Nav bar

Jumatatu, 26 Januari 2026

DKT. BASHIRU AZIAGIZA LITA, TARILI KUFANYA MAGEUZI SEKTA YA MIFUGO

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ameitaka Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kutumia mafunzo na tafiti za mifugo za kisasa  kuwanufaisha wafugaji nchini.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo leo Januari 24, 2026 wakati wa ziara yake kwenye taasisi hizo zilizopo Mabuki mkoani Mwanza, ambapo amesema tafiti na mafunzo  ya mifugo yanayoendana na wakati yatumike kuwabadilisha wafugaji kufuga kisasa.

“Utafiti wetu mzuri, mafunzo yetu mazuri vitumike kwenda kubadilisha wafugaji, sisi tuwachague wale ambao wameshabadilika na wamewekeza , tuwape utaalam zaidi ili watumike kama wasambazaji wa teknolojia” alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru aliitaka LITA kufanya ufuatiliaji wa utaalam unaotolewa kwa wafugaji kutokana na mafunzo yanayotolewa na Wakala huo huku TALIRI ikiagizwa kufuatilia matumizi ya tafiti kutoka kwa wadau wa sekta ya mifugo.

Katika hatua nyingine alihimiza wataalam kuzingatia maadili ya taaluma katika kuwahudumia wafugaji ili kuimarisha ushirikiano utakaokuza sekta ya mifugo nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa  akitoa maelekezo  kwa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhusu mageuzi ya sekta ya mifugo nchini wakati wa ziara yake  kwenye  taasisi hizo leo Januari 24, 2026 Mabuki, Mkoani Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (wapili, kulia) akizungumza na baadhi ya wanafunzi wanasoma  katika Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA)  wakati alipotembelea  kukagua shughuli zinazofanywa na wakala hao leo Januari 24, 2026 Mabuki, Mkoani Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kulia) akikagua Mitamba inayopatikana katika shamba la kuzalishia mifugo la Mabuki wakati wa Ziara yake  leo Januari 24, 2026 Mabuki, Mkoani Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kulia) akikagua Mitamba inayozalishwa katika shamba la kuzalishia mifugo la Mabuki wakati wa Ziara yake  leo Januari 24, 2026 Mabuki, Mkoani Mwanza.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Wa nne, Kushoto) akikagua Mbegu ya Mbuzi  wanaozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakati alipotembelea taasisi hiyo leo Januari 24, 2026 Mabuki, Mkoani Mwanza.


TAWFA YAJIVUNIA MAFANIKIO WALIYOYAFIKIA, WAISHUKURU SERIKALI

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wanaojishughulisha na Uvuvi Tanzania (TAWFA), Bi. Beatrice Mmbaga amekutana na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena, Jijini Dodoma Januari 22, 2026 kwa lengo la kuishukuru serikali na kueleza mafanikio waliyoyapata  tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019. 

Mwenyekiti huyo  wa TAWFA, Bi. Mmbaga akiwasilisha taarifa yake ya mafanikio alisema  kuwa TAWFA imefanikiwa kuanzisha kanda mbalimbali ikiwemo  Kanda ya Maji ya Bahari na Pwani, Kanda ya Ziwa Tanganyika, Kanda ya Ziwa Victoria pamoja , Kanda ya Ziwa Nyasa na Maji Madogo huku akifafanua kuwa hatua hiyo imeongeza ushiriki wa wanawake, upatikanaji wa mitaji elimu na vitendea kazi. 

“Zaidi ya wanawake 2000 wa TAWFA wamefaidika na VICOBA kwa kupata mikopo yenye riba nafuu yenye thamani ya Tshs. zaidi ya 160,000,000, huku TAWFA ikiendelea  kuimarika kwa kitambulika kikanda na Kimataifa ambapo sasa ni mwanachama wa World FisherFolks na African Women FishWorkers Association (AWFISHNET)”, alibainisha Bi. Mmbaga

Akiwasilisha taarifa yake hiyo, Bi. Mmbaga alisema vipaumbele vyao mbalimbali ikiwemo kupata ithibati ya ubora ya TBS ili waweze kusafirisha bidhaa zao nje ya nchi, upatikanaji  wa vitambulisho, kuwaunganisha  wanachama wao na taasisi za kifedha pamoja na Masoko ya Nje na kuwawezesha Wanachama mafunzo ya uongozi na elimu ya namna ya kuendesha vikundi vyao huku wakiiomba wizara kuwasaidia vitendea kazi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena baada ya kusilikiliza taarifa yao hiyo aliwaeleza kuwa Wizara kama mlezi wao itaendelea kushirikiana na TAWFA kwa kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za kifedha  pamoja na benki, hatua itakayowasaidia wanachama wa chama hicho kupata mikopo na mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uvuvi.

Aidha, Bi. Meena aliwahimiza  viongozi hao wa TAWFA kuendelea kujiimarisha zaidi kwa lengo la kuweka misingi mizuri ya kujitegemea zaidi kiuchumi na kukuza shughuli zao ili kuimarisha mchango wa wanawake katika sekta ya uvuvi nchini huku akiwahimiza  kuanzisha vyama vya ushirika vya  kifedha (SACCOS) ili kuwawezesha wanachama kupata mitaji.  

Awali,  Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bi. Prisca  Issangya alieleza kuwa  lengo la FAO ni kuinua wanawake kiuchumi kwa kuwawezesha kupata elimu na uwezo huku akiendelea kubainisha kuwa FAO iko tayari kushirikiana na TAWFA katika kuwaunganisha wanawake na mashirika ya fedha ili kuwasaidia kupata rasilimali zitakazowawezesha kukuza shughuli zao.

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, watendaji wa Wizara na viongozi wa TAWFA baada ya kikao cha kujadili maendeleo ya wanawake katika sekta ya mifugo na uvuvi  Januari 22, 2026 Mtumba Jijini Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena, akizungumza na viongozi wa TAWFA kuhusu umuhimu wakujiimsrisha zaidi Ili kuweza kujijengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi, upatikanaji wa mitaji na kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta ya mifugo na uvuvi Januari 22, 2026 Mtumba Jijini Dodoma

Mwenyekiti wa TAWFA Bi. Beatrice Mmbaga akiwasilisha taarifa ya mafanikio, changamoto na vipaumbele vya chama wakati wa kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Januari 22, 2026 Mtumba Jijini Dodoma

Mwakilishi wa FAO, Bi. Prisca John, akitoa maelezo kuhusu mchango wa FAO katika kuinua wanawake katika sekta ya  uvuvi wakati wa kikao cha TAWFA kilichofanyika Januari 22, 2026 Mtumba Jijini Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi Dkt. Baraka Sekadende akizungumza wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na viongozi wa TAWFA kilichofanyika Januari 22, 2026 Makao Makuu ya Wizara, Mtumba Jijini Dodoma


SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KUONGOZWA KISAYANSI

Na. Edward Kondela

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali itazingatia masuala ya kitaalamu, ushauri wa kisayansi na tafiti katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.

Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amebainisha hayo leo (22.01.2026), alipofanya ziara ya kikazi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro, ili kuweka pamoja makubaliano ya kushirikiana kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na SUA.

Akizungumza na baadhi ya wanachuo, wakati akijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa chuoni hapo, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza kuzingatia masuala ya kitaalamu, ushauri wa kisayansi na tafiti katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.

“Wizara imepewa maelekezo ya Mhe. Rais pamoja na Dira ya Maendeleo ya miaka 25 inatuelekeza kutoka kufuga kienyeji na kufuga kisasa pamoja na kufuga kwa tija na ufanisi.” Amefafanua Mhe. Balozi Dkt. Bashiru

Aidha, ameongeza kuwa SUA ni moja ya vyuo vyenye heshima nchini katika masuala ya mafunzo, ushauri wa kitaalamu na masuala ya utafiti kwenye kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

Amewataka wanachuo hao kusoma na baadae kufanya tafiti, kwa kuwa eneo la malisho ya mifugo lina biashara kubwa zikiwemo mbegu zake na kwamba wizara na SUA zimeunda kamati katika maeneo ya utafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu, hususan katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa, malisho ya mifugo, maabara pamoja na kuongeza nguvu katika ufugaji wa kuku.

Awali, akizungumza wakati wa kikao kilichoshirikisha uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na SUA, Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amesema kutokana na tasnia ya maziwa kuendelea kuku hapa nchini, chuo hicho kimeamua kuanzisha kozi kwa ajili ya kutoa wataalamu wa tasnia hiyo.

Amefafanua kuwa lengo la chuo ni kuboresha ili kila mhitimu anayetoka chuoni hapo awe na utaalamu wa kujitosheleza katika nyanja mbalimbali na kuweza kufanya kazi kwa ufasaha katika sekta binafsi na umma.

Pia, amesema kwa upande wa madaktari wa mifugo SUA imeendelea kuboresha vifaa vya kufundishia ili kuhakikisha wanatoka madktari wenye uwezo zaidi kadri muda unavyozidi kwenda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akizungumzia uzalishaji wa vifaranga vya samaki, amesema ni wakati wa kuzingatia mbari za aina ya vifaranga ili kupata vinavyoweza kuzalishwa kwa muda mfupi.

Amesema ni muhimu kupatikana kwa vifaranga vya namna hiyo kulingana na uhitaji wa soko kwa kuwa watu wengi wamekuwa wakijikita katika ufugaji wa samaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto), akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Edwin Mhede wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro, ambapo alipata fursa ya kushuhudia hatua za uzalishaji wa vifaranga vya samaki. (22.01.2026)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akipanda mbegu za malisho wakati alipofanya ziara ya kikazi Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro. (22.01.2026)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto), akishuhudia namna wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro, wakimfanyia upasuaji paka katika hospitali ya rufaa ya wanyama iliyopo chuoni hapo. (22.01.2026)

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro, wakifurahia jambo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kulia), alipofanya ziara ya kikazi chuoni hapo na kutembelea hospitali ya rufaa ya wanyama. (22.01.2026)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akipatiwa maelezo juu ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya kambale, baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro. (22.01.2026)

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Mkoani Morogoro, Prof. Raphael Chibunda (kulia), akizungumza na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Edwin Mhede wakati Mhe. Balozi Bashiru alipofanya ziara ya kikazi katika chuo hicho ili kuimarisha ushirikiano na makubaliano kati ya wizara na SUA kwenye masuala ya kitaalamu, ushauri wa kisayansi na tafiti. (22.01.2026)


SEMINA YA MAFUNZO ELEKEZI KUHUSU SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI YAKAMILIKA

 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini yake imehitimisha Semina ya Mafunzo Elekezi iliyotolewa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhusu shughuli zinazo ratibiwa na kusimamiwa na Wizara hiyo.

Akizungumza kwenye tamati ya semina, Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Deudatus Mwanyika aliwapongeza viongozi pamoja na wataalam wa wizara hiyo kwa uwasilishaji mzuri wa semina hiyo ya siku 2 iliyoanza Januari 19, 2026 na kuhitimishwa leo Januari 20, 2026 Bungeni Jijini Dodoma.

Aidha Mhe. Mwanyika amesisitiza wizara kuendelea kuboresha matumizi ya teknolojia za kisasa za kitafiti pamoja na mafunzo yanayoendana na teknolojia hiyo kwa watumishi na wataalamu wa sekta zote ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi.

Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema Wizara yake inaendelea kuimarisha na kuboresha huduma zinazotolewa na sekta hizo na kuahidi ushirikiano wa dhati na kamati hiyo. 

Aidha aliongeza kuwa yapo mabadiliko mengi yanayoendelea kwenye sekta hiyo yanayolenga kutatua changamoto za wananchi pamoja na wadau wa sekta hiyo ya mifugo na uvuvi.

Semina hiyo ililenga kuliongezea Bunge uelewa kuhusu sekta ya Mifugo na Uvuvi na mabadiliko yanayotarajiwa katika sekta hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza wakati wa semina ya kuipitisha  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwenye majukumu na Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi iliyokamilika leo Januari 20,2026 Bungeni jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika akitoa maelekezo kwa Viongozi na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kamati yake kupitishwa kwenye majukumu na maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi Januari 20, 2026 Bungeni jijini Dodoma.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakitoa maoni na ushauri mara baada ya kupokea Semina elekezi ya kujengewa uelewa kuhusu shughuli zinazo Simamiwa na Kuratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokamilika leo Januari 20, 2025 Bungeni jijini Dodoma.

Sehemu ya Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye semina elekezi ya kuipitisha kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwenye majukumu na Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi iliyokamilika leo Januari 20,2026 Bungeni jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhusu shughuli zinazosimamiwa na taasisi hiyo wakati wa mafunzo ya Semina elekezi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokamilika leo January 20, 2025, Bungeni jijini Dodoma.


Jumatatu, 19 Januari 2026

BUNGE LAPIGWA MSASA KUHUSU SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wamepewa semina  kuhusu Majukumu mbali mbali yanayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi zake.

Semina hiyo ya siku 2 imeanza leo Januari 19, 2026 Bungeni Jijini Dodoma ambapo mara baada ya kupewa semina hiyo wabunge hao kupitia kwa Mwenyekiti  wa Kamati hiyo Mhe. Deudatus Mwanyika walitoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kuharakisha mchakato wa kuunda Mamlaka ya uvuvi nchini ili kusaidia usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kuongeza tija ya kiuchumi na usalama wa chakula kupitia uzalishaji wa malisho ya mifugo.

“Pamoja na Jitihada hizo, lakini tunaomba huu mchakato wa kuunda mamlaka ya uvuvi uharakishwe kwa sababu usimamizi wa uvuvi bado unachangamoto, vilevile suala la malisho liangalieni “ alisema Mhe. Mwanyika.

Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema Wizara yake inaendelea kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kujenga Bandari ya Uvuvi ambayo  ujenzi wake umefikia asimia 90 na mkandarasi anatarajiwa kukabidhi bandari hiyo ifikapo Machi 31 Mwaka huu. 

Balozi Dkt. Bashiru amesema baada ya kukamilika kwa bandari hiyo, serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itanunua meli mbili kwa ajili ya shughuli za uvuvi wa bahari kuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la serikali la kuwa na meli tano za uvuvi.

Semina hiyo iliyolenga kuliongezea Bunge uelewa kuhusu sekta ya Mifugo na Uvuvi na mabadiliko yanayotarajiwa katika sekta hiyo itaendelea Januari 20,2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika akitoa maelekezo kwa Viongozi na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara baada ya kamati yake kupitishwa kwenye majukumu na maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi Januari 19,2026 Bungeni jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza wakati wa semina ya kuipitisha  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwenye majukumu na Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi iliyofanyika Januari 19,2026 Bungeni jijini Dodoma.

Sehemu ya Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiwa kwenye semina elekezi ya kuipitisha kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwenye majukumu na Maendeleo ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi iliyofanyika Januari 19,2026 Bungeni jijini Dodoma.

SERIKALI, IFAD KUENDELEZA MIRADI YA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ambapo wamejadili kuhusu miradi inayotekelezwa kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi.

Akizungumza katika Kikao hicho kilichofanyika leo Januari 16, 2026, Ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru ameonesha kufurahishwa na ujio wa ujumbe huo ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa IFAD nchini.

Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha mazingira kuwa rafiki ili kuruhusu wawekezaji na sekta binafsi kushiriki katika kusukuma maendeleo ya wananchi.

Ujumbe huo wa IFAD  umeongozwa na Mkurugenzi wa Nchi na Mwakilishi wake nchini Tanzania Bw. Seth Meng pamoja na Mratibu wa Mpango wa Nchi wa IFAD Bi. Jacqueline Machangu.

Majadiliano hayo yalijikita kujadili mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) na Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayotekelezwa kati ya sekta ya mifugo na uvuvi.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Wa kwanza, kushoto) akizungumza Ujumbe wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) nchini Tanzania kujadili miradi inayotekelezwa katika sekta ya mifugo na uvuvi, wakati wa Kikao kilichofanyika ofisini kwake leo Januari 16, 2026 Mtumba, Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi  wa Nchi na Mwakilishi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Seth Meng (Katikati) akielezea mpango wa utekelezaji wa miradi ya sekta ya mifugo na uvuvi  Januari 16, 2026 Mtumba, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Nchi na Mwakilishi wa IFAD Bw. Seth Meng (Kulia) akimpa maelezo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya sekta za mifugo na uvuvi wakati wa majadiliano yaliyofanyika Ofisi ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Januari 16, 2026 Mtumba, Jijini Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Katikati), Mkurugenzi wa Nchi na Mwakilishi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD Bw. Seth Meng (Kushoto) na Mratibu wa Mpango wa Nchi wa IFAD Bi. Jaqueline Machangu (Kulia) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya majadiliano yaliyofanyika Ofisi ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Januari 16, 2026 Mtumba, Jijini Dodoma.

WAKUZAJI VIUMBEMAJI 2000 KUJENGEWA UWEZO WA MBINU BORA ZA UFUGAJI SAMAKI

Na. Stanley Brayton, WMUV

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wakuzaji viumbemaji katika uzalishaji wa samaki, kutengeneza chakula cha samaki, usimamizi wa mabwawa na masuala ya jinsia na lishe ili kuimarisha mifumo jumuishi ya usalama wa chakula.

Akizungumza katika kikao kazi cha kutekeleza programu hiyo, leo Januari 15, 2026 wilayani Songea mkoani Ruvuma, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Ruvuma, Bw. Deogratius Sibula amesema  programu ya (AFDP), inayotekelezwa kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni nyenzo muhimu ya Serikali katika kuimarisha Sekta ya Ukuzaji viumbemaji nchini.

“Programu hii itafanyika katika halmashauri tano za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Halmashauri za Wilaya ya Mbiga, Namtumbo, Nyasa na Tunduru.” amesema Bw. Sibula

Aidha, Bw. Sibula amesema kuwa Utekelezaji wa Majukumu ya Programu hiyo inalenga kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbemaji 2,000 katika Mkoa wa Ruvuma, ambapo, katika awamu hii utafanyika katika kata 25 ndani ya Halmashauri hizo 5 za Mkoa wa Ruvuma, kuanzia tarehe 15 Januari 2026 hadi tarehe 22 Januari 2026.

Vilevile, Bw. Sibula amebainisha kuwa mafunzo haya ni fursa kwa wakuzaji viumbemaji na yatakuwa na tija kubwa kwa wafugaji wa samaki wa Mkoani Ruvuma na kuhamsha hali ya ufugaji kutoka ule wa kujikimu na kuwa na ufugaji wa kibiashara unaozingatia mbinu bora za ufugaji.

Kwa Upande wake, Afisa Uvuvi Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni Afisa Kiungo wa Programu ya AFDP, Bi. Mkomanile Mahundi amesema zoezi hilo litajumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu (PMO) pamoja na wataalam kutoka Halmashauri nane za mkoa wa Ruvuma. 

Bi. Mahundi amebainisha kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yataendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Morogoro, Tanga, Geita pamoja na Mkoa wa Tabora.

Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali Mkoa wa Ruvuma, Bw. Deogratius Sibula (mstari wa mbele katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Sekta ya Uvuvi, baada ya Kikao kazi cha kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kinacholenga kuwajengea uwezo wakuzaji Viumbemaji nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, Januari 15, 2026 Ruvuma.

Afisa Uvuvi Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye ni Afisa Kiungo wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), Bi. Mkomanile Mahundi, akizungumza na wadau wa Sekta ya Uvuvi, katika Kikao kazi cha kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kinacholenga kuwajengea Uwezo wakuzaji Viumbemaji nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, Januari 15, 2026 Ruvuma.

Mtaalamu wa Jinsia na Lishe Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Irene Mmbando, akiwasilisha Mada kuhusu utambuzi wa walengwa wanaojihusisha na masuala ya Ukuzaji Viumbe Maji (Samaki) kwenye Mabwawa, watika wa Kikao kazi cha kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kinacholenga kuwajengea Uwezo wakuzaji Viumbemaji nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, Januari 15, 2026 Ruvuma.

Picha ni baadhi ya wadau wa Sekta ya Uvuvi, wakimsikiliza Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali, Bw. Deogratius Sibula (hayupo pichani), katika Kikao kazi cha kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kinacholenga kuwajengea Uwezo wakuzaji Viumbemaji nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, Januari 15, 2026 Ruvuma.





Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji Mali, Bw. Deogratius Sibula, akihutubia wadau wa Sekta ya Uvuvi, katika Kikao kazi cha kutekeleza Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kinacholenga kuwajengea Uwezo wakuzaji Viumbemaji nchini, kilichofanyika katika Ukumbi wa Songea Club, Januari 15, 2026 Ruvuma.




DKT. BASHIRU APIGA MARUFUKU MAAMUZI YANAYOATHIRI BIASHARA ZA WAFUGAJI, WAVUVI

◼️Ni kufuatia mzozo uliotokea mkoani Tanga

◼️Asisitiza mazungumzo yachukue nafasi kubwa zaidi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amepiga marufuku kwa wasimamizi wa sheria katika ngazi zote kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi kufanya maamuzi yatakayoathiri mwenendo wa biashara kwa wadau wa sekta hizo.

Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo Januari 15, 2025 mkoani Dodoma wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa machinjio ya nyama ya Serikali iliyopo maeneo ya Kizota ambapo amewataka wasimamizi hao kuhakikisha wanaafikiana na wawekezaji na wafanyabiashara hao kwa njia ya mazungumzo.

“Haya niliyoyaona Tanga hata kama ni Halmashauri bado ni Serikali na bahati nzuri Halmashauri zote zipo chini ya Mhe. Waziri Mkuu kwa hiyo Halmashauri zote na Wizara tujizuie kufanya kazi za udhibiti kwa namna ambayo itatikisa na kuathiri shughuli za kiuchumi kwenye sekta hizi” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amewataka wataalam hao kutoa muda nyongeza kwa wafanyabishara hao na notisi ili kuwapa fursa ya kutekeleza matakwa ya sheria kabla ya kufunga bishara zao.

“Ukifunga shughuli yake kwa siku moja, watoto wake hawawezi kula na hiyo pesa hupati” Amehitimisha Balozi Dkt. Bashiru.

Kuhusiana na Machinjio ya Serikali aliyoikagua, Balozi Dkt. Bashiru amemtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambaye Machinjio hiyo ipo chini yake Bw. Mohamedi Mbwana kushughulikia dosari zote alizoziona na kuhakikisha inakuwa kwenye mazingira mazuri wakati wote.






Jumanne, 13 Januari 2026

BADILISHENI HATIMILIKI YA KIWANJA CHA UJENZI WA TAASISI - DKT. BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameagiza kubadilishwa kwa hati miliki ya kiwanja kinachotumika kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya Taasisi sita zilizo chini ya Wizara yake kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo Januari 13, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa eneo la Njedengwa jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kiutawala na kisheria na itahakikisha umiliki halali wa mali ya Serikali na kuwezesha matumizi endelevu ya jengo hilo mara baada ya kukamilika.

Balozi Dkt. Kakurwa amesema kuwa jengo hilo linajengwa kwa lengo la kuzikutanisha taasisi hizo ili kuboresha uratibu wa shughuli za kiutendaji, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi zilizokuwa zikitumika maeneo tofauti.

“Ni lazima taratibu zote za umiliki wa ardhi zikamilishwe kwa wakati ili kuepusha changamoto za kisheria na kiutendaji hapo baadaye na hati ya kiwanja hiki inapaswa kuwa chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ili kuwezesha usimamizi mzuri wa mradi na jengo lenyewe,” amesema Balozi Dkt. Bashiru

Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amewataka wasimamizi wa mradi na wakandarasi kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora, thamani ya fedha na ratiba ya utekelezaji kama ilivyoainishwa kwenye mkataba huku akisisitiza kuwa Serikali haina nia ya kuona miradi ya maendeleo ikikwama kutokana na uzembe au kutokamilisha taratibu muhimu ambapo amemtaka Mshauri Mwelekezi wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo nchini (TBA) kuhakikisha anapitisha vibali vyote muhimu kwa haraka ili kuepuka kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo.

Kwa upande wao, viongozi na wataalamu wa Wizara hiyo wamekiri kupokea maelekezo hayo ambapo wameahidi  kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa kufuata  taratibu zote za kisheria, sambamba na kuendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi huo ili kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya taasisi sita zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi unaotarajiwa kutumia zaidi ya Tshs. Bilioni 49 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha utendaji wa Wizara, kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuchochea maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini.




Jumatatu, 12 Januari 2026

DKT. BASHIRU ACHARUKA WAFUGAJI KUJERUHI WAKULIMA IRAMBA

◼️Serikali kugharamia matibabu yao 

◼️Aagiza wahusika wakamatwe mara moja

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekasirishwa na kitendo cha wafugaji Wilaya ya Iramba mkoani Singida kuijeruhi vibaya kwa panga familia ya watu wawili wanaofanya shughuli za kilimo Wilayani humo.

Hayo yamefahamika alipofika Wilayani hapo Januari 10,2026 ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua changamoto za wafugaji na wavuvi nchini ambapo mmoja wa wakulima wa Wilaya hiyo Bw. Mkoma Mustapha alielezea namna wafugaji walivyomshambulia yeye na mtoto wa kaka yake.

“Kwenye tukio hilo mimi nilipigwa mkononi na kuvunjika vidole vitatu na mguuni nilipigwa nikapasuka na mgongoni nikivua shati utanionea huruma na nilipotoka hospitali nikaenda polisi ili kujua hatma ya walionijeruhi nikajibiwa kwamba walionifanyia hivi imeshindikana kuwakamata” Ameeleza Bw. Mustapha.

Akizungumza mara baada ya kumsikiliza mkulima huyo, Balozi Dkt. Bashiru alielekeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba igharamie matibabu yote ya Mkulima hiyo ikiwa ni pamoja na kurejesha gharama alizotumia mpaka sasa.

“La pili wote waliohusika kwenye tukio hilo watafutwe wakamatwe na wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria lakini tusichochee chuki kutokana na tukio hili” Amesema Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru ameuelekeza uongozi wa kijiji, Mtendaji wa kata na polisi jamii wa eneo husika chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Wilaya hiyo kwenda kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu umuhimu wa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na kujizuia kuchukua sheria mkononi.

Akiwa Wilayani Mkalama kwenye kijiji cha Nyahaa eneo la Bukundi Balozi Dkt. Bashiru alipokea malalamiko ya baadhi ya wafugaji wa eneo hilo kuvamiwa na kupigwa na wafugaji wa Wilaya ya Meatu ambapo aliwaeleza wafugaji hao kuwa atafanya jitihada za kwenda kuzungumza na kuwasikiliza wafugaji wa upande wa Simiyu kabla ya kufanya uamuzi wa jambo hilo.

Balozi Dkt. Bashiru na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani wamehitimisha rasmi ziara yao ya takribani mikoa 13 waliyoianza Desemba 10,2025 ambayo ililenga kujitambulisha,kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi nchini.

Jumamosi, 10 Januari 2026

DKT. BASHIRU AWAPIGIA CHAPUO WAFUGAJI KUPATA MIKOPO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa Serikali inakusudia kuweka utaratibu utakawawezesha wafugaji kupata mikopo kupitia Taasisi za fedha nchini kama ilivyo upande wa Wakulima.

Balozi Dkt. Bashiru amebainisha hayo Januari 09,2026 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi nchini.

“Wakulima wanakopeshwa lakini mara chache sana wafugaji kukopeshwa na kama huwezi kukopesheka ni vigumu sana kupiga hatua kubwa lakini tatizo tulilonalo mabenki yetu gharama za mikopo zipo juu watu wanaogopa kufilisiwa” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha mikopo itakayotolewa kwa wafugaji inakuwa ya gharama nafuu kwa upande wa riba huku pia ikiwa na uwezo wa kulipwa hatua ambayo ameeleza kuwa itawasaidia wafugaji hao kufuga kisasa.

Mbali na kuzungumza na wafugaji na wavuvi wa Wilaya ya Ushetu, Balozi Dkt. Bashiru pia alitembelea na kukagua kiwanda kinachotarajiwa kusindika maziwa cha Jambo ,Machinjio ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Eneo la kupumzishia Mifugo la Chibe.



MHE. KAMANI AHITIMISHA MAFUNZO KWA WAJASIRIAMALI 350 WA SEKTA YA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani amewataka wajasiriamali 350 wa sekta ya uvuvi waliopata mafunzo ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kutumia ujuzi walioupata kwa ajili ya kuongeza ajira, Kipato na kuchagia Maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa kufunga Mafunzo hayo Leo Januari 9, 2026 katika Ukumbi wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Nyegezi Mhe. Kamani amesema serikali inaendelea kuunga Mkono wajasiriamali wanaojihusisha na uongezaji wa thamani ya mazao ya uvuvi ili kupanua biashara zao.

"Mafunzo hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake na vijana, kupitia fursa za Uchumi wa Buluu, leo mnapopewa vyeti mnakabidhiwa dhima ya kwenda kutumia ujuzi wenu kuongeza ajira, kipato na maendeleo ya Taifa” alisema Mhe. Kamani.

Aidha, aliongeza kuwa serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi ili kuongeza ufanisi unaolenga kutoa mafunzo bora ya kukuza sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu

Kwa Upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji la ENABEL kupitia mradi wa Green and Smart Cities (IncluCities) yamelenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, ushindani wa bidhaa sokoni na kuongeza kipato cha kaya.

 Awali wawakilishi wa Kundi la Vijana na Kina Mama Wajasiriliamali wakiwasilisha risala yao kwa mgeni rasmi walieleza kuwa mafunzo hayo yataenda kubadilisha mfumo mzima wa uchakataji na uongezaji wa thamani wa mazao ya Uvuvi tofauti na hapo awali walipokuwa wakitumia njia za jadi.

Jumla ya kina mama wajasiriamali 200 wamehitimu mafunzo ya usindikaji wa mazao ya samaki, huku vijana 150 wakipata mafunzo ya utayari kazini katika ukuzaji viumbe maji.

Naibu waziri wa Mifugo Na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani( Wa pili, kulia) akitunuku cheti kwa Bi. Joyce Christopher akiwa ni mmoja kati ya washiriki 350 waliohitimu mafunzo ya muda mfupi juu ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo leo Januari 9, 2026.

Naibu waziri wa Mifugo Na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani( Wa kwanza, kulia) akikagua mazao ya uvuvi yalioongezewa thamani na Kina Mama wajasiriamali waliopata mafunzo ya muda mfupi juu ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi leo Januari 9, 2026.

Mtendaji Mkuu wa  Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt. Semvua Mzighani akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku vyeti vijana na  kina Mama Wajasiriamali  350 walioshiriki mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi Leo Januari 9, 2026.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji Dkt. Nazael Madalla akielezea hali ya sekta ya Uvuvi nchini wakati wa kufunga mafunzo ya muda mfupi juu ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi leo Januari 9, 2026.

Naibu waziri wa Mifugo Na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani (kati kati, waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja  na washiriki 350 waliohitimu mafunzo ya muda mfupi juu ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo leo Januari 9, 2026.

Naibu waziri wa Mifugo Na Uvuvi Mhe. Ng'wasi Kamani akizungumza na washiriki 350 waliohitimu mafunzo ya muda mfupi juu ya ufugaji samaki na ukuzaji viumbe maji FETA Nyegezi wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo leo Januari 9, 2026.