Nav bar

Alhamisi, 7 Machi 2024

VIBALI VYA UVUVI KWA NJIA YA KIELETRONIKI NDANI YA SIKU SABA

Na. Edward Kondela

Serikali imesema katika kipindi kifupi kijacho itahakikisha vibali vinavyohusu masuala ya uvuvi vinatolewa kwa njia ya kieletroniki ndani ya siku saba.

Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema hayo leo (27.02.2024) katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya kikao kifupi na baadhi ya wadau wa uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi.

Prof. Sheikh amesema kuwa mfumo wa kutoa vibali kwa njia ya kieletroniki utawezesha kutolewa vibali ndani ya siku saba ili kurahisisha huduma kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi kupata vibali popote walipo.

Ameongeza kuwa mikakati ya wizara ni kwamba kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2023/24 inatarajia kuanza rasmi utoaji wa vibali hivyo kwa nji ya kieletroniki.

Ameongeza kuwa nia ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kupunguza ucheleweshaji wa vibali na kuifanya Sekta ya Uvuvi kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.

Katika kikao hicho pia Prof. Sheikh amepata muda wa kuwaarifu wadau hao mikakati mbalimbali ya serikali katika kukuza Sekta ya Uvuvi pamoja na kujibu hoja na maswali mbalimbali kutoka kwa wadau juu ya kuimarisha sekta hiyo.

Baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi waliohudhuria kikao hicho, wamepongeza namna serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyofanya jitiohada mbalimbali za kukuza sekta hiyo ikiwemo ya kuhakikisha uwepo wa zana bora za uvuvi.

Wamesema wako pamoja na serikali katika kuhakikisha uvuvi haramu unadhibitiwa ili kulinda rasilimali za uvuvi na kuomba uwepo wa mikakati zaidi ya kudhibitiwa kwa nyavu haramu ambao hazitakiwi nchini. 


Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh akizungumza na baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi (hawapo pichani) wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi ambapo amewahakikishia kuwa katika kipindi kifupi kijacho serikali itaanza kutoa vibali vinavyohusu masuala ya uvuvi kwa njia ya kieletroniki ndani ya siku saba. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. (27.02.2024)

Mratibu wa mradi wa Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (TASFAM) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nichrous Mlalila akisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi, wakati wa kikao alichohitisha Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (hayupo pichani) na wadau hao kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. (27.02.2024)

Picha ya pamoja ya Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh (wa tatu kutoka kulia, mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaojishughulisha na uuzaji wa nyavu za uvuvi na maafisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, baada ya kikao kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam, kujadili namna ya kuboresha sekta hiyo. (27.02.2024)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni