Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema serikali itazingatia masuala ya kitaalamu, ushauri wa kisayansi na tafiti katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.
Mhe. Balozi Dkt. Bashiru amebainisha hayo leo (22.01.2026), alipofanya ziara ya kikazi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro, ili kuweka pamoja makubaliano ya kushirikiana kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na SUA.
Akizungumza na baadhi ya wanachuo, wakati akijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa chuoni hapo, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza kuzingatia masuala ya kitaalamu, ushauri wa kisayansi na tafiti katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.
“Wizara imepewa maelekezo ya Mhe. Rais pamoja na Dira ya Maendeleo ya miaka 25 inatuelekeza kutoka kufuga kienyeji na kufuga kisasa pamoja na kufuga kwa tija na ufanisi.” Amefafanua Mhe. Balozi Dkt. Bashiru
Aidha, ameongeza kuwa SUA ni moja ya vyuo vyenye heshima nchini katika masuala ya mafunzo, ushauri wa kitaalamu na masuala ya utafiti kwenye kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.
Amewataka wanachuo hao kusoma na baadae kufanya tafiti, kwa kuwa eneo la malisho ya mifugo lina biashara kubwa zikiwemo mbegu zake na kwamba wizara na SUA zimeunda kamati katika maeneo ya utafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu, hususan katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa, malisho ya mifugo, maabara pamoja na kuongeza nguvu katika ufugaji wa kuku.
Awali, akizungumza wakati wa kikao kilichoshirikisha uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na SUA, Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amesema kutokana na tasnia ya maziwa kuendelea kuku hapa nchini, chuo hicho kimeamua kuanzisha kozi kwa ajili ya kutoa wataalamu wa tasnia hiyo.
Amefafanua kuwa lengo la chuo ni kuboresha ili kila mhitimu anayetoka chuoni hapo awe na utaalamu wa kujitosheleza katika nyanja mbalimbali na kuweza kufanya kazi kwa ufasaha katika sekta binafsi na umma.
Pia, amesema kwa upande wa madaktari wa mifugo SUA imeendelea kuboresha vifaa vya kufundishia ili kuhakikisha wanatoka madktari wenye uwezo zaidi kadri muda unavyozidi kwenda.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akizungumzia uzalishaji wa vifaranga vya samaki, amesema ni wakati wa kuzingatia mbari za aina ya vifaranga ili kupata vinavyoweza kuzalishwa kwa muda mfupi.
Amesema ni muhimu kupatikana kwa vifaranga vya namna hiyo kulingana na uhitaji wa soko kwa kuwa watu wengi wamekuwa wakijikita katika ufugaji wa samaki.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni