Nav bar

Jumamosi, 26 Desemba 2020

GEKUL AWAAGIZA WAKURUGENZI HALMASHAURI KUTENGA FEDHA ZA MIFUGO

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza Waraka wa mwaka 2002 ambao unawataka kutenga asilimia 15 ya mapato yanayotokana na shughuli za Sekta ya Mifugo na Uvuvi na kuzirejesha kwenye sekta hizo ili kuboresha shughuli zake.

 

Gekul alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro alipotembelea kukagua shughuli za Sekta ya mifugo na uvuvi zinazotekelezwa Wilayani humo Disemba 23, 2020.

 

Kwa mujibu wa Gekul, mwaka 2002 Serikali ilitoa waraka ambao unaelekeza kuwa Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa mapato yanayopatikana kutokana na shughuli za sekta ya mifugo na uvuvi itengwe asilimia 15 na zirudishwe kwa sekta hizo ili kuboresha huduma kwa mifugo ikiwemo ukarabati wa majosho, minada na kununua chanjo za mifugo.

“Wakurugenzi rejeeni huo waraka ambao unadumu mpaka mwaka 2025 ili mtekeleze kama ulivyoagiza na tukifanya hivyo itasaidia kuboresha huduma za mifugo yetu na tupate mazao bora yanayotokana na mifugo hiyo,” alisema Gekul

 

Aliendelea kusema kuwa miundombinu mingi ya kuhudumia mifugo imechoka akitolea mfano minada ya kuuzia ng’ombe kuwa mingi haina uzio, mifugo inauzwa katika maeneo ya wazi jambo ambalo linachangia upotevu wa mapato ya Halmashauri.

 

“Najua katika Halmashauri zetu mara nyingi fedha huwa hazitoshi lakini ni muhimu kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha na tukifanya hivyo itakuwa rahisi kutenga hizo pesa ili kuboresha sekta za mifugo na uvuvi, hivyo naagiza baada ya kutoka hapa tukatekeleze hilo,” alisisitiza Gekul

 

Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa muelekeo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha majosho yanaboreshwa, minada inakarabatiwa na chanjo zinapatikana kwa urahisi ili wananchi wasihangaike kupata huduma kwa ajili ya mifugo yao.

 

Pia, aliwataka maafisa mifugo kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili kuzuia upotevu wa mapato kwani makusanyo yakiwa mazuri na huduma za mifugo zitaboreshwa.

Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi (wapili kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (katikati) kuhusu moja ya nyavu inayotumiwa na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro. Waziri Gekul alikwenda katika Mwalo wa bwawa hilo kukagua shughuli zinazoendelea hapo Disemba 23, 2020. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.

Wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu (kushoto) wakimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) Samaki aina ya Perege waliovuliwa kutoka katika bwawa hilo muda mfupi baada ya kumaliza kuongea na wavuvi wanaoishi kandokando mwa bwawa hilo lililopo Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Disemba 23, 2020.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson akieleza jambo katika mkutano wa Wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto aliyekaa) uliofanyika  Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Disemba 23, 2020. Kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni