Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

TANZANIA YAKABIDHIWA BOTI KUDHIBITI UVUVI HARAMU

Na. Edward Kondela

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhiwa boti mbili kutoka Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kufanya doria na kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria.

Akikabidhiwa boti hizo pamoja na injini tatu na redio maalum kwa ajili ya mawasiliano leo (04.03.2024) jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema vifaa hivyo vitasaidia katika juhudi za serikali kulinda, kuendeleza na kukuza rasilimali za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria na Tanzania kwa ujumla.

Amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukuza Sekta ya Uvuvi na kukuza mahusiano katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda ambazo zinatumia Ziwa Victoria.

Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inalinda rasilimali za uvuvi huku akitaja hatua ambazo zimechukuliwa ikiwemo ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Januari 30 mwaka huu, ambapo aligawa boti za uvuvi za kisasa 55 kati ya 160, lengo likiwa ni kuwawezesha wavuvi kuwa na vifaa bora kwa ajili ya uvuvi ndani ya Ziwa Victoria.

Amebainisha kuwa LVFO wameamua kuja na mradi wa pamoja ili kulinda rasilimali za uvuvi wakiwezeshwa na Umoja wa Ulaya ili kuhakikisha samaki wanapatikana kwa wingi na kufikishwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.

Pia, amesema baada ya kukabidhiwa vifaa kutakuwa na mafunzo kwa maofisa ili kuhakikisha wanapambana na uhalifu wa uvuvi haramu kwa kutumia njia za kisasa na kuwakamata wahalifu.

Kwa upande wake Bw. Lukunya Edward akimwakilisha Katibu Mtendaji wa LVFO wakati wa kukabidhi boti hizo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema vifaa hivyo vitatumika zaidi katika kudhibiti uvuvi haramu na kutunza rasilimali za uvuvi.

Amefafanua kuwa katika kudhibiti uvuvi haramu kutasaidia kukuza samaki kwa wingi na kuongeza upatikanaji wa samaki na kuwezesha jamii zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria kunufaika na mazao ya uvuvi.

Tanzania kukabidhiwa boti mbili zenye thamani ya takriban Shilingi Milioni 100 pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya doria ndani ya Ziwa Victoria ni mradi uliopita kwenye Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo jumla ya boti sita na injini tisa zimegaiwa kwa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (wa kwanza kulia) akikagua boti mbili za doria kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria, kabla ya kukabidhiwa boti hizo kwa serikali kutoka Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. (04.03.2024)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (mwenye koti jeusi, katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa boti mbili za doria kwa serikali ili kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria. (04.03.2024)

Moja ya boti za kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria, iliyokabidhiwa kwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwa kwenye majaribio, ambapo Tanzania imekabidhiwa boti mbili zenye thamani ya takriban Shilingi Milioni 100 pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya doria ndani ya Ziwa Victoria kupitia mradi wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo jumla ya boti sita na injini tisa zimegaiwa kwa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda. (04.03.2024)


 








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni