Nav bar

Jumanne, 13 Januari 2026

BADILISHENI HATIMILIKI YA KIWANJA CHA UJENZI WA TAASISI - DKT. BASHIRU

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameagiza kubadilishwa kwa hati miliki ya kiwanja kinachotumika kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya Taasisi sita zilizo chini ya Wizara yake kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Balozi Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo Januari 13, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa eneo la Njedengwa jijini Dodoma ambapo amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kiutawala na kisheria na itahakikisha umiliki halali wa mali ya Serikali na kuwezesha matumizi endelevu ya jengo hilo mara baada ya kukamilika.

Balozi Dkt. Kakurwa amesema kuwa jengo hilo linajengwa kwa lengo la kuzikutanisha taasisi hizo ili kuboresha uratibu wa shughuli za kiutendaji, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi zilizokuwa zikitumika maeneo tofauti.

“Ni lazima taratibu zote za umiliki wa ardhi zikamilishwe kwa wakati ili kuepusha changamoto za kisheria na kiutendaji hapo baadaye na hati ya kiwanja hiki inapaswa kuwa chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ili kuwezesha usimamizi mzuri wa mradi na jengo lenyewe,” amesema Balozi Dkt. Bashiru

Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amewataka wasimamizi wa mradi na wakandarasi kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora, thamani ya fedha na ratiba ya utekelezaji kama ilivyoainishwa kwenye mkataba huku akisisitiza kuwa Serikali haina nia ya kuona miradi ya maendeleo ikikwama kutokana na uzembe au kutokamilisha taratibu muhimu ambapo amemtaka Mshauri Mwelekezi wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo nchini (TBA) kuhakikisha anapitisha vibali vyote muhimu kwa haraka ili kuepuka kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo.

Kwa upande wao, viongozi na wataalamu wa Wizara hiyo wamekiri kupokea maelekezo hayo ambapo wameahidi  kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa kufuata  taratibu zote za kisheria, sambamba na kuendelea kusimamia utekelezaji wa ujenzi huo ili kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya taasisi sita zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi unaotarajiwa kutumia zaidi ya Tshs. Bilioni 49 ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha utendaji wa Wizara, kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuchochea maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni