Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

WAFUGAJI MSOMERA WAZURU LITA, TALIRI TANGA

Wafugaji kutoka kijiji cha Msomera kilichopo Handeni mkoani Tanga leo februari 28, 2024 wametembea taasisi za Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Buhuri mkoani humo na ile ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki ambapo wamefurahishwa na elimu ya ufugaji waliyoipata kwenye Taasisi hizo.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara hiyo ya siku moja, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera Bw. Martin Paraketi ambaye mbali na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi zake kwa kuwawezesha fursa hiyo ya mafunzo amewataka wafugaji wa kijiji chake kuwa mabalozi kwa wafugaji wengine kupitia yale waliyojifunza kutoka kwa wataalam wa taasisi zake.

"Tunatambua Serikali imetambua umuhimu wetu kuja kujifunza hapa ili tushirikiane na wataalam wake kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wenzetu tuliowaacha huko hivyo nitoe rai kwa wenzangu kila mmoja kutimiza wajibu wa kuelimisha kaya inayomzunguka kule Msomera" Amesema Bw. Paraketi

Aidha Bw. Paraketi ameiomba Serikali kuwashirikisha wananchi wa kijiji chake wakati wote wa utafiti wa masuala mbalimbali yanayolenga ufugaji bora jambo ambalo anaamini litazidi kuongeza ujuzi kwa wafugaji waliopo kijijini hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TALIRI kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku amewahamasisha wafugaji hao kuchangamkia fursa ya biashara ya malisho ya Mifugo inayoonekana kuongezeka thamani kadri siku zinavyoenda.

"Kwa sasa mbegu za malisho aina ya "cenchrus" zinauzwa shilingi 25,000 kwa kilo na hiyo ni kwa bei ya Serikali lakini kwa upande wa Taasisi binafsi zinauzwa 35,000 hadi 40,000 kwa kilo hivyo niwaombe mgeukie na kwenye fursa hii itakayowasaidia sana" Amesema Bw. Nziku.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Mkugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa amesema kuwa ziara hiyo ni miongoni mwa jitihada za Serikali kupitia Wizara yake katika kuhakikisha wafugaji wa kijiji cha Msomera wanajifunza kwa vitendo namna ya kufanya ufugaji bora na wenye tija.

"Taasisi hizi ni zenu na mnakaribishwa kuzitembela na kujifunza wakati wowote hata kama mtawezeshwa na wadau wengine kufanya hivyo na sisi tunaangalia namna ya kuja kutoa mafunzo kwenye vitongoji vya Olmolot, Urkung'u, Mkababu, katikati na eneo lote la "area F" Ameongeza Dkt. Mwilawa.

Mbali na kupewa elimu ya uzalishaji na utunzaji wa malisho bora ya mifugo, wafugaji hao wa kijiji cha Msomera walipewa mbegu za malisho hayo ili wakapande kwenye eneo watakalotumia kama shamba darasa kijijini kwao.


Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa (kushoto) akiwaelimisha wafugaji wa kijiji cha Msomera kuhusu kilimo cha Malisho bora ya Mifugo walipofika kwenye Shamba la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki mkoani Tanga Februari 28, 2024.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku (kushoto) akiwaeleza wafugaji wa kijiji cha Msomera kuhusu shughuli zinazofanywa na TALIRI kwenye kanda hiyo muda mfupi walipowasili hapo februari 28, 2024 mkoani Tanga.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa kijiji cha Msomera Bw.Martin Paraketi sehemu ya mbegu za malisho ya Mifugo zitakazopandwa kwenye shamba darasa la kijiji hicho wakati wa ziara ya wafugaji hao kwenye Taasisi hiyo kanda ya Mashariki mkoani Tanga februari 28, 2024.




  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni