Nav bar

Jumatatu, 1 Juni 2020

SERIKALI YATEKELEZA KWA VITENDO ILANI YA UCHAGUZI KWA WAVUVI





Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha awamu ya kwanza imeweka mikakati mizuri na kuthubutu kuhakikisha wavuvi wanaanza kuaminika na kukopeshwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amezungumza hayo katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, wakati akikabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kutoka TADB kwa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Bukasiga na kufafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameweka mazingira ya kufanya wavuvi waweze kuaminika na taasisi za kifedha na kupewa mikopo ili kujiimarisha katika shughuli zao.

“Hii benki tangu ianze ina miaka mitano sasa na katika miaka mitano ya Dkt. John Magufuli imewakopesha watanzania katika nyanja za kilimo, mifugo na uvuvi zaidi ya Shilingi Bilioni 170 na tangu uhai wa taifa hili wavuvi wameanza kuaminika na kukopeshwa pesa.” amesema Mhe. Ulega

Ameongeza kuwa wavuvi walikuwa wanaonekana ni watu wa kuhamahama lakini kwa uthubutu, uzalendo na utayari wavuvi wanaanza kuaminika na kuhamasishwa kujiunga katika vikundi vya ushirika na kupatiwa mikopo ya masharti nafuu ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ibara ya 27 na msimamo wa Rais Dkt. John Magufuli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) Bw. Japhet Justine akizungumza katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 200 kwa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Bukasiga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha barafu, amesema wameweza kutekeleza upatikanaji wa mkopo huo baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati ya kuhakikisha inatekeleza uvuvi uwe wa kisasa utakaoonesha fursa zaidi.

Akitoa neno la shukran kwa niaba ya wanachama wa kikundi cha Bukasiga makamu mwenyekiti wa chama hicho Bw. Jumbula Lugola amesema wanashukuru kwa mkopo huo kwa kuwa shughuli zao za uvuvi zitabadilika na kufanyika kisasa zaidi kwa kuwa CCM imeweka mkakati mzuri ili kuhakikisha wavuvi wanaufaika kupitia mikopo.

Ameongeza kuwa kwa juhudi za Rais Magufuli hatimaye wameweza kupatiwa mkopo na TADB wa Shilingi Milioni 200 na kumuahidi Rais Magufuli kuwa mkopo waliopatiwa watahakikisha wanautumia vyema ili uwanufauishe pia watanzania wengine.


Picha ya pamoja: Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyevaa koti jeusi) akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwemo Mratibu wa Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo Bw. Steven Michael (wa tatu kutoka kushoto) ambaye ameongoza dawati lake kufanikisha mikopo ya wavuvi kutoka TADB. (31.05.2020) 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni