Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

WIZARA YAZIDI KUKUTANA NA WADAU WA UVUVI KUTEKELEZA AGIZO LA MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Na. Edward Kondela

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwataka watendaji wa wizara hiyo kuendelea kuwatembelea wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kutatua changamoto zao.

Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi) Bi. Agness Meena amebainisha hayo leo (28.02.2024) katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi ili kusikiliza hoja zao na changamoto zinazowakabili.

Bi. Meena amesema wizara inataka kupunguza changamoto zilizopo katika Sekta ya Uvuvi kwa kufanya mikutano na wadau na kufanya maboresho yakiwemo ya kisera na kisheria ili sekta hiyo izidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la taifa.

Amebainisha kuwa kupitia hotuba aliyotoa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kugawa boti na vizimba jijini Mwanza, amesema lengo la serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kutatua changamoto za sekta hiyo kupitia vikao endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema wizara imepokea maoni yote yaliyotolewa na wadau hao na kwamba watahakikisha yanafanyiwa kazi na kwamba katika kikao kijacho hoja zao zitakuwa zimefanyiwa kazi.

Amesema katika kikao hicho wadau hao hawapaswi kukata tamaa kwa kuwa baadhi ya hoja huenda zikawa zinafanyiwa kazi hatua kwa hatua hadi kufikia muafaka.

Nao baadhi ya wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi waliohudhuria kikao hicho wamepongeza namna serikali inavyoendelea kuwajali na kuwapa fursa ya kuwasikiliza huku wakishauri hatua zaidi ziendelee kuchukuliwa ikiwemo elimu dhidi ya uvuvi haramu.

Wameongeza kuwa kwa sasa serikali imechukua hatua kubwa katika kulinda rasilimali za uvuvi huku wakiomba kuboreshwa zaidi kwa mazingira ya uwekezaji ili wapate masoko zaidi ya mazao hayo hususan nje ya nchi.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na vikao vya kukutana na wadau wa Sekta ya Uvuvi maeneo mbalimbali nchini ili kupata maoni na hoja za wadau hao ili zifanyiwe kazi lengo likiwa ni kukuza zaidi na kuongeza tija katika sekta hiyo.


Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi) Bi. Agness Meena akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwataka watendaji wa wizara hiyo kuendelea kuwatembelea wadau wa Sekta ya Uvuvi ili kutatua changamoto zao. (28.02.2024)

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, ambapo amewahakikishia wadau hao kuwa maoni yao yatafanyiwa kazi na kupatiwa mrejesho katika vikao vijavyo ili kukuza Sekta ya Uvuvi nchini. (28.02.2024)


Picha ya pamoja ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bi. Agness Meena (wa tano kutoka kulia, mstari wa kwanza) akiwa na baadhi ya watendaji kutoka wizarani na wadau wa viwanda na biashara ya mazao ya uvuvi, baada ya kikao kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam ili kusikiliza maswali na hoja zao katika kukuza Sekta ya Uvuvi nchini. (28.02.2024)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni