Nav bar

Jumatano, 6 Machi 2024

SERIKALI YAZINDUA BBT-LIFE (UVUVI) AWAMU YA PILI.

 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu imezindua awamu ya pili ya program ya Jenga kesho iliyo bora kwa wanawake na vijana kwa upande wa sekta ya Uvuvi maarufu kama “BBT-LIFE” tukio lililofanyika leo februari 23, 2024 kwenye  Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Mbegani Bagamoyo mkoani Pwani.

Uzinduzi huo ambao umetanguliwa na mafunzo ya siku 5 ya kubadili fikra kwa vijana na wanawake 300 waliochaguliwa kunufaika na awamu ya pili  program hiyo umefanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bi. Agness Meena ambaye amewasisitiza vijana hao kuhakikisha wanatumia vema mafunzo kwa vitendo watakayopewa kwa muda wa miezi 3 kwenye vituo walivypangiwa baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo ya Nadharia.

“Baada ya kukamilika kwa mafunzo ya siku 5 ya “mind-set transformation” mnaenda kwenye mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi 3, nitoe rai kwenu wote mkazingatie yale yote mtakayojifunza huko ili mkitoka huko muweze kujiajiri na kuajiri wenzenu ambao hawakupata fursa ya kushiriki kwenye programu kwa awamu hii” Amesema Bi. Meena.

Bi. Meena ameongeza kuwa lengo la Wizara yake ni kutengeneza vijana na wanawake watakaokuwa wajasiriamali wakubwa kwenye upande wa sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji wa samaki kwenye  vyanzo vya asili vya maji chumvi na baridi, mabwawa na kilimo cha zao la mwani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw.Robert Masingiri amebainisha kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE ni sehemu ya utekelezaji wa program ya Taifa ya kukuza ujuzi nchini kupitia kipengele cha mafunzo ya wanagenzi.

“Programu hii yote inagharamiwa na Serikali na kila mwaka huwa inatenga kiasi cha Bil.9 kwa ajili ya kuhakikisha vijana na wanawake wanapata ujuzi stahiki ili waweze kujiajiri na mpaka sasa imeshatoa kiasi cha shilingi Bil. 5.5 kwa ajili ya utekelezaji wa program hiyo” Amesizitiza Bw. Masingiri.

Akizungumzia namna Taasisi yake ilivyojipanga kuwawezesha mikopo wahitimu wa program hiyo, Mwakilishi wa benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Bw. Kezilahabi Jumanne amesema kuwa walipata nafasi ya kutoa elimu ya uandaaji maandiko ya kibiashara kwa wanufaika hao hivyo anaamini baada ya kuhitimu mafunzo hayo baadhi yao watakuwa wateja wao wa moja kwa moja kupitia mikopo watakayowawezesha.

Wakizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzao wao, Mshiriki kutoka Zanzibar Bi. Samia Othman na mwingine kutoka Kagera Bw. Marius Juvinali wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kuingia kwenye awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE ambapo wameahidi kuzingatia yale yote watakayoelekezwa wakati wa mafunzo kwa vitendo kwenye vituo walivyopangiwa.

Utekelezaji wa programu ya “Jenga Kesho iliyo bora kwa wanawake na vijana kupitia sekta ya Uvuvi kwa mwaka huu unafanyika kwa mara ya pili ambapo kwa mwaka jana Programu hii ilihusisha vijana na wanawake 200 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanufaika wa BBT-LIFE waliokuwa na changamoto ya usikivu hafifu Bw. Sayid Ngasa (kulia nyuma) na Bi. Maria Mahona (katikati nyuma) muda mfupi baada ya uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Leo Februari 23, 2024 Bagamoyo mkoani Pwani. Kushoto nyuma ni Mtafsiri wao wa lugha ya alama Bw. Mmanga Haji.  Wengine pichani ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw. Robert Masingiri (kulia mbele) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanufaika wa awamu ya pili ya programu ya BBT-LIFE (Uvuvi) muda mfupi baada ya uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Leo Februari 23, 2024 Bagamoyo mkoani Pwani. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Bw. Robert Masingiri na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni