Nav bar

Jumatatu, 21 Julai 2025

UWEZESHAJI WAVUVI WAONGEZA MAVUNO YA SAMAKI KUFIKIA TANI ZAIDI YA LAKI 5 KWA MWAKA

Na. Hamisi Hussein, Lindi

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema Programu ya utoaji wa boti za kisasa za uvuvi pamoja na programu nyingine zimelenga  kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na shughuli za uvuvi hapa nchini.

Akikabidhi boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake awamu ya pili kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, hafla iliyofanyika katika Bandari ya Lindi leo Julai 18, 2025,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amesema uwezeshwaji wa wavuvi wadogo umeongeza tija katika sekta ya uvuvi ambapo kiwango cha samaki kinachovunwa kwa mwaka kimeongezeka zaidi  baada ya uwezeshaji huo.

"Zoezi la ugawaji wa boti za kisasa za uvuvi na Vifaa vyake lililozinduliwa na Mhe. Rais ni sehemu ya juhudi za serikali kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na sekta ya uvuvi, na juhudi hizi zimeongeza kiwango cha samaki wanaovunwa kutoka tani 387,542.56 zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.74 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 529,668.01 zenye thamani ya Shilingi trilioni 4.5 mwaka 2024/2025" alisema

Bi. Meena aliongeza kwa kusema kuwa ongezeko hilo pia limeonekana kwenye mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi ambapo yameongezeka kutoka tani 44.939.79 hadi tani 59,746.41 sawa na ongezeko la tani 14,806.7.

Katika hatua nyingine, Bi. Meena amewataka Wananchi waliokabidhiwa boti za kisasa za uvuvi  kukemea na kukataa vitendo vya Uvuvi haramu kwani serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutumia teknolojia ya kisasa ya kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu na maziwa ili kulinda rasilimali za uvuvi nchini.

 "Ni matumaini yangu kuwa ninyi mnaokabidhiwa boti hizi hivi leo mtakuwa mstari wa mbele katika kukemea na kukataza vitendo vya uvuvi haramu.  Pia nitoe rai kwa wavuvi wote nchini kuendelea kupinga vitendo hivi viovu, kwa pamoja tulinde rasilimali zetu kwa kizazi cha sasa na kijacho"

Aidha, alibainisha kuwa Idadi ya watu wanaojipatia kipato kupitia shughuli za uvuvi nchini imeongezeka kutoka watu milioni 4 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya watu milioni 6 mwaka 2025, hii ni kutokana na uwezeshwaji wa wavuvi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta ya uvuvi unaofanywa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amesema jumla ya boti 10 za uvuvi zilizokabidhiwa kwa mkoa wa Lindi na Mtwara zitawanufaisha wanufaika 427 kati ya hayo wanaume 391 wanwake 36.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bw. Nathalis Linuma amesema katika kuhakikisha wavuvi wanaunganishwa na taasisi za fedha, Mkoa huo umeendelea kufanya usajili  wa vikundi ili viweze kupatiwa mikopo ambapo hadi sasa jumla ya vikundi 8 vya ushirika wa wavuvi vimesajiliwa.

Nao baadhi ya wanufaika wa Boti hizo wameishukuru  Serikali kwa kupatiwa  vifaa hivyo kwani vitasaidia kuwa na uhakika wa samaki jambo litakaloongeza tija katika sekta ya uvuvi.

Katibu Mkuu wa. Wizara  ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (kushoto) akikabidhi Boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake  kwa wawakilishi wa vikundi vya mikoa ya Lindi na Mtwara muda mfupi baada ya uzinduzi wa zoezi hilo Julai 18, 2025 Mkoani Lindi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena  akizungumza na wavuvi ambao ni wanufaika wa mikopo ya boti za kisasa za Uvuvi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara  wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena (Kulia) akikabidhi cheti kwa mwakilishi wa kikundi cha wanufaika wa mikopo ya boti za kisasa za Uvuvi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara  wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Nathalis Linuma akizungumzia hali ya sekta ya Uvuvi kwa Mkoa wa Lindi wakati wa Hafla ya ugawaji boti hizo za Uvuvi awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 mkoani Lindi.

Sehemu ya Boti 10 za Kisasa za Uvuvi zilizokabidhiwa kwa wanufaika wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa Hafla ya ugawaji Boti hizo awamu ya pili iliyofanyika Julai 18, 2025 Mkoani Lindi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni