Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amewataka watendaji wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu kufanya maandalizi ya kupata kanuni bora za
kusimamia Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na watendaji wa mamlaka hiyo Mjini Unguja Visiwani
Zanzibar akifuatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame
Ali Ussi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ulega aliwataka watendaji hao
kuunda kanuni bora zitakazoenda sambamba na mfumo wa biashara kwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anataka kuona namna ukanda
wa bahari unavyosaidia kuinua uchumi wa taifa.
“Jumla ya vipengele vyote vya sheria takriban 104 tumevifanyia
kazi na vipengele kama 23 ambavyo havijaguswa lakini vingine vyote vimeguswa
kuendana na uchumi wa bahari ili kuwa na mchango kwa mtu mmoja mmoja na taifa
kwa ujumla katika kufanya maboresho ya uvuvi na bahari kuu, rai yangu kwa
mamlaka mmefanya kazi nzuri kwa utengenezaji wa sheria lazima kwenda mbio sasa
ndani ya miezi miwili tuwe tumepata kanuni zitakazoenda sambamba na biashara ya
leo bila kuathiri maslahi mapana ya taifa letu.” Alisema Ulega
Aliongeza kuwa matumizi ya sheria hiyo yatakayoenda sambamba na
kanuni bora za utekelezaji wake zitakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji kwa raia
kutoka nje ya nchi kuja na meli zao hapa nchini na kufanya shughuli za uvuvi na
wengine kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa samaki kwa kuwa Ukanda wa
Pwani ya Bahari Hindi bado hakuna uwekezaji wa kutosha wa viwanda hivyo.
Aidha, aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa
na Rais Dkt. John Magufuli ilivyoboresha mazingira kwenye maziwa na mito hali
iliyopelekea ndege za mizigo kubeba minofu ya samaki kutoka katika uwanja wa
ndege wa Mwanza na kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Pia, Naibu Waziri Ulega alifafanua kuwa wakati watendaji
wa Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu wanaandaa kanuni za kusimamia
sheria hiyo watambue kuwa ushirikiano ni muhimu katika utekezaji huo na
kutokuwa na mvutano wowote kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Ali Mohamed
Shein wanataka kuona mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi.
“Lazima mfanye kazi pamoja mshirikiane msiwe na aina
yoyote ya mvutano, lazima mfanye kazi nzuri ya kushirikiana lazima taifa letu
linufaike, Tanzania kwanza, tunaenda kufungua uvuvi wa bahari kuu tunaenda
kufungua uchumi wa bluu tunataka uvuvi utoke kuchangia Asilimia 1.9 katika pato
la taifa kusiwe na jambo la kunyoosheana vidole.” Alifafanua Ulega
Ulega akizungumza katika kikao hicho alisema ni muda muafaka kwa
wavuvi hapa nchini kuondakana na uvuvi wa kuwinda bali uendane na teknolojia ya
kisasa kufahamu maeneo mahsusi kwa ajili ya uvuvi ili kupunguza gharama kwa
kutengwa vituo maalum vya kutolea taarifa ya maeneo yenye samaki na umbali wa
kufikia maeneo hayo.
Alibainisha kuwa ni lazima uwepo mfumo wa kitaaalamu kwenye
vyombo vyao vya uvuvi ili mvuvi anapotoka pwani kwenda baharini kuvua awe na
uhakika wa mahali anapokwenda kuvua samaki na kuwataka watendaji hao kulifanyia
kazi suala hilo haraka ili kufikia malengo ya wavuvi kunufaika zaidi kupitia
sekta hiyo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, akiwa katika ziara
maalum visiwani Zanzibar alitembelea kituo cha utotoaji wa vifaranga vya
samaki, majongoo na kaa eneo la Maruhubi Mjini Unguja, ambapo alisema ipo
miradi midogomidogo itakayoweza kutumika ikiwemo ya uvuvi wa samaki, majongoo
na kaa ambayo ina soko kubwa duniani.
Ulega alisema uzalishaji wa bahari ndio nguzo kuu ya kukuza
uchumi kwa wakaazi wa Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Tanzania baada ya kufanikiwa
katika ukuzaji viumbe maji kwenye maji baridi hivyo mapinduzi makubwa
yanaelekezwa katika ukuzaji viumbe maji kwenye bahari.
“Serikali imeamua kwa dhati bahari yetu iweze kutunufaisha
na kuwa na mchango chanya wakati wa kuhamia katika uvuvi wa bahari kuu na jamii
iweze kufuga na kukuza kipato katika viumbe ambavyo vinauzika na kuhitajika
duniani kama kaa na majongoo bahari ambao wanahitajika katika mataifa ya nje ya
nchi yetu na wamekuwa wakiuzwa kwa bei kubwa.”
Ulega alisema, juhudi hizo zinaendana na mikakati ya serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kufanya mapinduzi katika sekta ya kilimo itakayoinua jamii ya Ukanda wa Pwani
kupitia miradi hiyo midogo.
"Tunafanya haya yote kwa ajili tunapata vyanzo vingi vya
mapato vitakavyosaidia uchumi wa nchi pamoja na wananchi ambayo itatusaidia
Tanzania kukuza maendeleo yake kwa haraka, kama ni utalii tunapongeza viongozi
wetu wakuu kwa kusimamia haya na elimu hii iende mbali zaidi uzalishaji viumbe
maji kwenye bahari unaweza kusababisha kuinuka kama taifa na kufanya vizuri
zaidi kiuchumi na kuinua pato la taifa.”
Aliongeza kuwa licha ya kuelekea mpango wa uvuvi katika bahari
kuu tayari miradi kama hiyo imeleta mageuzi makubwa katika maji baridi kwa
maana ya maeneo ya maziwa na mito kwa upande wa Tanzania Bara.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Mifugo, Dkt. Makame
Ali Ussi, alisema, Zanzibar inaendelea na mpango wa uchumi wa bahari, kwa kuwa
una nafasi kubwa ya kuingiza mapato ya haraka pamoja na kuwanufaisha wananchi
wengi.
“Tunaelekea kwenye uchumi wa bluu unaohitaji kutunza mazingira
ya bahari, ninawashauri watanzania sehemu zote za pwani watunze maeneo ya
bahari kwa kutunza maeneo ya mazalia ya samaki yakiwemo matumbawe.” Alisema
Ussi
Pamoja na hayo, alisema kuwa miradi hiyo ya uzalishaji wa samaki
imekuwa na nafasi kubwa katika kukuza mazingira ya bahari ambayo tayari sehemu
kubwa ya maeneo yanayotegemewa kwa uvuvi yameshaathirika.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja
visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha sekta ya
uvuvi inazidi kunufaisha zaidi taifa na mvuvi mmoja mmoja na kuongeza
ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na kubadilishana uzoefu
katika sekta hiyo.
![]() |
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Abdallah Ulega (wa kwanza kulia) akishuhudia kaa, alipotembelea kituo
cha utotoleshaji vifaranga vya samaki, majongoo bahari na kaa mjini Unguja,
wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Visiwani Zanzibar.
Akiambatana na
Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi wa SMZ Dkt. Makame Ali Ussi
![]() |
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyevaa
koti jeusi) akipata maelezo ya ufuatiliaji wa meli zinazoingia katika maji ya
Tanzania kwenye Bahari ya Hindi mara baada ya kutembelea ofisi za Mamlaka
ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu visiwani Zanzibar. (02.06.2020)
![]() |
Naibu Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Abdallah Ulega (aliyesimama) akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (hawapo pichani) katika ofisi za mamlaka hiyo
Visiwani Zanzibar, aliyekaa kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Makame Ali Ussi. (02.06.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni