Na. Martha Mbena, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa rai na ushauri kwa taasisi za fedha nchini, hasa benki, kutoa masuluhisho ya kifedha na mikopo yenye riba himilifu kwa wafugaji na wadau wa mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo ili waweze kufanya biashara shindani ya mifugo na mazao yake na kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, leo Julai 23, 2025 katika Hoteli ya Gerwill Jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la kujadili fursa za sekta ya Mifugo na ngozi ulioandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na benki ya Equity Tanzania Ltd.
"Watu wetu watakapokuja kukopa nawaomba sana tuzingatie kutokwenda zaidi ya ukomo wa riba uliowekwa na mdhibiti wa sekta ya fedha (Benki Kuu ya Tanzania). Tufanye kama vile ambavyo kiongozi wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alivyothubutu kuweka fedha ya umma kwenye afua mbalimbali ili kuwasaidia wafugaji wetu", amesema Dkt. Mhede.
Pia, ameipongeza Benki ya Equity Tanzania Ltd kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa kongamano hilo muhimu, na kuonesha utayari wa kushirikiana na Serikali katika kuwezesha mitaji, kuboresha biashara za wafugaji, kutoa mafunzo, pamoja na kuimarisha minyororo ya thamani katika sekta ya Mifugo na mazao yake, hususani sekta ya ngozi na bidhaa za ngozi.
“Kongamano hili ni fursa ya kipekee ya kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya sekta ya Mifugo. Kupitia jukwaa hili, tunaweza kuona fursa zilizopo na changamoto zinazoikabili sekta, ili kwa pamoja tuweze kuchukua hatua sahihi za kimaendeleo katika safari yetu ya Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Mifugo ili kuinua uchumi wa wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo na ngozi,” ameeleza
Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya Mifugo ni uti wa mgongo kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo ushirikiano wa karibu na taasisi kama Benki ya Equity Tanzania Ltd ni msingi imara wa mageuzi chanya katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Vile vile, Dkt. Mhede, ametoa wito kwa wadau wengine kutoka sekta mbalimbali kuiga mfano wa Benki ya Equity Tanzania Ltd kwa kuwekeza katika sekta ya Mifugo, kwa kuwa ina fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu, hasa kwenye maeneo ya uzalishaji wa ngozi bora, usindikaji wa mazao ya mifugo, na upatikanaji wa masoko ya uhakika na yenye thamani stahiki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity Tanzania Ltd, Dkt.Florens Turuka, amesema kuwa benki hiyo imeona fursa nyingi katika sekta ya Ngozi, hali iliyowasukuma kuwekeza moja kwa moja katika sekta hiyo ili kusaidia wafugaji kufikia maendeleo.
“Fursa zilizopo kwenye sekta ndogo ya ngozi ni nyingi, hivyo wafugaji wanapaswa kujitokeza kushirikiana nasi ili waendelee kukuza biashara yao,” amesema Dkt. Turuka.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania Ltd, Bi. Isabela Maganga, amesema kuwa benki hiyo imejipanga kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya Mifugo, hasa zao la Ngozi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua wigo wa biashara na kusaidia wananchi.
Ukuaji wa sekta ya Ngozi nchini Tanzania umeendelea kuimarika ambapo mwaka 2020/2021 jumla ya vipande million 11.7 vilizalishwa ikilinganishwa na vipande milioni 15.2 vya Ngozi mwaka 2024/2025 (sawa na ongezeko la asilimia 29.9), hivyo ushirikiano wa Serikali na wadau wengine kupitia mjadala ulioandaliwa na benki ya Equity utasaidia kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza sekta ya Ngozi nchini na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na mtu mmoja mmoja kwenye mnyororo wa thamani wa kisekta.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede, akizungumza wakati akifungua kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23.2025 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity, Dkt.Florens Turuka, akizungumza wakati wa kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23.2025 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity, Bi. Isabela Maganga, (aliyesimama) akizungumza wakati wa kongamano la ngazi ya juu kuhusu kufungua fursa za minyororo ya thamani ya mifugo na ngozi nchini Tanzania lililoandaliwa na Benki ya Equity lililofanyika leo Julai 23,2025 jijini Dodoma.