Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

SERIKALI YATOA EKARI 1000 ZA RANCHI KWA WANANCHI MKOANI KILIMANJARO

  •  Pia Yawarasimishia ekari 200 walizokuwa wakimiliki awali kinyume na utaratibu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewapa wananchi wa kijiji cha Kalimaji eneo lenye ukubwa wa ekari 1000 zilizokuwa zinamilikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha West Kilimanjaro kilichopo kanda ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro.

Akikabidhi eneo hilo kwa kamati ya Usalama ya Mkoa huo leo Machi, 05, 2024 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Wizara yake imeridhia kutoa eneo hilo na kurasimisha ekari 200 za awali zilizokuwa zikitwaliwa na wananchi hao kinyume na utaratibu na kufanya kijiji hicho kuwa na eneo lenye ukubwa wa ekari 1200.

"Mhe. Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama sisi kama Wizara tumeridhia kutoa eneo hilo la sehemu ya kituo chetu cha Utafiti cha West Kilimanjaro na tunabariki taratibu zote za kuwamilikisha wananchi wa kijiji hicho ziendelee" Amesisitiza Prof. Mushi.

Akizungumza kufuatia uamuzi huo Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu ameipongeza Wizara kwa uamuzi huo ambapo ameongeza kuwa hatua hiyo inaakisi nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania kupitia shughuli za uzalishaji kiuchumi zitakazofanywa na wananchi hao kwenye eneo walilopewa.

Uamuzi huo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoketi Agosti 07, 2021 ambapo kiliamua baadhi ya maeneo ya Serikali kumegwa kwa manufaa ya wananchi ili waweze kuyatumia kwa shughuli zao za kijamii na kiuchumi.



Katibu Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (wa pili kushoto) na timu ya wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) muda mfupi kabla ya makabidhiano ya ekari 1000 za eneo la Kituo cha Utafiti wa Mifugo cha west Kilimanjaro kwa wananchi wa mkoa huo leo Machi 05, 2024.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (wa pili kushoto) akifafanua jambo ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda (katikati) muda mfupi kabla ya kuikabidhi kamati ya Usalama ya Mkoa huo ekari 1000 za eneo la  Kituo cha Utafiti wa Mifugo cha West Kilimanjaro  leo Machi 05, 2024.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni