Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake wanaojishughulisha na Uvuvi Tanzania (TAWFA), Bi. Beatrice Mmbaga amekutana na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agness Meena, Jijini Dodoma Januari 22, 2026 kwa lengo la kuishukuru serikali na kueleza mafanikio waliyoyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.
Mwenyekiti huyo wa TAWFA, Bi. Mmbaga akiwasilisha taarifa yake ya mafanikio alisema kuwa TAWFA imefanikiwa kuanzisha kanda mbalimbali ikiwemo Kanda ya Maji ya Bahari na Pwani, Kanda ya Ziwa Tanganyika, Kanda ya Ziwa Victoria pamoja , Kanda ya Ziwa Nyasa na Maji Madogo huku akifafanua kuwa hatua hiyo imeongeza ushiriki wa wanawake, upatikanaji wa mitaji elimu na vitendea kazi.
“Zaidi ya wanawake 2000 wa TAWFA wamefaidika na VICOBA kwa kupata mikopo yenye riba nafuu yenye thamani ya Tshs. zaidi ya 160,000,000, huku TAWFA ikiendelea kuimarika kwa kitambulika kikanda na Kimataifa ambapo sasa ni mwanachama wa World FisherFolks na African Women FishWorkers Association (AWFISHNET)”, alibainisha Bi. Mmbaga
Akiwasilisha taarifa yake hiyo, Bi. Mmbaga alisema vipaumbele vyao mbalimbali ikiwemo kupata ithibati ya ubora ya TBS ili waweze kusafirisha bidhaa zao nje ya nchi, upatikanaji wa vitambulisho, kuwaunganisha wanachama wao na taasisi za kifedha pamoja na Masoko ya Nje na kuwawezesha Wanachama mafunzo ya uongozi na elimu ya namna ya kuendesha vikundi vyao huku wakiiomba wizara kuwasaidia vitendea kazi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena baada ya kusilikiliza taarifa yao hiyo aliwaeleza kuwa Wizara kama mlezi wao itaendelea kushirikiana na TAWFA kwa kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na benki, hatua itakayowasaidia wanachama wa chama hicho kupata mikopo na mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uvuvi.
Aidha, Bi. Meena aliwahimiza viongozi hao wa TAWFA kuendelea kujiimarisha zaidi kwa lengo la kuweka misingi mizuri ya kujitegemea zaidi kiuchumi na kukuza shughuli zao ili kuimarisha mchango wa wanawake katika sekta ya uvuvi nchini huku akiwahimiza kuanzisha vyama vya ushirika vya kifedha (SACCOS) ili kuwawezesha wanachama kupata mitaji.
Awali, Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bi. Prisca Issangya alieleza kuwa lengo la FAO ni kuinua wanawake kiuchumi kwa kuwawezesha kupata elimu na uwezo huku akiendelea kubainisha kuwa FAO iko tayari kushirikiana na TAWFA katika kuwaunganisha wanawake na mashirika ya fedha ili kuwasaidia kupata rasilimali zitakazowawezesha kukuza shughuli zao.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni