kupiga chapa mifugo yao jambo linalosabisha ngozi kukosa thamani huku magojwa kama Exiima na Lab Skin ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakishambulia mifugo.

 

“Changamoto tunazopata mara nyingi ni mifugo inakuja hapa ikiwa imepigwa chapa na mingine imeshambuliwa na magonjwa ya ngozi sasa ikifika hapa inakuwa tayari haina thamani hata hatuwezi kuichuna kwa sababu haiwezi kununuliwa na inatokana na baadhi ya wafugaji kutokuwa na elimu yakutosha juu ya umuhimu wa ngozi” alisema Kupa

 

Kwa upande wake mwenyekiti wa wachunaji wa ngozi katika machinjio ya manispaa ya Morogoro, Mapinduzi Ernest ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa elimu waliyowapa ambayo inawasaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ngozi bora na kuiomba Serikali kufikisha elimu kwa wafugaji juu ya upigaji chapa ili kupata ngozi bora.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura (katikati) akiangalia Ngozi kwenye kiwanda cha ACE Limited kilichopo mkoani Morogoro wakati wa ziara yao mkoani humo. Kulia ni Afisa Mifugo kutoka WMUV, Bi. Mariam Muchakila na kushoto ni Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. George Obol. (15.03.2021)

Mkaguzi wa Ngozi kutoka kiwanda cha Ngozi cha ACE Limited, Bw. Godson Shayla (wa tatu kutoka kushoto) akitoa maelezo kwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura(wa nne kutoka kushoto) ya namna ya kuchuna Ngozi na jinsi walivyopanga kutoa adhabu kwa yoyote atakayetoboa Ngozi wakati wa kuchuna Ngozi hizo kwenye Machinjio ya Manispaa ya Morogoro. (15.03.2021)

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka WMUV, Bw. Gabriel Bura ( wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Machinjio ya Manispaa ya morogoro na wachunaji wa ngozi za Mifugo mara baada ya kukagua namna yanavyofanya uchunaji kwa kuzingatia sheria na kanuni katika Machinjio Iyo mkoani Morogoro. (15.03.2021)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni