Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wamepewa semina kuhusu Majukumu mbali mbali yanayofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi zake.
Semina hiyo ya siku 2 imeanza leo Januari 19, 2026 Bungeni Jijini Dodoma ambapo mara baada ya kupewa semina hiyo wabunge hao kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deudatus Mwanyika walitoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kuharakisha mchakato wa kuunda Mamlaka ya uvuvi nchini ili kusaidia usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kuongeza tija ya kiuchumi na usalama wa chakula kupitia uzalishaji wa malisho ya mifugo.
“Pamoja na Jitihada hizo, lakini tunaomba huu mchakato wa kuunda mamlaka ya uvuvi uharakishwe kwa sababu usimamizi wa uvuvi bado unachangamoto, vilevile suala la malisho liangalieni “ alisema Mhe. Mwanyika.
Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema Wizara yake inaendelea kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kujenga Bandari ya Uvuvi ambayo ujenzi wake umefikia asimia 90 na mkandarasi anatarajiwa kukabidhi bandari hiyo ifikapo Machi 31 Mwaka huu.
Balozi Dkt. Bashiru amesema baada ya kukamilika kwa bandari hiyo, serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itanunua meli mbili kwa ajili ya shughuli za uvuvi wa bahari kuu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la serikali la kuwa na meli tano za uvuvi.
Semina hiyo iliyolenga kuliongezea Bunge uelewa kuhusu sekta ya Mifugo na Uvuvi na mabadiliko yanayotarajiwa katika sekta hiyo itaendelea Januari 20,2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni